Kitabu Cha Biblia Namba 3—Mambo Ya Walawi
Mwandikaji: Musa
Mahali Kilipoandikiwa: Jangwani
Uandikaji Ulikamilishwa: 1512 K.W.K.
Wakati Uliohusishwa: Mwezi 1 (1512 K.W.K.)
1. (a) Kwa nini jina Mambo ya Walawi lafaa? (b) Ni majina gani mengine kimepewa Mambo ya Walawi?
JINA la kawaida zaidi la kitabu cha tatu cha Biblia ni Leviticus (katika Kiingereza, Kiswahili ni Mambo ya Walawi), linalotokana na Leu·i·ti·konʹ la Septuagint ya Kigiriki kutoka kwa “Leviticus” la Vulgate ya Kilatini. Jina hilo lafaa, hata ingawa Walawi watajwa kijuu-juu (kwenye 25:32, 33), kwa maana kitabu hicho hasa chajumlisha matakwa ya ukuhani wa Kilawi, uliochaguliwa kutoka kabila la Lawi, na sheria ambazo makuhani walifunza watu: “Kwa maana yapasa midomo ya kuhani ihifadhi maarifa, tena yawapasa watu kuitafuta sheria kinywani mwake.” (Mal. 2:7) Katika maandishi ya Kiebrania, kitabu hicho kimepewa jina kutokana na usemi wacho wa ufunguzi, Wai·yiq·ra’ʹ, kwa uhalisi, “Na yeye akachukua hatua ya kuita.” Miongoni mwa Wayahudi wa baadaye, kitabu hicho kiliitwa pia Sheria ya Makuhani na Sheria ya Matoleo.—Law. 1:1, NW, kielezi-chini.
2. Kuna ushuhuda gani wa kuunga mkono uandikaji wa Musa?
2 Hakuna shaka kwamba Musa aliandika Mambo ya Walawi. Umalizio, au tamati, wataarifu hivi: “Haya ndiyo maagizo, BWANA [Yehova, NW] aliyomwagiza Musa kwa ajili ya wana wa Israeli katika mlima wa Sinai.” (27:34) Taarifa ifananayo na hiyo yapatikana katika Mambo ya Walawi 26:46. Ushuhuda ulioonyeshwa mbele kuthibitisha kwamba Musa aliandika Mwanzo na Kutoka waunga mkono pia kwamba ndiye aliyeandika Mambo ya Walawi, kwa kuwa Pentateuki kwa wazi hapo awali ilikuwa hati-kunjo moja. Zaidi ya hayo, Mambo ya Walawi (katika New World Translation) kimeunganishwa na vitabu vinavyotangulia kwa kiunganishi “na.” Na ushuhuda wenye nguvu zaidi ya wote ni kwamba Yesu Kristo na watumishi wengine wa Yehova waliopuliziwa na Mungu mara nyingi hunukuu au hurejezea mara nyingi sheria na kanuni katika Mambo ya Walawi na kuzihesabia Musa.—Law. 23:34, 40-43—Neh. 8:14, 15; Law. 14:1-32—Mt. 8:2-4; Law. 12:2—Luka 2:22; Law. 12:3—Yn. 7:22; Law. 18:5—Rum. 10:5.
3. Ni kipindi gani cha wakati chahusishwa na Mambo ya Walawi?
3 Mambo ya Walawi chahusisha kipindi gani? Kitabu cha Kutoka chamalizia kwa kusimamishwa kwa tabenakulo “mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili, siku ya kwanza ya mwezi.” Kitabu cha Hesabu (kikifuatisha bila kukawia simulizi la Mambo ya Walawi) chafungua kwa Yehova kunena na Musa “siku ya kwanza ya mwezi wa pili, katika mwaka wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri.” Kwa hiyo, ni muda wa zaidi ya mwezi mmoja uliopita kabla ya kutukia kwa matukio machache ya Mambo ya Walawi, sehemu kubwa ya kitabu hicho ikiwa ni sheria na matakwa.—Kut. 40:17; Hes. 1:1; Law. 8:1–10:7; 24:10-23.
4. Mambo ya Walawi kiliandikwa lini?
4 Musa aliandika Mambo ya Walawi lini? Ni jambo la akili kukata maneno kwamba alitunza maandishi ya matukio yalipokuwa yakitukia na kuandika maagizo ya Mungu kwa kadiri alivyoyapokea. Hilo ladokezwa na amri ya Mungu kwa Musa juu ya kuandika maangamizi ya Waamaleki mara tu baada ya Israeli kuwashinda katika pigano. Tarehe ya mapema yadokezwa pia na mambo fulani katika kitabu hicho. Kwa kielelezo, Waisraeli waliamriwa walete wanyama waliotaka kutumia kuwa chakula kwenye mwingilio wa hema la kukutania kwa ajili ya machinjo. Amri hiyo ingetolewa na kuandikwa muda mfupi baada ya kuwekwa kwa ukuhani. Maagizo mengi yametolewa kwa ajili ya kuongoza Waisraeli wakati wa safari yao ya jangwani. Yote hayo yaelekeza kwenye Musa kuandika Mambo ya Walawi wakati wa 1512 K.W.K.—Kut. 17:14; Law. 17:3, 4; 26:46.
