Mafunzo Juu ya Maandiko Yenye Pumzi ya Mungu na Habari ya Msingi Yayo
Funzo Namba 1—Ziara Kwenye Bara Lililoahidiwa
Mikoa ya bara hilo, sura zalo za nchi, milima na mabonde yalo, mito na maziwa yalo, na halihewa, udongo, na namna namna za uoto walo.
1. (a) Kwa nini mtajo “Bara la Ahadi” wafaa sana? (b) Ni taraja gani tukufu tunaloweza kuwa nalo akilini tuchunguzapo jiografia ya bara hilo?
MIPAKA ya Bara Lililoahidiwa la kale iliwekwa na Yehova Mungu. (Kut. 23:31; Hes. 34:1-12; Yos. 1:4) Kwa karne nyingi eneo hili lilirejezewa na wengine kuwa bara la Palestina, jina linalotokana na Palaestina la Kilatini na Pa·lai·stiʹne la Kigiriki. Neno hilo la mwisho latolewa kutoka Peleʹsheth la Kiebrania. Katika Maandiko ya Kiebrania, Peleʹsheth hutafsiriwa “Filistia,” na hurejezea eneo la Wafilisti pekee, waliokuwa maadui wa watu wa Mungu. (Kut. 15:14) Hata hivyo, kwa kuwa Yehova aliahidi Abrahamu mwaminifu na wazao wake bara hilo, mtajo “Bara Lililoahidiwa,” au “Bara la Ahadi,” wafaa zaidi. (Mwa. 15:18, NW; Kum. 9:27, 28, NW; Ebr. 11:9, NW) Bara hilo ni la kutokeza kwa unamna-namna wa jiografia yalo, sehemu hii ndogo ikijumlisha sura tofauti-tofauti na vipeo vinavyopatikana duniani kote. Ikiwa Yehova angeweza kuwapa mashahidi wake wa kale hilo bara la ahadi lenye unamna-namna wote wa uzuri kuwa urithi wao, basi kwa hakika yeye aweza bado kuwapa waabudu wake walio wakfu paradiso tukufu ya ulimwengu mpya yenye kuenea duniani pote, yenye milima, mabonde, mito, na maziwa, ili kuwaletea upendezi mwingi. Sasa na tukaze fikira kwa makini kwenye sura za kijiografia za Bara la Ahadi, tutembeapo kwa utalii wa kuwazia.a
UKUBWA KWA UJUMLA
2. Wayahudi walikalia kadiri gani hilo Bara Lililoahidiwa, na katika eneo gani la nyongeza?
2 Kulingana na mipaka yalo lililopewa na Mungu kama inavyoelezwa kwenye Hesabu 34:1-12, bara lililoahidiwa Israeli lingekuwa ukanda wa eneo jembamba. Lingekuwa la kilometa 480 hivi kutoka kaskazini mpaka kusini na kilometa 56 hivi kwa upana, kwa wastani. Haikuwa mpaka wakati wa tawala za Mfalme Daudi na Sulemani kwamba eneo lote lililoahidiwa likakaliwa kijeshi, na vikundi vingi vya watu vilivyotiishwa. Hata hivyo, kisehemu hicho kilichokaliwa na Wayahudi kwa ujumla huelezwa kuwa kile kinachoenea kuanzia Dani mpaka Beer-sheba, ambacho toka kaskazini mpaka kusini kilikuwa na urefu wa kilometa 240 hivi. (1 Fal. 4:25) Mvuko wa nchi hiyo kutoka Mlima Karmeli mpaka Bahari ya Galilaya ni urefu wa kilometa 51 hivi, na katika upande wa kusini ambako mwambao wa Mediterrania hupinda hatua kwa hatua kwenda kusini-magharibi, ni wa kilometa 80 kuanzia Gaza mpaka Bahari ya Chumvi. Eneo hilo lililokaliwa upande wa magharibi wa Mto Yordani lilikuwa la kama kilometa za mraba 15,000 pekee. Hata hivyo, kwa kuongezea Waisraeli walikalia mabara ya upande wa mashariki mwa Yordani (mabara yasiyotiwa ndani ya mipaka ya awali iliyoahidiwa), na kufanya eneo lote lililokaliwa kwa ujumla kupungua kidogo kilometa za mraba 26,000.
MIKOA YA ASILI
3. Ukitumia ramani “Mikoa ya Asili ya Bara Lililoahidiwa” pamoja na fungu hili, kifupi tambulisha maeneo yanayotiwa katika migawanyo ya asili ifuatayo ya bara hilo: (a) nyanda za upande wa magharibi wa Yordani, (b) mikoa yenye milima-milima upande wa magharibi wa Yordani, (c) milima na mabara-miinuko-tambarare upande wa mashariki wa Yordani.
3 Ziara yetu kwenye Bara Lililoahidiwa itatupitisha kwenye migawanyo ya asili ya nchi ifuatayo. Muhtasari ulio chini watoa ufunguo wa ramani inayofuata, yenye kuonyesha inayoelekea kuwa mipaka ya maeneo yanayozungumzwa.
Mikoa ya Kijiografia
A. Pwani ya Bahari Kuu.—Yos. 15:12.
B. Nyanda za upande wa Magharibi mwa Yordani
1.Uwanda wa Asheri.—Amu. 5:17.
2. Ukanda wa Pwani wa Dori.—Yos. 12:23.
3. Malisho ya Sharoni.—1 Nya. 5:16.
4. Uwanda wa Filistia.—Mwa. 21:32; Kut. 13:17.
5. Bonde la Kati upande wa Mashariki-Magharibi
a. Uwanda wa Megido (Esdraeloni).—2 Nya. 35:22.
b. Uwanda wa Chini wa Yezreeli.—Amu. 6:33.
