Wamishonari Wangesafiri Hadi Wapi Upande wa Mashariki?
MIAKA 30 hivi baada ya Yesu kufa, mtume Paulo aliandika kwamba habari njema ilikuwa ikihubiriwa katika “uumbaji wote” ulio chini ya mbingu. (Wakolosai 1:23) Maneno yake hayapaswi kueleweka kihalisi kana kwamba kila mtu aliyekuwa hai wakati huo alikuwa amesikia habari njema. Lakini, maneno ya Paulo yalikuwa wazi: Wamishonari Wakristo walikuwa wakihubiri sana katika maeneo ya ulimwengu uliojulikana wakati huo.
Huenda walifika mbali kadiri gani? Maandiko yanaonyesha kwamba meli za biashara zilimwezesha Paulo kuhubiri maeneo ya magharibi kufikia Italia. Mmishonari huyo mwenye bidii alitaka pia kuhubiri huko Hispania.—Matendo 27:1; 28:30, 31; Waroma 15:28.
Vipi kuhusu upande wa mashariki? Wahubiri Wakristo wa mapema walienda mbali kadiri gani upande mashariki? Hatuwezi kuwa na hakika, kwa kuwa Biblia haituambii. Hata hivyo, huenda ukashangaa kujua kwamba njia za biashara kati ya maeneo ya Mediterania na Mashariki zilikuwa zimefika hadi wapi katika karne ya kwanza W.K. Ingawa hatujui Wamishonari Wakristo walienda mbali kadiri gani, kuwepo kwa biashara hizo kunaonyesha kulikuwa na uwezekano mkubwa kwamba walisafiri hadi maeneo ya mashariki.
Urithi wa Aleksanda
Aleksanda Mkuu alishinda na kuteka maeneo ya mashariki kuanzia Babilonia, Uajemi, kutia ndani maeneo ya mbali kufikia Punjab, kaskazini mwa India. Ushindi huo uliwawezesha Wagiriki kufahamu maeneo ya pwani kuanzia mlango wa Mto Efrati katika Ghuba ya Uajemi, hadi mlango wa Mto Indus.
Baada ya muda mfupi, vikolezo na uvumba vilisafirishwa hadi maeneo ya Ugiriki ng’ambo ya Bahari ya Hindi kupitia Bahari Nyekundu. Mwanzoni biashara hiyo ilidhibitiwa na wafanyabiashara Wahindi na Waarabu. Lakini wafalme walioitwa Tolemi wa Misri walipogundua jinsi pepo zilivyovuma, wao pia walianza biashara ya Bahari ya Hindi.
Katika bahari hiyo, pepo zinavuma kutoka maeneo ya kusini-magharibi kuanzia Mei (Mwezi wa 5) hadi Septemba (Mwezi wa 9) na hivyo kuruhusu meli kusafiri kuanzia mlango wa Bahari Nyekundu kupitia pwani ya kusini ya Arabia au moja kwa moja hadi India kusini. Kati ya Novemba (Mwezi wa 11) na Machi (Mwezi wa 3), pepo zinabadilika na kuelekea upande tofauti na hivyo kuwawezesha kurudi nyumbani. Mabaharia Waarabu na Wahindi wametumia ujuzi wa pepo hizo kwa miaka mingi, na kusafiri kati ya India na Bahari Nyekundu wakiwa wamebeba kida, mdalasini, nardo, na pilipili.
Njia za Bahari za Aleksandria na Roma
Waroma waliposhinda maeneo yaliyotawaliwa na magavana waliotawala baada ya Aleksanda, Roma ikawa soko kuu la bidhaa zenye thamani kutoka Mashariki, kama vile pembe za tembo kutoka Afrika, uvumba na manemane kutoka Arabia, vikolezo na mawe yenye thamani kutoka India, na hata hariri kutoka China. Meli zilizobeba bidhaa hizo zilikutana kwenye bandari mbili kuu, yaani, Berenice na Myos Hormos kwenye Pwani ya Bahari Nyekundu huko Misri. Kutoka kwenye bandari hizo wafanyabiashara wangefuata njia zinazoelekea Coptos, kwenye Mto Nile.