5. Ni kusudi gani lililotimizwa na sheria kuhusu dhabihu na uchafu wa kisherehe?
5 Kwa nini Mambo ya Walawi kiliandikwa? Yehova alikuwa amekusudia kuwa na taifa takatifu, watu waliotakaswa, waliowekwa kando kwa ajili ya utumishi wake. Tangu wakati wa Abeli, wanadamu waaminifu wa Mungu walikuwa wakitolea Yehova dhabihu, lakini kwanza kwa taifa la Israeli ndiyo Yehova alitoa maagizo kamili kuhusu matoleo ya dhambi na dhabihu nyinginezo. Hizo, kama ielezwavyo kirefu katika Mambo ya Walawi, zilifanya Waisraeli watambue udhambi wenye kulemea wa dhambi na kukazia kwenye akili zao jinsi hilo lilivyowafanya kuwa wasiopendeza kwa Yehova. Matakwa hayo, yakiwa sehemu ya Sheria, yalitumika kuwa mfundishaji wa kuongoza Wayahudi kwa Kristo, kuwaonyesha uhitaji wa Mwokozi na wakati uo huo kutumikia kuwatunza kuwa kikundi cha watu walio tofauti na ulimwengu mwingine wote. Hasa sheria za Mungu zilizohusu utakato wa kisherehe zilitumikia kusudi hilo la mwisho.—Law. 11:44; Gal. 3:19-25.
6. Kwa nini uongozi wenye mambo mengi kutoka kwa Yehova ulikuwa sasa uhitaji maalumu?
6 Wakiwa taifa jipya lenye kufunga safari kuelekea bara jipya, Israeli walihitaji mwelekezo unaofaa. Ingali ilikuwa ni chini ya mwaka mmoja tangu Kutoka, na viwango vya maisha vya Misri na pia mazoea ya kidini yalikuwa wazi akilini. Ndoa ya ndugu na dada ilizoewa Misri. Ibada ya uwongo ilifanywa kwa kuheshimu miungu mingi, mingine yayo ikiwa miungu-wanyama. Sasa kundi hili kubwa lilikuwa likielekea Kanaani, ambako maisha na mazoea ya kidini yalikuwa yamepotoka hata zaidi. Lakini angalia tena kambi ya Israeli. Wenye kuongezea sana hesabu ya kundi hilo walikuwa wengi ambao walikuwa Wamisri kwa ukamili au kwa sehemu, halaiki iliyochanganyikana waliokuwa wanaishi mle mle miongoni mwa Waisraeli na ambao walikuwa wamezaliwa na wazazi Wamisri na kulelewa na kufundishwa katika njia, dini, na uzalendo wa Wamisri. Wengi wao bila shaka walikuwa wameshiriki katika mazoea yenye kuchukiza katika nchi ya kwao muda mfupi tu uliopita. Jinsi ilivyokuwa muhimu kwamba sasa wapokee mwongozo wenye mambo mengi kutoka kwa Yehova!
7. Ni katika njia gani matakwa ya Mambo ya Walawi yana muhuri wa utungaji wa kimungu?
7 Mambo ya Walawi chote kina muhuri wa upulizo wa kimungu. Wanadamu wanyonge hawangaliweza kubuni sheria na matakwa yacho ya hekima na haki. Amri zacho kuhusu chakula, maradhi, karantini (kutenga wagonjwa), na kushughulikia miili mifu hufunua maarifa ya mambo ya hakika ambayo hayakuthaminiwa na wanatiba wa kilimwengu mpaka maelfu ya miaka baadaye. Sheria ya Mungu kuhusu wanyama wachafu wasioliwa ingelinda Waisraeli walipokuwa wakisafiri. Ingewalinda na maradhi ya kutoka kwa nguruwe, homa ya matumboni na kiini cha homa ya matumboni kutoka kwa aina fulani za samaki, na ambukizo kutoka kwa wanyama waliopatikana tayari wamekufa. Sheria hizo zenye kutumika zilipasa kuelekeza dini na maisha zao ili wabaki wakiwa taifa takatifu na kufikia na kukalia Bara Lililoahidiwa. Historia huonyesha kwamba matakwa yaliyotolewa na Yehova yaliwapa Wayahudi faida iliyo wazi kushinda watu wengine katika habari ya afya.
