Imani Yajaribiwa
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA
RICHMOND ni mji maridadi huko North Yorkshire, Uingereza. Ukiwa katika kasri ya mji huo iliyojengwa baada tu ya ushindi wa Norman katika mwaka wa 1066, unaweza kuona waziwazi bonde la Mto Swale lililo mbele ya Mbuga ya Kitaifa ya Yorkshire Dales.
Kipindi cha televisheni kinachoitwa The Richmond Sixteen, kimefunua jambo muhimu kuhusu historia ya kisasa ya kasri hiyo, yaani, kilichowapata watu 16 waliofungwa huko kwa kukataa kupigana katika Vita vya Kwanza vya Ulimwengu kwa sababu ya dhamiri. Ni nini kilichowapata?
Kulazimishwa Kuingia Jeshini
Baada ya Uingereza kutangaza vita mwaka wa 1914, uzalendo uliwachochea wanaume milioni 2.5 hivi wajiunge na jeshi la Uingereza. Lakini, kama mwanahistoria wa vita Alan Lloyd anavyosema, “baadaye watu hawakuombwa tena waingie jeshini bali walilazimishwa” kwa kuwa idadi ya watu waliojeruhiwa au kuuawa vitani iliongezeka na ilionekana kwamba vita havingemalizika haraka kama wanasiasa walivyokuwa wameahidi. Hivyo, kwa mara ya kwanza katika historia ya Uingereza, wanaume waseja walilazimishwa kuingia jeshini katika Machi 1916.
Mahakama 2,000 zilianzishwa kusikiliza kesi za rufani, lakini watu wachache tu ndio walioruhusiwa kutoingia jeshini kwa sababu ya dhamiri. Wengi wao waliamriwa waunge mkono jitihada za kivita kwa kujiunga na vikosi ambavyo havikuenda vitani. Wale waliokataa kujiunga na vikosi hivyo bado walionwa kuwa wanajeshi na walifikishwa katika mahakama za kijeshi. Waliteswa na kufungwa gerezani, mara nyingi wakiwa wamesongamana katika hali mbaya.
Wafungwa Kumi na Sita wa Richmond
Kati ya Wafungwa Kumi na Sita waliokuwa huko Richmond, watano walikuwa Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa, kama Mashahidi wa Yehova walivyoitwa wakati huo. Herbert Senior, ambaye alianza kuwa Mwanafunzi wa Biblia katika mwaka wa 1905 akiwa na umri wa miaka 15, aliandika hivi karibu miaka 50 baadaye: “Tulifungwa katika magereza yaliyokuwa kama mapango. Inaonekana hayakuwa yametumiwa kwa miaka mingi, kwani kulikuwa na marundo ya takataka sakafuni yenye urefu wa sentimeta 5 mpaka 8.” Hivi majuzi, maandishi na michoro iliyofutika kidogo na mingine isiyoonekana vizuri ambayo ilichorwa na kuandikwa na wafungwa kwenye kuta nyeupe za gereza hilo, imegunduliwa. Ina majina, maneno, na michoro ya wapendwa wao, na maelezo kuhusu imani yao.
Mfungwa mmoja aliandika hivi: “Afadhali nife kwa sababu ya kushikilia kanuni kuliko kufa bila kanuni.” Maandishi mengi yanahusu Yesu Kristo na mafundisho yake. Pia kuna picha zilizochorwa vizuri za ile ishara ya msalaba na taji ambayo ilitumiwa wakati huo na Shirika la Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa (IBSA). Herbert Senior alisema kwamba alichora kwenye ukuta wa gereza “Chati ya Enzi” iliyo katika kitabu cha kujifunza Biblia The Divine Plan of the Ages, lakini haijagunduliwa. Huenda ilifutika kama maandishi mengine yaliyokuwa katika kuta za gereza kuu au kwingineko. Maandishi mengine yanasema hivi: ‘Clarence Hall, Leeds, I.B.S.A. Mei 29, 1916. Nimepelekwa Ufaransa.’
