Roho Takatifu—Kani ya Utendaji ya Mungu
KULINGANA na fundisho la Utatu, roho takatifu ndiye mtu (nafsi) wa tatu wa Uungu, aliye sawa na Baba na Mwana. Kama kisemavyo kitabu Our Orthodox Christian Faith: “Roho Mtakatifu ni Mungu kabisa.”
Katika Maandiko ya Kiebrania, neno ambalo hutumiwa mara nyingi sana kuhusu “roho” ni ruʹach, linalomaanisha “pumzi; upepo; roho.” Katika Maandiko ya Kigiriki, neno hilo ni pneuʹma, likiwa na maana kama hiyo. Je! maneno haya huonyesha kwamba roho takatifu ni sehemu ya Utatu?
Kani ya Utendaji
UTUMIZI wa Biblia wa “roho takatifu” huonyesha kwamba ni kani yenye kudhibitiwa ambayo Yehova Mungu hutumia kutimiza makusudi yake ya namna mbalimbali. Kwa kadiri fulani, yaweza kufananishwa na nguvu za umeme, kani ambayo yaweza kutumiwa kwa njia tofauti ili iendeshe mambo ya namna nyingi.
Kwenye Mwanzo 1:2, NW, Biblia hutaarifu kwamba “kani ya utendaji [“roho” (Kiebrania, ruʹach)] ya Mungu ilikuwa ikienda huko na huko juu ya uso wa maji.” Hapa, roho ya Mungu ilikuwa kani yake ya utendaji ikifanya kazi kuipa dunia umbo.
Mungu hutumia roho yake kuelimisha wale wenye kumtumikia. Daudi alisali hivi: “Nifundishe kufanya mapenzi yako, kwa maana wewe ni Mungu wangu. Roho yako [ruʹach] ni njema; iniongoze katika bara la unyoofu.” (Zaburi 143:10, NW) Wanaume 70 wenye uwezo walipowekwa kusaidia Musa, Mungu alisema kwake hivi: “Nitatwaa sehemu ya roho [ruʹach] iliyo juu yako na kuiweka juu yao.”—Hesabu 11:17.
Unabii wa Biblia uliandikwa wakati ambapo wanaume wa Mungu “walichukuliwa na roho takatifu [Kigiriki, kutokana na pneuʹma].” (2 Petro 1:20, 21, NW) Katika njia hii Biblia ‘ilivuviwa na Mungu,’ neno la Kigiriki la kusema hivyo likiwa ni The·oʹpneu·stos, linalomaanisha ‘yenye kutiwa pumzi na Mungu.’ (2 Timotheo 3:16, NW) Na roho takatifu iliongoza watu fulani waone njozi au wapate ndoto za kiunabii.—2 Samweli 23:2; Yoeli 2:28, 29; Luka 1:67; Matendo 1:16; 2:32, 33.
Roho takatifu ilisukuma Yesu aingie jangwani baada ya ubatizo wake. (Marko 1:12) Roho ilikuwa kama moto ndani ya watumishi wa Mungu, ikisababisha watiwe nishati na kani hiyo. Na iliwawezesha kunena wazi kwa ujasiri na kwa moyo mkuu.—Mika 3:8; Matendo 7:55-60; 18:25; Warumi 12:11; 1 Wathesalonike 5:19.
Kwa roho yake, Mungu hutekeleza hukumu zake juu ya wanadamu na mataifa. (Isaya 30:27, 28; 59:18, 19) Na roho ya Mungu yaweza kufika mahali popote, ikitenda kwa ajili ya watu au dhidi yao.—Zaburi 139:7-12.
‘Nguvu Izidiyo ya Kawaida’
ROHO ya Mungu yaweza pia kuwagawia “nguvu izidiyo iliyo ya kawaida” wale ambao humtumikia. (2 Wakorintho 4:7, NW) Hiyo huwawezesha wavumilie majaribu ya imani au wafanye mambo ambayo ama sivyo wasingeweza kuyafanya.
Kwa kielelezo, kuhusu Samsoni, Waamuzi 14:6 husimulia hivi: “Roho ya Yahweh ikambamba, na ingawa yeye hakuwa na silaha yoyote katika mkono wake alimrarua simba vipande vipande.” (JB) Je! kwa kweli mtu wa kimungu alimwingia au akabamba Samsoni, akiendesha mwili wake kufanya alivyofanya? Sivyo, kwa kweli “nguvu ya BWANA [ndiyo] ilifanya Samsoni kuwa imara.”—TEV.
