Chini ya Ardhi ya Paris
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UFARANSA
NAPIGA nambari, nikitumaini kwa hamu kwamba mtu fulani atajibu simu. “Halo! Halo!” nasema. “Funguo zangu za gari zimetumbukia bombani! Tafadhali njooni upesi!” Kikosi maalumu cha wafanyakazi wa mabomba ya maji machafu chawasili mara moja. Kazi yao ni kuzibua mabomba ya maji machafu, kuondoa maji kwenye maghala ya chini ya ardhi yaliyofurika, na kutafuta funguo, miwani, vibeti, na hata wanyama vipenzi ambao hupotea kwa kawaida katika mabomba yapatayo 18,000 huko Paris. Wao wanapata funguo zangu, nashusha pumzi na kuwashukuru sana.
Siku ifuatayo naamua kuzuru Musée des Égouts (Jumba la Makumbusho la Mabomba ya Maji Machafu) lililoko kwenye Ukingo wa Kushoto wa Mto Seine, unaoelekeana na mashua zetu mashuhuri za kuvinjari mtoni na chini ya Eiffel Tower. Kwa miaka ipatayo 130, watu wengi wamezuru chini ya ardhi ya Paris. Naelewa sababu kwa kufuata kielelezo cha zaidi ya watu 90,000 wenye kupendezwa ambao huzuru jumba hili la makumbusho la pekee kila mwaka. Jiunge nami nichunguzapo kwa makini zaidi kile ambacho mwandishi Mfaransa wa karne ya 19 Victor Hugo alikiita “Matumbo ya Leviathani”—mabomba ya maji machafu ya Paris.
“Matumbo” Yanayofikika
Nikisha shuka meta tano chini ya ardhi, naona ushahidi wa kwanza wa jumba la maonyesho—panya mfu aliyejazwa vitu ngozini. Anatisha kweli! Inasemekana kwamba kuna panya watatu kwa kila mkazi wa Paris, wanaomeng’enya hata sumu kali zaidi kwa njia nzuri ajabu. Kwa hakika wanalishwa vizuri. Kila siku panya hao hunyafua tani 100, au thuluthi ya taka zilizo mabombani.
Mawe, misumari, funguo, na vitu vingine vizito huchanganyika na maji machafu na maji ya mvua, na kuziba mabomba. Kukiwa na mvumo wa maji yanayotiririka, nachunguza mashine zinazosafisha sehemu ya “utumbo” huu mkubwa yenye umbali wa kilometa 2,100. Kila mwaka, takriban wafanyakazi elfu moja wa mabomba ya maji machafu huzoa kyubiti meta 15,000 za takataka. Utusitusi, manyunyu ya maji machafu yenye kuchukiza, kuta zenye utelezi, na kuongezeka ghafula kwa kiasi cha maji kwaweza kufanya kazi ya mfanyakazi wa mabomba ya maji machafu iwe ngumu sana.
Isitoshe, mifereji mingi ya kupitishia maji safi, nyaya za simu, na nyaya za taa za kuongozea magari hujipindapinda kwenye sehemu ya juu ya mabomba ya maji machafu.
Waroma Ndio Waanzilishi
Waroma ndio waliotengeneza mabomba ya maji machafu kwa mara ya kwanza katika Paris. Mabomba ya maji machafu yenye urefu wa meta 18 yaliyotengenezwa na Waroma yangali yamezikwa katika magofu ya mabafu ya Waroma ya maji moto katika Ukingo wa Kusini wa Mto Seine. Lakini Milki ya Roma ilipoporomoka, usafi wa kiafya haukuzingatiwa. Kwa karne nyingi jiji la Paris lilibaki likiwa chafu na hatari kwa afya, kukiwa na mabomba machache tu ya maji machafu (mabomba yaliyo katikati ya barabara) au mitaro inayopitisha maji machafu. Mitaro hiyo ilitoa uvundo na kueneza maambukizo. Mnamo mwaka wa 1131 mwana wa kwanza wa Mfalme Louis wa Sita alikufa kutokana na ambukizo baada ya kuanguka katika bomba wazi la maji machafu.
Takataka zilitupwa katika mitaro isiyofunikwa, na pia katika mitaro michache iliyofunikwa iliyotengenezwa karibuni, ambayo ilizibwa na uchafu kwa urahisi. Na jambo baya hata zaidi ni kwamba maji ya Mto Seine yalipoongezeka, mabomba ya maji machafu yalisambaza matope yenye uvundo na takataka. Nyakati hizo, mfumo wa Paris wa kuchukua maji machafu haukutosha. Mnamo mwaka wa 1636 mabomba ya maji machafu yalikuwa na urefu wa kilometa 23 tu na yalihudumia watu 415,000. Karne moja na nusu baadaye, urefu wake uliongezeka kwa kilometa tatu tu. Mabomba hayo yalikuwa yameziba kabisa wakati wa Napoléon.