8. Ni jinsi gani mambo ya kiunabii yaliyomo katika Mambo ya Walawi yaendelea kuthibitisha upulizio wa Mungu?
8 Utimizo wa unabii mbalimbali na vifananishi katika Mambo ya Walawi ni hatua zaidi kuthibitisha kilipuliziwa na Mungu. Historia ya mambo matakatifu na ya ki-nchi huandika utimizo wa maonyo ya Mambo ya Walawi juu ya matokeo ya kutokutii. Kati ya mambo mengine, kilitabiri kwamba akina mama wangewala watoto wao wenyewe kwa sababu ya njaa kubwa. Yeremia alidokeza kwamba hilo lilitimizwa kwenye uharibifu wa Yerusalemu katika 607 K.W.K., na Yosefo hueleza juu ya kutukia kwa hilo wakati wa uharibifu wa baadaye wa jiji hilo, katika 70 W.K. Ahadi ya kiunabii kwamba Yehova angewakumbuka kama wangetubu ilitimizwa waliporudi kutoka Babuloni katika 537 K.W.K. (Law. 26:29, 41-45; Omb. 2:20; 4:10; Ezra 1:1-6) Hatua nyingine zaidi yenye kuthibitisha upulizio wa Mungu wa Mambo ya Walawi ni manukuu ambayo waandikaji wengine wa Biblia hufanya kutoka kwacho kuwa Andiko lililopuliziwa. Kuongezea yale yaliyotangulia kuonyeshwa kuthibitisha Musa ni mwandikaji, tafadhali ona Mathayo 5:38; 12:4; 2 Wakorintho 6:16; na 1 Petro 1:16.
9. Mambo ya Walawi chaadhimishaje jina na utakatifu wa Yehova?
9 Kitabu cha Mambo ya Walawi chaadhimisha jina la Yehova na enzi kuu yake bila kigeu-geu. Mara zisizopungua 36 sheria zacho zasemekana ni za Yehova. Jina Yehova lenyewe laonekana, kwa wastani, mara kumi katika kila sura, na tena na tena utii kwa sheria za Mungu waimarishwa na kikumbusho, ‘Mimi ndimi Yehova.’ Kichwa kikuu cha utakatifu chaendelea kotekote katika Mambo ya Walawi, nacho chataja takwa hilo mara nyingi zaidi ya kitabu kinginecho chote cha Biblia. Waisraeli walipaswa kuwa watakatifu kwa sababu Yehova ni mtakatifu. Watu fulani, mahali, vitu, na vipindi vya wakati viliwekwa kando kuwa vitakatifu. Kwa kielelezo, Siku ya Upatanisho na mwaka wa Yubile viliwekwa kando kuwa majira ya mwadhimisho maalumu katika ibada ya Yehova.
10. Ni nini chakaziwa kuhusiana na dhabihu, na ni adhabu gani za dhambi zaonekana?
10 Kupatana na mkazo wacho juu ya utakatifu, kitabu cha Mambo ya Walawi hukazia sehemu ambayo humwagwa kwa damu, yaani, dhabihu ya uhai, ilishiriki katika msamaha wa dhambi. Dhabihu za wanyama zilihusu viumbe wa kufugwa na walio safi tu. Kwa dhambi fulani-fulani, kurudishwa, na malipo ya adhabu yalitakwa yawe nyongeza kwa dhabihu. Na bado kwa dhambi nyinginezo, adhabu ilikuwa kifo.
YALIYOMO KATIKA MAMBO YA WALAWI
11. Mambo ya Walawi chaweza kupangiliwa jinsi gani?
11 Mambo ya Walawi chajumlisha hasa uandikaji wa kisheria, mwingi wao ukiwa wa kiunabii pia. Kwa ujumla kitabu hicho kinafuatisha muhtasari wa vichwa-habari kimoja kimoja na chaweza kugawanywa katika visehemu vinane, ambavyo vyafuatana kwa utaratibu wa kimantiki (kiakili).
12. Kuna aina zipi za dhabihu za damu, nazo zapasa kutolewaje?
12 Matakwa ya dhabihu (1:1–7:38). Dhabihu mbalimbali zinagawanywa katika sehemu mbili kubwa: zenye damu, kujumlisha ng’ombe, kondoo, mbuzi, na nyuni; na zisizo na damu, zilizo za nafaka. Dhabihu za damu zapasa kutolewa zikiwa ama (1) za kuteketeza, (2) za ushirika, (3) za dhambi, au (4) matoleo ya hatia. Zote nne zafanana katika mambo haya matatu: Mtoaji lazima mwenyewe ailete kwenye mwingilio wa hema la mkutano, lazima aweke mikono yake juu yayo, halafu mnyama huyo achinjwe. Kufuatia kunyunyizwa kwa damu, ni lazima mzoga uondolewe kwa kulingana na aina ya dhabihu. Sasa na tuchunguze dhabihu za damu moja baada ya nyingine.
