Ongeza Rangi Fulani Kwenye Maisha Yako
HAIKUGHARIMU fedha zozote. Hukufanya uvutie zaidi. Hukupa uhakika zaidi. Ni nini?
Ni uwezo wa kufaanisha au kupatanisha rangi za mavazi unayovaa. Ingawa ni ustadi unaoweza kujifunzwa kwa urahisi, watu wengi huvurugika, hata kukata tamaa, inapofikia kuamua rangi gani inayofaa na inafaana na ipi.
Je! hivyo ndivyo unavyohisi unapojaribu kuamua kama unapaswa kuvaa manjano na buluu, au je! ni manjano na kijani kibichi? Ikiwa ndivyo, usivunjike moyo, kwa maana kufanyiza miunganisho ya rangi zinazofaa kati ya mavazi yako hakutaki kukumbuka sheria nyingi. Unalohitaji kujua tu ni jambo fulani juu ya asili ya rangi-rangi na jinsi zinavyoshirikiana. Kwa hiyo acheni tuangalie baadhi ya kanuni za msingi na kuona jinsi unavyoweza kuongeza rangi fulani kwenye maisha yako.
Kuna Rangi Ngapi?
“Tunapotazama upinde wa mvua tunawazia tu kuona nyekundu, rangi ya chungwa, manjano, kijani kibichi, buluu, nili, na urujuani, na kupuuza kabisa rangi zilizoko baina ya hizo,” mwanasayansi wa rangi Mjapani Kunihiko Takei aeleza Amkeni! “Kama vile rangi katika upinde wa mvua zinavyobadilika polepole kutoka nyekundu hadi urujuani, ndivyo kila rangi mahususi inavyoweza kubadilishwa kwa ustadi kutoka kuwa yenye kushika hadi kuwa hafifu, nyangavu hadi kuwa kiza-kiza. Kusema kuna mamia ya rangi yoyote ile moja ni kushikilia mambo ya kikale na hakufai.”
Maana ya hilo ni kwamba zile rangi mbalimbali si za kipekee-pekee. Zinahusiana, na kuelewa uhusiano huo ni kwenye thamani katika kujua jinsi ya kupatanisha rangi-rangi. Chombo chenye msaada katika jambo hilo ni lile gurudumu, au duara la rangi. Aina moja yalo yaonyeshwa kwenye ukurasa 17. Zile rangi za upinde wa mvua zimepangwa katika duara. Rangi za msingi—nyekundu, manjano, na buluu—zinatenganishwa na nafasi inayolingana kwenye gurudumu hilo.a Kwa kuchanganya rangi hizo kwa viwango mbalimbali, rangi nyingine zote, kwenye gurudumu zaweza kutokezwa.
Wakati rangi kwenye lile gurudumu inapochanganywa na kiwango kinacholingana cha rangi iliyo ng’ambo nyingine ya lile gurudumu, tokeo huwa nyeusi au nyeusi-kijivu. Ikiwa viwango visivyolingana vinachanganywa, matokeo yanakuwa zile rangi zilizoshika zaidi au za usawaziko za upande wa ndani wa gurudumu. Kwa sababu zina rangi zaidi, rangi hizo zilizosawazika zaweza kupatana na namna-namna za rangi. Kwa kielelezo, nyekundu ya katikati, haina nyekundu na kijani-kibichi tu bali pia manjano na buluu, ambazo ndizo hutokeza kijani-kibichi.
Njia nyingine ya kufanyiza rangi-rangi ni kwa kuongeza vipimo vyenye kutofautiana vya nyeupe, kijivu-jivu, au nyeusi. Kijivu-jivu hupunguza mng’ao, na matokeo ni rangi zisizong’aa za mshiko ule ule wa rangi. Mipunguzo ya rangi, au rangi nyangavu zaweza kutokezwa kwa kuongeza nyeupe, mishiko-shiko ya rangi, au rangi zilizoshika kutokezwa kwa kuongeza nyeusi. Chati ya rangi (chini kulia) yaonyesha zile rangi nyingi za mshiko ule ule wa rangi. Ongeza hizi kwa hesabu ya rangi au namna-namna za rangi, na uwezekano wa kusisimua wafikia mamilioni. Yakadiriwa kwamba kuna miongezo-ongezo, mipunguzo-punguzo, na mishiko-shiko ya rangi ipatayo 10,000,000.
‘Lakini hapo ndipo penye tatizo,’ huenda ukasema. ‘Rangi hizo zote!’ Tusikose kuona msitu kwa sababu ya miti. Jambo la maana ni kuona uhusiano uliopo kati ya rangi-rangi. Je! wakati mmoja ulikuwa na sweta nyekundu ambayo uliona haikukufanya upendeze na kwa hiyo ukaamua kwamba huwezi kuvaa nyekundu kamwe? Je! ilikuwa nyekundu-buluu au nyekundu ya rangi-chungwa, je! ilikuwa rangi ya mvinyo wenye rangi ulioshika au nyekundu nyeupe-nyeupe, je! ilikuwa hafifu au yenye rangi nyingi? Ukichanganua rangi kwa njia hiyo, utaona nyekundu nyingi-nyingi, au rangi nyinginezo, ambazo unaweza kuvaa kwa kufaa.
