‘Mabadiliko Makubwa Zaidi’
“Karne ya 20 imepatwa na mabadiliko makubwa na yenye kuenea zaidi kuliko karne yoyote katika historia ya binadamu.” —The Times Atlas of the 20th Century.
TUNAPOTAFAKARI juu ya karne ya 20, bila shaka wengi watakubaliana na Walter Isaacson, mhariri msimamizi wa gazeti Time, ambaye alisema: “Kwa kulinganishwa na karne nyinginezo, karne hii imekuwa mojawapo ya karne zenye kushangaza zaidi: yenye kutokeza, nyakati nyingine yenye kutisha, yenye kuvutia sana sikuzote.”
Hali kadhalika, Gro Harlem Brundtland, aliyekuwa waziri mkuu wa Norway, asema kwamba karne hii imeitwa “karne yenye hali zinazopita kiasi, . . . ambapo kumekuwa na uovu wa kibinadamu usio na kifani.” Asema kwamba imekuwa “karne ya maendeleo makubwa [na katika sehemu fulani ya] ukuzi wa kiuchumi usio na kifani.” Hata hivyo, wakati huohuo, maeneo ya mjini yenye umaskini yanakabili wakati ujao usio na tumaini wenye “idadi kubwa ya watu na visa vya maradhi yanayoletwa na umaskini na mazingira yasiyofaa.”
Mabadiliko Makubwa ya Kisiasa
Karne ya 20 ilipoanza, nasaba ya wafalme ya Manchu katika China, Milki ya Waturuki, na milki kadhaa za Ulaya zilidhibiti sehemu kubwa ya ulimwengu. Milki ya Uingereza pekee ilidhibiti robo moja ya tufe na kutawala mtu 1 kati ya watu 4 duniani. Muda mrefu kabla ya karne hiyo kwisha, milki hizo zote hazikuwapo tena. “Mnamo 1945,” chasema kichapo The Times Atlas of the 20th Century, “enzi ya ubeberu ilikuwa imekwisha.”
Kuporomoka kwa ukoloni kulitokeza ongezeko la utukuzo wa taifa lililoenea Ulaya kote kati ya karne ya 17 na ya 19 na kufikia sehemu nyingine za ulimwengu. Kichapo The New Encyclopædia Britannica chasema: “Baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili shauku nyingi ya uzalendo ilipungua katika mataifa mengi ya Ulaya . . . Hata hivyo, katika Afrika na Asia, utukuzo wa taifa ulikua haraka, hasa ikiwa ni itikio dhidi ya ukoloni.” Hatimaye, kulingana na The Collins Atlas of World History, “Nchi Zinazositawi zilikuwa zimejitokeza kwenye mandhari ya kihistoria, na enzi iliyoanza karne tano mapema kukiwa na mwanzo wa upanuzi wa Ulaya, sasa ilikuwa imefikia kikomo.”
Milki zilipoporomoka, mataifa huru yaliibuka—mengi yakiwa serikali za kidemokrasia. Mara nyingi, utawala wa kidemokrasia ulipingwa vikali na serikali kama zile za kiimla zenye nguvu katika Ulaya na Asia katika Vita ya Ulimwengu ya Pili. Tawala hizo zilizuia uhuru wa kibinafsi na kudhibiti kwa nguvu uchumi, vyombo vya habari, na majeshi. Hatimaye jitihada zao za kuutawala ulimwengu zilikomeshwa, lakini ni baada tu ya kutumia pesa nyingi na kuangamiza wanadamu wengi.
Karne ya Vita
Kwa kweli, jambo hususa linalofanya karne ya 20 iwe tofauti na karne nyingine za awali ni vita. Mwanahistoria Mjerumani Guido Knopp aandika hivi kuhusu Vita ya Ulimwengu ya Kwanza: “Agosti 1, 1914: Hakuna mtu aliyewazia kwamba karne ya 19 iliyokuwa imewapa Wazungu kipindi kirefu cha amani iliisha siku hiyo; na hakuna mtu aliyetambua kwamba kwa kweli karne ya 20 ilikuwa imeanza tu wakati huo—kikiwa kipindi cha vita kilichodumu kwa miongo mitatu na kuonyesha uhaini ambao mwanadamu anaweza kuwafanyia wanadamu wenzake.”
Hugh Brogan, profesa wa historia, alitukumbusha kwamba “vita hiyo iliathiri sana Marekani, ilifadhaisha, na bado inahisiwa leo [katika mwaka wa 1998].” Profesa wa historia katika Chuo Kikuu cha Harvard, Akira Iriye, aliandika: “Vita ya Ulimwengu ya Kwanza ilikuwa tukio kubwa lililobadili historia ya Asia Mashariki na Marekani kwa njia nyingi.”
Basi yaeleweka ni kwa nini kichapo The New Encyclopædia Britannica chataja vita ya ulimwengu ya kwanza na ya pili kuwa “mabadiliko makubwa ya karne ya 20 ya historia ya siasa ya nchi.” Kinasema kwamba “Vita ya Ulimwengu ya Kwanza iliongoza kwenye kuporomoka kwa nasaba nne kubwa za kifalme . . . , ikatokeza Mapinduzi ya Bolsheviki katika Urusi, na . . . kuweka msingi wa Vita ya Ulimwengu ya Pili.” Pia kinatuambia kwamba karibu vita vya ulimwengu viwe “bila kifani katika uuaji, umwagaji-damu, na uharibifu.” Hali kadhalika Guido Knopp asema hivi: “Ukatili na unyama wa kibinadamu ulizidi mataraja mabaya zaidi. Kwenye mitaro . . . mbegu zilipandwa kwa ajili ya muhula ambao wanadamu walionwa kuwa vitu, wala si watu.”
