Luka
7 Alipokuwa amekwisha kutimiliza semi zake zote na watu wakasikia, yeye akaingia Kapernaumu. 2 Sasa mtumwa wa ofisa-jeshi mmoja, aliyemthamini sana, alikuwa anaugua na alikuwa karibu kufa. 3 Aliposikia juu ya Yesu, akatuma kwake wanaume wazee wa Wayahudi kumwomba aje na kumleta mtumwa wake akiwa salama. 4 Ndipo wale waliomjia Yesu wakaanza kumsihi sana kwa bidii, wakisema: “Yeye astahili wewe kumjalia hili, 5 kwa maana apenda taifa letu naye mwenyewe alitujengea sinagogi.” 6 Kwa hiyo Yesu akaanza mwendo pamoja nao. Lakini alipokuwa hayuko mbali na hiyo nyumba, yule ofisa-jeshi alikuwa tayari ametuma marafiki wamwambie: “Bwana, usijisumbue, kwa maana mimi sistahili wewe kuingia chini ya paa yangu. 7 Kwa sababu hiyo sikujifikiria kustahili mimi mwenyewe kuja kwako. Lakini liseme neno, na acha mtumishi wangu aponywe. 8 Kwa maana mimi pia ni mtu aliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari-jeshi chini yangu, nami humwambia huyu, ‘Shika njia yako uende!’ naye hushika njia yake na kwenda, na kwa mwingine, ‘Njoo!’ naye huja, na kwa mtumwa wangu, ‘Fanya hili!’ naye hulifanya.” 9 Basi, Yesu aliposikia mambo hayo alimstaajabia, naye akageukia umati uliomfuata na kusema: “Mimi nawaambia nyinyi, Hata katika Israeli sijapata imani kubwa sana kadiri hii.” 10 Na wale waliokuwa wametumwa, waliporudi nyumbani, wakamkuta huyo mtumwa akiwa katika afya njema.
11 Muda mfupi kufuatia hilo akasafiri hadi jiji liitwalo Naini, na wanafunzi wake na umati mkubwa walikuwa wakisafiri pamoja naye. 12 Alipokaribia lango la jiji, kumbe! tazama! kulikuwa na mfu akiwa anapelekwa nje, mwana mzaliwa-pekee wa mama yake. Mbali na hilo, alikuwa ni mjane. Pia umati mkubwa kutoka kwenye jiji ulikuwa pamoja naye. 13 Na Bwana alipomwona mara hiyo akasukumwa na sikitiko kwa ajili yake, naye akamwambia: “Koma kutoa machozi.” 14 Ndipo akakaribia na kuligusa jeneza, na wachukuzi wakasimama tuli, naye akasema: “Mwanamume kijana, nakuambia, Inuka!” 15 Na huyo mfu akaketi na kuanza kusema, naye akampa huyo kwa mama yake. 16 Basi hofu ikawashika wote, nao wakaanza kumtukuza Mungu, wakisema: “Nabii mkubwa ameinuliwa miongoni mwetu,” na, “Mungu ameelekeza uangalifu wake kwa watu wake.” 17 Na habari hii kumhusu ikasambaa katika Yudea yote na nchi yote yenye kuzunguka.
18 Sasa wanafunzi wa Yohana wakaripoti kwake juu ya mambo yote haya. 19 Kwa hiyo Yohana akawaita wawili kati ya wanafunzi wake na kuwatuma kwa Bwana kusema: “Je, wewe ndiwe Yule Anayekuja au je, twapaswa kutarajia aliye tofauti?” 20 Walipokuja kwake hao wanaume wakasema: “Yohana Mbatizaji alitutuma kwako kusema: ‘Wewe ndiwe Yule Anayekuja au je, twapaswa kutarajia mwingine?’” 21 Katika saa hiyo akaponya wengi magonjwa na maradhi yenye kutia kihoro na roho waovu, na kuwapa vipofu wengi upendeleo wa kuona. 22 Kwa sababu hiyo kwa kujibu akawaambia hao wawili: “Shikeni njia yenu mwende, ripotini kwa Yohana yale mliyoona na kusikia: vipofu wanapata kuona, vilema wanatembea, wenye ukoma wanasafishwa na viziwi wanasikia, na wafu wanafufuliwa, maskini wanaambiwa ile habari njema. 23 Na mwenye furaha ni yeye ambaye hakukwazika juu yangu.”