‘Nijueje Rangi Zinazonifaa?’
Ingawa kuna rangi nyingi, hiyo haimaanishi kwamba zote zitafanya upendeze. Huenda ukapenda rangi-rangi fulani, lakini si lazima zikufanye upendeze. Badala yake, rangi-rangi unazokuwa umevaa wakati unapopongezwa zaidi ndizo zinazokufanya upendeze.
Kulingana na wataalamu wengi, kila mtu ni wa aina ya buluu au aina ya manjano. Wao husema wale wa aina-aina za buluu, huonekana wapendeza katika rangi-rangi kama buluu na nyekundu nyeupe-nyeupe mno na wanapaswa kuepuka rangi-rangi za chungwa na rangi-rangi za kahawia. Walio wa aina za manjano huonekana wapendeza wakiwa wamevaa manjano, rangi ya dhahabu, na rangi-rangi zilizoshika lakini yaelekea zambarau haitawafaa.
Njia rahisi zaidi ya kuamua ni rangi zipi zinazofanya upendeze ni kuziwekelea juu yako, moja moja, na kutazama katika kioo katika nuru ya mchana. Kulingana na Carole Jackson, mshauri wa rangi na mtungaji wa kitabu kilichouzwa sana Color Me Beautiful, rangi inayofaa “hulainisha na kuangaza ngozi yako” na “hutokeza rangi ya kupendeza usoni pako.” Kwa upande mwingine, rangi isiyofaa “huenda ikafanya ngozi yako ionekane imefifia, imeparara, au ‘kuchakaachakaa’” na hata huenda “ikazeesha uso wako.”
Vipi Juu ya Sheria-Sheria?
Lakini vipi juu ya zile sheria-sheria tunazosikia mno? Je! miunganisho fulani haifai kabisa?
“Sheria pekee iliyopo leo ni ‘Usiseme Haifai Kamwe,’” aliandika mshauri wa rangi na sura wa Hollywood, Leatrice Eiseman katika kitabu chake Images in Colour. “Fikiria miongozo badala ya sheria-sheria, ambazo zaweza kuzuia ubuni wako na kukuzuia usikubali mawazo mapya.”
Basi, miongozo hiyo ni nini? Kwa msingi kuna miwili tu ya kukumbuka: (1) Unganisha rangi zinazofaa, na (2) ziwe katika vipimo sahihi. Kwa kufuata miongozo hiyo, kuna hatua au taratibu fulani zinazoweza kusaidia. Kutumia gurudumu la rangi na chati ya rangi kutakusaidia uelewe jinsi taratibu hizo hufanya kazi.
Rangi za monokoromatiki. Maana yake hiyo ni kutumia familia za rangi-rangi au namna-namna za rangi ile ile. Chati ya rangi itakusaidia katika hilo. Je! waweza kuona jinsi mishiko-shiko ya rangi, miongezo-ongezo na mipunguzo-punguzo ya rangi inavyokubaliana? Hata ingawa ni rangi moja ya msingi inayotumiwa miunganisho ya rangi-moja yaweza kufaa sana wakati utofautiano unapofanyizwa kwa mishiko-shiko na mipunguzo-punguzo ya rangi. Miunganisho hiyo yaonekana yenye kupendeza, inapatana.
Rangi za duokromatiki, au rangi mbili. Huu ndio muunganisho ambao yaelekea utautumia zaidi katika mavazi. Rangi hizo mbili ama zapasa kukaribiana kwenye gurudumu la rangi au kuwa mbalimbali kwa kadiri kubwa iwezekanavyo. Rangi zinazopakana kwenye gurudumu, kama vile nyekundu na nyekundu-rangi ya chungwa au nyekundu na nyekundu-zambarau, huitwa zenye kupatana na hufaana. Kwa upande mwingine, rangi ambazo moja iko ng’ambo ya ile nyingine kwenye gurudumu, kama vile nyekundu na kijani-kibichi, au manjano na zambarau, huitwa zenye kukamilishana. Huzidishana na kufanya rangi hizo zitokeze. Ili kutumia rangi zenye kukamilishana kwa njia ya kuvutia, tumia rangi yako ya pili kwa uchache, au itumie ikiwa yenye mshiko zaidi wa rangi. Rangi yaweza pia kuunganishwa kwa kufaa na rangi zilizo jirani ya kikamilisho chazo kwenye gurudumu la rangi. Hiyo huitwa kikamilisho cha karibu. Manjano na buluu-zambarau au pamoja na nyekundu-zambarau hufanyiza muunganisho huo, na huenda ukataka kuzidisha hilo kwa kuvaa hiyo ya pili ikiwa mshiko zaidi wa rangi. Ikiwa rangi yaonekana chafu, unaiona kwa kuilinganisha na rangi zisizofaa. Tafuta mfaano bora zaidi.
