Maoni ya Biblia
Misherehekeo ya Carnival—Je, Yafaa au Haifai?
“HUWEZI kujizuia,” asema Michael. “Muziki hukusukuma uinuke kutoka kitini, huichezesha miguu yako, hukusisimua—una msisimuko wa carnival (sikukuu kabla ya majira ya kwaresima)!” Kwa kweli, kila mwaka carnival husisimua mamilioni ya watu ulimwenguni, lakini hakuna mahali ambapo msisimuko huwa mwingi kuliko katika nchi ambayo Michael huishi, Brazili. Juma la kabla ya Jumatano ya Majivu, watu wa Brazili huvalia mavazi yenye kupendeza zaidi, husahau wajibu wao na ratiba zao, na kujiingiza katika tamasha za nchini kote toka msitu wa Amazon hadi fuo za Rio de Janeiro. Huo ni wakati wa kuimba, kucheza dansi, na kusahau kila kitu.
“Hiyo ndiyo sababu moja ya kupendwa sana kwa carnival,” aeleza Michael, aliyekuwa msherehekeaji mwenye bidii wa carnival kwa miaka mingi. “Msherehekeo wa carnival huwapa watu fursa ya kusahau taabu zao.” Na hasa kwa mamilioni ya maskini—wanaoishi bila kuwa na maji ya kutosha, bila umeme, bila kazi ya kuajiriwa, na bila tumaini—kuna mengi ya kusahauliwa. Kwao carnival ni kama asprini: huenda isitibu matatizo, lakini angalau inatuliza maumivu. Kwa kuongezea, fikiria jinsi baadhi ya makasisi wa Katoliki ya Kiroma waonavyo carnival—askofu mmoja alisema kwamba carnival “ina manufaa mengi kwa ajili ya usawaziko wa kiakili wa watu.” Kwa hivyo ni rahisi kuona ni kwa nini watu wengi huhisi kwamba carnival ni kikengeusha fikira chenye msaada na kinachokubaliwa na kanisa. Ingawa hivyo, Biblia ina maoni gani juu ya carnival?
Je, Ni Kusherehekea au Ni Ulevi na Ulafi?
Neno la Mungu husema kwamba kuna “wakati wa kucheka, . . . na wakati wa kucheza.” (Mhubiri 3:4) Kwa kuwa neno la Kiebrania “cheka” laweza pia kutafsiriwa “sherehekea,” ni wazi kwamba kwa Muumba wetu, si kosa kujifurahisha. (Ona 1 Samweli 18:6, 7.) Kwa hakika, Neno la Mungu hutuambia tufurahi na kushangilia. (Mhubiri 3:22; 9:7) Hivyo Biblia huunga mkono kuwa na misherehekeo ifaayo.
Hata hivyo, Biblia haikubali aina zote za misherehekeo. Mtume Paulo asema kwamba ulevi na ulafi, au misherehekeo yenye makelele ni “matendo ya mwili” na kwamba walevi na walafi “hawataurithi ufalme wa Mungu.” (Wagalatia 5:19-21) Hivyo, Paulo aliwaonya kwa upole Wakristo ‘waenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi.’ (Warumi 13:13) Kwa hiyo swali ni hili, Carnival iko upande gani—kusherehekea tu au ulevi na ulafi mpotovu? Ili kujibu, kwanza acheni tueleze zaidi kuhusu kile ambacho Biblia hukiona kuwa ulevi na ulafi.
Maneno “ulevi na ulafi” au koʹmos katika Kigiriki, hupatikana mara tatu katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, sikuzote katika maana mbaya. (Warumi 13:13; Wagalatia 5:21; 1 Petro 4:3) Na si ajabu kwa kuwa koʹmos hutokana na misherehekeo yenye sifa mbaya iliyojulikana sana na Wakristo wa mapema waliosema Kigiriki. Misherehekeo ipi?
Mwanahistoria Will Durant aeleza: “Kikundi cha watu kilichokuwa kikibeba sanamu takatifu ya uume [mfano wa kiungo cha uzazi cha kiume] na kumwimbia nyimbo Dionysus . . . katika istilahi ya Kigiriki, ilikuwa komos, au ulevi na ulafi.” Dionysus, mungu wa divai katika ngano za Kigiriki, baadaye aliasilishwa na Warumi, ambao walimpa jina jipya Bacchus. Hata hivyo, ule uhusiano wa koʹmos haukuathiriwa na mabadiliko ya majina. Msomi wa Biblia Dakt. James Macknight aandika: ‘Neno koʹmois [wingi wa neno koʹmos] hutokana na Comus, mungu wa karamu na ulevi na ulafi. Ulevi na ulafi huo ulifanywa kwa heshima ya Bacchus, ambaye kwa sababu hiyo aliitwa Comastes.’ Ndiyo, misherehekeo kwa ajili ya Dionysus na Bacchus ndiyo iliyokuwa vyanzo vya ulevi na ulafi. Ni mambo gani yaliyohusishwa katika karamu hizo?