Katika karne ya 19, mabomba yaliyokuwapo ya maji machafu yalichunguzwa na ramani kuchorwa. Uchunguzi ulionyesha kwamba kulikuwa na njia zipatazo mia mbili za chini ya ardhi, nyingi zake hazikuwa zimejulikana hapo awali. Tani nyingi za matope ya kale sana ziliondolewaje? Uvumi wa kwamba vito vya thamani vingepatikana chini ya barabara za Paris ulienea kote. Kwa hiyo, watafutaji wa hazina wenye pupa wakaja kwa wingi. Walitembea matopeni, wakizoa sarafu, vito, na silaha.
Kukarabati Mabomba ya Maji Machafu
Hatimaye mabomba ya maji machafu yalifanyiwa ukarabati, yakafanywa kuwa ya kisasa, yakarefushwa, na kuunganishwa kwa kila nyumba. Mabomba makubwa vya kutosha kuweza kukabiliana na mafuriko yalitumiwa. Katika mwaka wa 1878, mitaro yenye urefu wa kilometa 650 inayopitika kwa chombo ilipitia chini ya vyumba vikubwa vya ardhini. “Mabomba hayo ni safi, . . . yameboreshwa,” akaandika Victor Hugo.
Ukubwa wa mfumo huo uliongezeka maradufu katika karne ya 20. Mabomba ya maji machafu yakapata kuwa mfano halisi wa jiji. Jinsi gani? Kila bomba limepewa jina la barabara linakopitia na nambari ya jengo lililo juu yake. Mradi wa ukarabati wenye thamani ya dola za Marekani milioni 330 ulioanza mwaka wa 1991 umeboresha zaidi mfumo huo. Ukarabati wa miaka kumi wa mfumo huu muhimu, unaopitisha kyubiti meta milioni 1.2 za maji kila siku, unatia ndani uwekaji wa vifaa vinavyosafisha moja kwa moja na vidhibiti vinavyoendeshwa na kompyuta.
Nafikia mwisho wa ziara yangu, nikiwa na hamu ya kutoka bombani ili nipumue hewa safi ya Paris. Hata hivyo, sijafikia mwisho wa safari yangu ya kuvinjari chini ya ardhi. “Ukitaka kuona sehemu ya Paris ya chini zaidi ardhini, zuru mapango ya kuzikia watu,” apendekeza mwuza-tunu mmoja. “Mifupa ya watu milioni sita imerundikwa kwenye kina cha [meta 20] ardhini.” Ilitoka wapi?
Makanisa Yaisumisha Hewa
Mifupa ya watu ilirundikwa katika mapango ya Paris ya kuzikia watu—makaburi yaliyo chini ya ardhi—katika karne ya 18 tu. Kuanzia Enzi za Kati, watu walizikwa ndani au karibu na makanisa. Makanisa yalichuma fedha kutokana na zoea hilo japo lilikuwa hatari sana kwa afya, kwa kuwa eneo la makaburi lilikuwa katikati ya mji. Watu walioishi karibu na eneo kubwa zaidi la makaburi la Saints-Innocents katika Paris, lenye ukubwa wa mita mraba 7,000, waliteseka sana, kwa kuwa miili ya wafu kutoka kwa takriban makanisa 20 pamoja na maiti nyingine zisizotambuliwa na maiti za watu waliokufa kutokana na tauni zilizikwa hapo.
Mnamo mwaka wa 1418, kulikuwa na maiti zipatazo 50,000 za watu waliokufa kutokana na Tauni ya Karne ya 14. Mnamo mwaka wa 1572, maelfu ya maiti za watu waliouawa katika machinjo ya Siku ya Mtakatifu Bartholomayo zilijazwa kabisa katika makaburi ya Saints-Innocents.a Kwa ujumla umma ulidai eneo hilo la makaburi lifungwe. Takriban miili milioni mbili, nyakati nyingine ikiwa imerundikwa kufikia kina cha meta 10, iliinua usawa wa ardhi kwa zaidi ya meta 2. Eneo hilo la makaburi lilisambaza sana maambukizo, na kutokeza uvundo mbaya kupindukia, ambao yaaminika uliweza kuchachusha maziwa au divai. Hata hivyo, makasisi walipinga vilio vya kufunga makaburi hayo ya jijini.
Mwaka wa 1780 kaburi la jumuiya lilipasuka na maiti zikatapakaa kwenye vyumba vingine vya ardhini vilivyo karibu. Watu walishindwa kuvumilia zaidi! Eneo hilo la makaburi likafungwa; na kuzika watu Paris, kukapigwa marufuku. Maiti zilihamishwa kutoka katika makaburi ya ujumla na kuzikwa kwenye machimbo yasiyotumiwa ya Tombe-Issoire. Misafara yenye kutisha ilihamisha mifupa kila usiku kwa muda wa miezi 15. Uhamishaji huo ulitia ndani maeneo mengine 17 ya makaburi na sehemu 300 za ibada. Mifupa hiyo ilimwagwa kwenye shimo lenye kina cha meta 17.5, ambamo sasa mna ngazi inayoanzia barabarani hadi shimoni kwenye mapango ya kuzikia watu.
