Sura 82
Yesu Aelekea Tena Yerusalemu
BAADA ya muda mfupi Yesu yuko katika mwendo tena, akifundisha jiji kwa jiji na kijiji kwa kijiji. Ni wazi yeye yumo katika wilaya ya Perea, ng’ambo ya Mto Yordani kutoka upande wa Yudea. Lakini mahali anakoenda ni Yerusalemu.
Labda ile falsafa ya Wayahudi ya kwamba hesabu ndogo tu ya watu ndio watastahili wokovu ndiyo inayomsukuma mwanamume mmoja kuuliza: “Bwana, je! wale wanaokolewa ni wachache?” Kwa jibu lake, Yesu anaonyesha watu lazima ya kufikiria kinachohitajiwa ili kupata wokovu: “Jikazeni kisulubu [yaani, ng’ang’anieni sana, au jiumizeni sana] ili mwingie kupitia ule mlango mwembamba.”
Jitihada kama hiyo ya kisulubu inahitajiwa kwa haraka “kwa sababu wengi,” Yesu anaendelea kusema, “watatafuta kuingia lakini hawataweza.” Kwa nini hawataweza? Yeye anaeleza kwamba ‘mara mwenye nyumba akiisha kuinuka na kutia kufuli kwenye mlango na watu wanasimama nje na kupiga hodi, wakisema, “Sahibu, tufungulie,” yeye atasema: “Mimi sijui nyinyi mwatoka wapi. Ondokeni kwangu, nyinyi nyote mlio wafanya kazi zisizo za uadilifu!”’
Wale wanaofungiwa nje kwa kufuli yaonekana wanakuja wakati unaowafaa wao wenyewe tu. Lakini kufikia hapo mlango wa fursa unakuwa umefungwa na kutiwa makomeo. Ili waingie, ingaliwapasa waje mapema kidogo, hata ingawa huenda ikawa wakati huo usingaliwafaa kufanya hivyo. Kweli kweli, ni tokeo la kuhuzunisha linalowangojea wale wanaoahirisha kufanya ibada ya Yehova iwe ndilo kusudi lao kuu maishani!
Wayahudi ambao Yesu ametumwa kwao akawahudumie wameshindwa, kwa sehemu kubwa zaidi ya yote, kushika fursa nzuri sana waliyo nayo ya kukubali uandalizi wa Mungu kwa ajili ya wokovu. Kwa hiyo Yesu anasema watalia machozi na kusaga meno yao wakati wanapotupwa nje. Kwa upande ule mwingine, watu kutoka “sehemu za mashariki na za magharibi, na kutoka kaskazini na kusini,” ndiyo, kutoka mataifa yote, “wataegemea mezani katika ufalme wa Mungu.”
Yesu anaendelea kusema: “Kuna wale walio wa mwisho [watu wasio Wayahudi wenye kudharauliwa, na pia Wayahudi wenye kukandamizwa] ambao watakuwa wa kwanza, na kuna wale waliokuwa wa kwanza [Wayahudi waliopendelewa kufanikiwa kwa vitu vya kimwili na kwa njia ya kidini] ambao watakuwa wa mwisho.” Kuwa kwao wa mwisho kunamaanisha kwamba wakosa-shukrani hao wenye kujikokota kwa mwendo wa polepole mno hawatakuwa katika Ufalme wa Mungu hata kidogo.
Sasa Mafarisayo wanamjia Yesu na kusema: “Toka hapa ushike njia uende zako, kwa sababu Herode [Antipa] anataka kukuua wewe.” Huenda ikawa Herode mwenyewe ndiye aliyeanzisha uvumi huo ili kusababisha Yesu akimbie kutoka eneo hilo. Huenda ikawa Herode aliogopa kuhusika katika kifo cha nabii mwingine wa Mungu kama vile alivyohusika katika kuua Yohana Mbatizaji. Lakini Yesu anawaambia Mafarisayo hao: “Nendeni mkamwambie mbweha huyo, ‘Tazama! Mimi ninafukuza roho waovu na kufanya uponyaji leo na kesho, na siku ya tatu nitakuwa nimekwisha maliza.’”
Baada ya kumaliza kazi yake huko, Yesu anaendelea na safari yake kuelekea Yerusalemu kwa sababu, kama vile yeye anavyoeleza, “hairuhusiki nabii kuharibiwa nje ya Yerusalemu.” Kwa nini inapasa kutarajiwa kwamba Yesu angeuawa katika Yerusalemu? Kwa sababu Yerusalemu ndilo jiji kuu, ilimo mahakama kuu ya Sanhedrini yenye washiriki 71 na ambamo dhabihu za wanyama hutolewa. Kwa hiyo, lingekuwa jambo lisiloruhusika “Mwana-Kondoo wa Mungu” auawe mahali pengine isipokuwa katika Yerusalemu.
“Yerusalemu, Yerusalemu, uliye muuaji wa manabii na mpigaji-mawe wale waliotumwa waende kwake,” Yesu anaomboleza, “ni mara nyingi kadiri gani mimi nimetaka kukusanya watoto wako pamoja kwa namna ambayo kuku hukusanya otamio la vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini nyinyi watu hamkutaka hivyo! Tazameni! Nyinyi mmeachiwa ukiwa nyumba yenu.” Kwa kumkataa Mwana wa Mungu, taifa hilo lilihukumiwa maangamizi!
Yesu anapoendelea kuelekea Yerusalemu, yeye anaalikwa kwenye nyumba ya mtawala mmoja wa Mafarisayo. Ni Sabato, na watu wanamtazama sana, kwa kuwa hapo pana mwanamume aliye na ugonjwa wa istiska (kujazana maji mwilini), labda katika mikono na miguu yake. Yesu anasema kwa Mafarisyo na wastadi wa Sheria waliopo, akiuliza: “Je! ni halali kisheria kuponya siku ya sabato au sivyo?”
Hakuna mtu anayesema neno. Kwa hiyo Yesu anaponya mwanamume huyo na kumwambia aende zake. Ndipo yeye anapouliza: “Ni nani kati yenu nyinyi, ikiwa mwana au fahali wake anatumbukia ndani ya kisima, ambaye hatamvuta nje mara hiyo siku ya sabato?” Tena, hakuna mtu anayesema neno kwa kujibu. Luka 13:22–14:6; Yohana 1:29, NW.
▪ Yesu anaonyesha ni nini kinachohitajiwa ili kupata wokovu, na kwa nini wengi wanafungiwa nje kwa kufuli?
▪ Walio “wa mwisho” wanaokuwa wa kwanza ni akina nani, na walio “wa kwanza” wanaokuwa wa mwisho ni akina nani?
▪ Inawezekana ni kwa nini ilisemwa kwamba Herode alitaka kuua Yesu?
▪ Kwa nini hairuhusiki nabii kuuawa nje ya Yerusalemu?