Makosa ni ya Nani?
“KULEWA kunakubalika” kwa watu wengi katika jamii, asema Jim Vanderwood wa Baraza la Mohawk Valley juu ya Kileo katika Jimbo la New York. Kwa kusikitisha, wachache sana wanaweza kukana kwa kweli kwamba kunywa, hata kupita kiasi, ni sehemu ya jamii yao.
Kwa miaka mingi jamii nyingi zimevumilia unywaji wa kawaida, na hata unywaji wa kupindukia. Hali hiyo imetia moyo wengine waige tabia hiyo ya uendekevu. Kama anavyotaarifu Vanderwood: “Tazama sinema mbalimbali. Sikuzote tumeshangilia watu wanaoweza kunywa mno na bado kwenda kuwa wapiganaji hodari. Kunywa kunaonwa kuwa kitu cha kujipatia uhakika. Waweza kukabilianaje na tabia hiyo?”
Hivyo, ingawa hatia ya msingi inabaki kwa wale wanaolemaza wengine kwa kunywa na kuendesha gari, jamii yenye uendekevu na yenye kujifurahisha na mwelekeo wao usiosawazika kuelekea kileo pia ina hatia kwa kadiri fulani.
“Unywaji haukubaliki tu, bali pia unaendelezwa kwa bidii,” ataarifu ofisa wa kuzuia uhalifu Jim Thompson. Aliambia Amkeni! hivi: “Michezo mingi hutegemezwa na viwanda vya kileo, kama vile kiwanda cha pombe.” Alitaja kwamba wakati wa michezo mingi, “matangazo ya biashara bora zaidi za TV huwa ni matangazo ya pombe, kukiwa na mabingwa mashuhuri wote wa jamii wakisifu bia wazipendazo.”
Mjadala wa serikali chini ya usimamizi wa C. Everett Koop aliyekuwa mkuu wa huduma ya afya wa U.S. wa zamani ulisusiwa na Shirika la Kitaifa la Watangazaji na watangazaji wa biashara. Kwa nini? Kwa sababu mjadala huo ulizungumzia na kuhusisha suala hilo la kuendesha gari chini ya uvutano wa kileo na kuwa na hatia. Dakt. Patricia Waller, aliyesimamia Baraza la Elimu la mjadala huo, alitaarifu hivi: “Uhakika ni kwamba sisi [jamii] tumesababisha tatizo hilo, na watu ni vipofu kiasi cha kutosha kushindwa na ule msongo ambao tumekuwa tukiwawekea tangu walipokuwa na umri wa kutosha kutazama televisheni. ‘Lakini,’ [jamii inasema] ‘sisi hatukusababisha tatizo hilo. Hilo si shauri letu.’”
Kijana Mtenda Makosa Leo—Kesho Mnywaji wa Kupindukia
Unywaji hutukuzwa kupitia njia nyingi kama vile televisheni, sinema, na matangazo ya biashara. Mambo hayo hufikia akili changa na iliyo nyepesi kushika mambo na ujumbe huu, ‘waweza kunywa na kuishi kwa furaha siku zote baadaye.’
“Mtoto wa kawaida ataona kileo kikinywewa mara 75,000 katika TV kabla ya kufikia umri rasmi wa kuanza kunywa,” ataarifu Dakt. T. Radecki wa Muungano wa Kitaifa wa Kupinga Jeuri ya Televisheni Katika United States. Mtafiti Mwingereza Anders Hansen alichunguza TV wakati inapotazamwa na wengi katika Uingereza na kupata kwamba asilimia 71 ya programu zote za hadithi zisizo za kweli hutia ndani unywaji. Kwa wastani, kulikuwa na matukio ya unywaji 3.4 kwa kila saa kukiwa na “mionyesho midogo sana ya unywaji wa kileo yenye matokeo hususa,” kama vile aksidenti za magari na mauaji, akalalamika Hansen.
Akiandikia The Washington Post, Colman McCarthy mwandishi wa safu katika magazeti analieleza wazo hilo hivi: “Jambo linalosababisha kuwaonyesha . . . waliokuwa wanariadha hapo kwanza wakifurahia starehe za kuwa wauzaji katika nyumba za pombe ni matangazo ya kibiashara na kampeni za kuongezea mauzo ya bidhaa ambayo hupangwa kwa njia ya kunasa fikira za watoto na kuwakazia wanunuzi wa koleji wazo la kwamba kunywa kileo, tena kwa wingi, kwahitajiwa sana kwa masilahi ya kijamii. Ebu sikia maoni ya wale vijana wasemao ‘ina ladha nzuri, na haishibishi sana,’ ya kwamba ikiwa wewe hunyanyui glasi, wewe ni mshamba.”
Katika Urusi, kunywa na kuendesha gari ni tatizo kubwa sana la taifa. Maofisa wengine huko hutia shaka kama tabia za unywaji zinaweza kubadilika. “Tabia hiyo imo katika damu ya Warusi,” akasema mmoja. Ingawa huenda hiyo ikawa kweli, kunaonwa na wengi kuwa njia ya tafrija. Hivyo wachanga wenye akili ya kushika mambo haraka hukua katika mazingira ya unywaji.
J. Vanderwood aeleza kwamba United States ina “utamaduni wa vijana wanywaji. Kileo huwa kwa hali moja na mchezo wa softiboli, mchezo wa kurusha mpira, na mpira wa mguu, na saa za furaha. Ikiwa ni tafrija, ni kileo, ikiwa ni kileo, basi ni tafrija.” Yeye asema hivi: “Huenda ukawacha hali hiyo ikiwa haujazoea kileo kisaikolojia, kisosholojia, au kimwili.” Lakini yeye aonya hivi: “Kitu kimoja tunachojua kutokana na utafiti, na kina ushuhuda mwingi ni kwamba ukianza kunywa kupindukia ukiwa na umri wa miaka 14, 15, au 16, waweza kukuza uzoevu katika muda wa mwaka mmoja. Ukianza katika miaka ya mapema ya 20, utakuza uzoevu katika miaka michache.”
