Kuutazama Ulimwengu
Upungufu wa Wazazi Wenye Ustadi
Uchunguzi wa kwanza wa kitaifa huko Kanada unaonyesha kwamba “[wazazi] wengi hawana hata ujuzi wa msingi wa ukuzi wa watoto na hata hawajui namna wazazi wanavyoweza kuchangia ukuzi huo,” lasema gazeti la National Post. Asilimia 92 ya akina “baba, mama, na mama wasio na wenzi zaidi ya 1,600 waliochunguzwa wenye watoto walio na umri wa chini ya miaka sita,” walikiri kwamba kuwa mzazi ndilo jambo muhimu zaidi wawezalo kufanya. Na bado, “idadi isiyozidi nusu walitambua kabisa kwamba wanaweza kuboresha uwezo wa akili wa watoto wao kwa kuwasomea, kucheza nao, kuwagusa, au kuwakumbatia.” Kwa kuongezea, takriban asilimia 30 “wanaamini kwamba kila mtoto mchanga huwa na uwezo fulani wa akili anapozaliwa, ambao hauwezi kuboreshwa au kupunguzwa na jinsi ambavyo wazazi huwatendea.” Matokeo hayo yanatisha, lasema gazeti la Post, kwa kuwa utafiti unaonyesha kwamba “miaka mitano ya kwanza ya mtoto ni muhimu sana katika kukuza uwezo wake wa kusoma, kubuni, kupenda, kutumaini, na kukuza hisia yenye nguvu ya kujistahi.”
Kanisa Kujitenga na Serikali Huko Sweden
Kanisa la Sweden limetangaza kwamba litajitenga na Serikali Januari 1, 2000. Hatua hiyo itavunja uhusiano ambao umekuwapo kati yake na serikali ya Sweden tangu karne ya 16. “Kufikia Januari mosi 1996 watoto wameweza kuwa washiriki wa Kanisa la Sweden punde baada ya kuzaliwa, mradi tu mzazi mmoja alikuwa mshiriki,” yasema habari rasmi ya kanisa hilo katika Internet. “Ubatizo haukuhitajiwa.” Badiliko hilo liliidhinishwa na serikali ya Sweden mnamo 1995 baada ya sinodi ya kanisa kujadili na kutetea badiliko hilo kwa miongo minne. Takriban asilimia 88 ya watu wa Sweden ni washiriki wa Kanisa la Sweden.
Jeuri Dhidi ya Kompyuta
“Wewe hufanya nini kompyuta yako inaposhindwa kufanya kazi unayotaka ifanye?” lauliza gazeti la Ujerumani la kompyuta PC Welt. “Je, wewe huigonga kompyuta? Au wewe huitupa nje kupitia dirishani mara moja?” Maitikio hayo ni ya kawaida. Uchunguzi wa ulimwenguni pote wa mameneja 150 wa tekinolojia ya kompyuta, ulionyesha kwamba asilimia 83 hushikwa na hasira kali au huitendea kompyuta jeuri ya wazi. Watumiaji wa kompyuta wanaokatishwa tamaa na muda mrefu ambao kompyuta hutumia kuleta ujumbe au na usukani wa kompyuta unaokwama nyakati nyingine huvunjavunja kiwambo, hupiga ngumi kibodi, hugongesha usukani kwenye ukuta, au hata hupiga teke kompyuta. Ingawa kompyuta huelekezewa hasira inayotokana na kukata tamaa kwa mtumiaji, mara nyingi tatizo hilo husababishwa na mtumiaji huyo. Kwa mfano, mfanyakazi mmoja alikasirikia programu yake ya E-mail kwa sababu haikuweza kupeleka jumbe. Baadaye iligunduliwa kwamba badala ya kuingiza anwani ya E-mail, alikuwa ameingiza anwani ya mtaa.
