Marko
6 Naye akaondoka kutoka huko na kuja kuingia katika eneo lake la nyumbani, na wanafunzi wake wakamfuata. 2 Ilipokuwa siku ya sabato, akaanza kufundisha katika sinagogi; na idadi kubwa zaidi ya wale waliokuwa wakisikiliza wakastaajabu na kusema: “Mtu huyu alipata wapi mambo haya? Na kwa nini hekima hii ingalipasa kupewa kwa mtu huyu, na kazi zenye nguvu namna hiyo kufanywa kupitia mikono yake? 3 Je, huyu si seremala mwana wa Maria na ndugu ya Yakobo na Yosefu na Yudasi na Simoni? Na dada zake wapo hapa pamoja nasi, sivyo?” Kwa hiyo wakaanza kukwazika juu yake. 4 Lakini Yesu akaendelea kuwaambia: “Nabii hakosi kuheshimiwa ila katika eneo lake la nyumbani na miongoni mwa jamaa zake na katika nyumba yake mwenyewe.” 5 Kwa hiyo alikuwa hawezi kufanya kazi zenye nguvu huko ila kuweka mikono yake juu ya wagonjwa-wagonjwa wachache na kuwaponya. 6 Kwa kweli, alistaajabia ukosefu wao wa imani. Naye akaenda akizunguka huku na huku vijijini katika mzunguko, akifundisha.
7 Sasa akawaita wale kumi na wawili, naye akaanzisha kuwatuma wawili-wawili, naye akaanza kuwapa mamlaka juu ya roho wasio safi. 8 Pia, akawapa maagizo kutochukua kitu chochote kwa ajili ya safari, wala mkate, wala mfuko wa chakula, wala sarafu ya shaba katika vifuko vyao vya mshipini ila fimbo tu, 9 lakini wafunge makubazi, na kutovaa mavazi ya ndani mawili. 10 Zaidi, akawaambia: “Popote pale mwingiapo katika nyumba, kaeni hapo mpaka mtakapoenda kutoka mahali hapo. 11 Na mahali fulani popote ambapo hapatawapokea wala kuwasikia, mnapoenda kutoka hapo yakung’uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu ili kuwa ushahidi kwao.” 12 Kwa hiyo wakaondoka na kuhubiri ili watu wapate kutubu; 13 nao walikuwa wakitoa roho waovu wengi na kupaka mafuta watu wengi wagonjwa-wagonjwa na kuwaponya.
14 Basi ikafika masikioni mwa Mfalme Herode, kwa maana jina la Yesu lilipata kujulikana na watu wote, na watu walikuwa wakisema: “Yohana mbatizaji amefufuliwa kutoka kwa wafu, na kwa sababu hiyo kazi zenye nguvu zinatenda ndani yake.” 15 Lakini wengine walikuwa wakisema: “Ni Eliya.” Bado wengine walikuwa wakisema: “Ni nabii kama mmoja wa manabii.” 16 Lakini Herode aliposikia hilo akaanza kusema: “Yohana ambaye nilimkata kichwa, ndiye huyo amefufuliwa.” 17 Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu na kumkamata Yohana akamfunga gerezani kwa sababu ya Herodiasi mke wa Filipo ndugu yake, kwa sababu Herode alikuwa amemwoa. 18 Kwa maana Yohana alikuwa amemwambia Herode kwa kurudia-rudia: “Hairuhusiki kisheria wewe kuwa na mke wa ndugu yako.” 19 Lakini Herodiasi alikuwa akifungia moyoni kinyongo dhidi yake na alikuwa akitaka kumuua, lakini hakuweza. 20 Kwa maana Herode alikuwa akimhofu Yohana, akimjua kuwa mtu mwadilifu na mtakatifu; naye alikuwa akimtunza salama. Na baada ya kumsikia akawa hajui kabisa la kufanya, lakini aliendelea kumsikia kwa mteremo.
21 Lakini siku fulani ifaayo ikafika wakati Herode alipoandaa mlo wa jioni kwenye siku ya kuzaliwa kwake kwa ajili ya wenye daraja la juu na makamanda wake wa kijeshi na walio wa cheo cha kwanza kabisa wa Galilaya. 22 Na binti ya huyuhuyu Herodiasi akaingia akacheza dansi na kumpendeza Herode na wale wenye kuegama pamoja naye. Mfalme akamwambia mwanamwali: “Uniombe mimi chochote kile utakacho, nami hakika nitakupa hicho.” 23 Ndiyo, akaapa kwake: “Chochote kile uniombacho, hakika nitakupa hicho, mpaka nusu ya ufalme wangu.” 24 Naye akatoka kwenda akamwambia mama yake: “Niombe nini?” Yeye akamwambia: “Kichwa cha Yohana mbatizaji.” 25 Mara akaingia kwa hima hadi aliko mfalme na kutoa ombi lake, akisema: “Nataka unipe saa hiihii juu ya sinia kichwa cha Yohana Mbatizaji.” 26 Ijapokuwa mfalme alikuwa mwenye kutiwa kihoro sana, lakini hakutaka kukosa kumstahi, kwa kufikiria vile viapo na wale wenye kuegama kwenye meza. 27 Kwa hiyo mara mfalme akatuma mlinzi wa mfalme na kumwamuru alete kichwa chake. Naye akaenda akamkata kichwa gerezani 28 akaleta kichwa chake juu ya sinia, naye akampa yule mwanamwali, na huyo mwanamwali akampa mama yake. 29 Wanafunzi wake waliposikia juu ya hilo wakaja wakachukua maiti yake na kuilaza katika kaburi la ukumbusho.
