Mathayo
14 Kwenye wakati maalumu huo Herode, mtawala wa wilaya, akasikia ripoti juu ya Yesu 2 na kuwaambia watumishi wake: “Huyu ndiye Yohana Mbatizaji. Yeye alifufuliwa kutoka kwa wafu, na hii ndiyo sababu kazi zenye nguvu zinatenda ndani yake.” 3 Kwa maana Herode alikuwa amemkamata Yohana na kumfunga na kumweka mbali gerezani kwa sababu ya Herodiasi mke wa Filipo ndugu yake. 4 Kwa maana Yohana alikuwa amekuwa akimwambia: “Hairuhusiki kisheria wewe kuwa na mwanamke huyo.” 5 Hata hivyo, ijapokuwa alitaka kumuua, aliuhofu umati, kwa sababu ulimchukua yeye kuwa nabii. 6 Lakini siku ya kuzaliwa kwa Herode ilipokuwa ikisherehekewa binti ya Herodiasi aliichezea dansi na kumpendeza Herode sana 7 hivi kwamba akaahidi kwa kiapo kumpa chochote kile ambacho angeomba. 8 Ndipo yeye, chini ya mwelekezo wa mama yake, akasema: “Nipe hapa juu ya sinia kichwa cha Yohana Mbatizaji.” 9 Ajapokuwa na kihoro, mfalme kwa kufikiria viapo vyake na kwa ajili ya wale wenye kuegama pamoja naye akaamuru apewe hicho; 10 naye akatuma na kufanya Yohana akatwe kichwa gerezani. 11 Na kichwa chake kikaletwa juu ya sinia na kupewa kwa yule mwanamwali, naye akakileta kwa mama yake. 12 Mwishowe wanafunzi wake wakaja na kuiondoa maiti na kumzika nao wakaja na kuripoti kwa Yesu. 13 Aliposikia hilo Yesu akaondoka hapo kwa mashua kwenda katika mahali pa upweke ili kuwa peke yake; lakini umati, ukipata kusikia juu ya hilo, ukamfuata kwa miguu kutoka kwenye majiji.
14 Basi alipotokea akaona umati mkubwa; naye akahisi sikitiko kwa ajili yao, naye akaponya wagonjwa wao. 15 Lakini ilipokuwa jioni wanafunzi wake wakamjia na kusema: “Hapa mahali pako upweke na saa tayari imesonga sana; acha umati uende zao, ili upate kwenda kuingia katika vijiji na kujinunulia wenyewe vitu vya kula.” 16 Hata hivyo, Yesu akawaambia: “Haiwabidi kuondoka: Nyinyi wapeni kitu cha kula.” 17 Wakamwambia: “Hatuna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili.” 18 Yeye akasema: “Vileteni hapa kwangu.” 19 Halafu akauamuru umati uegame juu ya nyasi naye akachukua ile mikate mitano na samaki wawili, na, akitazama juu mbinguni, akasema baraka na, baada ya kuimega ile mikate, akaigawa kwa wanafunzi, nao wanafunzi wakaigawa kwa ule umati. 20 Kwa hiyo wote wakala na kushiba, nao wakaokota ziada ya vipande vidogo, vikapu kumi na viwili vyenye kujaa. 21 Na bado wale wenye kula walikuwa wanaume karibu elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto wachanga. 22 Ndipo, bila kukawia, akawashurutisha wanafunzi wake kuipanda mashua na kwenda mbele yake upande ule mwingine, huku yeye akiacha umati uende zao.
23 Mwishowe, akiisha kuacha umati uende zao, yeye akapanda kwenda katika mlima akiwa peke yake mwenyewe ili kusali. Ingawa ilikuwa jioni-jioni, alikuwa huko peke yake. 24 Kufikia sasa mashua ilikuwa mamia mengi ya meta mbali na nchi kavu, ikitaabishwa sana na mawimbi, kwa sababu upepo ulikuwa dhidi yao. 25 Lakini katika kipindi cha lindo la nne la usiku akawajia, akitembea juu ya bahari. 26 Walipoona mara hiyo akitembea juu ya bahari, wanafunzi walihangaika, wakisema: “Ni mzuka!” Nao wakapaaza kilio katika hofu yao. 27 Lakini mara moja Yesu akasema nao kwa maneno haya: “Jipeni moyo, ni mimi; msiwe na hofu.” 28 Kwa kujibu Petro akamwambia: “Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nikujie wewe juu ya maji.” 29 Yeye akasema: “Njoo!” Mara Petro, akishuka kutoka kwenye mashua, akatembea juu ya maji na kwenda kumwelekea Yesu. 30 Lakini akitazama ile dhoruba ya upepo, akaogopa na, baada ya kuanza kuzama, akapaaza kilio: “Bwana, niokoe!” 31 Mara akinyoosha mkono wake Yesu akamshika na kumwambia: “Wewe mwenye imani kidogo, kwa nini ukashindwa na shaka?” 32 Na baada ya wao kupanda katika mashua, dhoruba ya upepo ikapunguka. 33 Ndipo wale waliokuwamo katika mashua wakamsujudia, wakisema: “Wewe kwa kweli ni Mwana wa Mungu.” 34 Nao wakavuka na kuja kwenye nchi kavu katika Genesareti.
35 Walipomtambua yeye wanaume wa mahali hapo wakapeleka habari katika nchi yote hiyo yenye kuzingira, na watu wakamletea wote wale waliokuwa wagonjwa. 36 Nao wakaanza kumsihi sana ili wapate kugusa tu upindo wenye matamvua wa vazi lake la nje; na wote wale waliougusa wakaponywa kabisa.