Ufunuo
12 Na ishara kubwa ilionwa mbinguni, mwanamke aliyepambwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake kulikuwa na taji la nyota kumi na mbili, 2 naye alikuwa na mimba. Naye hupaaza kilio akiwa katika maumivu yake na katika uchungu wake mkali wa kuzaa.
3 Na ishara nyingine ilionwa mbinguni, na, tazama! joka kubwa la rangi-moto, lenye vichwa saba na pembe kumi na juu ya vichwa vyalo vilemba saba; 4 na mkia walo wakokota theluthi moja ya nyota za mbinguni, nalo likazivurumisha chini hadi kwenye dunia. Nalo joka kubwa likafuliza kusimama mbele ya huyo mwanamke aliyekuwa karibu kuzaa, ili, azaapo, lipate kunyafua mtoto wake.
5 Naye akazaa mwana, wa kiume, atakayechunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hadi kwa Mungu na kwenye kiti chake cha ufalme. 6 Na mwanamke akakimbilia nyikani, ambako ana mahali palipotayarishwa na Mungu, ili wamlishe huko siku elfu moja mia mbili na sitini.
7 Na vita ikatokea ghafula mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na joka kubwa, hilo joka na malaika zalo walipigana 8 lakini halikuweza, wala mahali hapakupatikana mbinguni kwa ajili yao tena. 9 Kwa hiyo likavurumishwa chini hilo joka kubwa mno, nyoka wa awali, yeye aitwaye Ibilisi na Shetani, anayeiongoza vibaya dunia nzima inayokaliwa; akavurumishwa chini kwenye dunia, na malaika zake wakavurumishwa chini pamoja naye. 10 Nami nikasikia sauti kubwa mbinguni ikisema:
“Sasa umekuwa wokovu na nguvu na ufalme wa Mungu wetu na mamlaka ya Kristo wake, kwa sababu mshtaki wa ndugu zetu amekwisha kuvurumishwa chini, ambaye huwashtaki wao mchana na usiku mbele ya Mungu wetu! 11 Nao wakamshinda kwa sababu ya damu ya Mwana-Kondoo na kwa sababu ya neno la kutoa kwao ushahidi, nao hawakupenda nafsi zao hata usoni pa kifo. 12 Kwa ajili ya hili teremeni, nyinyi mbingu nanyi mkaao ndani yazo! Ole wa dunia na wa bahari, kwa sababu Ibilisi ameteremka kwenu, akiwa na hasira kubwa, akijua ana kipindi kifupi cha wakati.”
13 Sasa wakati joka kubwa lilipoona kwamba lilivurumishwa chini kwenye dunia, lilimnyanyasa mwanamke aliyezaa mtoto wa kiume. 14 Lakini mabawa mawili ya tai mkubwa akapewa mwanamke, ili apate kuruka kuingia katika nyika hadi mahali pake; huko ndiko alishwako kwa wakati na nyakati na nusu wakati mbali na uso wa nyoka.
15 Naye nyoka akatapika maji kama mto kutoka katika kinywa chake nyuma ya mwanamke, ili kumfanya azamishwe na huo mto. 16 Lakini dunia ikaja kumsaidia mwanamke, nayo dunia ikafungua kinywa chayo na kuumeza kabisa mto ambao joka kubwa liliutapika kutoka katika kinywa chalo. 17 Nalo joka kubwa likaingiwa na hasira ya kisasi kuelekea huyo mwanamke, na likaenda zalo kufanya vita na waliobaki wa mbegu yake, washikao amri za Mungu na walio na kazi ya kutoa ushahidi kuhusu Yesu.