Wenye Kupatwa na Msiba Wakabili Wenye Makosa
KIKAO: Halmashauri ya waliopatwa na msiba ya DWI katika Eneo la Genesee Jimbo la Upper New York. Mandhari: Watu sita wakiwa wameunganishwa na huzuni wanayoona na wakiwa wamebeba picha za wapendwa wao, wanashiriki katika jaribio lenye uchungu la kuonyesha washtakiwa wenye kuendesha gari wakiwa wamepumbaa-pombe hasara ya kufanya hivyo.
Zinazofuata ni teuzi za maneno walioyasema, yakifanyiwa muhtasari na Amkeni!
Wenye Kupatwa na Msiba
Baba mmoja: “Huyu ni mwana wetu Eric. Alikuwa kijana mzuri, mfurahifu sana, na mwenye kutabasamu nyakati zote. Sasa mimi ni baba mwenye huzuni, na mwenye majonzi nikiwa na mwana wa miaka 17 aliyekufa. Kwa ghafula tu, ndoto zetu, matumaini yetu ya wakati ujao, na upendo wetu ulitoweka—kauawa na dereva mlevi.
“Mimi na mke wangu huenda makaburini. Ndiyo njia ya mwisho sisi twaweza kumkumbuka. Sisi husoma maneno ya Eric ambayo yameandikwa kwenye kaburi lake: ‘Nitasikitika kuwaacha, na natumaini hatutakuwa tumetenganishwa kwa umbali sana; na iwapo hivyo, nitalia kwa sababu sikutaka kamwe kusema kwaheri.’ Na sisi pia hatutaki kusema kwaheri.”
Mjane mwenye umri mdogo: “Hii ndiyo familia yangu. Mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 22 alitoka kwenye karamu ya arusi akidai kwamba hakuwa amelewa. Akiwa katika kilori chake, na akisafiri kwa mwendo wa kasi kwenye barabara yenye giza na ambayo hakuifahamu, alikaribia ishara ya kutoa onyo na akaipuuza tu, kisha akaendelea kupita ishara ya kusimama na kutugonga. Wakati ninaoweza kukumbuka ni mimi nikipata ufahamu huku nikiwa na msongo wenye maumivu makali kifuani mwangu. Nilipojaribu kufumbua macho, niliweza kumwona mume wangu akiwa amelalia usukani. Nikamsikia mtoto wangu akilia. Nakumbuka nikiuliza, ‘Ni nini kimetukia?’
“Hakuna aliyejibu. Mume wangu, Bill, mwenye umri wa miaka 31; mwana wangu mkubwa zaidi, akiwa na umri wa miaka 6; wavulana wawili mapacha, wenye umri wa miaka 4, walikuwa wamekufa. Tumaini langu pekee lililobaki lilikuwa binti yangu mwenye umri wa miezi tisa, aliyelazwa hospitalini akiwa na majeraha mabaya ya kichwa.
“Nilipokuwa nimelala hospitalini asubuhi moja ya Jumatano yenye mvua na isiyopendeza, mume wangu na wavulana watatu walizikwa. Niliwazia juu ya majeneza manne, miili minne iliyovunjika-vunjika, watu wanne ambao singewaona, kuwasikia, au kuwagusa tena. Mimi nilipaswa niendeleeje?
“Binti yangu mdogo pamoja nami tulilazimishwa kuanzisha maisha mapya. Niliuza makao yangu, kwa vile nilishindwa kuishi na mawazo. Naona vigumu kukabiliana na uhakika wa kwamba mume wangu na wavulana watatu warembo wamo makaburini. Utunzaji, hangaiko, na upendo wote haukutosha kuwalinda. Ule uchungu, mfadhaiko, na upweke ninaohisi hauwezi kuelezeka. Waliishi kwa muda mfupi sana.
“Mtu aliyeua familia yangu hakuwa mhalifu wa kidesturi au mlevi wa kupindukia au mrudia makosa—ni mtu tu wa kawaida aliyetoka jioni kukutana na wengine. Mimi ninapatwa na mabaya hayo kwa sababu mtu fulani alichagua kunywa na kuendesha gari. Hili na lisikutendekee kamwe wala mtu unayempenda.”
