Maswali Kutoka kwa Wasomaji
◼ Je! Mashahidi wa Yehova hukubali sindano zenye kisehemu kidogo cha damu, kama vile globyulini au albyumini ya kutia kinga mwilini?
Baadhi yao hukubali, wakiamini kwamba Maandiko hayakatazi wazi kukubali sindano yenye kisehemu kidogo sana cha damu, au kifanyizo kilichotolewa katika damu.
Kwanza Muumba aliweka juu ya ainabinadamu wajibu wa kuepuka kuingiza damu ndani yao: “Kila kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula chenu . . . Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile.” (Mwanzo 9:3, 4) Damu ilikuwa takatifu na kwa hiyo ingeweza kutumiwa katika dhabihu tu. Isipotumiwa kwa njia hiyo, iliondolewa mbali kwa kumwagwa ardhini.—Walawi 17:13, 14; Kumbukumbu 12:15, 16.
Hiki hakikuwa kizuizi cha muda tu kwa Wayahudi. Uhitaji wa kushika mwiko wa damu ulitaarifiwa upya kwa Wakristo. (Matendo 21:25) Katika eneo lenye kuwazunguka katika Milki ya Kiroma, ilikuwa kawaida kuvunja sheria ya Mungu, kwa kuwa watu walikula chakula kilichotayarishwa kwa damu. Pia ilivunjwa kwa sababu “za kitiba”; Tertullian aripoti kwamba watu fulani waliingiza damu ndani yao wakifikiri kwamba ingeweza kuponya kifafa. ‘Kwa kiu yenye pupa walifyonza damu ya wahalifu waliochinjwa katika arena.’ Aliongeza hivi: “Aibikeni kwa sababu ya njia zenu mbovu mbele ya Wakristo, ambao hawana hata damu ya wanyama kwenye milo yao.” Leo Mashahidi wa Yehova wamepiga moyo konde jinsi hiyo hiyo ili wasivunje sheria ya Mungu, hata kama wengine wana kawaida iliyoje ya kula chakula kilichotayarishwa kwa damu. Katika miaka ya 1940, visa vya kutia damu mishipani vilienea sana, na Mashahidi wakaona kwamba kutii Mungu kulitaka kwamba wao waepuke kutiwa damu mishipani, hata ikiwa madaktari walihimiza hivyo.
Hapo kwanza, utiaji mwingi wa damu mishipani ulikuwa wa damu ya jumla. Baadaye, watafiti walianza kutenganisha damu kwa vifanyizo vyayo mbalimbali vya msingi, kwa maana madaktari walikata shauri kwamba mgonjwa fulani huenda asihitaji sehemu zote kubwa za damu. Kama wangempa sehemu moja tu, ingekuwa si hatari sana kwake, na madaktari wangeweza kutumia damu iliyopo kwa mambo mengi zaidi.
Damu ya kibinadamu yaweza kutenganishwa iwe kitu cheusi chenye chembe za uhai na umajimaji wa kimanjano (plasma, au seramu). Ile sehemu yenye chembe (asilimia 45 ya ujazo) huwa ni mjumliko wa chembe nyekundu, chembe nyeupe, na visahani. Asilimia ile nyingine 55 ndiyo plasma. Hii huwa ni maji asilimia 90, lakini huwa na kiasi kidogo-kidogo cha protini nyingi, hormoni, chumvi za namna-namna, na enzaimu. Leo, kiasi kikubwa cha damu yenye kuchangwa hutenganishwa kuwa zile sehemu za msingi. Huenda mgonjwa mmoja akatiwa plasma mishipani (labda FFP, “fresh frozen plasma” [plasma iliyogandishwa karibuni] ili kutibu mshtuko. Lakini mgonjwa mwenye damu-pungufu angeweza kupewa chembe nyekundu zilizosombwa, yaani, chembe nyekundu zilizokuwa zimewekwa akibani halafu zikatiwa katika umajimaji fulani na kutiwa mishipani. Pia visahani na chembe nyeupe hutiwa mishipani lakini si kwa kawaida sana.
Katika nyakati za Biblia wanadamu hawakuwa wamefanya mbinu hizo za kutumia sehemu hizo. Mungu aliamuru hivi tu: ‘Shikeni mwiko wa damu.’ (Matendo 15:28, 29, NW) Lakini kwa nini mtu yeyote afikiri kwamba kungekuwa na tofauti ikiwa ni damu ya jumla au imetenganishwa ikawa ya sehemu-sehemu hizo? Ingawa wanaume fulani walikunywa damu, Wakristo walikataa hata ikiwa katao lao liliwaletea kifo. Je! wewe wafikiri itikio lao lingalikuwa tofauti kama mtu fulani angalikusanya damu, akaruhusu itenganishwe, halafu awatolee plasma tu au sehemu ile iliyogandamana tu, labda ikiwa katika utumbo wenye damu (soseji)? Sivyo, kamwe! Kwa hiyo, Mashahidi wa Yehova hawakubali kutiwa mishipani damu nzima-nzima au sehemu zayo za msingi (chembe nyekundu, chembe nyeupe, visahani, au plasma) zenye kutumiwa kwa kusudi kama hilo.
Ingawa hivyo, kama swali lidokezavyo, wanasayansi wamejifunza juu ya visehemu maalumu vya damu na jinsi ya kuvitumia. Suala moja la kawaida lahusu protini za plasma—namna za globyulini, albyumini, na fibrinojeni. Yaelekea kwamba, utumizi wa matibabu yaliyoenea sana ya vitu hivyo ni ule wa kudunga sindano ili kutia mwilini globyulini yenye kinga. Jambo hilo hufanywa kwa nini?