Biblia husema kwamba Yesu alipobatizwa, roho takatifu ilishuka juu yake ikionekana kama njiwa, si kama umbo la kibinadamu. (Marko 1:10) Hii kani ya utendaji ya Mungu iliwezesha Yesu kuponya wagonjwa na kuinua wafu. Kama vile Luka 5:17 isemavyo: “Nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye [Yesu] kwa ajili ya kuponyea.”—HNWW.
Pia roho ya Mungu iliwatia nguvu wanafunzi wa Yesu kufanya mambo ya kimwujiza. Matendo 2:1-4, NW, husimulia kwamba wanafunzi walikuwa wamekusanyika pamoja kwenye Pentekoste wakati “ghafula kukatukia toka mbinguni kelele kama ile ya upepo mgumu wenye kwenda kasi, . . . nao wote wakajawa na roho takatifu na wakaanza kusema kwa lugha zilizo tofauti, kwa kadiri roho ilivyokuwa ikiwapa kutamka.”
Kwa hiyo roho takatifu ilimpa Yesu na watumishi wengine wa Mungu nguvu ya kufanya yale ambayo kwa kawaida wanadamu hawangeweza kufanya.
Si Mtu (Nafsi)
HATA hivyo je! hakuna mistari ya Biblia ambayo hunena juu ya roho takatifu kama mtu? Ndiyo, lakini angalia yale ambayo mwanatheolojia Mkatoliki Edmund Fortman husema juu ya hilo katika The Triune God: “Ingawa roho hii hufasiliwa mara nyingi kwa jinsi ya mtu, yaonekana wazi kwamba waandikaji watakatifu [wa Maandiko ya Kiebrania] hawakuiwazia wala kuionyesha kamwe roho hii kuwa mtu aliye tofauti.”
Katika Maandiko si jambo lisilo la kawaida kitu kupewa hali ya mtu. Hekima husemwa kuwa ina watoto. (Luka 7:35) Dhambi na kifo huitwa wafalme. (Warumi 5:14, 21) Kwenye Mwanzo 4:7 The New English Bible (NE) husema hivi: “Dhambi ni daimoni anayeotea kwenye mlango,” ikiipa dhambi hali ya mtu kuwa roho mwovu anayeotea kwenye mlango wa Kaini. Lakini, bila shaka, dhambi si mtu-roho; wala kuipa roho takatifu hali ya mtu hakuifanyi mtu-roho.
Vivyo hivyo, kwenye 1 Yohana 5:6-8 (NE) si roho tu bali pia “maji, na damu” husemwa kuwa ni “mashahidi.” Lakini kwa wazi maji na damu si watu, na wala roho takatifu si mtu.
Kupatana na hilo ni jinsi Biblia inavyotumia kwa ujumla mtajo “roho takatifu” kwa njia inayoonyesha kuwa si mtu, kama vile kuilinganisha na maji na moto. (Mathayo 3:11; Marko 1:8) Watu huhimizwa wajawe na roho takatifu badala ya divai. (Waefeso 5:18) Wao hunenwa kuwa wakijawa na roho takatifu kwa njia ile ile ambayo wao hujawa na sifa kama hekima, imani, na shangwe. (Matendo 6:3; 11:24; 13:52) Na kwenye 2 Wakorintho 6:6 roho takatifu hutiwa miongoni mwa sifa kadhaa. Kama kweli roho takatifu ingekuwa ni mtu, semi za jinsi hiyo hazingekuwa za kawaida sana.
Halafu, pia, ingawa maandiko fulani husema kwamba roho hunena, maandiko mengine huonyesha kwamba hilo hasa lilifanywa kupitia wanadamu au malaika. (Mathayo 10:19, 20; Matendo 4:24, 25; 28:25; Waebrania 2:2) Kitendo cha roho katika visa hivyo ni kama kile cha mawimbi ya redio yanayopeleka jumbe kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine aliye mbali.
Kwenye Mathayo 28:19, NW, rejezo hufanywa kwa “jina . . . la roho takatifu.” Lakini neno “jina” halimaanishi sikuzote jina la kibinafsi, ama katika Kigiriki ama katika Kiswahili. Tusemapo “katika jina la sheria,” hatuwi tunarejezea mtu. Huwa twamaanisha jambo lile ambalo sheria yasimamia, mamlaka yayo. Word Pictures in the New Testament ya Robertson husema hivi: “Katika Septuagint na mafunjo ni jambo la kawaida kutumia jina (onoma) hapa kwa kusema nguvu au mamlaka.” Kwa hiyo ubatizo ‘katika jina la roho takatifu’ hutambua mamlaka ya roho, ambayo hutoka kwa Mungu na hutenda kazi kwa mapenzi ya kimungu.