Mama mmoja: “Binti yangu anaitwa Rhonda Lynn. Alipaswa kuhitimu kutoka shule ya upili siku ya Juni 21. Siku ya Juni 10 alikuwa akichukua somo lake la mwisho la mtaala wa elimu ya uendeshaji gari. Katika siku hiyo watu wawili waliokuwa wakisherehekea na kunywa chakari waliamua kizembe kuendesha gari. Kwa ghafula, wakafanya siku hiyo iwe ya mwisho ya uhai wa Rhonda, pia na uhai wa mwalimu wake wa elimu ya uendeshaji gari na wanadarasa wawili wenzake.
“Alasiri hiyo nilipokea simu ikisema kwamba Rhonda alihusika katika aksidenti. Wazo langu la pekee lilikuwa kwamba ni lazima niwe naye. Nilipofika hospitalini, niliambiwa nisiingie kumwona Rhonda. Lakini ilikuwa ni lazima niwe na uhakika. Niliwalazimisha waondoe shiti. Uso wake ulivimba mno na kukwaruzwa vibaya. Niliendelea kuangalia macho yake mazuri na kumshika mkono, lakini nisingeweza kufanya mwili wake uliovunjika-vunjika uwe afadhali. Kile ningeweza kufanya tu ni kupapasa-papasa nywele zake nzuri. Hakuitikia. Alikuwa amekufa.
“Nikawa na jukumu gumu la kuambia babake na ndugu zake kwamba alikuwa amekufa. Sasa siku zetu si kama zilivyokuwa kwa sababu ya pengo kubwa aliloacha. Iwapo tu tungeweza kumkumbatia, kumshika mara moja tu zaidi. Maisha hayawezi kamwe kuwa vile yalivyokuwa. Ni mawazo tu ndiyo tumebaki nayo.”
Mkosaji
Mwanamume kijana: “Hadithi yangu ni tofauti na zile ambazo tayari mmekwisha sikia. Inaanzia miezi 23 iliyopita. Naikumbuka kana kwamba ilikuwa jana. Msichana rafiki yangu alikuwa akirusha mpira kwenye mchezo wa shirikisho usiku huo, basi nikaamua ninywe kidogo huku nikimtazama akirusha mpira. Nikanywa glasi tano au sita za pombe kwa saa mbili na nusu zilizofuata. Nikaona nitakuwa timamu na ningoje saa nzima kabla ya kuendesha gari kuelekea nyumbani.
“Karibu dakika 30 za kuendesha gari kuelekea nyumbani, kulikuwa na ambulensi barabarani, na kulikuwa na mwanamume katikati ya barabara akiongoza miendo ya magari. Mimi sikumwona mwanamume huyo mpaka nilipochelewa mno. Nilijaribu kuepa na kukanyaga breki. Kioo changu cha mbele kilipovunjika vipande-vipande, nikajiambia: ‘Afadhali awe ni kulungu au mbwa!’ Lakini nilijua haikuwa hivyo. Nilitoka nje ya gari nikamkaribia huku nikipiga kelele, ‘Umeumia? Umeumia?’ Hakunijibu. Nakumbuka nikisimama kando yake, nikitazama uso wake. Ulikuwa katika hali mbaya sana.
“Askari wakaja wakaniuliza maswali. Kisha wakasema: ‘Kweli kweli unashirikiana nasi vizuri, lakini wewe watembea kwa njia isiyo ya kawaida na unasema kwa njia isiyo ya kawaida. Je! umekuwa ukinywa?’ Wakanipeleka kwenye kituo cha polisi na kunipima. Nilikuwa na kileo cha kiwango 0.08 [Hicho ni kiwango ambacho hakikubaliki katika sehemu nyingi za United States]. Sikuamini kwamba jambo hilo lilikuwa likitokea kwangu. Nilikuwa nadhani kwamba jambo kama hilo halingenitokea kamwe. Na sasa nilikuwa nakabili mashtaka ya uhalifu wa kuua kwa kutokujali, DWAI [“Driving While Ability Impaired” au Kuendesha Hali Uwezo Wako Umepunguka].
“Kulikuwa kumebaki mwezi mmoja tu kabla nipate cheti changu cha kufundisha. Fikiria jinsi jamii huona walimu. Wanawatarajia hao kuwa na maadili yasiyo na waa. Ndilo jambo nililokuwa nikifanyia kazi, na sasa nilikuwa natazamia kulipoteza.