Mavazi Yaletayo Mafanikio
Unapojitayarisha kwa mahoji ya kazi, ni vema kukumbuka kwamba “watu waliovalia nadhifu huonwa kwa njia inayofaa,” lasema gazeti la Toronto Star. Kwa sababu wazo la kwanza ndilo hudumu kwa muda mrefu. Kwa hiyo, “maoni ya kawaida ya wale wanaohusika na biashara ni kwamba: Ikiwa hujali sura yako, basi mkataa ni kwamba wewe ni mtu asiyejali,” yasema ripoti hiyo. Wataalamu wanasema kwamba mtu aliye nadhifu na safi anatoa uhakikishio pasipo neno kwamba wale wanaotazamia kuwa waajiri au wateja wake wanaweza kutarajia huduma bora. Washauri wa sura hukazia pia kwamba “kusimama wima na kuwa jasiri hutoa wazo la kwanza lenye nguvu. Namna yako ya sauti na mwendo wa kuongea huathiri sana matokeo.”
Maharamia wa Siku ya Kisasa
“Kwa wazi uharamia ndilo tisho kuu zaidi kwa meli leo,” laripoti gazeti la International Herald Tribune. Mashambulizi ya maharamia yanaongezeka, hasa katika bahari zilizo Kusini-mashariki ya Asia, hasa yanasababishwa na kupungua kwa ulindaji doria wa jeshi la wanamaji katika eneo hilo. Bahari hii, yenye milangobahari ya meli yenye shughuli nyingi zaidi ulimwenguni, huwa na maharamia wanaodhaniwa kuwa wenyeji wa visiwa vingi vilivyojitenga kwenye eneo hilo wanaopora mali zenye thamani kubwa. Maharamia wenye silaha hutumia mashua za kasi ili kupora shehena zilizo kwenye meli usiku. Maofisa husema kwamba maharamia hao, wasiopatikana kwa urahisi baharini, waweza tu kukomeshwa endapo watasakwa kwenye nchi, wanakouza mali wanazopora.
Machimbo ya Dhahabu ya Misri
Inasemekana kwamba machimbo ya dhahabu ya Misri yalitoa tani 1,500 za dhahabu nyakati za kale. Ijapokuwa miaka 2,000 imepita tangu kiasi kikubwa cha dhahabu kilipochimbwa huko, wanajiolojia wanakisia kwamba dhahabu nyingi bado ingali ardhini. “Tungependa kurudisha utukufu wa Farao na hivyo tutafungua tena machimbo yetu ya zaidi ya miaka 6,000 iliyopita,” akasema Sami El-Raghy, meneja mkurugenzi wa kampuni ya Australia ya kuchimba dhahabu. Serikali ya Misri imeiidhinisha kampuni hiyo ikague eneo la Jangwa la Mashariki kando ya Bahari Nyekundu, pajulikanapo kuwa na machimbo 16 ya Farao. Hata hivyo, ramani ya miaka 2,900 iliyopita iliyogunduliwa mnamo 1820 katika Luxor (Thebes la kale) yaonyesha pia kwamba kuna machimbo 104 yaliyofunikwa kwa mchanga wa jangwani kwenye eneo hilo. Kulingana na jarida la The Wall Street Journal, yaaminika kwamba kwa kutumia mbinu za kisasa huenda baadhi yake yakawa tena machimbo ya dhahabu yenye faida.
Idadi ya Watu Ni Bilioni Sita na Inaongezeka
Shirika la Hazina ya Watu la Umoja wa Mataifa lakadiria kwamba idadi ya watu ulimwenguni ilifikia bilioni sita katika Oktoba 12, 1999. Idadi ya watu ulimwenguni imeongezeka kutoka watu bilioni tano hadi bilioni sita kwa kipindi cha miaka 12 tu, akasema Carl Haub, wa Shirika la Kuchunguza Idadi ya Watu. Kulingana na ripoti ya shirika hilo, “idadi ya watu ulimwenguni iliongezeka kwa bilioni 4.4 katika karne ya 20,” ilhali katika karne ya 19, “idadi ya watu iliongezeka kwa takriban milioni 600 tu.” Kuongezeka kwa matarajio ya muda wa kuishi ndiyo sababu ya msingi ya kuongezeka kwa idadi ya watu ulimwenguni katika karne ya 20. “Leo, takriban asilimia 98 ya ongezeko la idadi ya watu ulimwenguni hutukia katika nchi maskini,” akasema Haub.