Yule “Msaidiaji”
YESU aliinena roho takatifu kuwa “msaidiaji,” na akasema ingefundisha, iongoze, na kunena. (Yohana 14:16, 26; 16:13) Neno la Kigiriki lililotumiwa hapa kwa msaidiaji (pa·raʹkle·tos) limo katika hali ya kiume. Kwa hiyo Yesu aliporejezea kile ambacho msaidiaji huyo angefanya, alitumia viwakilishi-nafsi (pronomino) vya kutaja mtu vya hali ya kiume. (Yohana 16:7, 8) Kwa upande mwingine, wakati neno la Kigiriki la hali huru la kusema roho (pneuʹma) litumiwapo, kiwakilishi-nafsi-huru (pronomino nyuta) “i” hutumiwa kwa kufaa.
Watafsiri Wanautatu walio wengi huficha uhakika huo, kama vile New American Bible ya Katoliki hukiri wazi kuhusu Yohana 14:17: “Neno la Kigiriki la kusema ‘Roho’ ni la hali huru, na ingawa sisi hutumia viwakilishi-nafsi (pronomino) katika Kiingereza (‘he’ [ndiye], ‘his’ [-ake], ‘him’ [yeye]), hatimkono zilizo nyingi za Kigiriki hutumia ‘it’ [hi-, -ki-, -cho].”
Kwa hiyo Biblia itumiapo viwakilishi-nafsi vya hali ya kiume kuhusiana na pa·raʹkle·tos kwenye Yohana 16:7, 8, huwa ikifuata kanuni za sarufi, wala haiwi ikieleza fundisho.
Si Sehemu ya Utatu
VYANZO mbalimbali hukiri kwamba Biblia haiungi mkono wazo la kwamba roho takatifu ni mtu (nafsi) wa tatu wa Utatu. Kwa kielelezo:
The Catholic Encyclopedia: “Katika Agano la Kale hamna mahali popote ambapo twapata kionyeshi chochote cha wazi juu ya Mtu wa Tatu.”
Mwanatheolojia Mkatoliki Fortman: “Wayahudi hawakuiona kamwe roho kuwa mtu; wala hakuna uthibitisho wowote imara kwamba mwandikaji yeyote wa Agano la Kale alishikilia maoni haya. . . . Kwa kawaida Roho Takatifu huonyeshwa katika Masimulizi [Gospeli] na katika Matendo kuwa ni kani au nguvu ya kimungu.”
New Catholic Encyclopedia: “Kwa wazi A[gano la] K[ale] haliwazii roho ya Mungu kuwa mtu . . . Roho ya Mungu ni nguvu tu ya Mungu. Ikiwa nyakati fulani hiyo huwakilishwa kuwa tofauti na Mungu, ni kwa sababu pumzi ya Yahweh hutenda kitendo cha nje-nje.” Yasema hivi pia: “Maandiko yaliyo mengi ya A[gano] J[ipya] hufunua roho ya Mungu kuwa kitu fulani, si mtu fulani; hasa inaonwa katika milingano kati ya roho na nguvu za Mungu.”—Italiki ni zetu.
A Catholic Dictionary: “Kwa ujumla, Agano Jipya, kama lile la Kale, huinena roho kuwa nishati au nguvu ya kimungu.”
Kwa hiyo, wala Wayahudi wala Wakristo wa mapema hawakuiona roho takatifu kuwa sehemu ya Utatu. Fundisho hilo lilikuja karne kadhaa baadaye. Kama vile A Catholic Dictionary huarifu: “Wazo la Mtu wa tatu lilikazaniwa kwenye Baraza la Aleksandria katika 362 . . . na mwishowe na Baraza la Konstantinopo la 381”—zapata karne tatu na nusu baada ya roho takatifu kujaza wanafunzi kwenye Pentekoste!
Sivyo, roho takatifu si mtu na si sehemu ya Utatu. Roho takatifu ni kani ya utendaji ya Mungu ambayo yeye hutumia kutimiza mapenzi yake. Hiyo si sawa na Mungu bali sikuzote huwa ikitenda kulingana na nia yake na huwa ya cheo kidogo kwake.
[Blabu katika ukurasa wa 22]
“Kwa ujumla, Agano Jipya, kama lile la Kale, huinena roho kuwa nishati au nguvu ya kimungu.”—A Catholic Dictionary
[Picha katika ukurasa wa 21]
Katika pindi moja roho takatifu ilitokea ikionekana kama njiwa. Katika pindi nyingine ilitokea ikionekana kama ndimi za moto—si ikiwa mtu kamwe