30 Nao mitume wakakusanyika pamoja mbele ya Yesu na kuripoti kwake mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha. 31 Naye akawaambia: “Njoni, nyinyi wenyewe, kwa faragha mwingie katika mahali pa upweke mpumzike kidogo.” Kwa maana kulikuwa na wengi wakija na kwenda, nao hawakuwa hata na wasaa wa kula mlo. 32 Kwa hiyo wakaenda zao wakiwa katika mashua wakawe mahali pa upweke peke yao wenyewe. 33 Lakini watu wakawaona wakienda na wengi wakapata kujua hilo, na kutoka katika majiji yote wakakimbia kwenda huko pamoja kwa miguu na kufika mbele yao. 34 Basi, aliposhuka, akaona umati mkubwa, lakini akasukumwa na sikitiko kwa ajili yao, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji. Naye akaanza kuwafundisha mambo mengi.
35 Kufikia sasa saa ilikuwa imesonga sana, na wanafunzi wake wakamjia na kuanza kusema: “Mahali hapa ni pa upweke, na saa tayari imesonga sana. 36 Waache waende zao, ili wapate kwenda zao kuingia mashambani na vijiji vyenye kuzunguka wajinunulie wenyewe kitu cha kula.” 37 Kwa kujibu akawaambia: “Nyinyi wapeni kitu cha kula.” Ndipo wakamwambia: “Je, tutakwenda zetu na kununua mikate yenye thamani ya dinari mia mbili na kuwapa watu hiyo ili wale?” 38 Akawaambia: “Mna mikate mingapi? Nendeni mkaone!” Baada ya kuhakikisha hilo, wakasema: “Mitano, mbali na kuwa na samaki wawili.” 39 Naye akawaagiza watu wote waegame wakiwa vikundi-vikundi juu ya zile nyasi za kijani kibichi. 40 Nao wakajilaza wenyewe chini katika vikundi vya mia na vya hamsini. 41 Sasa akichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili akatazama juu mbinguni akasema baraka, akaimega ile mikate na kuanza kuwapa wanafunzi, ili hao wapate kuiweka mbele ya hao watu; naye akagawanya wale samaki wawili kwa ajili ya wote. 42 Kwa hiyo wote wakala wakashiba; 43 nao wakaokota vipande vidogo, vikapu kumi na viwili vyenye kujaa, mbali na wale samaki. 44 Zaidi ya hilo, wale waliokula kutokana na ile mikate walikuwa wanaume elfu tano.
45 Na, bila kukawia, akawashurutisha wanafunzi wake kuipanda mashua na kuendelea mbele hadi ukingo wa pili kuelekea Bethsaida, huku yeye mwenyewe akiuruhusu umati uende. 46 Lakini baada ya kuwaambia kwaheri akaenda zake kuingia mlimani ili asali. 47 Sasa kulipokuwa jioni, mashua ilikuwa katikati ya bahari, lakini yeye alikuwa peke yake juu ya nchi kavu. 48 Na alipowaona wakitaabishwa sana katika kuvuta kwao makasia, kwa maana upepo ulikuwa dhidi yao, karibu lindo la nne la usiku akaja kuwaelekea, akitembea juu ya bahari; lakini alikuwa na mwelekeo wa kuwapita kando. 49 Walipomwona mara hiyo akitembea juu ya bahari wakafikiri: “Ni mzuka!” nao wakalia kwa sauti kubwa. 50 Kwa maana wote walimwona na walikuwa wenye kutaabishwa. Lakini mara hiyo akasema nao, naye akawaambia: “Jipeni moyo, ni mimi; msiwe na hofu.” 51 Naye akapanda kuingia katika mashua pamoja nao, na upepo ukapunguka. Ndipo wakashangaa sana ndani yao wenyewe, 52 kwa maana hawakuwa wamefahamu maana ya ile mikate, bali mioyo yao iliendelea kuwa mizito bila kuelewa.
53 Na walipovuka hadi nchi kavu, wakaja kuingia Genesareti na kutia meli nanga hapo karibu. 54 Lakini mara tu waliposhuka kutoka katika mashua, watu wakamtambua yeye, 55 nao wakakimbia kuzunguka mkoa wote huo na kuanza kuwachukua huku na huku juu ya vitanda wale waliokuwa wakiugua hadi kule walikosikia alikuwako. 56 Na kokote alikokuwa akiingia vijijini au majijini au mashambani walikuwa wakiweka wale wagonjwa katika mahali pa masoko, nao walikuwa wakiomba ili wapate kuugusa tu upindo wenye matamvua wa vazi lake la nje. Na wengi kadiri walivyougusa wakaponywa.