Tamasha za Kutoka Bara Lililoahidiwa
Jangwa la Yuda Halizai Lakini Linasisimua
WEWE wawazia jangwa la Yuda katika Bara Lililoahidiwa kuwa namna gani? Watu fulani hufikiria msitu mkubwa sana uliojazana miti. Wengine huwazia jangwa kama Sahara lililo na mitandao mirefu ya mchanga.
Hakuna lolote la mawazio hayo hulingana na jangwa hili, kama vile wewe waweza kuona kutokana na fotografu iliyo juu. Katika mandhari hii, wewe unatazama sehemu ya jangwa hilo ambayo yahusianishwa na Yesu. Pokeo husema kwamba Shetani alionyesha Yesu “milki zote za ulimwengu” akiwa kwenye kileleta hiki, ambacho kipo katika ukingo wa jangwa na chakabiliana na jiji la Yeriko lenye mapambo ya mitende katika Bonde la Yordani upande wa mashariki.—Mathayo 3:1; 4:1-11.
Kutoka sehemu hii ya kaskazini-mashariki, jangwa la Yuda latandaa kuteremka chini kandokando ya upande wa magharibi wa Bahari ya Chumvi (ya Ufu). Huenda ikakusaidia kupiga picha ya mawazo kuhusu eneo hili ukitazama ramani ya jaladani iliyo katika 1989 Calendar of Jehovah’s Witnesses. (Pia kalenda hiyo ina namna kubwa ya picha iliyo hapa juu.) Lile jangwa (lenye upana wa kilometa 16 hadi 24) liko katika miinamo ya mashariki ya milima ya Yudea, kuteremka hadi fuo za Bahari ya Chumvi.
Milima hiyo yazuia sehemu kubwa ya unyevunyevu unaotoka katika Bahari Mediterania. Kwa hiyo vilima vyororo vitupu vya kichokaa ambavyo viko upande wa mashariki hupokea mvua kidogo isipokuwa wakati wa miezi ya kipupwe ya Novemba na Desemba. Wakati huo nyasi huchanua, hiyo ikiwezesha makundi ya kondoo yalishe hapa. Hivyo, “mazizi-kondoo yenye mawe” ambayo yatajwa kwenye 1 Samweli 24:3, NW, yaeleza jimbo hili kwa usahihi.
Nyasi ambazo hukua hapa hazidumu muda mrefu. Pepo za mashariki kutoka kwenye jangwa hugeuza rangi ile ya kijani kibichi kuwa rangi ya kahawia iliyokaushwa. Jambo hili latoa kielezi kizuri sana juu ya elezo hili la kiunabii: “Majani yakauka, ua lanyauka; bali neno la Mungu wetu litasimama milele.” —Isaya 40:8; 1 Petro 1:24, 25.
Labda Yesu alifikiria andiko hili alipokuwa anatanga-tanga katika jangwa hili kwa vipindi 40 vya mchana na 40 vya usiku. Fikiria jinsi ambavyo ni lazima Yesu awe alihisi akiwa chini ya jua lenye kuunguza ambalo huigonga miamba na vibonde vile visivyo na miti. (Isaya 32:2) Lo, lilikuwa jambo la kuelewa hali kama nini kwamba baadaye ‘walikuja malaika wakamtumikia’!—Mathayo 4:1-11.
Kwa sababu ya hali yalo ya kutozaa na ukosefu wa wakaaji, mara nyingi jangwa la Yudea lilitumiwa kuwa mahali pa kimbilio. Daudi alipokuwa akimkimbia Mfalme Sauli mwenye hasira kali, alipata himaya humo, akieleza kuwa ni “bara kavu lenye uchovu mwingi, ambamo hamna maji.” (Zaburi 63:1 na maandishi ya juu ya sura, NW; 1 Samweli 23:29) Kwa muda fulani alifanya maficho yake katika pango, labda kama lile Pango Umm Qatafa katika Wadi Khareitun (bonde ambalo lasonga kutoka mashariki mwa Bethlehemu kuelekea Bahari ya Chumvi). (Waebrania 11:32, 38) Katika mandhari hii yenye kuonekana kutoka kwenye pango hilo, katika upande wa kulia chini waweza kuona kondoo fulani weusi wakitafuta-tafuta majani yaliyotapakaa.
Daudi alikuwa katika pango katika jimbo la Engedi wakati Sauli alipoingia ajipumzishe. Ingawa Daudi alikata rinda la koti la Sauli, yeye hakutaka kamwe kudhuru “mpakwa mafuta wa Yehova.” Baadaye Daudi alipaaza wito kwa Sauli, labda wakati mfalme alipokuwa chini kati ya majani-majani mengi ya hapo. (1 Samweli 24:1-22) ‘Eti majani-majani mengi ya hapa?’ huenda wewe ukajiuliza kwa mshangao.
Ndiyo, kukiwa na maji mengi, jangwa hili laweza kuchanua. Engedi ni kielelezo. Maji yenye kupenya katika mwamba ule wenye vipenyo huibuka yakiwa vibubujiko na maporomoko ya maji katika bonde hili ambalo hufunguka wazi hadi ufuo wa magharibi wa Bahari ya Chumvi. Hiyo hufanya Engedi iwe pori halisi, yenye mimea mingi. Ukizuru huko, waweza kupata namna nyingi za maua na matunda. Ungeweza pia kuona wanyama-mwitu, wakitofautiana kuanzia nguchiro wa miambani hadi mbuzi wa milimani; hata kuna chui katika eneo hilo! — 1 Samweli 24:2; Wimbo Ulio Bora 1:14.
Jambo la kwamba jangwa hilo lisilozaa la Yuda laweza kuwa na ubichi mwingi laongezea wingi wa uelewevu wetu kuhusu njozi ya Ezekieli ya maji yanayotiririka kutoka hekaluni Yerusalemu. Mtiririko huo uliongezeka mpaka ukawa bubujiko kubwa linalosonga upande wa mashariki kuteremka kupitia jangwa la Yudea. Tokeo likiwa nini? Ezekieli aliandika hivi: “Naam, tazama! katika ukingo wa bubujiko ilikuwako miti mingi sana . . . Na matunda yayo ni lazima yathibitike kuwa chakula na majani yayo kuwa ponyo.” Maji hayo yalitiririka kuingia ndani ya Bahari ya Chumvi, yakiponya hata maji yayo yasiyo na uhai—Ezekieli 47:1-12, NW, Isaya 35:1, 6, 7.
Kwa sababu hiyo, ingawa jangwa la Yuda ni la nusu-ukame na ukiwa, pia ni jimbo linalosisimua lenye hali tofauti-tofauti ambalo laonekana katika masimulizi mengi ya Biblia. — Luka 10:29-37.
[Hisani Line katika ukurasa wa 16]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est
[Hisani katika ukurasa wa 17]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.