Maisha na Huduma ya Yesu
Kwenye Bahari ya Galilaya
MITUME sasa warudi Galilaya, kama vile Yesu alivyokuwa amewaagiza wafanye hapo mapema. Lakini hawana uhakika juu ya wanalopaswa kufanya huko. Baada ya muda, Petro amwambia Tomaso, Nathanaeli, Yakobo na ndugu yake Yohana, na mitume wengine wawili hivi: “Naenda kuvua samaki.”
“Sisi nasi tutakwenda nawe,” wajibu wale sita.
Usiku kucha, wanashindwa kupata chochote. Hata hivyo, mwangaza unapoanza kuingia, Yesu atokea ufuoni, lakini mitume hawatambui kwamba yule ni Yesu. Yeye apaza sauti: “Wanangu, mna kitoweo?”
“La,” wapaza sauti kwake ng’ambo ya maji.
“Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata,” yeye asema. Na wanapofanya hivyo, hawawezi kulivuta jarife lao kwa sababu ya samaki wote wale. “Ndiye Bwana[!]” Yohana apaliza sauti. Petro ajivika vazi lake la juu, ajitupa ndani ya bahari, na aogelea meta tisini hivi kwenda ufuoni. Mitume wale wengine wamfuata katika mashua ile ndogo, wakilivuta jarife lililojaa samaki.
Wanapofika pwani, pana moto wa makaa, ulio na samaki juu yao, na pana mkate. “Leteni hapa baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi,” Yesu asema. Petro apanda chomboni na avuta jarife pwani. Lina samaki wakubwa 153!
“Njoni mfungue kinywa,” Yesu awaalika.
Hakuna yeyote wao aliye na moyo mkuu wa kutosha kumwuliza, “U nani wewe?” kwa sababu wanajua ni Yesu. Hili ni tokeo lake la saba baada ya ufufuo, na lake la tatu kwa mitume wakiwa kikundi. Sasa apakua kiamsha-kinywa, akimpa kila mmoja wao mkate na samaki.
Wanapomaliza kula, Yesu labda ainamisha kichwa kuelekea ule mpato mkubwa wa samaki na amwuliza Petro: “Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa?” Labda amaanisha, Je! umefungamana zaidi na shughuli ya uvuvi kuliko kazi ambayo nimekutayarisha ufanye?
“Wajua kuwa nakupenda,” Petro aitikia.
“Lisha wana-kondoo wangu,” Yesu ajibu.
Tena, mara ya pili, auliza hivi: “Simoni wa Yohana, wanipenda?”
“Ndiyo Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda,” Petro ajibu.
“Chunga kondoo zangu,” Yesu aamuru tena.
Halafu, hata mara ya tatu, auliza hivi: “Simoni wa Yohana, wanipenda?”
Kufikia sasa Petro amehuzunika. Huenda ashangaa kama Yesu aonea shaka uaminifu mshikamanifu wake. Hata hivyo, Yesu alipokuwa akihukumiwa hivi karibuni kwa ajili ya uhai wake, Petro alikana mara tatu kwamba hamjui Yesu. Kwa hiyo Petro asema hivi: “Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda.”
“Lisha kondoo zangu,” Yesu aamuru mara ya tatu.
Yesu kwa hiyo atumia Petro kama mfano ili akazie kwa wale wengine pia kazi ambayo awataka wafanye. Karibuni ataondoka duniani, na awataka watangulie katika kuhudumia wale watakaovutwa katika zizi la kondoo la Mungu.
Kama vile Yesu alivyokamatwa na kuuawa kwa sababu alifanya kazi ambayo Mungu alimwagiza afanye, sasa basi, afunua kwamba Petro atateseka kwa kupatwa na yale yale. “Wakati ulipokuwa kijana,” Yesu amwambia, “ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka.” Ijapokuwa kifo cha kufia imani kinachomngoja Petro, Yesu amhimiza hivi: “Nifuate [Endelea kunifuata, NW].”
Anapogeuka, Petro amwona Yohana na auliza hivi: “Bwana, na huyu je?”
“Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo,” Yesu ajibu, “imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi [uendelee kunifuata, NW].”
Maneno haya ya Yesu yalikuja kufahamiwa na wengi wa wanafunzi kumaanisha kwamba mtume Yohana hangekufa kamwe. Hata hivyo, kama vile mtume Yohana alivyoeleza baadaye, Yesu hakusema kwamba hangekufa, bali Yesu alisema hivi tu: “Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe?”ohana 21:1-25; Mathayo 26:32; 28:7, 10.
◆ Jambo gani linaonyesha kwamba mitume hawana uhakika juu ya wanalopaswa kufanya katika Galilaya?
◆ Mitume wamtambuaje Yesu kwenye Bahari ya Galilaya?
◆ Yesu ametokea mara ngapi tangu ufufuo wake?
◆ Yesu akaziaje anayotaka wanafunzi wake wafanye?
◆ Yesu aonyeshaje jinsi Petro atakufa?
◆ Ni maelezo gani ya Yesu juu ya Yohana yaliyofahamiwa vibaya na wengi wa wanafunzi?