24 Wajumbe wa Yohana walipokuwa wamekwenda zao, akaanza kuuambia umati kuhusu Yohana: “Mlitoka kwenda katika nyika kuona nini? Tete likitikiswa na upepo? 25 Basi, ni nini mlichotoka kwenda kuona? Mtu aliyevaa mavazi ya nje mororo? Kwani! wale wenye kuvaa vazi maridadi na wenye kuwa katika anasa wamo katika nyumba za kifalme. 26 Basi, kwa kweli mlichotoka kwenda kuona ni nini? Nabii? Ndiyo, mimi nawaambia nyinyi, na ni zaidi sana kuliko nabii. 27 Huyu ndiye ambaye kuhusu yeye imeandikwa, ‘Tazama! Mimi ninatuma mjumbe wangu mbele ya uso wako, ambaye atatayarisha njia yako mbele yako.’ 28 Nawaambia nyinyi, Miongoni mwa wale waliozaliwa na wanawake hakuna hata mmoja aliye mkubwa zaidi kuliko Yohana; lakini mtu ambaye ni mdogo zaidi katika ufalme wa Mungu ni mkubwa zaidi kuliko yeye.” 29 (Na watu wote na wakusanya-kodi, waliposikia hili, wakamtangaza Mungu kuwa mwadilifu, wao wakiwa wamekwisha kubatizwa kwa ubatizo wa Yohana. 30 Lakini Mafarisayo na wale wenye kuijua sana Sheria walikosa kustahi shauri la Mungu kwao, kwa kuwa hawakuwa wamebatizwa naye.)
31 “Basi, mimi nitalinganisha watu wa kizazi hiki na nani, nao ni kama nani? 32 Wao ni kama watoto wachanga ambao wameketi katika mahali pa soko na kupaaziana kilio, na ambao wasema, ‘Tuliwapigia nyinyi filimbi, lakini hamkucheza dansi; tulitoa sauti za kuomboleza, lakini hamkutoa machozi.’ 33 Kwa kulingana na hilo, Yohana Mbatizaji amekuja akiwa hali mkate wala kunywa divai, lakini mwasema, ‘Ana roho mwovu.’ 34 Mwana wa binadamu amekuja akila na kunywa, lakini mwasema, ‘Tazama! Mtu aliye mlafi na mwenye tabia ya kunywa divai, rafiki ya wakusanya-kodi na watenda-dhambi!’ 35 Hata hivyo, hekima huthibitishwa kuwa yenye uadilifu kwa watoto wayo wote.”
36 Basi mtu mmoja wa Mafarisayo alifuliza kumwomba ili ale mlo-mkuu pamoja naye. Basi akaingia katika nyumba ya huyo Farisayo na kuegama kwenye meza. 37 Na, tazama! mwanamke aliyejulikana katika jiji kuwa mtenda-dhambi akapata habari kwamba alikuwa akiegama kwenye mlo katika nyumba ya Farisayo, naye akaleta chupa ya alabasta iliyo na mafuta yenye marashi, 38 na, akichukua kikao nyuma kwenye miguu yake, akatoa machozi na kuanza kulowesha miguu yake kwa machozi yake naye akawa akiyafuta kwa nywele za kichwa chake. Pia, alibusu miguu yake kwa wororo na kuipaka mafuta yenye marashi. 39 Kwa kuona hayo yule Farisayo aliyemwalika akajisemea ndani yake mwenyewe: “Mtu huyu, kama angekuwa ni nabii, angejua ni nani na ni wa aina gani mwanamke anayemgusa, kwamba ni mtenda-dhambi.” 40 Lakini kwa kujibu Yesu akamwambia: “Simoni, nina jambo fulani la kukuambia.” Akasema: “Mwalimu, liseme!”
41 “Watu wawili walikuwa wadeni kwa mkopeshaji fulani; mmoja alikuwa na deni la dinari mia tano, lakini yule mwingine la hamsini. 42 Walipokuwa hawana kitu chochote cha kulipa, aliwasamehe kwa hiari wote wawili. Kwa hiyo, ni yupi kati yao atampenda zaidi?” 43 Kwa kujibu Simoni akasema: “Nadhani ni yeye ambaye alimsamehe kwa hiari zilizo nyingi zaidi.” Akamwambia: “Ulihukumu kwa usahihi.” 44 Ndipo akamgeukia huyo mwanamke na kumwambia Simoni: “Wamwona mwanamke huyu? Niliingia katika nyumba yako; wewe hukunipa maji kwa ajili ya miguu yangu. Lakini mwanamke huyu alilowesha miguu yangu kwa machozi yake na kuyafuta kwa nywele zake. 45 Wewe hukunipa busu yoyote; lakini mwanamke huyu, tangu ile saa nilipoingia, hakuacha kubusu miguu yangu kwa wororo. 46 Wewe hukupaka kichwa changu mafuta; lakini mwanamke huyu alipaka miguu yangu mafuta yenye marashi. 47 Kwa msingi huu, mimi nakuambia wewe, dhambi zake, ingawa ni nyingi, zimesamehewa, kwa sababu alipenda sana; lakini yeye ambaye asamehewa kidogo, hupenda kidogo.” 48 Ndipo akamwambia huyo mwanamke: “Dhambi zako zimesamehewa.” 49 Ndipo wale wenye kuegama kwenye meza pamoja naye wakaanza kujisemea ndani yao wenyewe: “Ni nani mtu huyu ambaye hata husamehe dhambi?” 50 Lakini akamwambia yule mwanamke: “Imani yako imekuokoa; shika njia yako uende kwa amani.”