Mwanzo
30 Raheli alipoona kwamba hajamzalia Yakobo watoto, alimwonea wivu dada yake, akaanza kumwambia Yakobo: “Nipe watoto, la sivyo nitakufa.” 2 Ndipo hasira ya Yakobo ikawaka dhidi ya Raheli, akamwambia: “Je, nimechukua nafasi ya Mungu, ambaye amekuzuia kuzaa watoto?”* 3 Raheli akamwambia: “Ndiye huyu kijakazi wangu Bilha.+ Lala naye ili anizalie watoto,* na ili kupitia yeye, mimi pia nipate watoto.” 4 Basi akampa Bilha kijakazi wake awe mke wake, Yakobo akalala naye.+ 5 Bilha akapata mimba na baada ya muda akamzalia Yakobo mwana. 6 Raheli akasema: “Mungu amekuwa mwamuzi wangu, naye ameisikiliza pia sauti yangu, akanipa mwana.” Ndiyo sababu alimpa jina Dani.*+ 7 Bilha, kijakazi wa Raheli, akapata mimba tena na kumzalia Yakobo mwana wa pili. 8 Kisha Raheli akasema: “Nimepigana mieleka mikali sana na dada yangu. Na pia nimeibuka mshindi!” Kwa hiyo akampa jina Naftali.*+
9 Lea alipoona kwamba ameacha kuzaa, alimchukua Zilpa kijakazi wake na kumpa Yakobo awe mke wake.+ 10 Na Zilpa kijakazi wa Lea akamzalia Yakobo mwana. 11 Kisha Lea akasema: “Kwa neema!” Basi akampa jina Gadi.*+ 12 Kisha Zilpa kijakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana wa pili. 13 Lea akasema: “Kwa furaha yangu! Kwa maana hakika mabinti watanitangaza kuwa mwenye furaha.”+ Basi akampa jina Asheri.*+
14 Sasa Rubeni+ alikuwa akitembea siku za mavuno ya ngano, akapata dudai shambani. Kwa hiyo akamletea Lea mama yake. Basi Raheli akamwambia Lea: “Tafadhali, nipe baadhi ya dudai za mwana wako.” 15 Lea akamwambia: “Unafikiri ni jambo dogo kumchukua mume wangu?+ Unataka pia kuchukua dudai za mwanangu?” Raheli akasema: “Ni sawa. Yakobo atalala nawe usiku wa leo ukinipa dudai za mwana wako.”
16 Yakobo alipokuwa akirudi kutoka shambani jioni, Lea alienda kumpokea, akamwambia: “Utalala nami kwa sababu nimekukodi kikamili kwa dudai za mwanangu.” Basi akalala naye usiku huo. 17 Na Mungu akamsikiliza Lea na kumjibu, naye akapata mimba na baada ya muda akamzalia Yakobo mwana wa tano. 18 Kisha Lea akasema: “Mungu amenipa mshahara wangu* kwa sababu nimempa mume wangu kijakazi wangu.” Kwa hiyo akampa jina Isakari.*+ 19 Lea akapata mimba tena na baada ya muda akamzalia Yakobo+ mwana wa sita. 20 Lea akasema: “Mungu amenipa mimi zawadi, naam, amenipa mimi zawadi nzuri. Hatimaye, mume wangu atanivumilia,+ kwa maana nimemzalia wana sita.”+ Basi akampa jina Zabuloni.*+ 21 Baadaye akazaa binti na kumpa jina Dina.+
22 Mwishowe Mungu akamkumbuka Raheli, na Mungu akamsikia na kumjibu kwa kumwezesha kupata mimba.*+ 23 Akapata mimba na kuzaa mwana. Akasema: “Mungu ameiondoa aibu yangu!”+ 24 Basi akampa mwana huyo jina Yosefu,*+ akisema: “Yehova ananiongezea mwana mwingine.”