Kuzuru Mapango ya Paris ya Kuzikia Watu
Kutoka kwenye Uwanja wa Denfert-Rochereau, upande wa kusini wa Ukingo wa Kusini wa Mto Seine, ndipo nishukapo kwa vidato 91 vinavyoelekea mapangoni. Mnamo mwaka wa 1787 wanawake wa makao ya mfalme walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutembelea eneo la makaburi lililo chini ya ardhi kwa kutumia nuru ya mienge. Leo, wageni wapatao 160,000 huzuru eneo hilo kila mwaka.
Baada ya ngazi kuna safu ya mapango yanayoonekana kuwa bila mwisho ambamo maiti huhifadhiwa. Natembea kwa uangalifu, nikifikiria uhakika wa kwamba mapango hayo yako katika eneo lenye ukubwa unaozidi meta za mraba 11,000. Mwanamume aitwaye Philibert Aspairt alitafuta sifa ya pekee alipojaribu kupitia vijia hivi vyenye umbali wa mamia ya kilometa. Mnamo mwaka wa 1793 alipotea katika mzingile huo. Kiunzi chake kilipatikana miaka 11 baadaye, kilitambuliwa kwa sababu ya funguo zake na mavazi.
Takriban asilimia 30 ya eneo la chini ya ardhi ya Paris limechimbwa. Kazi ya uchimbaji haikudhibitiwa kwa muda mrefu. Hata hivyo, mnamo mwaka wa 1774, sehemu ya barabara ya rue d’Enfer yenye umbali wa meta 300 (Barabara ya Hell, sasa ni Denfert-Rochereau) iliporomoka kwenye shimo refu lenye kina cha meta 30. Jiji la Paris lilikuwa katika hatari ya kuporomoka. Mawe “tunayoyaona yakiwa yamechomoza juu ya ardhi,” akatamka ghafula mwandikaji mmoja, “yanadhoofisha misingi.” Matao yenye kuvutia yalijengwa ili kutegemeza vijia vilivyo ardhini.
“Inasikitisha kwamba walipokuwa wakijenga vijia vilivyo ardhini hawakuvitia lami,” nalalamika, nitazamapo viatu vyangu vyenye tope. Nateleza topeni, kisha nafaulu kujishikilia kwenye mlango mzito wa shaba. Nyuma ya mlango huo kuna ujia wenye kuta zilizojengwa kwa mifupa ya wanadamu. Mafuvu ya vichwa yaliyokunjamana na mifupa ya mapaja na miundi myepesi iliyopangwa kwa safu na kwa umbo la misalaba na shada za maua hufanyiza mandhari yenye kuogofya. Mistari ya Biblia na mashairi yanayodhihirisha maoni ya mwanadamu juu ya kusudi la uhai na kifo yamechongwa kwenye mabamba.
Niondokapo kwenye mapango ya kuzikia watu, nasafisha viatu vyangu mferejini ili kuondoa tope, huku nikihakikisha kwamba funguo zangu hazitatumbukia tena katika mabomba ya Paris ya maji machafu! Ziara yangu kwenye sehemu yenye kuvutia sana ya chini ya ardhi ya Paris ni jambo la pekee sana ambalo nitalikumbuka kwa muda mrefu. Bila shaka, jiji la Paris lina mengi zaidi kuliko linavyoonekana kijuujuu.
[Maelezo ya Chini]
[Picha katika ukurasa wa25]
Sehemu wazi ya mabomba ya Paris ya maji machafu
[Hisani]
Valentin, Musée Carnavalet, © Photothèque des Musées de la Ville de Paris/Cliché: Giet
[Picha katika ukurasa wa 25]
Kuzuru mabomba ya maji machafu
[Hisani]
J. Pelcoq, Mashua, Musée Carnavalet, © Photothèque des Musées de la Ville de Paris/Cliché: Giet
[Picha katika ukurasa wa 25]
Mabomba ya Paris ya maji machafu kwa sehemu
[Hisani]
Ferat, Musée Carnavalet, © Photothèque des Musées de la Ville de Paris/Cliché: Briant
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mafuvu ya vichwa yaliyokunjamana na miundi myepesi iliyopangwa kwa safu na kwa umbo la misalaba na shada za maua
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mwandiko huu uko mbele ya mlango wa kutokea: “Kichomi kinachotokeza kifo ni dhambi.”—1 Wakorintho 15:56, “King James Version”
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mashine za kusafishia mabomba ya maji machafu
[Picha katika ukurasa wa 24]
Ramani zilizoonyeshwa kwenye ukurasa wa 24-27: Encyclopædia Britannica/9th Edition (1899)