SURA YA 37
Yesu Amfufua Mwana wa Mjane
UFUFUO HUKO NAINI
Mara tu baada ya kumponya mtumwa wa ofisa wa jeshi, Yesu anaondoka Kapernaumu na kuelekea Naini, jiji lililo zaidi ya kilomita 32 upande wa kusini magharibi. Hayuko peke yake. Anasafiri pamoja na wanafunzi wake na umati mkubwa. Inawezekana ni jioni wanapokaribia maeneo yaliyo nje ya jiji la Naini. Hapo wanakutana na kikundi kikubwa cha Wayahudi wakiwa katika msafara wa mazishi. Wamebeba maiti ya kijana fulani kutoka jijini ili wakamzike.
Aliye na huzuni kuliko wote ni mama ya yule kijana. Yeye ni mjane, na sasa mwana wake wa pekee amekufa. Mume wake alipokufa, angalau bado alikuwa na mwana wake mpendwa. Wazia jinsi alivyompenda mwana huyo, kwa maana matumaini yake na usalama wake wa wakati ujao ulimtegemea mwana wake. Sasa mwana huyo pia amekufa. Ni nani atakayeishi pamoja naye na kumtegemeza?
Yesu anapomwona mwanamke huyo, anaguswa moyo na huzuni yake nyingi na hali yake yenye kusikitisha. Kwa wororo na uhakikisho unaomsaidia awe na imani, anamwambia: “Acha kulia.” Lakini anafanya mengi zaidi. Anakaribia na kuligusa jeneza lililotumiwa kuibeba ile maiti. (Luka 7:13, 14) Anatenda kwa njia inayowafanya watu waliotoka jijini wasimame ghafla. ‘Anamaanisha nini, naye atafanya nini?’ wengi wanajiuliza.
Namna gani wale wanaosafiri pamoja na Yesu ambao wamemwona akifanya miujiza, akiponya magonjwa mengi? Kwa kweli hawajawahi kumwona Yesu akimfufua mtu aliyekufa. Ingawa kuna watu waliofufuliwa zamani za kale, je, Yesu anaweza kufanya jambo kama hilo? (1 Wafalme 17:17-23; 2 Wafalme 4:32-37) Yesu anatoa agizo hili: “Kijana, ninakuambia, inuka!” (Luka 7:14) Na inakuwa hivyo. Yule kijana anaketi na kuanza kuongea! Yesu anamkabidhi kwa mama yake ambaye ingawa ameshtuka, ana shangwe nyingi. Hayuko peke yake tena.
Watu wanapoona kwamba kweli yule kijana yuko hai, wanamsifu Yehova ambaye ndiye Mpaji wa Uhai, wakisema: “Nabii mkuu ameinuliwa kati yetu.” Wengine wanaelewa maana ya tendo hilo la Yesu la kustaajabisha, nao wanasema: “Mungu amewakumbuka watu wake.” (Luka 7:16) Habari kuhusu jambo hilo la kushangaza zinaenea haraka katika maeneo yaliyo karibu na huenda mpaka kwenye mji wa nyumbani wa Yesu huko Nazareti, ulio umbali wa kilomita 10 hivi. Habari hizo zinaenea hata mpaka upande wa kusini huko Yudea.
Bado Yohana Mbatizaji yuko gerezani, na anapendezwa sana na kazi ambazo Yesu anafanya. Wanafunzi wa Yohana wanamwambia kuhusu miujiza hiyo. Anaitikiaje?