13-16. (a) Toa muhtasari wa matakwa ya (1) matoleo ya kuteketezwa, (2) dhabihu za ushirika, (3) matoleo ya dhambi, na (4) sadaka za hatia. (b) Kwa kukamatana na dhabihu za damu, ni nini kinachokatazwa kwa kurudiwa-rudiwa?
13 (1) Matoleo ya kuteketezwa yangeweza kuwa fahali, kondoo-ndume, mbuzi, au njiwa au ya njiwa-mwitu, ikitegemea uwezo wa mtoaji. Yapasa kukatwa vipande-vipande na yote, isipokuwa ngozi, iteketezwe juu ya madhabahu. Kwa habari ya njiwa-mwitu au ninga, kichwa kilipasa kukatwa bali si kukatwa mpaka kuanguka, na gole (kibofu cha kooni) na manyoya kuondolewa.—1:1-17; 6:8-13; 5:8.
14 (2) Matoleo ya ushirika yangeweza kuwa ama dume au jike, la ng’ombe au kondoo na mbuzi. Sehemu zayo zenye shahamu tu ndizo za kuliwa na moto juu ya madhabahu, kisehemu fulani kikimwendea kuhani na masalio yakiliwa na mtoaji. Kwa kufaa yaitwa dhabihu ya ushirika, kwa maana kwayo mtoaji ashiriki mlo, au ana ushirika, kama ilivyo, na Yehova na kuhani.—3:1-17; 7:11-36.
15 (3) Matoleo ya dhambi yatakwa kwa dhambi zisizo za kukusudia, au dhambi zilizofanywa kwa kukosea. Aina ya mnyama atolewaye yategemea ni dhambi ya nani iliyokuwa ikipatanishwa—ile ya kuhani, watu kwa ujumla, jumbe, au mtu wa kawaida. Tofauti na matoleo ya kuteketezwa ya hiari na ya ushirika kwa ajili ya watu mmoja mmoja, matoleo ya dhambi ni ya lazima.—4:1-35; 6:24-30.
16 (4) Matoleo ya hatia yahitajiwa ili kufunika hatia ya kibinafsi kwa sababu ya kutoaminika, udanganyifu, au unyang’anyi. Katika visa fulani hatia yataka ungamo na dhabihu kulingana na uwezo wa mtu. Katika vingine, kulipa ridhaa iliyolingana na hasara na kuongezea asilimia 20 na dhabihu ya kondoo-ndume kwahitajiwa. Katika kisehemu hiki cha Mambo ya Walawi kinachoshughulika na matoleo, ulaji wa damu wakatazwa kwa mkazo na kwa kurudiwa-rudiwa.—5:1–6:7; 7:1-7, 26, 27; 3:17.
17. Dhabihu zisizo na damu zapasa kutolewaje?
17 Dhabihu zisizo na damu zapasa kuwa nafaka na zapasa kutolewa zikiwa ama zimekaangwa hali zi kamili, zimesagwa vipande vikubwa, au zikiwa unga mwembamba; na zapasa kutayarishwa katika njia mbalimbali, kama kwa kuokwa, kukaushwa, au kukaangwa katika shahamu nyingi. Zapasa kutolewa pamoja na chumvi na mafuta na nyakati nyingine na uvumba, lakini ni lazima ziwe bila chachu au asali kabisa. Kwa dhabihu fulani kisehemu fulani kitakuwa mali ya kuhani.—2:1-16.
18. Kuwekwa kwa ukuhani kwafikia tamati kwa tamasha gani yenye kutia nguvu imani?
18 Kuwekwa kwa ukuhani (8:1–10:20). Sasa wafika wakati wa pindi kubwa katika Israeli, kuwekwa kwa ukuhani. Musa ashughulikia hilo mpaka nukta yalo ya mwisho, sawa na ambavyo Yehova alimwamuru. “Basi Haruni na wanawe wakafanya mambo hayo yote BWANA [Yehova, NW] aliyoyaagiza kwa mkono wa Musa.” (8:36) Baada ya zile siku saba za kushughulikia kuwekwa, kwatokea tamasha ya kimwujiza na yenye kutia imani nguvu. Kusanyiko lote lipo. Ni sasa tu makuhani wamemaliza kutoa dhabihu. Haruni na Musa wamebariki watu. Halafu, tazama! “Utukufu wa BWANA [Yehova, NW] ukawatokea watu wote. Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA [Yehova, NW], na kuiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na yale mafuta juu ya madhabahu; watu wote walipouona huo moto wakapiga kelele wakapomoka kifudifudi.” (9:23, 24) Hakika, Yehova astahili utii na ibada yao!
