SURA YA 116
Afundisha Kuhusu Unyenyekevu Kwenye Pasaka ya Mwisho
MATHAYO 26:20 MARKO 14:17 LUKA 22:14-18 YOHANA 13:1-17
YESU ANAKULA PASAKA YAKE YA MWISHO PAMOJA NA MITUME
AFUNDISHA SOMO KWA KUWAOSHA MITUME MIGUU
Tayari Petro na Yohana wamefika Yerusalemu kufanya matayarisho kwa ajili ya Pasaka, kama Yesu alivyowaagiza. Baadaye, Yesu na wale mitume wengine kumi wanaelekea huko. Ni alasiri na jua linatua wakati Yesu na wanafunzi wake wanapoteremka kwenye Mlima wa Mizeituni. Hii ni mara ya mwisho kwa Yesu kuwa kwenye mlima huo mchana hadi atakapofufuliwa.
Baada ya muda mfupi, Yesu na wanafunzi wake wanafika jijini na kwenda kwenye nyumba ambamo watakula mlo wa Pasaka. Wanapanda ngazi na kwenda kwenye chumba kikubwa ghorofani. Humo wanapata matayarisho yote yakiwa yamefanywa kwa ajili ya mlo wao wa faragha. Yesu amekuwa akitazamia sana pindi hiyo kwa kuwa anasema: “Nimetamani sana kula Pasaka hii pamoja nanyi kabla sijateseka.”—Luka 22:15.
Desturi ya kupitisha vikombe kadhaa vya divai kati ya watu wanaokula pamoja mlo wa Pasaka ilianzishwa miaka mingi iliyopita. Sasa baada ya Yesu kupokea kikombe kimoja, anatoa shukrani na kusema: “Chukueni kikombe hiki na mkipitishe kutoka kwa mmoja mpaka kwa mwingine kati yenu, kwa maana ninawaambia, kuanzia sasa sitakunywa tena divai ya mzabibu mpaka Ufalme wa Mungu utakapokuja.” (Luka 22:17, 18) Ni wazi kwamba kifo chake kinakaribia.
Wakiwa wanaendelea na mlo wa Pasaka, jambo lisilo la kawaida linatokea. Yesu anasimama, anavua mavazi yake ya nje, na kuchukua taulo. Kisha anaweka maji katika beseni iliyo hapo karibu. Ilikuwa kawaida kwa mwenye nyumba kuhakikisha kwamba miguu ya wageni wake imeoshwa, labda na mfanyakazi. (Luka 7:44) Katika pindi hii, mwenye nyumba hayupo, basi Yesu anafanya kazi hiyo. Yeyote kati ya mitume wake angetumia fursa hiyo kufanya hivyo, lakini hakuna anayefanya hivyo. Je, labda ni kwa sababu bado wanashindana? Vyovyote vile, wanaaibika Yesu anapoosha miguu yao.
Yesu anapomfikia Petro, anakataa akisema: “Hutaosha kamwe miguu yangu.” Yesu anamjibu: “Nisipokuosha, wewe huna sehemu pamoja nami.” Petro anamwambia hivi kwa hisia: “Bwana, usioshe miguu yangu tu, bali pia mikono na kichwa changu.” Bila shaka, Petro anashangazwa na jinsi Yesu anavyomjibu: “Yeyote ambaye ameoga hahitaji kuoshwa zaidi ya miguu yake, yuko safi kabisa. Nanyi mko safi, lakini sio nyote.”—Yohana 13:8-10.
Yesu anawaosha miguu mitume wote 12, kutia ndani Yuda Iskariote. Baada ya kuvaa mavazi yake ya nje na kuketi tena mezani, Yesu anawauliza: “Je, mnaelewa jambo ambalo nimewafanyia? Ninyi huniita, ‘Mwalimu,’ na, ‘Bwana,’ nanyi hamjakosea, kwa maana ndivyo nilivyo. Kwa hiyo, ingawa mimi ni Bwana na Mwalimu, niliiosha miguu yenu, basi ninyi pia mnapaswa kuoshana miguu. Kwa maana nimewawekea kielelezo, ili mfanye kama nilivyowafanyia. Kwa kweli ninawaambia, mtumwa si mkuu kuliko bwana wake, wala yule aliyetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma. Ikiwa mnajua mambo haya, mtakuwa wenye furaha mkiyatenda.”—Yohana 13:12-17.
Hilo ni somo zuri sana kuhusu kutumikia kwa unyenyekevu! Wafuasi wa Yesu hawapaswi kujitafutia mahali pa kwanza, wakifikiri kwamba wao ni watu muhimu na wanapaswa kuhudumiwa. Badala yake, wanapaswa kuiga mfano wa Yesu, si kwa kuwa na desturi ya kuoshana miguu, bali kwa kuwa tayari kutumikia kwa unyenyekevu na bila ubaguzi.