C. Mikoa ya Milima-Milima Magharibi mwa Yordani.
1. Vilima vya Galilaya.—Yos. 20:7; Isa. 9:1.
2. Vilima vya Karmeli.—1 Fal. 18:19, 20, 42.
3. Vilima vya Samaria.—Yer. 31:5; Amo. 3:9.
4. Shefela.—Yos. 11:2; Amu. 1:9.
5. Nchi ya Vilima ya Yuda.—Yos. 11:21.
6. Nyika ya Yuda (Yeshimoni).—Amu. 1:16; 1 Sam. 23:19.
7. Negebu.—Mwa. 12:9; Hes. 21:1.
8. Nyika ya Parani.—Mwa. 21:21; Hes. 13:1-3.
D. Ile Araba Kuu (Bonde la Ufa).—2 Sam. 2:29; Yer. 52:7.
1. Kibonde cha Hula
2. Mkoa wa Kuzunguka Bahari ya Galilaya.—Mt. 14:34; Yn. 6:1.
3. Wilaya ya Bonde la Yordani (Ghori).—1 Fal. 7:46; 2 Nya. 4:17; Luka 3:3.
4. Bahari ya Chumvi (Bahari ya Araba).—Hes. 34:3; Kum. 4:49; Yos. 3:16.
5. Araba (upande wa kusini kutoka Bahari ya Chumvi).—Kum. 2:8.
E. Milima na Mabara-Miinuko-Tambarare Mashariki mwa Yordani.—Yos. 13:9, 16, 17, 21; 20:8.
1. Bara la Bashani.—1 Nya. 5:11; Zab. 68:15.
2. Bara la Gileadi.—Yos. 22:9.
3. Bara la Amoni na la Moabu.—Yos. 13:25; 1 Nya. 19:2; Kum. 1:5.
4. Mlima-Uwanda wa Juu wa Edomu.—Hes. 21:4; Amu. 11:18.
F. Milima ya Lebanoni.—Yos. 13:5.
A. PWANI YA BAHARI KUU
4. Ni tabia na halihewa gani za nchi za mwambao huo?
4 Tukianza ziara yetu kutoka magharibi, kwanza twaona pwani inayojinyoosha kando ya Mediterrania ya buluu inayopendeza. Kwa sababu ya sehemu kubwa za matuta ya mchanga, bandari pekee nzuri ya asili iliyo chini ya Mlima Karmeli iko Yopa; lakini kaskazini mwa Karmeli kuna bandari kadhaa nzuri za asili. Wafoinike, walioishi katika nchi iliyo kando ya sehemu hii ya pwani, walikuja kuwa kikundi cha watu wenye kujulikana sana katika ubaharia. Halijoto ya wastani yenye kupenedeza ya kila mwaka kando ya pwani hiyo yenye jua-jua ni digrii 19 Selsio, ijapokuwa viangazi huwa vyenye joto sana, kukiwa na halijoto ya mchana ya wastani wa kama digrii 34 Selsio katika Gaza.
B-1 UWANDA WA ASHERI
5, 6. Eleza kifupi (a) Uwanda wa Asheri, (b) ukanda wa pwani wa Dori.
5 Uwanda huu wa pwani hunyooka kaskazini toka Mlima Karmeli kwa kilometa kama 40. Upana wao mkubwa zaidi ni karibu kilometa 13, nao ni sehemu ya bara lililogawiwa kabila la Asheri. (Yos. 19:24-30) Ulikuwa ukanda mwembamba wa uwanda wenye rutuba na ulizaa vizuri, ukitoa chakula kwa ajili ya meza ya kifalme ya Sulemani.—Mwa. 49:20; 1 Fal. 4:7, 16.
B-2 UKANDA WA PWANI WA DORI
6 Ukanda huu wa bara hupakana na Mfulizo-Milima wa Karmeli kwa kilometa 32 hivi. Ni wenye upana wa kilometa 4 hivi. Kwa ujumla huo ni ukanda wa pwani wa bara lililo kati ya Karmeli na Mediterrania. Katika sehemu yao ya kusini, kuna jiji-bandari la Dori, na kusini mwalo, matuta ya mchanga yaanza. Vilima vilivyo nyuma ya Dori vilizaa chakula kinono kwa ajili ya karamu za Sulemani. Mmojawapo wa binti za Sulemani alikuwa ameolewa na mtawala mwakilishi wa mkoa huo.—1 Fal. 4:7, 11.
B-3 MALISHO YA SHARONI
7. (a) Sharoni hurejezewaje katika unabii, na kwa nini? (b) Katika nyakati za Waebrania mkoa huu ulitumiwa kwa ajili ya nini?
7 Kwa sababu ya uzuri wa kimithali wa maua yayo, yafaa kwamba Sharoni yatajwa katika njozi ya kiunabii ya Isaya ya bara lililorejeshwa la Israeli. (Isa. 35:2) Hili ni bara lenye rutuba, lenye maji ya kutosha. Ni uwanda wenye upana wenye kubadilika-badilika wa kilometa 16 mpaka 19, likinyooka kwa karibu kilometa 64 kuelekea kusini kutoka ukanda wa pwani wa Dori. Katika nyakati za Kiebrania, misitu yenye miti oak ilikua katika sehemu ya kaskazini ya Sharoni. Mifugo mingi ililisha huko baada ya nafaka kukatwa. Ni kwa sababu hii kwamba liliitwa malisho ya Sharoni. Katika wakati wa Mfalme Daudi, mifugo ya kifalme ilichungiwa Sharoni. (1 Nya. 27:29) Leo miti ya jamii ya michungwa hupatikana katika eneo hilo.
B-4 UWANDA WA FILISTIA
8. Uwanda wa Filistia u wapi, na ni zipi sura zao za nchi?
8 Kisehemu hiki cha bara kiko kusini mwa malisho ya Sharoni, kikinyooka kilometa 80 hivi kando ya pwani na karibu kilometa 24 kwenda barani. (1 Fal. 4:21) Matuta ya mchanga yaliyo kando ya mwambao huingia ndani nyakati nyingine kufikia kilometa sita. Huu ni uwanda wenye kusambaa, unaoinuka juu kuanzia meta 30 hata kufikia meta 200 nyuma ya Gaza upande wa kusini. Udongo ni wenye rutuba; lakini mvua si nyingi sana, na sikuzote kuna hatari ya ukame.
B-5 BONDE LA KATI UPANDE WA MASHARIKI-MAGHARIBI
9. (a) Ni sehemu zipi mbili zinazofanyiza bonde la kati la mashariki-magharibi, nalo lilikuwa lenye ubora gani wenye kutumika? (b) Kwa kutumia michoro ya “Sehemu-Mkato Halisi za Bara Lililoahidiwa,” eleza umbo la nchi la ujumla la eneo hilo.
