Yohana
Kulingana na Yohana
1 Hapo mwanzoni Neno alikuwako, na Neno alikuwa pamoja na Mungu, na Neno alikuwa mungu. 2 Huyo alikuwa hapo mwanzoni pamoja na Mungu. 3 Vitu vyote vilikuja kuwako kupitia yeye, na bila yeye hata kitu kimoja hakikuja kuwako.
Kile ambacho kimekuja kuwako 4 kupitia kwake kilikuwa uhai, na uhai ulikuwa ndio nuru ya watu. 5 Na nuru inang’aa katika giza, lakini giza halikuizidi nguvu.
6 Kulitokea mtu aliyetumwa awe mwakilishi wa Mungu: jina lake lilikuwa Yohana. 7 Mtu huyu alikuja kwa ajili ya ushahidi, kusudi atoe ushahidi juu ya nuru, ili watu wa namna zote wapate kuamini kupitia yeye. 8 Yeye hakuwa nuru hiyo, bali alikusudiwa atoe ushahidi juu ya nuru hiyo.
9 Nuru ya kweli ambayo humpa nuru mtu wa kila namna, ilikuwa karibu kuja ulimwenguni. 10 Yeye alikuwa ulimwenguni, na ulimwengu ulikuja kuwako kupitia yeye, lakini ulimwengu haukumjua. 11 Yeye alikuja nyumbani kwake mwenyewe, lakini watu wake mwenyewe hawakumkaribisha. 12 Hata hivyo, wengi kadiri ileile waliompokea, aliwapa mamlaka ya kuwa watoto wa Mungu, kwa sababu walikuwa wakidhihirisha imani katika jina lake; 13 nao walizaliwa, si kutokana na damu au kutokana na mapenzi ya kimwili au kutokana na mapenzi ya mwanamume, bali kutokana na Mungu.
14 Kwa hiyo Neno akawa mwili na akakaa miongoni mwetu, nasi tukapata kutazama utukufu wake, utukufu kama ule ulio wa mwana mzaliwa-pekee kutoka kwa baba; naye alikuwa mwenye kujaa fadhili isiyostahiliwa na kweli. 15 (Yohana alitoa ushahidi juu yake, ndiyo, kwa kweli alipaaza kilio—huyu ndiye aliyesema hilo—akisema: “Yule anayekuja nyuma yangu amekwenda mbele yangu, kwa sababu alikuwako kabla yangu.”) 16 Kwa maana sisi sote tulipokea kutoka katika ujao wake, hata fadhili isiyostahiliwa juu ya fadhili isiyostahiliwa. 17 Kwa sababu Sheria ilitolewa kupitia Musa, fadhili isiyostahiliwa na kweli zilikuja kuwa kupitia Yesu Kristo. 18 Hakuna mtu ambaye amemwona Mungu wakati wowote; mungu mzaliwa-pekee aliye katika mahali pa kifua na Baba ndiye ambaye amemweleza yeye.
19 Basi huu ndio ushahidi wa Yohana wakati Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu wamuulize: “Wewe ni nani?” 20 Naye aliungama wala hakukana, bali aliungama: “Mimi siye Kristo.” 21 Nao wakamuuliza: “Nini, basi? Je, wewe ndiwe Eliya?” Naye akasema: “Mimi siye.” “Je, wewe ndiwe Yule Nabii?” Naye akajibu: “La!” 22 Kwa hiyo wakamwambia: “Wewe ni nani? ili tupate kuwapa jibu wale waliotutuma sisi. Wewe wasema nini juu yako mwenyewe?” 23 Yeye akasema: “Mimi ni sauti ya mtu anayepaaza kilio nyikani, ‘Fanyeni njia ya Yehova iwe nyoofu,’ kama vile Isaya nabii alivyosema.” 24 Sasa wale waliotumwa walikuwa kutoka kwa Mafarisayo. 25 Kwa hiyo walimuuliza swali na kumwambia: “Kwa nini, basi, wewe wabatiza ikiwa wewe mwenyewe siye Kristo au Eliya au Yule Nabii?” 26 Yohana akawajibu, akisema: “Mimi nabatiza katika maji. Katikati yenu mmoja amesimama msiyemjua nyinyi, 27 yule anayekuja nyuma yangu, lakini ambaye gidamu ya kubazi lake mimi sistahili kuifungua.” 28 Mambo hayo yalitendeka katika Bethania ng’ambo ya Yordani, ambako Yohana alikuwa akibatizia.
