Wakati Ujao wa Dini kwa Kutegemea Wakati Wayo Uliopita
Sehemu ya 17: 1530 na kuendelea —Uprotestanti—Je! Ni Marekebisho?
“Kufanya badiliko jipya si kurekebisha.”—Edmund Burke, mshiriki wa karne ya 18 wa Bunge la Uingereza
WANAHISTORIA Waprotestanti huuona Mrekebisho wa Kiprotestanti kuwa ulirudisha Ukristo wa kweli. Kwa upande mwingine, wanachuo Wakatoliki husema ulitokeza kosa la kitheolojia. Hata hivyo, je! maoni ya watazamaji juu ya historia ya kidini huko nyuma hufunua nini? Je! Mrekebisho wa Kiprotestanti ulikuwa kweli mrekebisho, au ulikuwa badiliko jipya tu, kubadili namna moja ya ibada yenye dosari kwa kuweka nyingine?
Neno la Mungu Lapewa Cheo Maalumu
Warekebishi Waprotestanti walikazia umaana wa Maandiko. Walikataa mapokeo, ingawa Martin Marty, mhariri wa cheo cha chuu wa gazeti The Christian Century, asema kwamba katika karne iliyopita, “Waprotestanti zaidi na zaidi wamekuwa na nia ya kuona kukiwa na uhusiano kati ya Biblia na mapokeo.” Hata hivyo, “babu zao wa kale katika imani” hawakuwa hivyo. Kwa maoni yao “Biblia ilikuwa na cheo maalumu, na mapokeo wala mamlaka ya kipapa hayangeweza kamwe kulingana nayo.”
Mwelekeo huu ulichochea upendezi wa kutafsiri, kugawanya, na kujifunza Biblia. Katikati ya karne ya 15—zaidi ya nusu-karne kabla ule Mrekebisho haujaanza—Johannes Gutenberg Mjeremani mwenzi wa Lutheri aliandaa chombo chenye mafaa kwa Uprotestanti ambao ungetokea huko mbele. Akiisha kusitawisha njia ya kupiga chapa kwa herufi za mhamisho, Gutenberg alitokeza Biblia ya kwanza iliyopigwa chapa. Lutheri aliona uwezekano mkubwa katika uvumbuzi huu, naye akauita uchapaji “kazi ya karibuni zaidi na iliyo bora zaidi ya Mungu kueneza dini ya kweli kotekote ulimwenguni.”
Sasa watu wengi zaidi wangeweza kuwa na Biblia yao wenyewe, hilo likiwa ni tukio ambalo halikuungwa mkono na Kanisa Katoliki. Katika 1559 Papa Paul 4 aliamuru kwamba hakuna Biblia ingeweza kuchapwa katika lugha ya kienyeji bila idhini ya kanisa, na kanisa lilikataa kutoa idhini hiyo. Kwa uhakika, katika 1564 Papa Pius 4 alitaarifu hivi: “Yaliyoonwa yameonyesha kwamba ruhusa ikitolewa ili Biblia isomwe na watu wowote tu katika katika lugha za kienyeji, . . . madhara yatakuwa mengi kuliko faida za kufanya hivyo.”
Mrekebisho ulitokeza aina mpya ya “Ukristo.” Uliweka hiari ya kibinafsi badala ya mamlaka ya kipapa. Liturjia (ibada ya hadharani) ya Kiprotestanti iliwekwa badala ya Misa ya Kikatoliki, na makanisa ya Kiprotestanti yasiyo na fahari kubwa sana yakawekwa badala ya makathedro makubwa sana ya Kikatoliki.
Manufaa Zisizotarajiwa
Historia hutufundisha kwamba harakati ambazo huwa na asili ya kidini hugeuka mara nyingi zikaingiwa na utetezi wa mambo ya kijamii na kisiasa. Ilithibitika kuwa hivyo kuhusu Mrekebisho wa Kiprotestanti. Profesa wa historia kwenye Chuo Kikuu cha Kolumbia, Eugene F. Rice, Jr., afafanua hivi: “Katika zile Enzi za Kati kanisa la Magharibi lilikuwa limekuwa shirika la Kiulaya. Katika nusu ya kwanza ya karne ya kumi na sita lilivunjika likawa makanisa mengi sana ya kienyeji . . . [ambayo] watawala wa kilimwengu waliyadhibiti kwa kadiri kubwa zaidi.” Tokeo likawa ni “kufikia upeo kwa mng’ang’ano wa muda mrefu kati ya mamlaka ya kilimwengu na ya kikasisi. . . . Mwishowe usawaziko wa mamlaka ulikoma serikali ikawa ndiyo yenye mamlaka kuliko kanisa na mtu wa kawaida kuliko padri.”