9 Bonde la kati upande wa mashariki-magharibi kwa kweli lajumlisha sehemu mbili, Uwanda wa Bonde wa Megido, au Esdraeloni, upande wa magharibi, na Uwanda wa Chini wa Yezreeli upande wa mashariki. (2 Nya. 35:22; Amu. 6:33) Bonde hili lote la kati liliwezesha usafiri rahisi wa kuvuka nchi toka bonde la ufa la Yordani mpaka Pwani ya Mediterrania, nalo likaja kuwa barabara muhimu ya biashara. Uwanda wa Megido hunyweshwa maji na bonde la mfo Kishoni, ambao hujipenyeza kupitia pengo jembamba kati ya Mlima Karmeli na vilima vya Galilaya na kuingia Uwanda wa Asheri na kutoka hapo mpaka Mediterrania. Njia hii ya maji machache hukauka wakati wa miezi ya kiangazi, lakini nyakati nyingine hububujika kuwa mfo.—Amu. 5:21.
10. (a) Eleza juu ya Uwanda wa Chini wa Yezreeli. (b) Eneo hilo hushirikishwa na matukio gani ya Kibiblia?
10 Uwanda wa Chini wa Yezreeli hupitisha maji upande wa kusini-mashariki kuelekea Yordani. Kipitio hiki cha bonde, Uwanda wa Yezreeli, kina upana wa kilometa 3.2 hivi na huenea masafa ya karibu kilometa 19. Mwinuko huanza panapo zaidi ya meta 90, na kisha hushuka hatua kwa hatua kufikia karibu meta 120 chini ya usawa wa bahari karibu na Beth-sheani. Bonde lote la kati ni lenye rutuba sana, kile kisehemu cha Yezreeli kikiwa mojawapo wa sehemu zenye rutuba zaidi za nchi hiyo yote. Yezreeli yenyewe humaanisha “Mungu Atapanda Mbegu.” (Hos. 2:22, NW) Maandiko hunena juu ya upendezi na uzuri wa wilaya hii. (Mwa. 49:15) Megido na Yezreeli yalifaa sana katika mapigano yaliyopiganwa na Israeli na mataifa jirani, na ni hapa ambapo Baraka, Gideoni, Mfalme Sauli, na Yehu walipigana.—Amu. 5:19-21; 7:12; 1 Sam. 29:1; 31:1, 7; 2 Fal. 9:27.
C-1 VILIMA VYA GALILAYA
11, 12. (a) Galilaya ilihusika kwa kadiri gani katika huduma ya Yesu, na ni nani waliotoka wilaya hiyo? (b) Tofautisha Galilaya ya Chini na Galilaya ya Juu.
11 Ni katika sehemu ya upande wa kusini ya vilima vya Galilaya (na kuzunguka Bahari ya Galilaya) kwamba Yesu alifanya sehemu kubwa zaidi ya utoaji ushahidi kwa jina la Yehova na Ufalme. (Mt. 4:15-17; Mk. 3:7) Wengi wa wafuasi wa Yesu, kutia ndani mitume wake wote waaminifu 11, walitoka Galilaya. (Mdo. 2:7) Katika wilaya hii ambayo wakati mwingine huitwa Galilaya ya Chini, nchi ni yenye upendezi kikweli, vilima vikiinuka si zaidi ya meta 600. Tangu vuli mpaka masika, hakuna ukosefu wa mvua kwenye bara hili lenye upendezi, na kwa hiyo si mkoa wa jangwa. Wakati wa masika kila upande wa kilima huchanua maua, na kila kibonde katika bonde kubwa huwa na nafaka tele. Kwenye miinuko-tambarare midogo-midogo, kuna udongo wenye rutuba kwa ukulima, na vilima vyafaa sana kwa ukuzi wa mizeituni na mizabibu. Miji yenye sifa ya Biblia katika eneo hili ni Nazareti, Kana, na Naini. (Mt. 2:22, 23; Yn. 2:1; Luka 7:11) Eneo hili lilimpa Yesu msingi wenye mambo mengi ya kutumia katika kuunda vielezi.—Mt. 6:25-32; 9:37, 38.
12 Katika kisehemu cha kaskazini, au Galilaya ya Juu, vilima huinuka kufikia zaidi ya meta 1,100, na kuwa, kihalisi, sehemu za chini za Milima ya Lebanoni. Galilaya ya Juu iko peke yake na huvumwa na upepo mwingi, na mvua ni kubwa sana. Katika nyakati za Biblia mitelemko ya upande wa magharibi ilikuwa na miitu iliyosongamana. Mkoa huu ulipewa kabila la Naftali.—Yos. 20:7.
C-2 VILIMA VYA KARMELI
13. (a) Kwa halisi Karmeli ni nini? (b) Ni mtajo gani unaofanywa kwayo katika Biblia?
13 Kilele cha Mlima Karmeli huchomoza kwa kutokeza kwenye Bahari ya Mediterrania. Kwa kweli Karmeli ni mfulizo wa milima-milima, yenye urefu wa karibu kilometa 48, na huinuka juu kufikia meta 545 juu ya usawa wa bahari. Hunyooka tangu vilima vya Samaria mpaka Mediterrania, na rasi yayo, ambayo hufanyiza mwinuko mkuu kwenye ncha ya kaskazini-magharibi, haisahauliki katika fahari na uzuri wayo. (Wimbo Ulio Bora 7:5) Jina Karmeli humaanisha “Shamba la Matunda,” ambalo lafaa kikweli mchomoko huo wenye rutuba, uliorembwa kwa mashamba yao ya mizabibu na miti ya matunda na mizeituni ijulikanayo sana. Isaya 35:2 huutumia kuwa mfano wa utukufu wenye kuzaa matunda wa bara la Israeli lililorejeshwa: ‘Litapewa utukufu wa Karmeli.’ Ni hapa ambapo Eliya alitolea makuhani wa Baali mwito wa ushindani na ambapo ‘moto wa Yehova ulishuka’ katika kuthibitisha ukuu wake, na ni kutoka kilele cha Karmeli kwamba Eliya alielekeza fikira kwenye wingu dogo lililokuja kuwa mvua kubwa, hivyo kumaliza kimwujiza ukame juu ya Israeli.—1 Fal. 18:17-46.