19. Ni ukosaji gani unaotukia, ukifuatwa na nini?
19 Hata hivyo kuna mikiuko (kuvunja) ya Sheria. Kwa kielelezo, wana wa Haruni, Nadabu na Abihu watoa moto usio halali mbele za Yehova. “Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA [Yehova, NW], nao ukawala, nao wakafa mbele za BWANA [Yehova, NW].” (10:2) Ili kutoa dhabihu yenye kukubalika na kuonea shangwe kibali cha Yehova, watu na kuhani pia ni lazima wafuate maagizo ya Yehova. Mara tu baada ya hilo, Mungu atoa amri kwamba ni lazima makuhani wasinywe vileo wanapotumikia kwenye tabenakulo, ikidokeza kwamba kulewa huenda kulichangia kule kukosa kwa wana wawili wa Haruni.
20, 21. Ni matakwa gani ambayo yahusisha utakato na usafi wa kiafya ufaao?
20 Sheria juu ya utakato (11:1–15:33). Kisehemu hiki chashughulika na utakato wa kisherehe na kiafya. Wanyama fulani, wa kufugwa na wa porini, ni wachafu. Miili mifu yote ni michafu na husababisha wale wanaoigusa kuwa wachafu. Kuzaliwa kwa mtoto pia hutokeza uchafu na hutaka kutengwa na dhabihu maalumu.
21 Maradhi fulani ya ngozi, kama ukoma, pia husababisha uchafu wa kisherehe, na kutakasa kwapasa kuhusu si watu tu bali pia hata mavazi na nyumba. Kuweka karantini (kutengwa kwa mgonjwa) ni takwa. Hedhi na kutokwa na shahawa pia kwatokeza uchafu, sawa na mitoko yenye kutiririka. Kutengwa kwahitajiwa katika visa hivyo, na baada ya kupata nafuu, kuongezea, kuoga mwili au kutoa dhabihu au vyote viwili ni takwa.
22. (a) Ni kwa nini sura ya 16 ni ya kutokeza? (b) Ni nini utaratibu wa Siku ya Upatanisho?
22 Siku ya Upatanisho (16:1-34). Hii ni sura yenye kutokeza, kwa maana ina maagizo juu ya siku ya maana zaidi ya Israeli, Siku ya Upatanisho, ambayo huja siku ya kumi ya mwezi wa saba. Ni siku ya kuipiga nafsi (yaelekea sana kwa kufunga), na siku hiyo hakuna kazi ya kimwili itakayoruhusiwa. Yaanza kwa kutolewa kwa fahali kwa ajili ya dhambi za Haruni na nyumba yake, kabila la Lawi, kisha kutolewa kwa mbuzi kwa ajili ya sehemu ile nyingine ya taifa. Baada ya kuchoma ubani, baadhi ya damu ya kila mnyama yaletwa, kwa zamu, ndani ya Patakatifu Zaidi pa tabenakulo, ili inyunyizwe mbele za kifuniko cha Sanduku. Baadaye mizoga ya wanyama ni lazima itolewe nje ya kambi na kuteketezwa. Katika siku hii mbuzi aliye hai pia apasa atolewe mbele za Yehova, na juu yake dhambi zote za watu zatangazwa, baada ya hilo aongozwa aende zake jangwani. Kisha kondoo-ndume wawili ni lazima kutolewa kuwa sadaka za kuteketezwa, mmoja kwa ajili ya Haruni na nyumba yake na mwingine kwa ajili ya sehemu ile nyingine ya taifa.
23. (a) Ni wapi tupatapo mojawapo taarifa za Biblia zilizo wazi zaidi juu ya damu? (b) Ni matakwa gani mengine ambayo yafuata?
23 Amri juu ya damu na mambo mengine (17:1–20:27). Kisehemu hiki kinazo amri nyingi zilizotolewa kwa ajili ya watu. Kwa mara nyingine damu yakatazwa katika mojawapo taarifa zilizo wazi kabisa juu ya damu zipatikanazo popote katika Maandiko. (17:10-14) Damu yaweza kutumiwa kwa kufaa juu ya madhabahu, lakini si ya kula. Mazoea yenye kuchukiza, kama ngono haramu ya kiukoo, usodoma (ulawiti), na ngono na mnyama, vyakatazwa. Kuna matakwa ya kulinda wenye taabu, wa cheo cha chini, na mgeni, na amri yatolewa, “Umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi BWANA [Yehova, NW].” (19:18) Hali njema ya kijamii na ya kiuchumi ya taifa yalindwa, na hatari za kiroho, kama vile ibada ya Moleki na uwasiliani-roho, yaharamishwa, adhabu ikiwa ni kifo. Kwa mara nyingine Mungu akazia utofauti wa watu wake: “Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa mimi BWANA [Yehova, NW] ni mtakatifu, nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu.”—20:26.