Hiyo ililetea watu mmoja mmoja uhuru mkubwa zaidi, wa kidini na kiraia pia. Tofauti na Ukatoliki, Uprotestanti haukuwa na shirika kuu la kuelekeza mafundisho au kawaida za ibada, hiyo ikiruhusu kuwe na namna nyingi za maoni ya kidini. Jambo hilo, nalo, liliendeleza pole kwa pole uvumilio wa maoni ya kidini na mwelekeo wa kuachia watu hiari ambayo ilikuwa bado haiwaziki wakati wa ule Mrekebisho.
Uhuru mkubwa zaidi ulifungulia ghafula nishati zilizokuwa hazijatumiwa. Watu fulani hudai kwamba hicho ndicho kichochezi kilichohitajiwa ili kufyatusha matukio ya kijamii, kisiasa, na kiufundi ambayo yaliturusha ndani ya kipindi chetu cha ki-siku-hizi. Maadili ya kazi ya Kiprotestanti ‘yalihusishwa katika serikali na maisha ya kila siku pia,’ aandika Theodore White mtungaji aliyekufa. Alieleza jambo hilo kuwa “imani ya kwamba binadamu ahusika moja kwa moja mbele za Mungu kwa dhamiri yake na vitendo vyake, bila mhusiko wala upatanisho kupitia kwa mapadri. . . . Kama binadamu angefanya kazi kwa bidii, alime kabisa, bila kujilegeza wala kufanya ugoigoi, na atunze mke wake na watoto, hapo nasibu ama Mungu ingethawabisha jitihada zake.”
Je! pande hizi za Uprotestanti ambazo zaonekana kuwa na mwelekeo chanya zapasa kutupofusha tusione mapungukio yao? Mrekebisho wa Kiprotestanti ulikuwa pia “pindi ya maovu makubwa sana,” yasema Encyclopædia of Religion and Ethics, ikiongeza hivi: “Kipindi cha Wayeswiti na Baraza la Kuhukumu Wazushi kilikomeshwa . . . kumbe kikafuatwa na kitu fulani chenye sifa mbaya hata zaidi. Ikiwa kile kilichokuwako katika zile Enzi za Kati ni ujinga usio wa kukusudia, kilichoko sasa ni ubandia mwingi uliopangwa kitengenezo.”
‘Ubandia Uliopangwa Kitengenezo’—Katika Njia Gani?
Ulikuwa ‘ubandia uliopangwa kitengenezo’ kwa sababu Uprotestanti uliahidi mrekebisho wa kimafundisho lakini ukashindwa kuutekeleza. Mara nyingi, mwongozo wa kanisa, wala si ukosefu wa kusema kweli katika mafundisho, ndio uliochochea kasirani ya warekebishi. Sana-sana, Uprotestanti ulibaki na mawazo na mazoea ya kidini ya Ukatoliki uliotiwa doa na upagani. Jinsi gani? Kielelezo cha kutokeza ni fundisho la Utatu, ambalo ndio msingi mkuu wa kuwa mwanachama katika Baraza la Makanisa ya Kiprotestanti Ulimwenguni. Ushikamano kwa fundisho hili ni imara sana, ingawa The Encyclopedia of Religion hukiri kwamba ‘wakosoaji wenye kufafanua maandiko na wanatheolojia leo huafikiana kwamba katika Biblia hakuna mahali ambapo fundisho hilo hufundishwa wazi kabisa.’
Je! Uprotestanti uligeuza namna yenye ufisadi ya serikali ya kanisa? Sivyo. Badala ya hivyo, ‘uliendeleza vigezo vya mamlaka kutoka Ukatoliki wa zile enzi za kati,” asema Martin Marty, na ‘ulichofanya tu ni kujitenga na dini ya Katoliki ya Kiroma ili kufanyiza namna za Kiprotestanti.”