“Nilihukumiwa kifungo cha nje cha mwaka mmoja, nikapoteza leseni yangu ya kuendesha gari kwa muda wa miezi 19, kutozwa faini ya dola 250, kufungwa gerezani mwisho juma mmoja, nikafanya saa 600 za utumishi wa jamii, na kupitia mafunzo ya mashauri juu ya kileo kwa muda wa majuma tisa. Zaidi ya hayo, nakumbuka masiku yale ningeweza kuamka nikitetemeka, picha ya uso wa yule mtu ikiwa akilini mwangu. Na ilikuwa ni lazima nirudi nikutane na rafiki zangu wote na familia yangu. Ilionekana kwamba kuendeleza maisha yangu kulihitaji jitihada nyingi sana. Sikuwa na uhakika kama jitihada hiyo ilistahili kufanywa. Ilikuwa ni lazima nirudi kufundisha wanafunzi na kuwatazama wanafunzi hao wote. Singeweza kujizuia kufikiria kwamba ni wangapi kati yao waliojua nilichotenda. Na nilijawa na hatia na majuto kuelekea familia ya mtu huyo.
“Usiku wa aksidenti hiyo, nilihitaji kufanya jambo gumu zaidi ambalo nimepata kufanya kwa wakati wowote maishani mwangu—kumpigia simu mama yangu na kumwambia, ‘Mama, niliua mtu katika aksidenti. Nahitaji lifti kurudi nyumbani.’ Alipokuja, tulikumbatiana tu na kulia. Nisingependa hata adui yangu wa mwisho apitie nilichopitia. Watu wanaokunywa na kuendesha gari—hilo ni tatizo ningependa kusaidia kutatua. Unapotoka kwenye mkutano huu, uende ukitukumbuka. Usitusahau kamwe.”
Halmashauri Hiyo Yamalizia
Patricia Johnston, mratibu wa halmashauri hiyo ya wenye kupatwa na msiba, alimalizia na oni lake mwenyewe la msiba wa aksidenti uliompata baba yake mlevi. Yeye alisema: “Ikiwa ningeweza kuweka majonzi yanayosababishwa na kileo katika chupa na kuifanya iwe ‘kinywaji cha kunywewa kabla tu ya kuendesha gari’ kusingekuwa kamwe haja ya programu kama hii!”
Mwishowe, mwamuzi aliuliza kama yeyote alikuwa na maswali. Hakuna maswali yaliyoulizwa. Lakini kulikuwako wengi wenye machozi waliosema: “Hamtasikia kamwe kwamba ninakunywa na kuendesha gari tena.”
Kupita kwa wakati tu ndiko kutaonyesha halmashauri hizo zitapata matokeo gani katika kufanya wakosaji waliokamatwa wasirudierudie kuendesha magari wakiwa walevi. Lakini linalofanya tatizo hilo litie hofu ni idadi kubwa sana, mamilioni, ya wale ambao huendesha magari wakiwa wamedhoofishwa na pombe na wasikamatwe.
Ripoti za hivi karibuni kutoka kwa Ofisi ya Serikali ya Takwimu za Hukumu ya Idara ya Hukumu ya U.S. zilionyesha kwamba katika mwaka mmoja wa hivi majuzi, karibu watu milioni mbili walikamatwa kwa kosa la DUI (“Driving Under the Influence” au Kuendesha Gari Ukiwa Umeathiriwa na Pombe). Lakini takwimu zilionyesha pia kwamba kila mmoja anayeshikwa kwa kosa la DWI (“Driving While Intoxicated” au Kuendesha Gari Ukiwa Umepumbaa-Pombe), wengi kufikia zaidi ya 2,000 huenda wakaendesha bila kupatikana katika maeneo ambayo hamna polisi, hesabu zinazongoja kutokeza wajeruhiwa.
Ni nini kimeleta hali hii inayochochea matendo hayo yaliyo hatari na ya kutokujali? Kwa nini vita dhidi ya unywaji na uendeshaji gari inaendelea kupiganwa lakini isishindwe? Hebu tuone baadhi ya majibu.
[Picha katika ukurasa wa 18]
Mtenda makosa aliyeamuriwa kukabili halmashauri ya wenye kupatwa na msiba