C-3 VILIMA VYA SAMARIA
14. Ni makabila gani yaliyokalia vilima vya Samaria, nalo eneo hilo lafaa kwa mazao gani?
14 Sehemu ya upande wa kusini ya mkoa huu ndio wenye vilima-vilima zaidi, ukiinuka kufikia zaidi ya meta 900 katika mashariki. (1 Sam. 1:1) Katika jambo hili, kuna mvua kubwa zaidi na yenye kutegemeka zaidi kuliko katika Yuda upande wa kusini. Mkoa huu ulikaliwa na wazao wa Efraimu, mwana mdogo wa Yusufu. Sehemu ya kaskazini ya mkoa huu, iliyopewa nusu kabila la Manase, mwana mkubwa wa Yusufu, yatia ndani vibonde katika bonde na nyanda ndogo zilizozungukwa na vilima. Bara hilo lenye vilima halina rutuba sana, ingawa kuna mashamba ya mizabibu na ya mizeituni, ambayo yamewezeshwa na kututia sana pande za chini za vilima. (Yer. 31:5) Hata hivyo, vibonde vikubwa katika mabonde vyafaa sana kwa ukuzaji wa nafaka na ukulima wa jumla. Majiji mengi yalikuwa katika mkoa huu nyakati za Biblia. Wakati wa ufalme wa kaskazini, Manase lilitoa majiji makuu matatu mfululizo—Shekemu, Tirza, na Samaria—na mkoa wote ukaja kuitwa Samaria, kufuatia jiji kuu.—1 Fal. 12:25; 15:33; 16:24.
15. (a) Baraka ya Musa kwa Yusufu ilitimizwaje katika mkoa wa Samaria? (b) Bara hilo lilibarikiwaje zaidi wakati wa Yesu?
15 Baraka ya Musa juu ya Yusufu ilitimizwa kikweli kuelekea bara hili. “Na Yusufu akamnena, Nchi yake na ibarikiwe na BWANA [Yehova, NW]; kwa vitu vya thamani vya mbinguni, kwa huo umande, . . . na kwa vitu vilivyo bora vya matunda ya jua, na kwa vitu vilivyo bora vya maongeo ya miezi, na kwa vitu viteule vya milima ya kale, na kwa vitu vilivyo bora vya vilima vya milele.” (Kum. 33:13-15) Ndiyo, hii ilikuwa nchi yenye kupendeza. Milima yayo ilikuwa yenye miitu iliyosongamana, mabonde yayo yalikuwa yenye kuzaa sana, na ilikuja kujawa na ufanisi na majiji yenye idadi kubwa za watu. (1 Fal. 12:25; 2 Nya. 15:8) Katika nyakati za baadaye Yesu alihubiri katika bara la Samaria, na ndivyo na wanafunzi wake, na Ukristo ulipata wengi wenye kuunga mkono huko.—Yn. 4:4-10; Mdo. 1:8; 8:1, 14.
C-4 SHEFELA
16. (a) Ni vipi vitambulisho vya Shefela? (b) Wilaya hiyo ilikuwa yenye umaana gani katika nyakati za Biblia?
16 Ingawa jina Shefela humaanisha “Bara la Chini,” kwa kweli hilo ni eneo la vilima-vilima linalofikia mwinuko wa karibu meta 450 katika kisehemu cha upande wa kusini na lapitwa na mabonde mengi-mengi yanayotoka mashariki kwenda magharibi. (2 Nya. 26:10) Lainuka upande wa mashariki wa uwanda wa pwani wa Filistia na ni la kuonwa kuwa bara la chini kwa kulinganishwa tu na vilima vilivyoinuka juu zaidi vya Yuda mbali zaidi upande wa mashariki. (Yos. 12:8) Vilima vyalo, ambavyo vilikuwa vimefunikwa na mierezi, sasa vina mashamba ya mizabibu na mizeituni. (1 Fal. 10:27) Lilikuwa na majiji mengi. Katika historia ya Biblia lilitumika kuwa eneo la kutenganisha Israeli na Wafilisti au majeshi yoyote yenye kuvamia yaliyojaribu kuingia Yuda kutoka upande wa uwanda wa pwani.—2 Fal. 12:17; Oba. 19.
C-5 NCHI YA VILIMA YA YUDA
17. (a) Nchi yenye vilima ya Yuda ilikuwa yenye kuzaa jinsi gani katika nyakati za Biblia, na vipi leo? (b) Ni kwa ajili ya nini Yuda ilifikiriwa kuwa mahali pazuri?
17 Hili ni eneo lililo juu la miamba lenye urefu wa karibu kilometa 80 na lenye kupungua upana wa kilometa 32, likiwa na miinuko yenye kutofautiana tangu meta 600 mpaka 1,000 juu ya usawa wa bahari. Katika nyakati za Biblia eneo hilo lilikuwa limefunikwa na miti, na hasa upande wa magharibi, vilima na mabonde yalijawa na mashamba ya nafaka, mizeituni, na mashamba ya mizabibu. Hii ilikuwa wilaya iliyozaa nafaka nzuri tele, mafuta, na divai kwa ajili ya Israeli. Hasa eneo linalozunguka Yerusalemu limefyekwa sana miti baada ya nyakati za Biblia na kwa hiyo huonekana kuwa lisilozaa kwa kulinganishwa na lilivyokuwa wakati mmoja. Katika majira ya baridi, wakati mwingine theluji huanguka kwenye miinuko mikubwa zaidi ya katikati, kama vile kule Bethlehemu. Katika nyakati za kale Yuda ilionwa kuwa mahali pazuri kwa ajili ya majiji na maboma, na katika nyakati za matata watu wangeweza kukimbilia milima hii wapate usalama.—2 Nya. 27:4.
18. (a) Yerusalemu lilikuwa jiji kuu la Israeli na Yuda wakati gani? (b) Ni zipi baadhi ya sura zenye kupendeza za jiji hilo?