Pia Uprotestanti uliahidi kurudisha “umoja wa imani.” Hata hivyo, ahadi hii ya Kibiblia ilipita bila kutimizwa kwa kutokea mafarakano mengi ya Kiprotestanti yenye mgawanyiko.—Waefeso 4:13.
Mvurugo Uliopangwa Kitengenezo—Kwa Nini?
Leo, katika 1990, Uprotestanti umemonyoka-monyoka ukawa mafarakano na madhehebu nyingi sana hivi kwamba haingewezekana kujua hesabu ya jumla. Kabla mtu hajaweza kumaliza kuhesabu, vikundi vipya vingekuwa vimefanyizwa au vingine vingekuwa vimetoweka.
Hata hivyo, World Christian Encyclopedia hufanya “yasiyowezekana” kwa kugawanya Jumuiya ya Wakristo (kufikia 1980) ikawa “madhehebu tofauti-tofauti za Kikristo 20,780,” zilizo nyingi sana zikiwa ni za Kiprotestanti.a Hizo ni kutia ndani vikundi vya zamani 7,889 vya Kiprotestanti, dini za Kiprotestanti 10,065 za kienyeji ambazo sana-sana ni za wasio weupe, madhehebu 225 za Kianglikana, na vikundi 1,345 vingine vya kandokando vya Kiprotestanti.
Katika kueleza jinsi unamna-namna huu wenye kuvuruga, wenye kuitwa “ishara ya afya na ya ugonjwa pia,” ulitokea, kitabu Protestant Christianity hutaja kwamba “huenda ikawa ni kwa sababu ya akili za ubuni wa kibinadamu na kutokamilika kwa kibinadamu; na hata zaidi huenda ikawa ni kwa sababu ya watu wenye kujaa kiburi ambao hufikiria mno maoni yao wenyewe juu ya maisha.”
Hiyo ni kweli kabisa! Bila kuufikiria vya kutosha ukweli wa kimungu, wanadamu wenye kujaa kiburi hutoa njia mpya za kupata wokovu, ukombozi, au utimizo. Wingi wa dini hauungwi mkono katika Biblia.
Katika kutetea wingi wa dini, Uprotestanti huelekea kudokeza kwamba Mungu hana miongozo ambayo yeye ataabudiwa kulingana nayo. Je! mvurugo huo uliopangwa kitengenezo hupatana na Mungu wa ukweli, ambaye Biblia husema “Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani”? Je! lile wazo la Kiprotestanti ambalo husikiwa mara nyingi kwamba nenda-kanisa-la-uchaguzi-wako-mwenyewe ni tofauti hata kidogo na kufikiri kulikoongoza Adamu na Hawa katika imani yenye makosa na matata baadaye?—1 Wakorintho 14:33; ona Mwanzo 2:9; 3:17-19.
Kupuuza Hadhi Maalumu ya Biblia
Biblia ijapogawiwa hadhi (heshima) maalumu na warekebishi wa mapema, baadaye wanatheolojia Waprotestanti walizaa uchambuzi wa juu zaidi na “hivyo wakatendea andishi la kibiblia kama vile wangetendea andishi jingine lolote la fasihi za kale,” asema Marty. Hawakukubali kuwapa “waandikaji wa Biblia hadhi yoyote ya kwamba walivuviwa.”
Kwa hiyo, kwa kutilia shaka kuvuviwa kimungu kwa Biblia, wanatheolojia Waprotestanti walilegeza imani katika kitu kile ambacho Warekebishi walikiona kuwa ndio msingi halisi wa Uprotestanti. Hiyo ilifungulia njia mawazo ya kudhania-dhania mambo, kufikiri kama kila mtu ajitakiavyo, na kupunguza uzito wa mambo. Ndiyo sababu wanachuo wengi huuona Mrekebisho kuwa kisababishi kikubwa cha tabia ya ulimwengu wa ki-siku-hizi.