Kutoka Coptos, bidhaa zilipitia Mto Nile, njia kuu ya Misri kuelekea Aleksandria ambako zilipakiwa kwenye meli na kusafirishwa hadi Italia na kwingineko. Njia nyingine ya kwenda Aleksandria ilikuwa kupitia mfereji uliounganisha chanzo cha Bahari Nyekundu pamoja na Mto Nile, karibu na Suez ya kisasa. Bila shaka, Misri na bandari zake zilikuwa karibu na maeneo ambayo Yesu alihubiri na zingeweza kufikiwa kwa urahisi kutoka maeneo hayo.
Strabo mwanajiografia Mgiriki wa karne ya kwanza, anasema kwamba katika siku zake, meli 120 za Aleksandria zilisafiri kila mwaka kutoka Myos Hormos ili kufanya biashara na India. Kitabu fulani cha karne ya kwanza kuhusu usafiri katika eneo hilo kipo hadi leo. Yaelekea kiliandikwa na mfanyabiashara Mmisri aliyezungumza Kigiriki kwa faida ya wafanyabiashara wenzake. Kitabu hicho cha kale kinafunua mambo gani?
Kitabu hicho ambacho mara nyingi kinatajwa kwa jina lake la Kilatini, Periplus Maris Erythraei (Kuabiri Bahari ya Erythra) kinaeleza kuhusu njia za baharini zenye urefu wa maelfu ya kilomita kusini ya Misri, kufika hadi Zanzibar. Kuelekea upande wa mashariki, mwandishi wa kitabu hicho anaonyesha umbali, mahali pa kutia nanga, maeneo ya biashara, bidhaa zilizouzwa, na mtazamo wa watu walioishi kando ya pwani ya kusini ya Arabia, kuelekea pwani ya magharibi ya India hadi Sri Lanka, kisha kuelekea pwani ya mashariki ya India kufikia Mto Ganges. Ufafanuzi sahihi na ulio wazi wa kitabu hicho unaonyesha kwamba mtungaji wake alitembelea maeneo aliyotaja.
Wazungu Huko India
Huko India wafanyabiashara kutoka Ulaya waliitwa Wayavana. Kulingana na kitabu Periplus, eneo moja ambalo walitembelea kwa ukawaida katika karne ya kwanza W.K. lilikuwa Muziris, karibu na ncha ya kusini ya India.a Mashairi ya Kitamili yaliyoandikwa katika karne za mapema W.K., yanataja mara nyingi kuhusu wafanyabiashara hao. “Meli maridadi za Wayavana zilileta dhahabu na kurudi na pilipili, na Muziris ikajaa kelele,” linasema shairi moja. Katika shairi lingine, mwana mmoja wa mfalme wa India kusini anasihiwa anywe divai bora iliyoletwa na Wayavana. Bidhaa nyingine kutoka Magharibi zilizouzwa kwa wingi huko India ni vyombo vya glasi, vyuma, marijani, na vitambaa.
Wachimbuzi wa vitu vya kale wamechimbua bidhaa nyingi zilizoletwa India kutoka Magharibi. Kwa mfano, huko Arikamedu kwenye pwani ya kusini-mashariki ya India, baadhi ya vitu ambavyo vimechimbuliwa ni vigae vya magudulia ya divai ya Waroma na vyombo vilivyo na mihuri ya wafinyanzi waliotengeneza bidhaa hizo huko Arezzo, Italia ya kati. “Fikira za mtafiti wa kisasa zinachochewa anapopata vigae vilivyo na majina ya wafinyanzi kwenye mchanga-tope katika Ghuba ya Bengal ambao tanuru zao ziko kwenye vitongoji vya Arezzo,” anasema mwandishi mmoja. Uthibitisho zaidi wa kwamba kulikuwa na biashara kati ya eneo la Mediterania na India unaonekana pia katika sarafu za Roma za dhahabu na fedha ambazo zimepatikana kusini mwa India. Sarafu nyingi kati ya hizo ni za karne ya kwanza W.K. na zina picha za Maliki Waroma Agusto, Tiberio, na Nero.