Mwili wako waweza kufanyiza viua-vijasumu dhidi ya magonjwa fulani, zikitia kinga ndani yako. Huo ndio msingi wa uchanjaji uliofanyiwa maendeleo wenye kutumia chanjo (toksoidi) dhidi ya polio, machubwichubwi (kufura shingoni), surua (ukambi), mchanganyiko wa kifaduro, diftheria na pepo-punda, na homa ya kuhara. Hata hivyo, ikiwa hivi majuzi mtu fulani amekuwa mahali penye magonjwa fulani mazito, huenda watabibu wakapendekeza sindano ya seramu (kiharibu-sumu) fulani ili kumpa kinga ya tahadhari kwa wakati huo. Mpaka hivi majuzi sindano hizi zimetayari-shwa kwa kutoa globyulini ya kinga mwilini, ambayo huwa na viua-vijasumu, kutoka kwa mtu ambaye tayari ana kinga mwilini.a Kinga hiyo ya tahadhari ambayo hupatikana kwa kudungwa sindano si yenye kudumu, kwa maana viua-vijasumu vyenye kuingizwa kwa kudunga sindano hutoka katika mfumo wake baada ya muda fulani.
Kwa sababu ya amri ya ‘kushika mwiko wa damu,’ Wakristo fulani wamehisi kwamba hawapaswi kukubali sindano ya globyulini (protini) ya kuwatia kinga mwilini, hata kama ni kisehemu kidogo tu cha damu. Msimamo wao uko wazi na sahili—hawataki sehemu yoyote ya damu kwa namna yoyote au kiasi chochote.
Wengine wamehisi kwamba seramu (kiharibu-sumu), kama vile globyulini ya kutia mwilini kinga, yenye kijisehemu kidogo tu cha plasma ya damu ya mchangaji na yenye kutumiwa kuimarisha ulinzi wao dhidi ya ugonjwa, si sawa na kutiwa mishipani damu yenye kuendeleza uhai. Kwa hiyo huenda dhamiri zao zisiwakataze kutwaa globyulini ya kuingiza mwilini kinga au visehemu vidogo vya namna hiyo.b Huenda wakakata shauri kwamba uamuzi wao utategemea hasa kama wana nia ya kukubali hatari zozote za kiafya zinazohusika katika kudungwa sindano ya kitu kilichofanyizwa kutokana na damu ya wengine.
Ni jambo la maana kuangalia kwamba mfumo wa damu ya mwanamke mwenye mimba ni tofauti na ule wa kijusi kilicho katika tumbo lake la uzazi; mara nyingi namna zao za damu huwa tofauti. Mama hapitishi damu yake kuiingiza katika kijusi. Elementi (chembe) zilizofanyika kutokana na damu ya mama hazivuki kile kizuizi cha plasenta (kondo la nyuma) na kuingia katika damu ya kijusi, wala plasma haifanyi hivyo. Kwa uhakika, damu ya mama na ya kijusi zikichangamana kupitia jeraha fulani, matatizo ya afya yaweza kusitawi baadaye (Rh au kutopatana kwa ABO). Hata hivyo, vitu fulani kutokana na plasma huvuka na kuingia katika mzunguko wa damu ya kijusi. Je! protini za plasma, kama globyulini na albyumini ya kukinga mwili huvuka jinsi hiyo? Ndiyo, baadhi yazo hufanya hivyo.
Mwanamke mwenye mimba ana utendaji fulani ambao kwa huo globyulini fulani ya kinga huhama kutoka kwenye damu ya mama kuja kwenye ile ya kijusi. Kwa sababu mhamo huu wa kiasili wa kuingia kwa viua-vijasumu katika kijusi hutukia katika mimba zote, watoto huzaliwa wakiwa na nguvu fulani za kikawaida za kinga dhidi ya maambukizo fulani.
Ndivyo ilivyo kuhusu albyumini, ambayo madaktari waweza kuagiza mtu aitumie kuwa matibabu ya mshtuko au hali fulani nyinginezo.c Watafiti wamethibitisha kwamba albyumini kutokana na plasma husafirishwa pia, ingawa kwa matokeo machache zaidi, kutoka kwa mama kuivuka plasenta (kondo la nyuma) kuingia katika kijusi chake.
Jambo la kwamba visehemu vidogo vya protini kutoka kwenye plasma huhama kiasili vikaingia katika mfumo wa damu wa mtu mwingine (kile kijusi) laweza kuwa ufikirio mwingine wakati Mkristo anapoamua kama atakubali kinga za globyulini, albyumini, au sindano kama hizo zenye visehemu vidogo vya plasma. Huenda mtu fulani akahisi kwamba aweza kukubali kwa dhamiri njema; huenda mwingine akakata shauri kwamba hawezi. Ni lazima kila mmoja aamue jambo hilo kibinafsi mbele za Mungu.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa kutumia mbinu za kuunganisha upya DNA, au uhandisi wa chembe za urithi, wanasayansi wanasitawisha vitu vya namna hiyo ambavyo havikufanyizwa kutokana na damu.
b Kielelezo kimoja ni globyulini ya Rh yenye kinga, ambayo huenda madaktari wakapendekeza wakati kunapokuwa na hali ya kutopatana kwa Rh kati ya mwanamke na kijusi chake. Nyingine ni “Factor VIII,” ambayo hupewa kwa wale ambao damu yao haina uwezo wa kugandamana wakati wa majeraha.
c Ushuhuda waonyesha kwamba majimaji yasiyo na damu, yaliyo ya kujazia kiasi kilichotoka, (kama vile “hetastarch” [HES]) yaweza kutumiwa kwa matokeo ili kutibu mshtuko na hali nyinginezo ambazo mchanganyo wa albyumini ungalitumiwa hapo kwanza.