Kuutazama Ulimwengu
◼ “Iwe ni kwa sababu ya kuongezeka kwa joto ulimwenguni au kwa sababu nyingine, misiba inayohusianishwa na hali ya hewa iliongezeka mara tatu kati ya miaka ya 1970 na miaka ya 1990.”—THE ECONOMIST, UINGEREZA.
◼ Mvulana mwenye umri wa miezi 10 ana kibali cha kumiliki bunduki katika jimbo la Illinois, Marekani. Kibali hicho ambacho kiliombwa na baba yake kinasema kwamba mtoto huyo ana urefu wa zaidi ya nusu mita, na uzito wa kilogramu 9. Mtu wa umri wowote anaweza kuomba kibali cha kumiliki bunduki katika jimbo hilo.—CABLE NEWS NETWORK, MAREKANI.
◼ Wanasayansi wamegeuza maji yaliyoshinikizwa yawe barafu “moto kuliko kiwango cha maji kuchemka.” Mbali na barafu ya “kawaida” kuna “angalau aina nyingine 11 za barafu zinazotengenezwa chini ya viwango mbalimbali vya joto na shinikizo.”—SANDIA NATIONAL LABORATORIES, MAREKANI.
Uhuru wa Ibada Watetewa Nchini Georgia
Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ilitoa hukumu dhidi ya serikali ya Georgia kwa kuruhusu ujeuri wa kidini dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Mahakama ilitangaza kwamba Mashahidi, wakiwa dini ya Kikristo inayojulikana, wana haki ya kukutana kwa ajili ya ibada na kujifunza Biblia na ikaamuru kuwa walipwe ridhaa kwa ajili ya mateso waliyopata na gharama za kesi. Kati ya Oktoba 1999 na Novemba (Mwezi wa 11) 2002, Mashahidi wa Yehova walishambuliwa mara 138 na wakawasilisha malalamiko 784 kwa serikali ya Georgia. Hata hivyo, hakuna uchunguzi wowote wa kina uliofanywa kuhusiana na malalamiko hayo. Polisi hata walikataa kuingilia kati na kuwalinda Mashahidi walioathiriwa. Jeuri hiyo imepungua sana tangu Novemba 2003.
Kituo cha Kale cha Kuchunguza Anga Nchini Peru
Wachimbuzi wa vitu vya kale wamesema kwamba huenda magofu fulani huko Peru yalikuwa kituo cha kuchunguzia jua miaka 2,300 iliyopita. Eneo hilo linaloitwa Chankillo, linatia ndani safu ya minara 13 iliyo kwenye kilele fulani, inayoonekana kama nusu duara “yenye meno.” Sehemu za kutazama jua “ziliwekwa hivi kwamba mara mbili kwa mwaka jua litachomoza na kutua kwenye minara iliyo kwenye miisho ya nusu duara hiyo, na hivyo kuwawezesha kujua mwanzo na katikati ya mwaka,” linaeleza gazeti Science. Minara ya katikati ilionyesha mahali ambapo jua lingechomoza na kutua nyakati nyingine za mwaka. Katika eneo hilo kame, kujua wakati wa kupanda mazao kulikuwa muhimu, kwa hiyo “watu [walihitaji] kujua tarehe hususa.”
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 29]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Solistasi mwezi wa Juni
Ikwinoksi
Solistasi mwezi wa Desemba
Kituo cha kuchunguza anga
[Hisani]
REUTERS/Ivan Ghezzi/Handout
Picha Ambazo Huwafanya Wanawake Wajichukie
Ripoti moja ya Chuo Kikuu cha Missouri-Columbia huko Marekani inasema: “Picha za wanawake wembamba warembo kwenye majalada ya magazeti huwafanya wanawake wote wachukie miili yao licha ya ukubwa, umbile, urefu, au umri wa mtazamaji.” Laurie Mintz, profesa wa saikolojia ya elimu, shule, na ushauri, alisema kwamba “zamani ilidhaniwa kwamba baada ya kuwatazama wanawake wembamba kwenye vyombo vya habari, wanawake wanene ndio waliojichukia sana kuliko wanawake wembamba.” Hata hivyo, “tuligundua kwamba haidhuru mwanamke ana unene gani, kutazama picha hizo humfanya ajichukie,” anasema Mintz.