24. Mambo ya Walawi chaorodhesha nini juu ya sifa za kikuhani na miadhimisho ya majira?
24 Ukuhani na miadhimisho (21:1–25:55). Sura tatu zifuatazo zashughulika hasa na ibada rasmi ya Israeli: amri za kuongoza makuhani, sifa zao za kimwili, wawezao kuwaoa, wawezao kula vitu vitakatifu, na matakwa juu ya wanyama wasio na kasoro wa kutumiwa katika dhabihu. Miadhimisho mitatu ya kitaifa ya majira yaamriwa, ikifanyiza pindi za ‘kufurahi mbele za BWANA [Yehova, NW] Mungu wenu.’ (23:40) Kama mtu mmoja, katika njia hiyo taifa litageuza uangalifu, sifa, na ibada kwa Yehova, litie nguvu uhusiano walo pamoja naye. Hiyo ni miadhimisho kwa Yehova, mikusanyiko mitakatifu ya kila mwaka. Kupitwa, pamoja na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, zimepangiwa masika ya mapema; Pentekoste, au Sikukuu ya Majuma, yafuata katika masika ya baadaye; na Siku ya Upatanisho na Sikukuu ya Vibanda au ya Kukusanya iliyo ya siku nane, ni za masika.
25. (a) Yaonyeshwaje kwamba “hilo Jina” ni lazima lichukuliwe kwa heshima? (b) Ni matakwa gani ambayo yahusisha namba “saba”?
25 Katika sura ya 24, maagizo yatolewa kuhusu mkate na mafuta ya kutumiwa katika utumishi wa tabenakulo. Kwafuata kisa ambacho katika hicho Yehova akata maneno kwamba mtu yeyote anayetumia vibaya “hilo Jina”—naam, lile jina Yehova—ni lazima apigwe mawe hadi kufa. Kisha atoa taarifa ya sheria ya kupewa adhabu ile ile, “jicho kwa jicho, jino kwa jino.” (24:11-16, 20) Katika sura 25, matakwa yapatikana yanayohusu Sabato ya mwaka mmoja, au mwaka wa pumziko, wa kuadhimishwa kila mwaka wa 7 na Yubile kila mwaka wa 50. Katika mwaka huu wa 50, uhuru ni lazima utangazwe katika bara lote, na mali ya urithi iliyouzwa au kupotezwa wakati wa miaka 49 iliyopita ni lazima irudishwe. Sheria za kulinda haki za maskini na za watumwa zatolewa. Katika kisehemu hiki namba “saba” yatokeza sana—siku ya saba, mwaka wa saba, miadhimisho ya siku saba, kipindi cha majuma saba, na Yubile, iliyokuja baada ya miaka saba mara saba.
26. Mambo ya Walawi chafikia upeo katika nini?
26 Matokeo ya utii na kukosa utii (26:1-46). Kitabu cha Mambo ya Walawi chafikia upeo katika sura hii. Yehova hapa aorodhesha thawabu za utii na adhabu za kukosa utii. Wakati uo huo, atoa tumaini kwa Waisraeli kama wakijinyenyekeza, akisema: “Kwa ajili yao nitalikumbuka agano la baba zao, niliowaleta watoke katika nchi ya Misri mbele ya macho ya mataifa, ili kwamba niwe Mungu wao; mimi ndimi BWANA [Yehova, NW].”—26:45.
27. Mambo ya Walawi chamaliziaje?
27 Amri nyinginezo (27:1-34). Mambo ya Walawi chamalizia kwa maagizo juu ya kushughulikia matoleo ya nadhiri, kuhusu mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya Yehova, na juu ya sehemu ya kumi ambayo huwa takatifu kwa Yehova. Kisha yaja kolofoni (umalizio) fupi: “Haya ndiyo maagizo, BWANA [Yehova, NW] aliyomwagiza Musa kwa ajili ya wana wa Israeli katika mlima wa Sinai.”—27:34.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
28. Mambo ya Walawi kina mafaa gani kwa Wakristo leo?
28 Kikiwa sehemu ya Maandiko yaliyopuliziwa na Mungu, kitabu cha Mambo ya Walawi ni chenye mafaa makubwa kwa Wakristo leo. Ni chenye msaada mzuri ajabu katika kuthamini Yehova, sifa zake, na njia zake za kushughulika na viumbe vyake, kama alivyoonyesha waziwazi sana kwa Israeli chini ya agano la Sheria. Mambo ya Walawi chaeleza kanuni nyingi za msingi ambazo sikuzote zitatumika, na kina vigezo vingi vya kiunabii, na pia unabii mbalimbali, ambao hutia imani nguvu ufikiriwapo. Nyingi za kanuni zacho zaelezwa tena katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, nyingine zazo zikinukuliwa moja kwa moja. Mambo saba yenye kutokeza yazungumzwa chini.
