Wakolosai
4 Nyinyi mabwana-wakubwa, fulizeni kutoa kilicho cha uadilifu na kilicho cha haki kwa watumwa wenu, mkijua kwamba nyinyi pia mna Bwana-mkubwa mbinguni.
2 Iweni mkidumu katika sala, mkibaki macho katika hiyo pamoja na utoaji-shukrani, 3 wakati huohuo mkisali pia kwa ajili yetu, ili Mungu apate kutufungulia mlango wa kutamka, kusema siri takatifu juu ya Kristo, ambayo kwa ajili yayo, kwa kweli, mimi nimo katika vifungo vya gereza; 4 ili niifanye dhahiri kama nipaswavyo kusema.
5 Endeleeni kutembea katika hekima kuelekea wale walio nje, mkijinunulia wenyewe kabisa wakati unaofaa. 6 Acheni tamko lenu liwe na upendezi sikuzote, lenye kukolezwa chumvi, ili kujua jinsi mpaswavyo kumpa jibu kila mmoja.
7 Mambo yangu yote, Tikiko ndugu yangu mpendwa na mhudumu mwaminifu na mtumwa mwenzi katika Bwana, atawajulisha nyinyi. 8 Kwa kusudi hilohilo la nyinyi kujua mambo yanayohusiana nasi na ili kwamba apate kufariji mioyo yenu, mimi ninamtuma yeye kwenu 9 pamoja na Onesimo, ndugu yangu mwaminifu na mpendwa, ambaye ni kutoka miongoni mwenu. Mambo yote ya hapa watawajulisha nyinyi.
10 Aristarko mateka mwenzangu awapelekea nyinyi salamu zake, na ndivyo pia Marko binamu ya Barnaba, (ambaye mlizipokea amri kuhusu yeye ili mmkaribishe iwapo aja kwenu,) 11 na Yesu aitwaye Yustasi, hawa wakiwa ni kati ya wale waliotahiriwa. Ni hawa tu walio wafanyakazi wenzangu kwa ajili ya ufalme wa Mungu, na hawahawa wamekuwa kwangu msaada wenye kutia nguvu. 12 Epafrasi, ambaye ni kutoka miongoni mwenu, mtumwa wa Kristo Yesu, awapelekea nyinyi salamu zake, akijikakamua mwenyewe sikuzote kwa ajili yenu katika sala zake, ili nyinyi mwishowe mpate kusimama mkiwa kamili na kwa usadikisho imara katika mapenzi yote ya Mungu. 13 Kwa kweli namtolea yeye ushahidi kwamba hujitahidi sana mwenyewe kwa niaba yenu na ya wale walio Laodikia na ya wale walio Hierapolisi.
14 Luka tabibu mpendwa awapelekea nyinyi salamu zake, na ndivyo pia Demasi. 15 Wapeni salamu zangu akina ndugu walio Laodikia na pia Nimfa na kutaniko lililo nyumbani mwake. 16 Na barua hii itakapokuwa imesomwa miongoni mwenu, pangeni ili isomwe pia katika kutaniko la Walaodikia na ili nyinyi pia msome ile ya kutoka Laodikia. 17 Pia, mwambieni Arkipo hivi: “Fuliza kuangalia huduma ambayo ulikubali katika Bwana, ili uitimize.”
18 Hii hapa salamu yangu, ya Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Endeleeni kuzingatia akilini vifungo vyangu vya gereza. Fadhili isiyostahiliwa iwe pamoja nanyi.