18 Lenye kutokeza katika historia ya Yuda na ya Israeli ni Yerusalemu, lililoitwa pia Sayuni, kufuatia jina la buruji yalo. (Zab. 48:1, 2) Hapo awali lilikuwa jiji la Kikanaani la Yebusi, lililokuwa kwenye ardhi iliyoinuka juu ya makutano ya Bonde la Hinomu na Bonde-Kidroni. Baada ya Daudi kuliteka na kulifanya kuwa jiji kuu, lilipanuliwa kuelekea kaskazini-magharibi, na hatimaye lilienea pia Bonde la Tiropoeni. Muda si muda Bonde la Hinomu likaja kuitwa Gehena. Kwa sababu Wayahudi walitoa dhabihu za kiibada ya sanamu hapo, likajulishwa rasmi kuwa najisi na kugeuzwa kuwa jaa la takataka na maiti za wahalifu waovu kabisa. (2 Fal. 23:10; Yer. 7:31-33) Kwa hiyo, mioto yayo ikawa mfano wa uangamizi kamili. (Mt. 10:28; Mk. 9:47, 48) Yerusalemu lilipata maji machache tu kutoka Kidimbwi cha Siloamu, magharibi mwa Bonde-Kidroni, na Hezekia aliyalinda kwa kujenga ukuta wa nje wa kuyafunika mpaka jijini.—Isa. 22:11; 2 Nya. 32:2-5.
C-6 NYIKA YA YUDA (YESHIMONI)
19. (a) Yeshimoni hufaaje maana ya jina lalo? (b) Ni matukio gani ya Biblia yaliyotokea katika mkoa huo?
19 Yeshimoni ndilo jina la Biblia la Nyika ya Yuda. Lamaanisha “Jangwa.” (1 Sam. 23:19, NW, kielezi-chini) Jinsi jina hilo linavyotoa maana na kufaa! Nyika hiyo ina mitelemko ya mawe-mawe ya upande wa mashariki ya michomozo ya chokaa iliyo mikavu ya vilima vya Yudea, ambavyo hushuka katika mwinuko zaidi ya meta 900 katika kilometa 24 vikaribiapo Bahari ya Chumvi, ambako kuna ukuta wa magenge yaliyochongoka-chongoka. Hakuna majiji yoyote na kuna makao machache katika Yeshimoni. Ni kwenye nyika hii ya Yuda alikotorokea Daudi kutoka kwa Mfalme Sauli, ni kati ya nyika hii na Yordani alikohubiri Yohana Mbatizaji, na ilikuwa katika mkoa huu alikokaa faraghani Yesu alipokuwa amefunga kwa siku 40.b—1 Sam. 23:14; Mt. 3:1; Luka 4:1.
C-7 NEGEBU
20. Eleza juu ya Negebu.
20 Kusini mwa vilima vya Yuda kuna Negebu, ambako wazee wa ukoo Abrahamu na Isaka walikaa kwa miaka mingi. (Mwa. 13:1-3; 24:62) Pia Biblia hurejezea sehemu ya kusini ya eneo hili kuwa “nyika ya Sini.” (Yos. 15:1, NW) Negebu iliyo nusu-jangwa yanyooka kutoka wilaya ya Beer-sheba upande wa kaskazini mpaka Kadesh-barnea upande wa kusini. (Mwa. 21:31; Hes. 13:1-3, 26; 32:8) Bara hilo hushuka toka vilima vya Yuda kwa mfuatano wa miinuko-miinuko, ambayo huanzia mashariki kwenda magharibi, kwa njia ambayo hutoa kizuizi cha asili juu ya upitaji au uvamizi kutoka kusini. Bara hilo hutelemka kutoka vilima upande wa mashariki wa Negebu mpaka kwenye uwanda wa jangwa upande wa magharibi, kando ya pwani ya bahari. Kiangazi hukuta bara hilo likiwa kavu kama jangwa, isipokuwa karibu na baadhi ya mabonde yenye mifuo. Hata hivyo, maji yaweza kupatikana kwa kuchimba kisima. (Mwa. 21:30, 31) Nchi ya Israeli ya ki-siku-hizi inanyunyiza na kusitawisha sehemu-sehemu za Negebu. “Mto wa Misri” ulitia alama ya mpaka wa upande wa kusini-magharibi wa Negebu na pia kuwa sehemu ya mpaka wa upande wa kusini wa Bara Lililoahidiwa.—Mwa. 15:18.
C-8 NYIKA YA PARANI
21. Parani liko wapi, nalo lilitimiza fungu gani katika historia ya Biblia?
21 Kusini mwa Negebu na ikiunganika na Nyika ya Sini ni Nyika ya Parani. Walipoondoka Sinai, Waisraeli walivuka nyika hii wakiwa njiani kwenda kwenye Bara Lililoahidiwa, na ni kutoka Parani kwamba Musa alipeleka wapelelezi 12.—Hes. 12:16–13:3.
D. ILE ARABA KUU (BONDE LA UFA)
22. Kwa kutumia ramani kwenye ukurasa 272 na michoro kwenye ukurasa 273, pamoja na fungu hili, kifupi eleza juu ya sura kuu za ile Araba (Bonde la Ufa) na uhusiano wazo na eneo linalozunguka.
22 Mojawapo maumbo ya bara lisilo la kawaida duniani hii ni Bonde la Ufa lililo kuu. Katika Biblia, sehemu inayokata kupitia Bara Lililoahidiwa kutoka kaskazini mpaka kusini yaitwa “hiyo Araba.” (Yos. 18:18) Katika 2 Samweli 2:29 mpasuko huu katika mwamba wa dunia waelezwa kuwa mtaro mkubwa. Upande walo wa kaskazini kuna Mlima Hermoni. (Yos. 12:1) Kuanzia sehemu ya chini ya Hermoni, Bonde la Ufa hushuka upesi kuelekea kusini kufikia karibu meta 800 chini ya usawa wa bahari kwenye sakafu ya Bahari ya Chumvi. Kutoka ncha ya upande wa kusini ya Bahari ya Chumvi, ile Araba huendelea, ikiinuka kufikia zaidi ya meta 200 juu ya usawa wa bahari karibu na katikati ya Bahari ya Chumvi na Ghuba la ‛Aqaba. Baada ya hapo hushuka haraka sana na kuingia ndani ya maji yenye uvuguvugu ya hori ya mashariki ya Bahari ya Shamu. Ramani za kisehemu kinachofuata zaonyesha uhusiano wa Bonde la Ufa na nchi inayozunguka.