Uwezekano wa kwamba raia wa Roma walianzisha koloni za kudumu za kibiashara huko India kusini unaonekana katika ramani ya kale ambayo nakala yake inapatikana hadi leo. Ramani hiyo, inayoitwa Mchoro wa Peutinger, ambayo inasemekana kuwa ni ramani ya Milki ya Roma kama ilivyokuwa katika karne ya kwanza W.K., inaonyesha hekalu la Agusto huko Muziris. “Jengo kama hilo,” kinasema kitabu fulani kuhusu biashara za Waroma (Rome’s Eastern Trade: International Commerce and Imperial Policy, 31 BC–AD 305), “lingeweza kujengwa tu na raia wa Milki ya Roma, na inadhaniwa kuwa wangekuwa raia walioishi Muziris au waliotumia wakati mwingi huko.”
Rekodi za Roma zinataja angalau ziara tatu za mabalozi wa India huko Roma wakati wa utawala wa Agusto kuanzia mwaka wa 27 K.W.K. hadi 14 W.K. “Mabalozi hao walikuwa na kusudi muhimu kutoka nchi yao,” unasema uchunguzi mmoja uliofanywa kuhusu jambo hilo, yaani, walienda ili kukubaliana kuhusu mahali ambapo biashara kati ya watu wa nchi mbalimbali ingefanywa, jinsi ya kutoza kodi, mahali ambapo watu wa nchi za kigeni wangeishi, na kadhalika.
Basi, katika karne ya kwanza W.K. lilikuwa jambo la kawaida kwa watu kusafiri kati ya bonde la Mediterania na India. Ingekuwa rahisi kwa wamishonari Wakristo katika eneo la kaskazini ya Bahari Nyekundu kuabiri meli inayoelekea India.
Namna Gani Mbali Zaidi ya India?
Ni vigumu kusema wafanyabiashara wa eneo la Mediterania na wasafiri wengine walienda mbali kadiri gani upande wa mashariki, na pia safari hizo zilianza wakati gani. Hata hivyo, inaaminiwa kwamba kufikia karne ya kwanza W.K., baadhi ya watu kutoka ulaya walisafiri hadi Thailand, Kambodia, Sumatra, na Java.
Maandishi ya Hou Han-Shou (Kumbukumbu za Kihistoria za Milki ya Baadaye ya Han), ya mwaka wa 23 W.K. hadi 220 W.K. yanaonyesha tarehe ya mojawapo ya safari hizo. Mnamo 166 W.K., balozi aliyeitwa An-tun, ambaye alitumwa na mfalme wa Daqin, aliwasili kwenye makao ya mfalme wa China akiwa na zawadi kwa ajili ya Maliki Huan-ti. Daqin lilikuwa jina la Kichina la Milki ya Roma, na yaelekea An-tun lilikuwa jina la Kichina la Antoninus, jina la familia ya Marcus Aurelius, aliyekuwa maliki Mroma wakati huo. Wanahistoria wanafikiri kwamba hiyo haikuwa ziara rasmi ya kibalozi bali ilikuwa jitihada iliyokusudiwa kuwasaidia wafanyabiashara wa ulaya wapate hariri moja kwa moja kutoka China badala ya kupitia kwa walanguzi.