Walipelekwa Ufaransa na Kurudishwa!
Watu waliojeruhiwa au kuuawa vitani huko Ufaransa na Ubelgiji waliongezeka haraka. Waziri wa vita Horatio Herbert Kitchener na Jenerali Mwingereza Douglas Haig, walihitaji sana wanajeshi zaidi, kutia ndani wanaume waliooa, ambao pia walilazimishwa kuingia jeshini kuanzia Mei 1916. Ili kuwashawishi waingie jeshini, maafisa waliamua kuwaadhibu watu wanaokataa kujiunga na jeshi. Hivyo, wakitishwa kupigwa risasi, wale Wafungwa Kumi na Sita wa Richmond waliingizwa ndani ya gari-moshi kisiri wakiwa wamefungwa pingu na kupelekwa Ufaransa kupitia njia ndefu. Kulingana na gazeti Heritage, walipokuwa kwenye ufuo wa jiji la Boulogne, “wanaume hao walifungwa kwenye milingoti kwa seng’enge kana kwamba walikuwa wanasulubiwa,” wakalazimishwa kumtazama askari Mwingereza aliyekuwa ametoroka vitani akipigwa risasi na kikosi cha wanajeshi. Waliambiwa kwamba iwapo hawangetii, janga hilohilo lingewapata.
Katikati ya Juni 1916, wafungwa hao walilazimishwa kutembea mbele ya wanajeshi 3,000 ili wahukumiwe kifo, lakini kufikia wakati huo Kitchener alikuwa amekufa na waziri mkuu wa Uingereza akaingilia kati. Wenye mamlaka huko London walikuwa wamepokea kadi yenye ujumbe wa siri na amri hiyo ya kijeshi ilikuwa imebatilishwa. Jenerali Haig aliamriwa kubadili hukumu ya kifo kuwa kifungo cha miaka kumi na kazi ngumu.
Ripoti moja ya serikali inasema kwamba wale wafungwa 16 waliporejea Uingereza, baadhi yao walipelekwa kwenye machimbo ya mawe ya matale huko Scotland kufanya “kazi ya kujenga taifa” katika hali mbaya sana. Wengine, kutia ndani Herbert Senior, walirudishwa kwenye magereza ya raia, wala si ya kijeshi.
Kumbukumbu
Kwa kuwa kuta za gereza hilo ni dhaifu, maonyesho makubwa katika Kasri ya Richmond, ambayo sasa inahifadhiwa na Shirika la Mirathi ya Uingereza, huwawezesha wageni kuona magereza na maandishi yake kupitia kompyuta bila kuyaharibu. Wanafunzi hufundishwa kwa nini watu waliokataa kwenda vitani walikuwa tayari kuadhibiwa, kufungwa, na labda kuuawa kwa sababu ya imani yao.
Wafungwa Kumi na Sita wa Richmond walifaulu “kufahamisha umma kuhusu msimamo wao wa kukataa kupigana kwa sababu ya dhamiri na hivyo wakaanza kuungwa mkono na kuheshimiwa.” Jambo hilo liliwafanya maafisa wa serikali kuwaelewa na kuwatendea vizuri watu waliokataa kupigana kwa sababu ya dhamiri katika Vita vya Pili vya Ulimwengu.
Katika mwaka wa 2002, sehemu fulani ya bustani maridadi ilitengwa kwenye kasri hiyo ili kukumbuka imani ya wale Wafungwa Kumi na Sita wa Richmond.
[Picha katika ukurasa wa 12, 13]
Kuanzia kushoto hadi kulia: Jengo la karne ya 12 la Kasri ya Richmond, na jengo la magereza
Herbert Senior, mmoja wa Wafungwa Kumi na Sita wa Richmond
Mojawapo ya magereza ya wafungwa hao
Nyuma: Baadhi ya maandishi yaliyoandikwa kwenye ukuta wa gereza