SURA YA 44
Yesu Atuliza Dhoruba Baharini
MATHAYO 8:18, 23-27 MARKO 4:35-41 LUKA 8:22-25
YESU ATULIZA DHORUBA KWENYE BAHARI YA GALILAYA
Yesu amekuwa na siku ndefu na yenye kuchosha. Inapofika jioni, anawaambia hivi wanafunzi: “Tuvuke twende ng’ambo ya bahari,” eneo lililo ng’ambo ya Kapernaumu.—Marko 4:35.
Eneo la Wagerasene liko upande wa mashariki wa ufuo wa Bahari ya Galilaya. Pia, eneo hili linaitwa Dekapoli. Majiji ya Dekapoli ni kitovu cha utamaduni wa Kigiriki, ingawa Wayahudi wengi wanaishi huko pia.
Watu wanatambua kwamba Yesu ameondoka Kapernaumu. Mashua nyingine zinaanza kuvuka bahari. (Marko 4:36) Kwa kweli si mbali sana. Bahari ya Galilaya ni kama ziwa kubwa, lenye urefu wa kilomita 21 na sehemu iliyo pana zaidi ina kilomita 12. Hata hivyo, bahari hiyo ina kina kirefu.
Ingawa Yesu ni mwanadamu mkamilifu, inaeleweka kwamba amechoka kutokana na huduma yake yenye shughuli nyingi. Basi baada ya kuanza safari, analala nyuma ya mashua, anaweka kichwa chake juu ya mto, na kulala usingizi.
Baadhi ya mitume wake wana uzoefu wa kuendesha mashua, hata hivyo hii haitakuwa safari rahisi. Eneo hilo limezungukwa na milima, na mara nyingi Bahari ya Galilaya ina joto. Nyakati nyingine, hewa yenye baridi kutoka milimani huteremka na kukutana na joto la maji ya bahari, na ghafla husababisha dhoruba kali za upepo baharini. Hicho ndicho kinachotokea sasa. Ghafla mawimbi yanaanza kuipiga mashua. Inaanza ‘kujaa maji na kukaribia kuzama.’ (Luka 8:23) Lakini, bado Yesu anaendelea kulala!
Mabaharia wanafanya juu chini kuiongoza mashua, wakitumia uzoefu wao wa zamani wa kupita katikati ya dhoruba. Lakini wakati huu mambo ni tofauti. Wakihofia uhai wao, wanamwamsha Yesu wakisema: “Bwana, tuokoe, tuko karibu kuangamia!” (Mathayo 8:25) Sasa wanafunzi wanahofu kwamba watazama!
Yesu anapoamka, anawaambia mitume: “Kwa nini mnaogopa sana, ninyi wenye imani ndogo?” (Mathayo 8:26) Kisha Yesu anaamuru upepo na bahari: “Nyamaza! Tulia!” (Marko 4:39) Upepo wenye nguvu unaacha kuvuma na bahari inatulia. (Marko na Luka wanasimulia tukio hilo lenye kusisimua, kwanza kwa kukazia kwamba Yesu anatuliza dhoruba kimuujiza, na kisha wanataja kwamba wanafunzi walikosa imani.)
Wazia jinsi jambo hilo linavyowachochea wanafunzi! Wameona jinsi bahari iliyokuwa na dhoruba kali ilivyotulia kabisa. Wanakuwa na hofu isiyo ya kawaida. Wanaambiana: “Kwa kweli, mtu huyu ni nani, hivi kwamba upepo na bahari vinamtii?” Kisha wanafika salama upande mwingine wa bahari. (Marko 4:41–5:1) Labda zile mashua nyingine zilizoanza safari zilifaulu kurudi kwenye ufuo wa magharibi.
Inafariji sana kujua kwamba Mwana wa Mungu ana nguvu za kudhibiti hali ya hewa! Atakapoelekeza fikira zake zote duniani wakati wa utawala wake, watu wote watakuwa salama, kwa maana hakutakuwa na majanga ya asili yenye kutisha!