D-1 KIBONDE CHA HULA
23. Mkoa wa Hula ulishirikishwa na nini katika nyakati za Biblia?
23 Likianzia kwenye sehemu ya chini ya Mlima Hermoni, Bonde la Ufa hushuka haraka zaidi ya meta 490 mpaka kwenye mkoa wa Hula, ambao karibu ni wa usawa wa bahari. Wilaya hii ina maji mengi na hudumu yakiwa ya kijani-kibichi cha kupendeza hata wakati wa miezi ya kiangazi chenye joto kali. Wadani walikalia jiji lao la Dani katika eneo hili, jiji lililotumika kuwa kitovu cha ibada ya sanamu tangu wakati wa waamuzi mpaka wakati wa ufalme wa Israeli wa makabila kumi. (Amu. 18:29-31; 2 Fal. 10:29) Ni katika Kaisaria Filipi, mji mmoja karibu na kituo cha Dani la kale, kwamba Yesu alihakikishia wanafunzi wake kwamba yeye alikuwa Kristo, na wengi huamini kwamba ilikuwa karibu na Mlima Hermoni kwamba ule mbadiliko wa sura ulitukia siku sita baadaye. Kutoka Hula, Bonde la Ufa lashuka kuingia Bahari ya Galilaya, ambayo iko karibu meta 210 chini ya usawa wa bahari.—Mt. 16:13-20; 17:1-9.
D-2 MKOA UNAOZUNGUKA BAHARI YA GALILAYA
24. (a) Bahari ya Galilaya huitwa kwa majina gani mengine katika Biblia? (b) Mazingira yayo yalikuwaje katika siku ya Yesu?
24 Bahari ya Galilaya na mazingira yake ni yenye kupendeza.c Upendezi katika mkoa huo wazidishwa kwa sababu ya visa vingi katika huduma ya Yesu vilivyotukia hapo. (Mt. 4:23) Bahari hiyo pia yaitwa Ziwa la Genesareti, au Kinerethi, na Bahari ya Tiberia. (Luka 5:1; Yos. 13:27; Yn. 21:1) Kwa uhalisi hilo ni ziwa lenye umbo la moyo, karibu kilometa 21 kwa urefu na upana wa karibu kilometa 11 kwenye ncha yalo iliyo pana zaidi, nalo ni akiba ya maji iliyo ya muhimu kwa bara lote. Limezingirwa karibu-karibu na vilima kwa karibu kila upande. Sakafu ya ziwa hilo ni karibu meta 210 chini ya usawa wa bahari, hilo likitokeza kipupwe chenye joto-joto la kupendeza, na viangazi virefu sana vyenye joto kali sana. Katika siku za Yesu, lilikuwa kitovu cha biashara ya uvuvi wa samaki iliyositawishwa sana, na majiji yenye kusitawi ya Korazini, Bethsaida, Kapernaumu, na Tiberia yalikuwa kando ya ziwa hilo au karibu nalo. Hali ya utulivu ya ziwa hili yaweza kuvurugwa upesi na tufani. (Luka 8:23) Ule uwanda mdogo wa Genesareti, wenye umbo la pembetatu, uko kwenye upande wa kaskazini-magharibi mwa ziwa hilo. Udongo ni wenye rutuba, ukizaa karibu kila aina ya zao linalojulikana katika Bara Lililoahidiwa. Wakati wa masika mitelemko yenye rangi-rangi nyangavu humeta-meta kwa uangavu usio na kifani kinginecho katika bara la Israeli.d
D-3 WILAYA YA BONDE LA YORDANI (ILE GHORI)
25. Sura kuu za Bonde la Yordani zilikuwa zipi?
25 Bonde hili lenye kushuka linalofanana na mtaro huitwa pia “hiyo Araba.” (Kum. 3:17) Leo Waarabu hulirejezea kuwa Ile Ghori, maana yake “Mshuko-chini.” Bonde hilo huanzia Bahari ya Galilaya na kwa ujumla ni pana—likiwa karibu kilometa 19 kwa upana sehemu fulani-fulani. Mto Yordani wenyewe uko karibu meta 46 chini ya uwanda wa bonde hilo, ukigeuka-geuka na kupinda-pinda katika mwendo wa kilometa 320 umalize kilometa 105 kuingia Bahari ya Chumvi.e Ukipanda na kushuka ngazi-miamba 27, unaanguka karibu meta 180 kufikia wakati unafika Bahari ya Chumvi. Yordani ya chini imepakana na vichaka vya miti na vijiti, hasa mikwaju, oleander, na mivinje, ambamo miongoni mwavyo simba na wana wao walijificha katika nyakati za Biblia. Leo hii yajulikana kuwa Zor na kwa sehemu hufurika maji katika masika. (Yer. 49:19) Yenye kuinuka juu kila upande wa ukanda huu mwembamba ulio kama pori ni Qattara, mpaka usiovutia uhai wa bara la weu lenye nyanda za juu na mitelemko inayokatwa yenye kuongoza mpaka kwenye nyanda za Ile Ghori yenyewe. Nyanda katika sehemu ya kaskazini mwa Ile Ghori, au Araba, zimelimwa vizuri. Hata katika sehemu ya kusini, kuelekea Bahari ya Chumvi (Ufu), mwinuko-tambarare wa Araba, ambao leo ni wenye ukame sana, wakati mmoja husemekana ulizaa tende za aina nyingi, na pia matunda mengine mengi ya tropiki. Yeriko lilikuwa na lingali jiji lijulikanalo zaidi katika Bonde la Yordani.—Yos. 6:2, 20; Mk. 10:46.
D-4 BAHARI YA CHUMVI (UFU)
26. (a) Ni nini baadhi ya mambo ya hakika yenye kutazamisha juu ya Bahari ya Chumvi? (b) Mkoa huo watoa ushuhuda gani wenye kutokeza kuhusu hukumu za Yehova?