Ulevi na Ulafi Waonyeshwa
Kulingana na Durant, wakati wa karamu za Kigiriki za kumheshimu Dionysus, umati wa wenye kusherehekea “walikunywa vileo bila kujizuia, na . . . walimwona mtu ambaye alijizuia kuwa mpumbavu. Walifanya maandamano yenye mchafuko, . . . na walipokuwa wakinywa na kucheza dansi waliingiwa na kichaa hivi kwamba walishindwa kujidhibiti.” Vivyo hivyo, karamu za Kiroma kwa heshima ya Bacchus (zilizoitwa Bacchanalia) zilikuwa na unywaji na nyimbo na miziki yenye kuamsha tamaa mbaya nazo zilikuwa na “matendo yasiyo ya heshima hata kidogo,” aandika Macknight. Hivyo, umati wenye kichaa, kunywa kupita kiasi, miziki na kucheza dansi kwenye kuamsha tamaa mbaya, na ngono isiyo ya adili yalifanyiza sehemu za msingi za sherehe za ulevi na ulafi za Ugiriki na Roma.
Je, carnival za leo hutia ndani sehemu hizo za sherehe za ulevi na ulafi? Fikiria manukuu machache kutoka ripoti za habari juu ya misherehekeo ya carnival: “Umati wenye ghasia kabisa.” “Siku nne usiku kucha za kunywa na tafrija.” “Athari za carnival zaweza kuendelea kuwapo siku kadhaa kwa walafi na walevi wengine.” Zile “sauti kubwa kabisa zilizo karibu hufanya yale maonyesho ya vikundi vya muziki wenye ‘mdundo mzito’ . . . yaonekane kuwa si kitu yalinganishwapo.” “Leo, misherehekeo yoyote ya carnival isiyo na wagoni-jinsia-moja ni kama chakula bila chumvi.” “Carnival imekuwa jina jingine la uchi.” Dansi za carnival zilionyesha “mandhari za kupiga punyeto . . . na aina mbalimbali za ngono.”
Kwa kweli, carnival ya leo na zile karamu za kale zafanana sana hivi kwamba ikiwa mlevi na mlafi wa siku za Bacchus angefufuka, carnival ya kisasa ikiendelea, angefaana sawasawa. Na hilo halipaswi kutushangaza, aeleza mtayarishaji wa vipindi vya televisheni wa Brazili Cláudio Petraglia, kwa kuwa asema kwamba carnival ya leo “hutokana na karamu za Dionysus na Bacchus na ulevi na ulafi huo, kwelikweli, ndio muundo wa carnival.” Buku la The New Encyclopædia Britannica lasema kwamba carnival yaweza kuhusianishwa na karamu ya kipagani Saturnalia ya Roma ya kale. Hivyo carnival, ingawa ni ya enzi tofauti, ni ya familia ileile sawa na zile zilizoitangulia. Jina la familia hiyo ni lipi? Ulevi na ulafi.
Ujuzi huo wapaswa kuwa na matokeo gani kwa Wakristo leo? Matokeo yaleyale uliokuwa nao kwa Wakristo wa Mapema walioishi katika mikoa iliyoongozwa na Wagiriki katika Asia Ndogo. Kabla ya kuwa Wakristo walizoea kujiingiza katika ‘mwenendo wa ufisadi, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi [koʹmois], na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali.’ (1 Petro 1:1; 4:3, 4) Hata hivyo, baada ya kujifunza kwamba Mungu huona ulevi na ulafi kuwa “matendo ya giza,” waliacha kushiriki katika misherehekeo kama carnival.—Warumi 13:12-14.
Michael, aliyetajwa mbeleni, alifanya vivyo hivyo. Yeye aeleza sababu: “Kadiri ujuzi wangu wa Biblia ulivyokua, niliiona misherehekeo ya carnival na kanuni za Biblia zilikuwa kama mafuta na maji—hayachanganyikani kabisa.” Katika 1979, Michael akafanya uamuzi. Aliacha misherehekeo ya carnival kabisa. Wewe utachagua kufanya nini?
[Picha katika ukurasa wa 14]
Gudulia la Ugiriki la kabla ya Ukristo lenye mchoro wa Dionysus (mchoro wa kushoto)
[Hisani]
Kwa Hisani ya The British Museum