25 Baada ya Raheli kumzaa Yosefu, mara moja Yakobo akamwambia Labani: “Niruhusu niondoke ili niende nyumbani, katika nchi yangu.+ 26 Nipe wake zangu na watoto wangu, ambao nimekutumikia ili niwapate, niende zangu, kwa maana unajua vema jinsi nilivyokutumikia.”+ 27 Labani akamwambia: “Ikiwa nimepata kibali machoni pako,—ishara za ubashiri zimenisaidia* kuelewa kwamba Yehova ananibariki kwa sababu yako.” 28 Kisha akasema: “Niambie mshahara wako, nami nitakulipa.”+ 29 Basi Yakobo akamwambia: “Unajua jinsi nilivyokutumikia na jinsi nilivyoitunza mifugo yako;+ 30 kabla sijaja ulikuwa na wanyama wachache, lakini sasa wameongezeka na kuwa wengi, naye Yehova amekubariki tangu nilipokuja. Basi nitaishughulikia lini nyumba yangu mwenyewe?”+
31 Kisha akamuuliza: “Nikupe nini?” Yakobo akajibu: “Usinipe chochote! Lakini ukinifanyia jambo hili moja, nitaendelea kuichunga mifugo yako na kuilinda.+ 32 Nitapita kati ya mifugo yako yote leo. Watenge kondoo wote wenye madoadoa na wenye mabakamabaka na kila mwanakondoo dume wa rangi ya kahawia na mbuzi jike yeyote mwenye madoadoa na mabakamabaka. Kuanzia sasa na kuendelea, watakuwa mshahara wangu.+ 33 Na uadilifu* wangu utathibitisha kazi yangu siku utakapokuja kuangalia mshahara wangu; na ikiwa nitakuwa na mbuzi jike yeyote ambaye hatakuwa na madoadoa au mabakamabaka na mwanakondoo yeyote dume ambaye hatakuwa na rangi ya kahawia, basi atakuwa ameibwa.”
34 Labani akasema: “Vema! Na iwe kama ulivyosema.”+ 35 Basi siku hiyo akawatenga mbuzi dume wenye mistarimistari na mabakamabaka na mbuzi jike wote wenye madoadoa na mabakamabaka, na kila mwanakondoo dume mwenye madoadoa meupe na wa rangi ya kahawia; akawapa wanawe ili wawatunze. 36 Baada ya hayo Labani akasafiri kwa siku tatu kwenda kuchunga mifugo mbali na Yakobo, naye Yakobo akabaki akichunga mifugo ya Labani iliyosalia.
37 Ndipo Yakobo akachukua fito mbichi za mti wa mlubna, mlozi, na mwaramoni, akazibambua ili madoa meupe yaonekane. 38 Kisha akaziweka zile fito alizobambua mbele ya mifugo, kwenye mitaro, kwenye vyombo vya kunyweshea, mahali ambapo wanyama walikuja kunywa maji, ili wazione fito hizo na kupata joto la kupandana wanapokuja kunywa maji.
39 Basi wanyama hao walipata joto na kupandana mbele ya fito hizo, nao walizaa wanyama wenye mistarimistari, madoadoa, na mabakamabaka. 40 Kisha Yakobo akawatenga wanakondoo dume, halafu akageuza wanyama wa Labani ili wawaangalie wanyama wenye mistarimistari na pia wanyama wote wa rangi ya kahawia kati ya mifugo ya Labani. Kisha akatenga mifugo yake, naye hakuichanganya na mifugo ya Labani. 41 Na kila mara wanyama wenye nguvu walipopata joto la kupandana, Yakobo aliweka zile fito kwenye mitaro ili wanyama hao wazione na kupata joto la kupandana. 42 Lakini wanyama walipokuwa dhaifu, hakuziweka fito hizo kwenye mitaro. Kwa hiyo sikuzote wanyama dhaifu walikuwa wa Labani, lakini wenye nguvu walikuwa wa Yakobo.+
43 Kwa hiyo Yakobo akatajirika sana, akawa na makundi makubwa ya wanyama na watumishi wa kiume na wa kike na ngamia na punda.+