Maisha na Huduma ya Yesu
Uguo Kali Katika Bustani
YESU amalizapo kusali, yeye na mitume wake waaminifu 11 wamwimbia Yehova nyimbo za sifa. Halafu washuka kutoka chumba cha juu, waingia ndani ya giza la usiku lenye baridi, na kusonga mbele warudie ng’ambo ya Bonde la Kidroni kuelekea Bethania. Lakini wakiwa njiani, wasimama mahali wapapendapo sana, bustani ya Gethsemane. Hii ipo juu ya au katika ujirani wa Mlima wa Mizeituni. Mara nyingi Yesu amekutana na mitume wake hapa katikati ya mizeituni.
Akiacha wanane wa mitume—labda karibu na mwingilio wa bustani—yeye awaagiza hivi: “Ketini hapa, hata niende kule nikaombe.” Halafu awachukua wale wengine watatu—Petro, Yakobo, na Yohana—na kusonga mbali zaidi katika bustani. Yesu aingiwa na kihoro na kufadhaika sana. “Roho [nafsi, NW] yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa,” awaambia. “Kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.”
Akisonga mbele kidogo, Yesu ajibwaga chini na uso wake ukiwa umeelekezwa kifudifudi aanza kusali hivi kwa moyo wa bidii: “Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.” Amaanisha nini? Kwa nini ‘ana huzuni nyingi kiasi cha kufa’? Je! anaepa uamuzi wake wa kufa na kuandaa ukombozi?
Sivyo hata kidogo! Yesu hasihi kwamba aepushwe na kifo. Hata ile fikira ya kuepuka kifo cha dhabihu, iliyodokezwa na Petro wakati mmoja, yamchukiza sana. Bali, yeye ana uguo kali kwa sababu ahofu kwamba njia ambayo karibuni atakufa kwayo—akiwa mhalifu mwenye kudharaulika—italeta suto juu ya jina la Baba yake. Sasa yeye ahisi kwamba katika muda wa saa chache atatundikwa juu ya mti kama mtu wa aina mbaya kabisa—mkufuru dhidi ya Mungu! Hilo ndilo lamfadhaisha sana.
Baada ya kusali kirefu, Yesu arudi na kukuta wale mitume watatu wamelala. Akielekeza maneno kwa Petro, yeye asema hivi: “Je! hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni.” Hata hivyo, akikiri kwamba wamekuwa chini ya mkazo na kwamba ni saa ya usiku sana, asema hivi: “Roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”
Ndipo Yesu aenda zake mara ya pili na kuomba kwamba Mungu amwondolee “kikombe hiki,” yaani, kisehemu au mapenzi aliyogawiwa na Yehova. Arudipo, akuta tena wale watatu wamelala wakati ambapo wangalipaswa kuwa wakisali ili wasiingie katika kishawishi. Yesu asemapo nao, hawajui la kumjibu.
Mwishowe, mara ya tatu, Yesu aenda umbali wa kutupa jiwe, na akiwa amepiga magoti na kwa vilio vikali na machozi, asali hivi: “Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki.” Yesu ahisi maumivu makali kwa sababu ya suto ambalo kifo chake kama mhalifu kitaleta juu ya jina la Baba yake. Kwani, kushtakiwa kuwa mkufuru—mtu alaaniye Mungu—kwakaribia kuzidi kiasi kiwezacho kuhimiliwa!
Hata hivyo, Yesu aendelea kusali hivi: “Walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.” Kwa utiifu Yesu atiisha mapenzi yake kwa yale ya Mungu. Iwapo hivyo, malaika kutoka mbinguni atokea na kumwimarisha kwa maneno ya kutia moyo. Yaelekea malaika amwambia Yesu kwamba yeye ana tabasamu ya kibali cha Baba yake.
Hata hivyo, mabega ya Yesu yamekaliwa na uzito ulioje! Uhai wa milele wake mwenyewe na wa jamii nzima ya kibinadamu umo katika hatari ya kuponyoka. Mkazo wa kihisia-moyo ni mwingi mno. Hivyo basi Yesu aendelea kusali kwa moyo wa bidii zaidi, na jasho lake lawa kama matone ya damu liangukapo chini. “Ingawa hii ni ajabu itukiayo mara chache sana,” lasema The Journal of the American Medical Association, “jasho lenye damu . . . laweza kutukia katika hali zenye hisia-moyo nyingi.”
Baadaye, Yesu awarudia mitume wake mara ya tatu, na tena awakuta wamelala. Wamenyong’onyea kwa kihoro kitupu. “Laleni sasa, mpumzike [wakati wa jinsi hii nyinyi mnalala na kupata pumziko lenu, NW],” yeye apaaza mshangao. “Yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu [wa binadamu, NW] anatiwa mikononi mwao wenye dhambi. Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia.”
Huku akiwa angali katika kusema, Yuda Iskariote akaribia, ameandamwa na umati mkubwa uliochukua mienge na taa na silaha. Mathayo 26:30, 36-47; 16:21-23; Marko 14:26, 32-43; Luka 22:39-47; Yohana 18:1-3; Waebrania 5:7.
◆ Baada ya kuondoka kwenye chumba cha juu, Yesu awaongoza mitume wapi, naye afanya nini huko?
◆ Huku Yesu akiwa katika kusali, mitume wanafanya nini?
◆ Kwa nini Yesu ana uguo kali, naye amwomba Mungu nini?
◆ Ni nini chaonyeshwa na kuwa kwa jasho la Yesu kama matone ya damu?y