29-31. Mambo ya Walawi chakaziaje staha kwa (a) enzi kuu, (b) jina, na (c) utakatifu wa Yehova?
29 (1) Enzi kuu ya Yehova. Yeye ndiye Mtoa-sheria, na sisi tukiwa viumbe wake twawajibika kumtolea hesabu. Yeye atuamuru kwa haki tumhofu yeye. Akiwa Mwenye Enzi Kuu ya Ulimwengu Wote Mzima, havumilii ushindani wowote, uwe ule wa namna ya ibada ya sanamu, uwasiliani-roho, au hali nyinginezo za mambo yanayohusu roho waovu.—Law. 18:4; 25:17; 26:1; Mt. 10:28; Mdo. 4:24.
30 (2) Jina la Yehova. Jina lake lapasa kutunzwa likiwa takatifu, nasi hatuthubutu kuliletea suto kwa maneno au kwa vitendo.—Law. 22:32; 24:10-16; Mt. 6:9.
31 (3) Utakatifu wa Yehova. Kwa sababu yeye ni mtakatifu, watu wake ni lazima pia wawe watakatifu, yaani, waliotakaswa, au kuwekwa kando kwa ajili ya utumishi wake. Hiyo inatia ndani kujiweka tofauti na ulimwengu usio na Mungu unaotuzunguka.—Law. 11:44; 20:26; Yak. 1:27; 1 Pet. 1:15, 16.
32-34. Ni kanuni gani zimepangiliwa kuhusu (a) dhambi, (b) damu, na (c) hatia husianifu?
32 (4) Udhambi wenye kuzidi wa dhambi. Mungu ndiye huamua dhambi ni nini, nasi ni lazima tupigane nayo. Sikuzote dhambi hutaka dhabihu ya kupatanisha. Kuongezea hilo, pia hutaka sisi tuungame, tutubu, na kufanya marekebisho kwa kadiri iwezekanayo. Kwa dhambi fulani hakuwezi kuwa msamaha.—Law. 4:2; 5:5; 20:2, 10; 1 Yn. 1:9; Ebr. 10:26-29.
33 (5) Utakatifu wa damu. Kwa sababu damu ni takatifu, haiwezi kutwaliwa mwilini katika namna yoyote. Matumizi pekee yaruhusiwayo ya damu ni upatanisho kwa ajili ya dhambi.—Law. 17:10-14; Mdo. 15:29; Ebr. 9:22.
34 (6) Uhusianishi katika hatia na adhabu. Si dhambi na watenda dhambi wote walioonwa kwa hali ile ile. Kadiri cheo kilivyokuwa cha juu, ndivyo daraka na adhabu ya dhambi ilivyokuwa ya juu. Dhambi ya kukusudia iliadhibiwa kwa ukali zaidi ya dhambi isiyo ya kukusudia. Mara nyingi adhabu zilipewa madaraja kulingana na uwezo wa kulipa. Iliyo kanuni ya uhusianishi ilitumiwa pia katika nyanja nyingine kando ya dhambi na adhabu, kama vile katika uchafu wa kisherehe.—Law. 4:3, 22-28; 5:7-11; 6:2-7; 12:8; 21:1-15; Luka 12:47, 48; Yak. 3:1; 1 Yn. 5:16.
35. Mambo ya Walawi chajumlishaje wajibu wetu kuelekea binadamu mwenzetu?
35 (7) Haki na upendo. Kikijumlisha wajibu wetu mbalimbali kuelekea binadamu mwenzetu, Mambo ya Walawi 19:18 chasema: “Umpende jirani yako kama nafsi yako.” Hilo latia ndani kila jambo. Haliruhusu kuonyesha upendeleo, kuiba, kusema uwongo, au kuchongea, na lataka kuonyesha ufikirio kwa waliolemaa, maskini, vipofu, na viziwi.—Law. 19:9-18; Mt. 22:39; Rum. 13:8-13.
36. Ni nini chathibitisha kwamba Mambo ya Walawi kina mafaa kwa kundi la Kikristo?
36 Pia yenye kuthibitisha kwamba Mambo ya Walawi ni chenye kutokeza kwa ‘kufaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki’ ndani ya kundi la Kikristo ni marejezo yacho yafanywayo na Yesu na mitume wake, hasa Paulo na Petro. Wao walielekeza uangalifu kwenye vigezo vingi vya kiunabii na vivuli vya mambo yaliyokuwa yakija. Kama alivyosema Paulo, “Sheria ina kivuli cha mambo mema yajayo.” Yaweka “uwakilishi na kivuli cha mambo ya kimbingu.”—2 Tim. 3:16; Ebr. 10:1; 8:5, NW.