Tukirudia swali tulilouliza mwanzoni, Meli za kale zingewasafirisha wamishonari Wakristo wa karne ya kwanza hadi wapi upande wa mashariki? Je, walifika India na hata mbali zaidi? Labda. Bila shaka, ujumbe wa Kikristo ulienezwa mbali sana hivi kwamba mtume Paulo angeweza kusema kwamba ulikuwa ‘ukizaa matunda na kuongezeka katika ulimwengu wote,’ yaani, kufikia maeneo ya mbali zaidi ya ulimwengu wa wakati huo.—Wakolosai 1:6.
[Maelezo ya chini]
a Ingawa haijulikani kabisa mahali Muziris lilikuwa, wasomi wanasema lilikuwa karibu na mlango wa Mto Periyar, katika Jimbo la Kerala.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 22]
Maliki Alalamika
Mnamo 22 W.K. Maliki Mroma Tiberio alilalamika kwamba raia zake walikuwa wakitumia mali kupita kiasi. Hamu yao isiyoweza kutoshelezwa ya anasa, na tamaa ya wanawake Waroma inayopita kiasi ya vito ilikuwa ikifuja mali ya milki yake, na kuipeleka kwa “mataifa mageni au yenye uhasama.” Pia, mwanahistoria Mroma Plini Mkubwa (23-79 W.K.) alilalamika kuhusu jambo hilo. Aliandika: “Kadirio la chini zaidi linaonyesha kwamba kila mwaka maeneo ya India, Seres, na Rasi ya Arabia, yanachukua kutoka kwa milki yetu sesterce milioni 100—kwa kweli tunatumia pesa nyingi kwa ajili ya anasa na wanawake wetu.”b
[Maelezo ya chini]
b Wachunguzi wanakadiria kwamba sesterce milioni 100 zilikuwa sawa na asilimia 2 ya uchumi wote wa Milki ya Roma.
[Hisani]
Museo della Civiltà Romana, Roma; Todd Bolen/Bible Places.com
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]
Wafanyabiashara Walitoa Wapi Bidhaa Zao?
Yesu alizungumza kuhusu “mwanabiashara msafiri anayetafuta lulu nzuri.” (Mathayo 13:45) Pia, kitabu cha Ufunuo kinataja “wanabiashara . . . wanaosafiri” ambao bidhaa zao zilitia ndani mawe ya thamani, hariri, mbao zenye manukato, pembe za tembo, mdalasini, uvumba, na vikolezo vya Wahindi. (Ufunuo 18:11-13) Bidhaa hizo zilitoka maeneo yaliyo mashariki ya Palestina yaliyokuwa kwenye njia za biashara. Mbao zenye manukato, kama vile, misandali, ilitoka India. Vito vyenye thamani vingeweza kupatikana katika Ghuba ya Uajemi, Bahari Nyekundu, na pia, kulingana na mwandishi wa kitabu kimoja (Periplus Maris Erythraei), vingepatikana katika eneo la Muziris na Sri Lanka. Yaelekea lulu za Bahari ya Hindi zilikuwa za hali ya juu kabisa na za bei ghali zaidi.
[Ramani katika ukurasa wa 20, 21]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Baadhi ya njia za biashara kati ya Roma na Asia katika karne ya kwanza
Arezzo
Roma
BAHARI YA MEDITERANIA
AFRIKA
Aleksandria
MISRI
Coptos
Mto Nile
Myos Hormos
Berenice
Zanzibar
Bahari Nyekundu
Yerusalemu
ARABIA
Mto Efrati
BABILONIA
Ghuba ya Uajemi
UAJEMI
↓ Pepo za kaskazini-mashariki
↑ Pepo za kusini-magharibi
Mto Indus
PUNJAB
Mto Ganges
Ghuba ya Bengal
INDIA
Arikamedu
Muziris
SRI LANKA
BAHARI YA HINDI (BAHARI YA ERYTHRA)
CHINA
MILKI YA HAN
THAILAND
KAMBODIA
VIETNAM
Sumatra
Java
[Picha katika ukurasa wa 21]
Meli ya Roma ya kubebea mizigo
[Hisani]
Ship: Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.