Kanaswa Katika Siasa
Tunda lililotajwa juu ni kizibiti cha wazi kwamba ijapokuwa warekebishi mmoja mmoja na wafuasi wao walikuwa na madhumuni mema, Uprotestanti haukurudisha Ukristo wa kweli. Badala ya kutetea amani kupitia kutokuwamo kwa Kikristo, ulijiingiza sana katika utukuzo wa taifa.
Hilo lilionekana mara tu mgawanyiko wa Jumuiya ya Wakristo kuwa Ukatoliki na Uprotestanti ulipotokea ukawa jambo halisi. Majeshi ya Kikatoliki na Kiprotestanti yalitiririsha damu ikavuka ng’ambo moja hadi ng’ambo nyingine ya kontinenti la Ulaya katika vita dazani moja au zaidi. The New Encyclopædia Britannica huviita “Vita vya Dini vilivyowashwa na Mrekebisho wa Kijeremani na Kiswisi katika miaka ya 1520.” Yenye kujulikana zaidi kati yavyo ilikuwa ile Vita ya Miaka Thelathini (1618-48), iliyohusisha tofauti za kisiasa na kidini pia kati ya Waprotestanti na Wakatoliki Wajeremani.
Damu ilitiririka katika Uingereza pia. Kati ya 1642 na 1649, Mfalme Charles 1 alifanya vita dhidi ya Bunge. Kwa kuwa hesabu kubwa ya wapinzani wa Mfalme ilikuwa ya upande wa Wapyuritani (wenye utakato) wa Kanisa la Uingereza, nyakati fulani vita hiyo hutajwa kuwa yale Mapinduzi Makubwa ya Kipyuritani. Ilimalizika kwa kumnyonga Mfalme na kuanzisha jumuiya-madola ya Kipyuritani iliyokuwa na maisha mafupi ikiwa chini ya Oliver Cromwell. Ingawa hii Vita ya Waingereza Wenyewe kwa Wenyewe haikuwa hasa mng’ang’ano wa kidini, wanahistoria huafikiana kwamba dini ilikuwa kisababishi kikubwa katika kuchagua pande zenye kuhusika.
Katika vita hii, kikundi cha kidini kijulikanacho kuwa Friends (Marafiki), au Wakweka, kilitokea. Kikundi hicho kilikabili upinzani thabiti kutoka kwa “ndugu” zao Waprotestanti. Washiriki mia kadhaa walifia gerezani, na maelfu wakatendwa mambo ya kuwavunjia heshima. Lakini harakati hiyo ilienea, hata kwenye koloni za Kiingereza katika Amerika, ambamo katika 1681 Charles 2 alimtolea William Penn mkataba wa kuanzisha koloni ya Wakweka, ambayo baadaye ikawa mkoa wa Pennsylvania.
Wakweka hawakuwa peke yao katika kutafuta waongofu kotekote, kwa maana dini nyinginezo zilikuwa zimefanya hivyo kabla ya hapo. Hata hivyo, sasa baada ya “Badiliko Jipya” la Uprotestanti, Wakatoliki, pamoja na hesabu kubwa ya vikundi vya Kiprotestanti, walianza kuongeza jitihada zao za kuwaletea “wasioamini” ujumbe wa Kristo wa ukweli na amani. Lakini kinyume gani hicho! Wakiwa “waamini,” Wakatoliki na Waprotestanti hawakuweza kuafikiana waufafanue ukweli wa kimungu kwa njia moja. Na hakika walishindwa kuonyesha amani na muungamano wa kidugu. Kwa sababu ya hali hii, ni jambo gani lingeweza kutarajiwa “Wakati ‘Wakristo’ na ‘Wasio Wakristo’ Walipokutana”? Soma sehemu ya 18 katika toleo hili.
[Maelezo ya Chini]
a Kichapo hiki cha marejezo, kilichochapishwa katika 1982, kilikuwa kimetokeza wazo la kwamba kufikia 1985 kungekuwa na 22,190, ikisema hivi: “Ongezeko la sasa ni la madhehebu mpya 270 kila mwaka (5 mapya kwa juma).”
