SURA YA 130
Yesu Akabidhiwa na Kupelekwa Akauawe
MATHAYO 27:31, 32 MARKO 15:20, 21 LUKA 23:24-31 YOHANA 19:6-17
PILATO AJARIBU KUMWEKA YESU HURU
YESU AHUKUMIWA NA KUPELEKWA KUUAWA
Licha ya kwamba Yesu amenyanyaswa kikatili na kudhihakiwa, jitihada za Pilato za kumweka huru haziwafanyi wakuu wa makuhani na wenzao wabadili mawazo. Hawataki jambo lolote lizuie Yesu asiuawe. Wanaendelea kupaza sauti: “Atundikwe mtini! Atundikwe mtini!” Pilato anajibu: “Mchukueni mkamuue ninyi wenyewe, kwa maana mimi sijampata na kosa lolote.”—Yohana 19:6.
Wayahudi wanashindwa kumsadikisha Pilato kwamba Yesu anapaswa kuuawa kwa mashtaka ya kisiasa, lakini namna gani mashtaka ya kidini? Wanarudia mashtaka yaliyohusu kukufuru ambayo yalizushwa katika kesi ya Yesu mbele ya Sanhedrini. Wanasema hivi: “Sisi tuna sheria, na kulingana na sheria anapaswa kufa, kwa sababu alijifanya kuwa mwana wa Mungu.” (Yohana 19:7) Pilato anasikia kuhusu mashtaka hayo kwa mara ya kwanza.
Anarudi kwenye jumba lake la kifalme na kujaribu kutafuta njia ya kumwachilia mtu huyu ambaye amevumilia mateso makali na ambaye mke wa Pilato aliota ndoto kumhusu. (Mathayo 27:19) Namna gani kuhusu mashtaka hayo mapya ya Wayahudi—kwamba mfungwa huyo ni “mwana wa Mungu”? Pilato anajua kwamba Yesu anatoka Galilaya. (Luka 23:5-7) Lakini anamuuliza Yesu: “Umetoka wapi?” (Yohana 19:9) Je, inawezekana kwamba Pilato anajiuliza ikiwa Yesu amewahi kuishi zamani, na kwa njia fulani anatokana na Mungu?
Pilato alisikia moja kwa moja kutoka kwa Yesu kwamba yeye ni mfalme lakini Ufalme wake si sehemu ya ulimwengu huu. Yesu haoni haja ya kufafanua jambo alilosema hapo awali, basi anakaa kimya. Yesu anapokosa kujibu, Pilato anaona kwamba anadharuliwa, na kwa hasira anamwambia hivi Yesu: “Unakataa kuzungumza nami? Je, hujui kwamba nina mamlaka ya kukufungua na mamlaka ya kukuua?”—Yohana 19:10.
Kwa ufupi Yesu anasema: “Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa kutoka juu. Ndiyo maana mtu aliyenitia mikononi mwako ana dhambi kubwa zaidi.” (Yohana 19:11) Inawezekana kwamba Yesu hazungumzii mtu mmoja tu. Badala yake anamaanisha kwamba Kayafa, wenzake, na Yuda Iskariote wana lawama kuliko Pilato.
Akiwa amevutiwa na utulivu na maneno ya Yesu, na hofu kwamba huenda Yesu ametoka kwa Mungu, Pilato anajiribu tena kumweka huru. Hata hivyo, Wayahudi wanatokeza jambo lingine ambalo lazima linamtia Pilato hofu. Wanamtisha hivi: “Ukimfungua mtu huyu, wewe si rafiki ya Kaisari. Kila mtu anayejifanya mfalme anasema vibaya kumhusu Kaisari.”—Yohana 19:12.
Gavana huyo anamtoa Yesu nje tena, na akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, anawaambia hivi watu: “Oneni! Mfalme wenu!” Hata hivyo, Wayahudi hawabadili mawazo yao. Wanapaza sauti hivi: “Mwondoe! Mwondoe! Atundikwe mtini!” Pilato anawauliza: “Je, mnataka nimuue mfalme wenu?” Kwa muda mrefu Wayahudi wamekandamizwa na utawala wa Waroma, lakini wakuu wa makuhani wanajibu: “Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.”—Yohana 19:14, 15.
Kwa woga, Pilato anakubali maombi ya Wayahudi wanaosisitiza, naye anamkabidhi Yesu akauawe. Wanajeshi wanamvua Yesu lile vazi la zambarau na kumvika mavazi yake ya nje. Yesu anapoondoka, analazimika kuubeba mti wake wa mateso.
Sasa ni Ijumaa asubuhi, Nisani 14. Yesu amekuwa macho tangu Alhamisi asubuhi na mapema na amepatwa na mateso mengi yenye kuumiza. Yesu anapojaribu kuubeba ule mti, anaishiwa na nguvu. Basi, wanajeshi wanamlazimisha mpita njia anayeitwa Simoni kutoka Kirene huko Afrika, aubebe mti mpaka kwenye eneo la kuuawa. Watu wengi wanafuata, baadhi yao wakijipigapiga kwa huzuni na kuomboleza jambo linalotendeka.
Yesu anawaambia hivi wanawake wanaoomboleza: “Binti za Yerusalemu, acheni kunililia. Bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu; kwa maana tazama! siku zinakuja ambapo watu watasema, ‘Wenye furaha ni wanawake walio tasa, na matiti ambayo hayakunyonyesha!’ Ndipo wataanza kuiambia milima, ‘Tuangukieni!’ na vilima, ‘Tufunikeni!’ Ikiwa wanafanya mambo haya wakati mti ni mbichi, itakuwaje utakapokauka?”—Luka 23:28-31.
Yesu anazungumza kuhusu taifa la Wayahudi. Ni kama mti unaokufa ambao bado una umajimaji, kwa kuwa bado Yesu yuko na pia baadhi ya Wayahudi wanaomwamini. Watu hao watakapoondolewa kutoka katika taifa hilo, taifa la kiroho lililokauka ndilo litakalobaki, kama mti uliokufa. Kutakuwa na kilio kikubwa majeshi ya Waroma yatakapotumiwa na Mungu kuliangamiza taifa hilo!