29 Siku iliyofuata alimwona Yesu akija kumwelekea, naye akasema: “Ona, Mwana-Kondoo wa Mungu ambaye huondolea mbali dhambi ya ulimwengu! 30 Huyu ndiye niliyesema juu yake, Nyuma yangu kwaja mwanamume ambaye amesonga mbele yangu, kwa sababu alikuwako kabla yangu. 31 Hata mimi sikumjua yeye, lakini sababu kwa nini mimi nilikuja nikibatiza katika maji ilikuwa kwamba apate kufanywa dhahiri kwa Israeli.” 32 Yohana pia alitoa ushahidi, akisema: “Mimi nilitazama roho ikiteremka kama njiwa kutoka mbinguni, nayo ikakaa juu yake. 33 Hata mimi sikumjua yeye, bali Yuleyule aliyenituma mimi nibatize katika maji aliniambia, ‘Yeyote yule ambaye waona roho ikiteremka na kukaa juu yake, huyo ndiye ambaye hubatiza katika roho takatifu.’ 34 Nami nimeona, na nimetoa ushahidi kwamba huyo ndiye Mwana wa Mungu.”
35 Tena siku iliyofuata Yohana alikuwa amesimama na wawili wa wanafunzi wake, 36 na alipotazama Yesu akitembea akasema: “Ona, Mwana-Kondoo wa Mungu!” 37 Na wanafunzi hao wawili wakamsikia yeye akisema, nao wakamfuata Yesu. 38 Ndipo Yesu akageuka na, akipata kuwaona wanafuata, akawaambia: “Mnatafuta nini?” Wao wakamwambia: “Rabi, (ambalo litafsiriwapo humaanisha, Mwalimu,) unakaa wapi?” 39 Akawaambia: “Njoni, nanyi mtaona.” Basi wakaenda wakaona ni wapi alikokuwa akikaa, nao wakakaa pamoja naye siku hiyo; ilikuwa karibu saa ya kumi. 40 Andrea ndugu ya Simoni Petro alikuwa mmoja wa wale wawili waliosikia aliyoyasema Yohana nao wakamfuata Yesu. 41 Kwanza huyu alipata ndugu yake mwenyewe, Simoni, na kumwambia: “Tumempata Mesiya” (ambalo litafsiriwapo humaanisha, Kristo). 42 Akamwongoza kwa Yesu. Yesu alipomtazama akasema: “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana; wewe utaitwa Kefa” (ambalo latafsiriwa Petro).
43 Siku iliyofuata alitamani kuondoka kwenda Galilaya. Kwa hiyo Yesu akamkuta Filipo na kumwambia: “Uwe mfuasi wangu.” 44 Basi Filipo alikuwa wa kutoka Bethsaida, kutoka jiji la Andrea na Petro. 45 Filipo alimkuta Nathanaeli na kumwambia: “Tumempata yeye ambaye Musa, katika Sheria, na Manabii waliandika juu yake, Yesu, mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti.” 46 Lakini Nathanaeli akamwambia: “Je, kitu chochote kilicho chema chaweza kuja kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia: “Njoo uone.” 47 Yesu akamwona Nathanaeli akija kumwelekea na kusema kumhusu yeye: “Ona, Mwisraeli kwa uhakika, ambaye katika yeye hamna udanganyi.” 48 Nathanaeli akamwambia: “Yawaje kwamba wanijua mimi?” Kwa kujibu Yesu akamwambia: “Kabla ya Filipo kukuita wewe, ulipokuwa chini ya mtini, nilikuona wewe.” 49 Nathanaeli akamjibu: “Rabi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu, wewe ndiwe Mfalme wa Israeli.” 50 Yesu kwa kujibu akamwambia: “Je, waamini kwa sababu nilikuambia nilikuona chini ya mtini? Utaona mambo makubwa zaidi kuliko haya.” 51 Akazidi kumwambia: “Kwa kweli kabisa nawaambia nyinyi watu, Mtaona mbingu imefunguliwa na malaika za Mungu wakipanda na kushuka hadi kwa Mwana wa binadamu.”