Je! inashangaza kwamba kisababishi kinachoongoza cha vifo katika United States kwa watu wenye umri wa miaka 16-24 ni aksidenti za magari zinazosababishwa na kileo? Bila shaka ndicho kisababishi kinachoongoza cha vifo katika nchi nyinginezo nyingi. Hivyo, Dakt. Waller amalizia kwamba wazazi wenye kudhamiria wanaojaribu kulea watoto wao katika mazingira ya nyumbani yanayovutia watoto kwa upande wa utulivu hukabiliwa na jamii yenye uendekevu “inayovuta kuelekea upande” ule mwingine.
Hivyo vijana wa leo wanaokunywa waweza kuwa wanywaji wa daima kesho. Na mara nyingi yeye hawezi kusaidika na mpango wa kumsaidia abadilike, hali ambayo inaleta hatari kubwa kwa usalama wa watu barabarani. Mmoja mwenye kurudiarudia kutenda kosa hilo mwenye umri wa miaka 34, baada ya kupitia programu ya lazima ya serikali kuhusu kileo, alikunywa chakari na kuendesha kilori chake kwa upande mbaya wa barabara kuu ya Kentucky. Aligongana dafurao na basi lililojaa matineja na kufanya watu 27—vijana 24 na watu wakubwa 3—wafe kwa kuteketea. Kwa kweli, imedhibitishwa kwamba zaidi ya watu robo moja ya wale wanaoshtakiwa kuendesha gari wakiwa walevi ni watu waliotangulia kufanya makosa hayo.
Kileo—Dawa ya Kulevya Inayokubalika
Mamlaka nyingi zinaarifu akili ya umma kwa kusema kileo ni dawa ya kulevya inayokubalika (imeidhinishwa kisheria). Wanafananisha kileo na dawa za kulevya nyinginezo.
Kwenye mkutano wa kutoa habari fupi wa White House, rais Bush wa U.S. alitangaza kwamba kuendesha gari ukiwa umepumbaa-pombe “kunadhuru kama dawa ya kulevya ya kraki. Na hutukia ghafula kama jeuri ya majambazi. Na huua watoto wengi kushinda kraki na jeuri ya majambazi zikiwa pamoja.” Pia alikazia kwamba ni “lazima sisi tufundishe watoto wetu kwamba kileo ni dawa ya kulevya.”
Ikiwa wewe hujafikiria kileo kuwa dawa ya kulevya hapo mbeleni, basi hauko peke yako. “Watu wengi hawaoni uhusiano uliopo,” asema C. Graziano, ambaye ni mkurugenzi wa usalama barabarani, akiongezea hivi: “Wanasheria, madaktari, mahakimu. Kileo kinaweza kudhuru mtu yeyote yule . . . kinaweza kupatikana. Na kinapatikana kwa urahisi!” Kwa sababu sheria inakiruhusu katika nchi nyingi, kinaweza kununuliwa katika maduka ya aina tofauti tofauti. Mara nyingi huwa kuna vizuizi vichache tu.
Kitekinolojia, kileo ni chakula kwa sababu kina kalori. Lakini ni lazima pia kionwe kuwa dawa ya kulevya kwa sababu kinadhoofisha mfumo wa neva wa kati. Kikitumiwa kwa wingi, kinakuwa na tokeo la kutia mwili usingizi kama vile dawa ya kulevya ya barbitureti. Kwa sababu ya hali yacho ya “kugeuza tabia, kinapunguza mkazo wa akili,” asema J. Vanderwood. “Kinalegeza hisia zako, kikigeuza namna ya kufikiri kwako. Waona kwamba waweza kutenda na kumbe kwa kweli huwezi.” Hapo ndipo lipo tatizo la kunywa na kuendesha gari. Ni kama vile yeye amalizia: “Una mtu aliyedhoofishwa na pombe akifanya uamuzi uliodhoofika.”
Wengine ambao wamo katika hali ngumu—kama talaka, kupoteza kazi, matatizo ya familia—mara nyingi huamua kunywa chakari ili kujaribu kukabiliana na msongo na mkazo wa akili. Katika hali hiyo wao hutenda “kipumbavu, na kwa njia isiyo ya kujali, kutia ndani kuendesha gari wakiwa wamepumbaa-pombe,” lasema Journal of Studies on Alcohol.
Hata hivyo, kwa habari ya kileo, mtu hahitaji kulewa ili utendaji wake uathiriwe. Chupa moja au mbili tu zatosha kuathiri uamuzi wa dereva na hivyo kumfanya awe tisho kwake mwenyewe na pia kwa wengine.
Pigo hilo kweli kweli ni msiba kwa jamii ambayo imejitia sumu kwa mchanganyiko hatari wa pupa ya kibiashara na mwelekeo wa uendekevu kuelekea kitu ambacho ni halali kisheria lakini kilicho hatari sana. Basi kuna faraja gani kwa wale wanaoomboleza msiba huo? Kuna tumaini gani halisi linaloweza kuwapo la kupata suluhisho?
[Blabu katika ukurasa wa 21)
Matineja ambao ni wanywaji wa kupindukia waweza kukuza uzoevu katika mwaka mmoja
[Blabu katika ukurasa wa 21)
Si lazima mtu alewe ili utendaji wake wa kuendesha gari uathiriwe
[Picha katika ukurasa wa 20]
Unywaji hutukuzwa kupitia njia nyingi kama vile televisheni