37. Ni matimizo gani ya vifananishi yanasimuliwa katika Waebrania?
37 Tabenakulo, ukuhani, dhabihu, na hasa Siku ya Upatanisho ya kila mwaka vilikuwa na umaana wenye kifananishi. Paulo, katika barua yake kwa Waebrania, hutusaidia tutambulishe milingano ya kiroho ya mambo hayo kwa kuhusiana na “hema ya kweli” ya ibada ya Yehova. (Ebr. 8:2) Kuhani mkuu Haruni afananisha Kristo Yesu “aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi.” (Ebr. 9:11; Law. 21:10) Damu ya dhabihu za wanyama yafananisha damu ya Yesu, ambayo hutokeza “ukombozi wa milele [kwa ajili yetu, NW].” (Ebr. 9:12) Chumba cha ndani zaidi cha tabenakulo, Patakatifu Zaidi, ambamo kuhani mkuu aliingia Siku ya Upatanisho ya kila mwaka ili kutoa damu ya kidhabihu, ni “nakala ya ule uhalisi,” “mbinguni kwenyewe,” ambako Yesu alipaa ili ‘aonekane mbele za uso wa Mungu kwa ajili yetu.’—Ebr. 9:24, NW; Law. 16:14, 15.
38. Dhabihu za ufananishi zilitimizwaje katika Yesu?
38 Wanyama waliotolewa dhabihu kihalisi—wanyama timamu, wasio na kasoro waliotolewa kama matoleo ya kuteketeza au ya dhambi—huwakilisha dhabihu kamilifu isiyo na kasoro ya mwili wa kibinadamu wa Yesu Kristo. (Ebr. 9:13, 14; 10:1-10; Law. 1:3) Kwa kupendeza, Paulo pia azungumza ile sehemu ya Siku ya Upatanisho ambayo mizoga ya wanyama kwa ajili ya matoleo ya dhambi ilipelekwa nje ya kambi na kuteketezwa. (Law. 16:27) “Kwa ajili hii Yesu naye,” aandika Paulo, “aliteswa nje ya lango. Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi, tukichukua shutumu lake.” (Ebr. 13:12, 13) Kwa fasiri hiyo iliyopuliziwa na Mungu, taratibu za kisherehe zilizoorodheshwa katika Mambo ya Walawi zachukua umaana wa ziada, nasi twaweza kuanza kuelewa jinsi kwa kustaajabisha Yehova alitokeza huko vivuli vya kutisha vyenye kuelekeza mbele kwenye uhalisi ambao ungeweza kubainishwa tu na roho takatifu. (Ebr. 9:8) Uelewevu huo ufaao ni muhimu kwa wale ambao watapata mafaa ya mpango wa uhai ambao Yehova hufanya kupitia Kristo Yesu, “kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu.”—Ebr. 10:19-25.
39. Mambo ya Walawi chaunganaje na “kila andiko” katika kujulisha makusudi ya Ufalme wa Yehova?
39 Kama vile nyumba ya kikuhani ya Haruni, Yesu Kristo akiwa Kuhani Mkuu ana makuhani wadogo ambao washirikiana naye. Wao wanenwa kuwa “ukuhani wa kifalme.” (1 Pet. 2:9) Mambo ya Walawi chaelekeza na kueleza wazi juu ya kazi ya kupatanisha dhambi ya Kuhani Mkuu na Mfalme wa Yehova na matakwa waliyowekewa washiriki wa nyumba Yake, ambao hunenwa kuwa “wenye furaha na watakatifu” na kuwa ‘makuhani wa Mungu na wa Kristo na kutawala wakiwa wafalme pamoja naye kwa ile miaka elfu.’ Ni baraka zilizoje ambazo kazi hiyo ya kikuhani itatimiza katika kuinua ainabinadamu kwenye ukamilifu, na ni furaha iliyoje itakayoletwa na Ufalme huo wa kimbingu kwa kurudisha amani na uadilifu duniani! Hakika, ni lazima sisi sote tumshukuru Mungu mtakatifu, Yehova, kwa ajili ya kupanga kuwe Kuhani Mkuu na Mfalme na ukuhani wa kifalme wa kujulisha rasmi wema Wake kotekote katika kutakasa jina Lake! Kweli kweli, Mambo ya Walawi chaungana vizuri sana pamoja na “kila andiko” katika kujulisha makusudi ya Ufalme wa Yehova.—Ufu. 20:6, NW.