Vipimo vya juu Sana vya Halijoto
“Mnamo 1998, kipimo cha wastani cha halijoto Duniani kilipita kipimo cha juu kilichowahi kurekodiwa,” yasema taarifa ya Taasisi ya Worldwatch. Halijoto ya juu zaidi ya angahewa husababisha mvukizo na mvua kubwa zaidi, ambazo kama tokeo, husababisha dhoruba zenye kuleta uharibifu zaidi. Kwa mfano, “uharibifu wote uliosababishwa na halihewa ulimwenguni pote mnamo 1998 ulitokeza hasara ya dola za Marekani bilioni 92, ongezeko la kustaajabisha la asilimia 53 kutoka kwa dola za Marekani bilioni 60 mwaka wa 1996, yasema Taasisi ya Worldwatch. Kwa kuongezea, dhoruba kali sana na mafuriko makubwa yaliwafanya takriban watu milioni 300 wahame makwao mwaka wa 1998. Wanasayansi hawana uhakika iwapo ni mwaka wa 1998 tu uliopita kiasi au uharibifu huu utaendelea. Hata hivyo, ripoti hiyo ilisema: “Vigezo vya tabia ya nchi vinadokeza kwamba matukio ya mwaka wa 1998 yaweza kuwa mfano wa yale yatakayotukia wakati ujao.”
Kupanda Miti Upya kwa Haraka
Eneo la msitu wa mvua wa Amazon lililoharibiwa na uchimbaji madini limegeuzwa kwa muda wa miaka miwili kuwa msitu wenye kusitawi, laripoti gazeti la New Scientist. Wanasayansi wa kituo cha Embrapa, kituo cha serikali cha utafiti wa kilimo huko Brazili, walibuni njia ya kutia bakteria inayoambisha nitrojeni katika mbegu za miti. Miti hukua kwa haraka sana inapopandwa. Mbinu hiyo ilifanikiwa sana katika Oriximiná, katika jimbo la kaskazini la Pará, ambako uchimbaji wa boksiti ulikuwa umesababisha uharibifu mkubwa wa msitu. Watafiti wanatumia mbinu hiyo mpya katika pwani iliyo mashariki mwa Brazili, ambako ni asilimia 6 tu ya msitu wa asili umesalia, lasema gazeti hilo.
Mshahara wa Mama
Kama ungejumlisha mishahara ya kazi zote zinazofanywa na mama kwa mwaka mzima, angelipwa fedha ngapi kwa kazi zote anazofanya? Kulingana na ripoti moja katika gazeti la The Washington Post, kwa mwaka mmoja angepokea dola 508,700 za Marekani! Kiasi hiki kinategemea mishahara ya wastani ya kazi zinazofanywa na akina mama kwa kawaida. Hizi ni baadhi ya kazi 17 zinazotajwa na ripoti hiyo, kutia na mshahara wa wastani wa mwaka: Mtunzaji-watoto, dola 13,000 za Marekani; dereva wa basi, dola 32,000; mwanasaikolojia, dola 29,000; mtunzaji wa wanyama, dola 17,000; muuguzi aliyesajiliwa, dola 35,000; mpishi stadi, dola 40,000; na karani wa kawaida wa ofisi, dola 19,000. Kulingana na Ric Edelman, mwenyekiti wa kampuni ya huduma za kifedha iliyofanya uchunguzi huo, malipo hayo hayatii ndani gharama kama za Social Security na malipo mengine ya uzeeni.