26 Hii ni mojawapo ya mkusanyo wa maji wenye kutazamisha juu ya uso wa dunia. Kwa kufaa huitwa ya ufu, kwa maana hakuna samaki wanaoishi ndani ya bahari hiyo na kuna majani machache kando yayo. Biblia huita Bahari ya Chumvi, au Bahari ya Araba, kwa kuwa imo katika bonde la ufa la Araba. (Mwa. 14:3; Yos. 12:3) Bahari hiyo ni karibu kilometa 75 kutoka kaskazini mpaka kusini na kilometa 15 kwa upana. Sakafu yayo ni karibu meta 400 chini ya ile ya Bahari ya Mediterrania, hilo likiifanya kuwa sehemu iliyo chini zaidi duniani. Katika sehemu yayo ya kaskazini, ina kina cha meta 400. Kila upande, bahari hiyo imezungukwa na vilima vyenye ukame na magenge yaliyoinuka sana. Ijapokuwa Mto Yordani huleta maji yasiyo na chumvi, hayana mlango wa kutokea isipokuwa kwa mvukizo, ambao ni wa haraka kama vile mwingizo wa maji. Maji hayo yaliyofungiwa yana karibu asilimia 25 ya mata iliyoyeyushwa, zaidi ikiwa ni chumvi, na ni yenye sumu kwa samaki na huumiza macho ya binadamu. Wageni katika sehemu kubwa inayozunguka Bahari ya Chumvi mara nyingi hujawa na hisia nyingi za ukiwa na uharibifu. Hapo ni mahali pa wafu. Ingawa wakati mmoja mkoa wote huo ulikuwa ‘una maji kama bustani ya Yehova,’ eneo linalozunguka Bahari ya Chumvi sasa kwa sehemu kubwa ni “ukiwa” na limekuwa hivyo kwa karibu miaka 4,000, hilo likiwa ni ushuhuda wenye kutokeza wa kutogeuka-geuka kwa hukumu za Yehova zilizotekelezwa huko juu ya Sodoma na Gomora.—Mwa. 13:10; 19:27-29; Sef. 2:9.
D-5 ARABA (KUSINI MWA BAHARI YA CHUMVI)
27. Ni eneo la aina gani lifanyizalo Araba ya upande wa kusini, na ni nani aliyetawala katika nyakati za kale?
27 Sehemu hii ya mwisho ya Bonde la Ufa huelekea kusini kwa kilometa 160 nyingine. Kwa ujumla mkoa huu ni jangwa. Mvua ni haba, na jua huchoma vikali. Pia Biblia huliita hili “hiyo Araba.” (Kum. 2:8) Karibu na katikati, hufikia kipeo chalo cha juu zaidi cha karibu meta 200 juu ya usawa wa bahari na kisha hushuka kuelekea kusini tena kwenye Ghuba la ‛Aqaba, ncha ya mashariki ya Bahari ya Shamu. Ni hapa, kwenye bandari ya Ezion-geberi, kwamba Sulemani alijenga meli kadhaa. (1 Fal. 9:26) Kwa kipindi kikubwa cha wafalme wa Yuda, sehemu hii ya Araba ilikuwa chini ya utawala wa ufalme wa Edomu.
E. MILIMA NA MABARA-MIINUKO-TAMBARARE MASHARIKI MWA YORDANI
28. Mabara ya Bashani na Gileadi yamekuwa yenye ubora gani kwa habari ya kilimo, na mikoa hiyo ilihusikaje katika historia ya Biblia?
28 “Ng’ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki” huinuka upesi kutoka Bonde la Ufa na kufanyiza mfululizo wa mabara-miinuko-tambarare. (Yos. 18:7; 13:9-12; 20:8) Upande wa kaskazini kuna bara la Bashani (E-1), ambalo, pamoja na nusu ya Gileadi, lilipewa kabila la Manase. (Yos. 13:29-31) Hii ilikuwa nchi ya mifugo ya ng’ombe, bara la wakulima, mwinuko-tambarare wenye rutuba wa karibu meta 600 juu ya usawa wa bahari. (Zab. 22:12; Eze. 39:18; Isa. 2:13; Zek. 11:2) Katika siku ya Yesu eneo hili liliuzia nchi za nje nafaka nyingi, na leo ni lenye kuzaa kwa habari ya kilimo. Kando yalo, upande wa kusini, kuna bara la Gileadi (E-2), nusu ya chini yalo liligawiwa kabila la Gadi. (Yos. 13:24, 25) Mkoa wenye milima-milima unaofikia meta 1,000, ukiwa unapata maji kutokana na mvua nyingi wakati wa baridi na umande mwingi wakati wa kiangazi, pia ilikuwa nchi nzuri ya mifugo na ilijulikana sana hasa kwa zeri yayo. Leo inajulikana kwa zabibu zayo tamutamu. (Hes. 32:1; Mwa. 37:25; Yer. 46:11) Bara la Gileadi ndilo ambalo Daudi alikimbilia kutoka kwa Absalomu, na katika sehemu ya magharibi, Yesu alihubiri katika “mipaka ya Dekapoli.”—2 Sam. 17:26-29; Mk. 7:31.
29. Upande wa mashariki wa Yordani, ni mabara gani yaliyokuwako kuelekea kusini, nayo yalijulikana kwa ajili ya nini?
29 “Nchi ya wana wa Amoni” (E-3) imepakana karibu na kusini mwa Gileadi, na nusu yayo lilipewa kabila la Gadi. (Yos. 13:24, 25; Amu. 11:12-28) Hiyo ni bara-mwinuko-tambarare lenye kusambaa, ambalo lafaa zaidi kwa ulishaji wa kondoo. (Eze. 25:5) Na bado kuelekea kusini zaidi kuna “nchi ya Moabu.” (Kum. 1:5) Wamoabi wenyewe walikuwa wachungaji-kondoo hodari, na mpaka leo uchungaji wa kondoo ndio kazi kuu ya eneo hilo. (2 Fal. 3:4) Kisha, kusini-mashariki mwa Bahari ya Chumvi, twaja kwenye mwinuko-tambarare wa mlima wa Edomu (E-4). Mabomoko ya ngome zayo kubwa za biashara, kama vile Petra, yangaliko mpaka leo.—Mwa. 36:19-21; Oba. 1-4.
30. Mabara-Miinuko-Tambarare yamepakana na nini upande wa mashariki?
30 Upande wa mashariki wa vilima na mabara-miinuko-tambarare hayo kuna nyika kubwa ya miamba ambayo ilizuia kabisa usafiri wa moja kwa moja kati ya Bara Lililoahidiwa na Mesopotamia, ikisababisha njia za misafara zizunguke kilometa nyingi kuelekea kaskazini. Upande wa kusini nyika hii hukutana na matuta ya mchanga ya jangwa kuu la Uarabu.
