‘Kuendelea Kutwaa Ndani Maarifa Kuhusu Mungu na Yesu’
“NA UZIMA wa milele ndio huu, Wakujue [kuendelea kwao kutwaa ndani maarifa kuhusu, NW] wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.” (Yohana 17:3) Ndivyo alivyosema Yesu katika sala kwa Baba yake wa kimbingu, na katika njia hiyo alionyesha takwa moja muhimu ili kupata uhai wa milele. Lakini, ni kwa nini New World Translation hufasiri mstari huo “kuendelea kutwaa ndani maarifa kuhusu . . . Mungu” badala ya “wakujue wewe, Mungu,” kama vile tafsiri nyinginezo za Biblia zinavyoufasiri?—Ona pia kielezi-chini cha Yohana 17:3.
Neno la Kigiriki linalotafsiriwa hapo ‘kuendelea kutwaa ndani maarifa’ au ‘kujua’ ni namna ya kitenzi gi·noʹsko. Na ufasiri katika New World Translation unakusudiwa utokeze kikamili iwezekanavyo maana ya neno hilo. Maana ya msingi ya gi·noʹsko ni ‘kujua,’ lakini neno la Kigiriki lina namna mbalimbali za maana. Angalia ufafanuzi mbalimbali ufuatao:
“GINŌSKŌ (γινώσκω) humaanisha kuwa ukitwaa ndani maarifa, kupata kujua, kutambua, kuelewa, au kuelewa kamili.” (Expository Dictionary of New Testament Words, W. E. Vine) Kwa sababu hiyo, kufasiri gi·noʹsko ‘kuendelea kutwaa ndani maarifa’ si ‘kubadili Biblia,’ kama vile wachambuzi wa New World Translation wametoa hoja. Katika mazungumzo ya namna mbalimbali za maana ambazo neno hilo laweza kutia ndani, mtunga kamusi mashuhuri James Hope Moulton ataarifu hivi: “Hali sahili ya wakati uliopo, γινώσκειν, ni ya kuendelea, ‘kuwa ukitwaa ndani maarifa.’”—A Grammar of New Testament Greek.
A Grammatical Analysis of the Greek New Testament hueleza gi·noʹsko kama linavyotokea kwenye Yohana 17:3 kuwa “likidokeza jambo linaloendelea.” Elezo zaidi kuhusu neno hilo la Kigiriki linatokea katika Word Studies in the New Testament, cha Marvin R. Vincent. Hilo lasema: “Uhai wa milele watia ndani maarifa, au ufuatiaji wa maarifa, kwa kuwa njeo (tense) ya wakati uliopo huonyesha mwendelezo, wazo lenye kuendelea.” (Italiki ni zake.) Word Pictures in the New Testament cha A. T. Robertson kinadokeza kutafsiri neno hilo “-paswa kuendelea kujua.”
Kwa hiyo, katika Kigiriki cha awali, maneno ya Yesu kwenye Yohana 17:3 hudokeza jitihada nyendelevu ili kupata kujua Mungu wa kweli na Mwana wake, Yesu Kristo, na hilo latokezwa vizuri katika fasiri ya New World Translation. Tunatwaa maarifa hayo kwa kujifunza Neno la Mungu kwa bidii nyendelevu na kwa utii kupatanisha maisha zetu na viwango vyalo. (Linganisha Hosea 4:1, 2; 8:2; 2 Timotheo 3:16, 17.) Ni zawadi gani njema inayowangojea wale wanaojipatia ufahamu wa utu wa Mungu na ule wa Mwana wake na kisha kujitahidi kuwaiga? Uhai wa milele!