Rangi za traikromatiki, rangi tatu. Hii yazidisha rangi-mbili kwa kuongeza rangi nyingine yenye kupatana au iliyo kikamilisho cha karibu. Nyekundu, nyekundu-rangi ya chungwa na rangi ya chungwa hufanyiza rangi-tatu zenye kupatana. Kielelezo cha rangi-tatu zenye kukamilishana kingekuwa ni nyekundu pamoja na manjano-kijani kibichi pamoja na buluu-kijani kibichi. Utaratibu mwingine wenye kupendeza, unaoitwa utatu, huunganisha rangi tatu ambazo baina yazo kuna nafasi ya kadiri ile ile kwenye gurudumu la rangi, kama vile zile rangi tatu za msingi—nyekundu, manjano, na buluu. Katika miunganisho hiyo, mara nyingi ni rangi moja tu inayokuwa nyangavu na zile nyingine huwa zimeongezwa, kusawazishwa, au kushikizwa.
Rangi za polikromatiki, au rangi nyingi. Uwe mwangalifu sana ikiwa unaunganisha rangi nne au zaidi. Hutaki kuonekana kama mchekeshaji wa sarakasi. Hata hivyo, mavazi yenye mchanganyiko wa rangi na yenye rangi nyingi ambayo rangi zayo tofauti-tofauti moja haitokezi zaidi ya nyingine ni sawa.
Hatimaye, zilizo peke yazo ni rangi zilizosawazika hudhurungi, kijivu-jivu, rangi kahawia nyeusinyeusi iliyoshika, na wakati mwingine, nyeusi na nyeupe. Taupe (mchanganyiko wa hudhurungi na kijivu-jivu) hukubaliana na karibu kila kitu. Rangi za usawaziko zafaa kwa bidhaa za bei kubwa, kama vile suti, kwa sababu zaweza kuambatana na namna nyingine nyingi. Rangi za usawaziko ndizo viwango vya upendezi vinavyokubaliwa kila mahali.
Usawaziko na Vipimo
Hata uchague muunganisho gani, tazama vizuri usawaziko wa ujumla na uruhusu jicho lako likuongoze. Kuweka sheria-sheria haiwezekani. Jicho huona vipimo kwa njia tofauti kwa kulingana na mambo kama vile nguo iliyotumiwa, mshiko au mng’ao wa rangi, kama rangi hiyo yaonekana upesi kama rangi ya chungwa, au polepole kama kijivu-jivu.
Rangi ambazo moja yatokeza zaidi ya nyingine hazipendezi. Kwa hiyo kwa ajili ya upatano, acha rangi moja itokeze na zile nyingine ziwe za chini, zitegemeze. Hilo lahusu miunganisho yote. Kwa mavazi, asilimia 75 hadi 90 yapasa kuwa ni rangi ile kuu, apendekeza Eiseman. Ukitumia rangi ya tatu katika mavazi yako, hakikisha ni nyonge tu, kiongezeo. Lakini kwa ajili ya upatano kamili, lazima ufikirie ngozi yako, macho yako, nywele zako—wewe.
Kumbuka, pia, kwamba rangi fulani zitakufanya uonekane mnono zaidi, nyingine mwembamba zaidi. Mbuni wa mitindo wa kimataifa Mary Quant asema hivi: “Ikiwa wewe ni mzito juu chagua vazi la juu lenye rangi iliyoshika. . . . Nyonga ni pana zaidi ya ambavyo ungependa? Vuta fikira kwingineko kwa sweta zenye rangi nyangavu. . . . Rangi zilizoshika hupunguza, hafifu hupanua.” Na Carole Jackson apendekeza mbinu hii ya kuwa mwembamba: “Rangi inayokufanya uvutie hufanya utazamwe usoni na si mwili wako.”
Baada ya kushauri wanasiasa wa Japan wafanye wanavyoonekana ivutie, mbuni wa mitindo wa kimataifa Hanae Mori aliongeza hivi: “Hakuna haja ya kujionyesha.” Miongozo hiyo myepesi itakusaidia usiruke mipaka ya kupendeza na bado ufurahie rangi. Haya, chukua hatua uone unaweza kufanyiza nini! Kuna rangi 10,000,000 zinazokusubiri tu uziongeze maishani mwako.
[Maelezo ya Chini]
a Nyekundu, manjano, na buluu ndizo zinazoitwa rangi za msingi. Viongeza rangi, au vitia rangi, vya rangi hizo vyaweza kuchanganywa ili kutokeza rangi-rangi nyinginezo. Kwa upande mwingine, nyekundu, kijani kibichi, na buluu huitwa rangi za msingi katika nuru. Wakati nuru za rangi hizo zinapotupwa kwenye kiwambo, huchanganyikana ili kutokeza rangi nyinginezo.
[Grafu/Picha katika ukurasa wa 17]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
BULUU
NYEKUNDU
MANJANO
Buluu na nyekundu hutokeza zambarau
Nyekundu na manjano hutokeza rangi ya chungwa
Buluu na manjano hutokeza kijani kibichi
[Grafu]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Mipunguzo-punguzo ya Nyekundu
10% 20% 30% 40% 50% 60% 70% 80% 90% 100%
[Picha katika ukurasa wa 19]
Upatanisho wa rangi waweza kuamua unavyoonekana