F. MILIMA YA LEBANONI
31. (a) Ni nini hufanyiza milima ya Lebanoni? (b) Ni sura zipi za Lebanoni zingalivyo kama zilivyokuwa katika nyakati za Biblia?
31 Yenye kutokeza kwenye sura ya Bara Lililoahidiwa ni milima ya Lebanoni. Kwa kweli kuna mifululizo-milima miwili yenye kunyooka mmoja kando ya mwingine. Sehemu za chini za Mfululizo-Mlima-Lebanoni wenyewe huendelea na kuingia Galilaya ya Juu. Katika sehemu nyingi vilima hivi huteteremka mpaka kwenye mwambao. Kilele kirefu zaidi katika mfululizo huo wa vilima ni karibu meta 3,000 juu ya usawa wa bahari. Kilele cha juu zaidi katika Mfululizo-Mlima-Anti-Lebanoni ni Mlima Hermoni wenye kupendeza ulio jirani, ambao unainuka meta 2,814 juu ya usawa wa bahari. Theluji yao yenye kuyeyuka hufanyiza chanzo kikubwa cha maji kwa Mto Yordani na chanzo cha umande wakati wa kipindi cha ukame cha mwisho wa masika. (Zab. 133:3) Milima ya Lebanoni ilijulikana hasa kwa ajili ya mierezi yayo mikubwa mno, mbao zayo zikiwa zilitumiwa katika ujenzi wa hekalu la Sulemani. (1 Fal. 5:6-10) Ingawa ni misitu michache tu ya mierezi inayosalia leo, mitelemko ya chini ingali ina mashamba ya mizabibu, mashamba ya mizeituni, na mashamba ya matunda, kama ilivyokuwa katika nyakati za Biblia.—Hos. 14:5-7.
32. Musa alielezaje kwa usahihi juu ya Bara Lililoahidiwa?
32 Tumaliziapo hivyo ziara yetu kwenye Bara Lililoahidiwa la Yehova, lililopachikwa kama ilivyo kati ya nyika ya kutisha upande wa mashariki na Bahari Kuu, twaweza kufanyiza picha ya kiakili juu ya utukufu ambao wakati mmoja ulilivika katika siku za Israeli. Kweli kweli, ilikuwa “nchi njema mno ya ajabu . . . , yenye wingi wa maziwa na asali.” (Hes. 14:7, 8; 13:23) Musa aliirejezea kwa maneno haya: “BWANA [Yehova, NW], Mungu wako, yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na vilima; nchi ya ngano na shayiri, na mizabibu, na mitini, na mikomamanga; nchi ya mizeituni yenye mafuta, na asali; nchi utakayokula mikate humo, pasina shida, hutapungukiwa na kitu ndani yake; nchi ambayo mawe yake ni chuma, na milima yake yafukuka shaba. Nawe utakula ushibe, utamshukuru BWANA [Yehova, NW], Mungu wako, kwa nchi nzuri aliyokupa.” (Kum. 8:7-10) Vilevile wote wanaopenda Yehova sasa na watoe shukrani kwamba yeye akusudia kufanya dunia yote paradiso tukufu, kufuatisha kigezo cha hilo Bara Lililoahidiwa lake la kale.—Zab. 104:10-24.
[Maelezo ya Chini]
a Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 332-3.
b Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 335.
c Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 336.
d Insight on the Scriptures, Buku 2, kurasa 737-40.
e Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 334.
[Ramani katika ukurasa wa 272]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MAENEO YA ASILI YA BARA LILILOAHIDIWA
(na eneo la viungani)
MI 0 10 20 30 40 50 60
KM 0 20 40 60 80
(Kwa sehemu-mkato V—V, W—W, X—X, Y—Y, na Z—Z, ona ukurasa unaoangaliana na huu)
UFUNGUO WA NAMBA
A Pwani ya ile Bahari Kuu
Yopa
B-1 Uwanda wa Asheri
B-2 Ukanda wa Pwani wa Dori
Dori
B-3 Malisho ya Sharoni
B-4 Uwanda wa Ufilisti
Ashdodi
Ashkeloni
Ekroni
Gathi
Gaza
B-5 Bonde la Kati la Mashariki-Magharibi (Uwanda wa Megido, Uwanda wa
Chini wa Yezreeli)
Beth-sheani
C-1 Vilima vya Galilaya
Naini
Nazarethi
Tiro
C-2 Vilima vya Karmeli
C-3 Vilima vya Samaria
Betheli
Yeriko
Samaria
Tirza
Shekemu
C-4 Shefela
Lakishi
C-5 Nchi ya Vilima ya Yuda
Bethlehemu
Geba
Hebroni
Yerusalemu
C-6 Nyika ya Yuda (Yeshimoni)
C-7 Negebu
Beer-sheba
Kadesh-barnea
Mto wa Misri
C-8 Nyika ya Parani
D-1 Kibonde cha Hula
Dani
Kaisaria Filipi
D-2 Mkoa Unaozunguka Bahari ya Galilaya
Bethsaida
Kapernaumu
Korazini
Bahari ya Galilaya
Tiberia
D-3 Wilaya ya Bonde la Yordani (Ile Ghori)
Mto Yordani
D-4 Bahari ya Chumvi (Ufu)
(Bahari ya ile Araba)
Bahari ya Chumvi
D-5 Araba (upande wa kusini kutoka Bahari ya Chumvi)
Ezion-geberi
Bahari ya Shamu
E-1 Bara la Bashani
Dameski
Edrei
E-2 Bara la Gileadi
Raba
Ramoth-gileadi
Mfo wa Bonde la Yaboki
E-3 Bara la Amoni na la Moabu
Heshboni
Kir-haresethi
Medeba
Mfo wa Bonde la Arnoni
Mfo wa Bonde la Zeredi
E-4 Mlima Mwinuko-Tambarare wa Edomu
Petra
F Milima ya Lebanoni
Sidoni
Ml. Lebanoni
Ml. Hermoni
[Ramani katika ukurasa wa 273]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)