Ili kuzuia vita zaidi vya namna hiyo vyenye kuleta msiba, Ushirika wa Mataifa ulianzishwa mnamo mwaka wa 1919. Uliposhindwa kutimiza mradi wake wa kudumisha amani duniani, mahali pake palichukuliwa na Umoja wa Mataifa. Ijapokuwa UM umefaulu kuzuia vita ya ulimwengu ya tatu, ulishindwa kuzuia Vita Baridi, ambayo kwa miongo kadhaa ilielekea kuongezeka na kuwa maangamizi ya nyuklia. Wala haujazuia mapambano madogo zaidi ulimwenguni kote, kama vile katika Balkani.
Kadiri idadi ya mataifa inavyoongezeka ulimwenguni, ndivyo na ugumu wa kudumisha amani miongoni mwao. Ulinganifu wa ramani ya kabla ya Vita ya Ulimwengu ya Kwanza na ramani ya kisasa wafunua kwamba mwanzoni mwa karne, angalau mataifa 51 ya Afrika na 44 ya Asia yaliyoko sasa hayakuwepo wakati huo. Kuhusu washiriki wa sasa 185 wa Umoja wa Mataifa, 116 hawakuwako wakiwa nchi huru UM ulipoanzishwa mwaka wa 1945!
“Mojawapo ya Mambo Yenye Kutazamisha Zaidi”
Karne ya 19 ilipokuwa ikikaribia kumalizika, Milki ya Urusi ndiyo iliyokuwa mamlaka iliyotawala sehemu kubwa zaidi ulimwenguni. Lakini ilikuwa ikipoteza utegemezo wake haraka sana. Kulingana na mtungaji Geoffrey Ponton, watu wengi walifikiri kwamba “mapinduzi badala ya marekebisho yalikuwa ya lazima.” Aongezea hivi: “Lakini ni kufuatia vita kubwa, Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, na mchafuko uliofuata baadaye, ndipo mapinduzi halisi yalipoanza kwa ghafula.”
Wabolsheviki walipopata mamlaka huko Urusi wakati huo msingi wa milki mpya uliwekwa—Ukomunisti wa ulimwengu uliofadhiliwa na Muungano wa Sovieti. Ijapokuwa ulianzishwa katikati ya vita ya ulimwengu, Milki ya Sovieti haikuishia vitani. Kitabu cha Michael Dobbs Down With Big Brother, chadai kwamba mwisho-mwisho wa miaka ya 1970, Muungano wa Sovieti ulikuwa “milki kubwa sana yenye mataifa mengi ambayo tayari ilikuwa ikididimia katika hali isiyoweza kurekebika.”
Hata hivyo, anguko lake lilikuja kwa ghafula. Kitabu Europe—A History, cha Norman Davies, chaeleza: “Mwendo wa anguko lake umeshinda maanguko mengi makubwa katika historia ya Ulaya,” na “lilitokezwa na visababishi vya asili.” Kwa kweli, “kuibuka, kukua na kuporomoka kwa Muungano wa Sovieti,” asema Ponton, kulikuwa “mojawapo ya mambo yenye kutokeza zaidi ya karne ya ishirini.”
Kwa kweli, kuporomoka kwa Muungano wa Sovieti kulikuwa mojawapo ya mabadiliko makubwa ya karne ya 20 ambayo yamekuwa na matokeo yenye kuenea kote. Bila shaka, mabadiliko ya kisiasa si mambo mapya. Yamekuwa yakitukia kwa maelfu ya miaka.
Hata hivyo, badiliko moja la maana sana hasa katika karne ya 20 linahusu serikali. Badiliko hilo na jinsi linavyokuathiri kibinafsi litazungumziwa baadaye.
Ingawa hivyo, ebu tuzungumzie kwanza, baadhi ya mafanikio ya sayansi katika karne ya 20. Kuhusu mafanikio hayo, Profesa Michael Howard amalizia hivi: “Watu wa Magharibi mwa Ulaya na Amerika Kaskazini walikuwa na sababu ya kukaribisha karne ya ishirini ikiwa mwanzo wa enzi mpya na yenye furaha zaidi katika historia ya mwanadamu.” Je, maendeleo hayo yangeongoza kwa yale yanaoitwa eti maisha ya hali ya juu?
[Chati/Picha katika ukurasa wa 2-7]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
1901
Malkia Victoria afa baada ya kutawala kwa miaka 64
Idadi ya watu ulimwenguni yafikia bilioni 1.6
1914
Dyuki -mkuu Ferdinand auawa. Vita ya ulimwengu ya kwanza yaanza
Zari wa mwisho, Nicholas wa Pili, pamoja na familia yake
1917
Lenin aongoza Urusi kwenye mapinduzi
1919
Ushirika wa Mataifa waanzishwa
1929
Kuporomoka kwa soko la hisa la Marekani kwa sababisha Mshuko Mkubwa wa Kiuchumi
Gandhi aendelea kupigania uhuru wa India
1939
Adolf Hitler avamia Poland, na kuanzisha Vita ya Ulimwengu ya Pili
Winston Churchill awa waziri mkuu wa Uingereza mwaka wa 1940
1941
Japani yapiga bomu Pearl Harbor
1945
Marekani yaangusha mabomu ya atomu huko Hiroshima na Nagasaki. Vita ya Ulimwengu ya Pili yaisha
1946
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lafanya mkutano wa kwanza
1949
Mao Tse-tung atangaza Jamhuri ya Watu wa China
1960
Mataifa mapya 17 ya Afrika yaanzishwa
1975
Vita ya Vietman yaisha
1989
Ukuta wa Berlin wabomolewa huku ukomunisti ukipoteza uwezo wake
1991
Muungano wa Sovieti wavunjika