[Sanduku katika ukurasa wa 14]
Mazao ya Mapema ya Mrekebisho
USHIRIKA WA KIANGLIKANA: 25 makanisa yenye kujisimamia na mashirika mengine 6 yenye kushiriki mafundisho, mwongozo, na liturjia (ibada ya hadhara) pamoja na Kanisa la Uingereza na kutambua uongozi wenye cheo cha jina tu cha Askofu Mkuu wa Canterbury. The Encyclopedia of Religion husema kwamba Uanglikana “umeendeleza imani katika mfuatano wa mitume wa maaskofu na kubakiza mazoea mengi yaliyoutangulia Mrekebisho.” Kilicho kikuu kwenye ibada yayo ni Book of Common Prayer, “liturjia ya pekee ambayo ingali yatumiwa kwa lugha ya kienyeji.” Waanglikana katika United States, waliovunja uhusiano na Kanisa la Uingereza na kufanyiza Kanisa Episkopali la Kiprotestanti katika 1789, walivunja uhusiano tena na mapokeo katika Februari 1989 kwa kutawaza askofu wa kwanza mwanamke katika historia ya Kianglikana.
MAKANISA YA KIBAPTISTI: Madhehebu 369 (1970) ambazo asili yazo ni Waanabaptisti wa karne ya 16, waliokazia ubatizo wa watu wazima kwa kuzamisha. The Encyclopedia of Religion chasema Wabaptisti “wameliona kuwa jambo gumu kudumisha muungamano wa kitengenezo au kitheolojia,” wakiongeza kwamba “jamaa ya Kibaptisti katika United States ni kubwa, . . . lakini, kama vile ilivyo katika jamaa nyingine kubwa-kubwa, washiriki fulani hawaneni na washiriki wengine.”
MAKANISA YA KILUTHERI: Madhehebu 240 (1970), zenye kujivunia kuwa na washiriki wengi zaidi ya kikundi chochote cha Kiprotestanti. Wao “wangali kwa njia fulani wamegawanywa kikabila (Wajeremani, Waswedeni, nk),” yasema The World Almanac and Book of Facts 1988, hata hivyo ikiongezea kwamba “migawanyiko mikubwa ni kati ya wenye kufasiri maana ya maandishi kwa uhalisi kabisa (wafundamentalisti) na wenye kuyafasiri kwa hiari nyingi.” Mgawanyo wa Walutheri katika kambi zenye kutukuza taifa ulionekana wazi sana katika Vita ya Ulimwengu 2, ambapo, kama vile asemavyo E. W. Gritsch wa Seminari ya Theolojia ya Kilutheri, “hesabu ndogo ya mapasta na makundi ya Kilutheri [katika Ujeremani] walimkinza Hitler, lakini Walutheri walio wengi ama walibaki kimya ama walishirikiana kutenda pamoja na utawala wa Nazi.”
MAKANISA YA KIMETHODISTI: Madhehebu 188 (1970) zilizotokana na harakati moja ndani ya Kanisa la Uingereza iliyoanzishwa katika 1738 na John Wesley. Baada ya kifo chake lilivunjika likiwa kikundi kilichojitenga; Wesley alieleza kwamba Mmethodisti ni “mtu ambaye huishi kulingana na methodi (njia) iliyowekwa katika Biblia.”
MAKANISA YA MREKEBISHO NA MAKANISA YA KIPRESBITERI: Makanisa ya mrekebisho (madhehebu 354 kufikia 1970) hufuata mafundisho ya Kalvini, badala ya yale ya Lutheri, na hujiona kuwa “Kanisa Katoliki, la mrekebisho.” “Kipresbiteri” huonyesha serikali ya kanisa yenye kuongozwa na wazee (wapresbiteri); makanisa yote ya Kipresbiteri ni makanisa ya Mrekebisho, lakini si makanisa yote ya Mrekebisho yaliyo na serikali ya namna ya kipresbiteri.
[Picha katika ukurasa wa 11]
Ukurasa wenye usanifu mzuri wa Biblia ya Gutenberg katika Kilatini
[Hisani]
Kwa ruhusa ya Maktaba ya Uingereza
[Picha katika ukurasa wa 12]
Gutenberg na matbaa yake ya herufi za mhamisho
[Picha katika ukurasa wa 13]
John Wesley, mwanzishi wa Kanisa Methodisti (1738)