Je! Ajali Itawale Maisha Yako?
KWENYE orodha hiyo, mtu pekee ambaye hakuamini katika ajali ni Yesu Kristo. Maoni yake yalikuwa nini?
Masimulizi ya wasifu ya karne ya kwanza juu ya Yesu (vitabu vya Biblia vya Mathayo, Marko, Luka, na Yohana) yataja imani yake kwamba watu mmoja mmoja waweza kuongoza wakati ujao wao, kwa usahili akimaanisha yale yanayowapata.
Mathalani, Yesu alisema kwamba Mungu “atawapa mema wao wamwombao” na kwamba “mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokolewa.” Vivyo hivyo, wakati wakaaji wa Yerusalemu walipopuuza maonyo ambayo yangaliokoa maisha zao, Yesu hakulaumu ajali kwa ajili ya tendo-itikio lao. Badala yake, yeye alisema: “hamkutaka.”—Mathayo 7:7-11; 23:37, 38; 24:13.
Pia twaweza kutambua mtazamo wa Yesu kwa yale aliyosema kuhusu aksidenti yenye kufisha iliyotukia katika Yerusalemu, akisema: “Wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo.” (Luka 13:4, 5) Angalia kwamba Yesu hakuhesabia ajali kifo cha wale wanaume 18, wala yeye hakusema walikufa kwa sababu ya wao kuwa waovu zaidi ya wengine. Badala yake, tofauti na Mafarisayo wa siku yake waliojaribu kupatanisha ajali na imani ya hiari ya binadamu, Yesu alifundisha kwamba binadamu aweza kuongoza wakati ujao wake binafsi.
Vivyo hivyo mitume wa Yesu walifundisha kwamba wokovu ni chaguo linalopatikana kwa wote. Mtume Paulo aliandika hivi: “Umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu.” Na mtume Petro alisema: “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu.” (2 Timotheo 3:15; 1 Petro 2:2; ona pia Matendo 10:34, 35; 17:26, 27.) Encyclopædia of Religion and Ethics ya Hasting yataja kwamba waandikaji wa karne ya pili na tatu, kama vile Justin Origeni, na Irenayo, ‘hawakujua lolote juu ya kadari isiyo na masharti; wao walifunza juu ya hiari.’
Lakini ikiwa wengi sana, kutia na Wayahudi wengi kuwazunguka, waliamini namna namna za ajali, ni kwa nini Yesu na Wakristo wa mapema hawakuamini kwamba ajali ya mtu imewekwa? Sababu moja ni kwamba wazo hilo lina matatizo chungu zima. Kutaja mawili: Imani katika ajali ni kinyume cha sifa za Yehova Mungu; yakanushwa na mambo ya hakika yaliyothibitishwa. Zaidi ya hayo, yaweza kuhatarisha maisha yako ya wakati huu na ule ujao. Mtazamo wa karibu zaidi utakuonyesha jinsi ilivyo hivyo.
Yanayomaanishwa na Imani Katika Ajali
na Sifa za Mungu
Nyuma katika karne ya tatu K.W.K., mwanafalsafa Zeno wa Sitio alifunza wanafunzi wake katika Athene “kukubali amri ya Ajali kuwa bora zaidi kwa njia fulani iliyofichwa.” Hata hivyo, siku moja, baada ya Zeno kujifunza kwamba mtumwa wake alikuwa na hatia ya kuiba, Zeno alikabiliwa kinagaubaga na yanayomaanishwa na falsafa yake mwenyewe. Vipi? Alipompiga mwizi huyo, mtumwa huyo alitamka hivi: “Lakini ilijaliwa kwamba napaswa kuiba.”
Mtumwa wa Zeno alikuwa na hoja. Ikiwa waamini kwamba kigezo cha maisha ya kila mtu kimeamuliwa kimbele, basi kulaumu mtu akiwa mwizi ni sawa na kulaumu mbegu ya chungwa kwa ajili ya kuwa mchungwa. Isitoshe, binadamu na mbegu hiyo husitawi tu kwa kufuata programu. Hata hivyo, hatimaye yanayomaanishwa na kuwaza huko ni nini?
Ikiwa wahalifu hufuata tu ajali yao, basi yule aliyeweka fungu lao ndiye mwenye lawama kwa ajili ya vitendo vyao. Huyo angekuwa nani? Kulingana na waamini-ajali, ni Mungu mwenyewe. Tukichukua hatua nyingine kubwa katika kuwaza huko, basi lazima Mungu awe ndiye Kisababishi cha Kwanza cha uovu wote, jeuri, na uonezi ambao umepata kufanywa na binadamu. Je! wewe wakubali hilo?
Makala fulani katika Nederlands Theologisch Tijdschrift (Jarida la Uholanzi la Theolojia) husema kwamba maoni hayo ya ajali “hudokeza mfano fulani wa Mungu ambao, kwa Wakristo angalau, si wa kiakili.” Kwa nini? Kwa sababu yanapinga mfano wa Mungu uliotolewa na waandikaji wa Biblia waliovuviwa. Mathalani, angalia, manukuu haya kutoka kitabu cha Zaburi kilichovuviwa: “Maana huwi Mungu apendezwaye na ubaya.” “Nafsi yake humchukia . . . mwenye kupenda udhalimu.” “[Mfalme wa Kimesiya mkusudiwa wa Mungu] atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimu.” (Zaburi 5:4; 11:5; 72:14) Kwa wazi, yanayomaanishwa na imani katika ajali hugongana dafurao na sifa za Mungu.
Imani Katika Ajali na Mambo ya Hakika
Lakini vipi juu ya maafaasilia? Je! hayakujaliwa yatukie na kwa hiyo haiwezekani kuyaepuka?
Mambo ya hakika yathibitisha nini? Angalia magunduzi ya utafiti fulani juu ya kisababishi cha maafaasilia, kama ilivyoripotiwa na gazeti la Uholanzi NRC Handelsblad: “Hadi sasa, matetemeko ya dunia, mafuriko, maporomoko ya ardhi, na tufani . . . daima yalionwa kuwa balaa za asili. Hata hiyvo, mfikirio wa kindani waonyesha kwamba mwingiliano wa kibinadamu ulio mkubwa na asilia umeathiri sana uwezo wa mazingira wa kujilinda dhidi ya misiba. Kama tokeo, maafaasilia yachukua maisha mengi kuliko wakati mwingineo wote.”—italiki ni zetu.
Yale mafuriko katika Bangladeshi yaliyotajwa katika makala iliyotangulia yaonyesha hilo. Wanasayansi husema kwamba “uharibifu wa maeneo makubwa sana ya misitu ya Nepali, India ya Kaskazini, na Bangladeshi umekuwa kisababishi kikubwa cha mafuriko ambayo yameipiga Bangladeshi katika miaka ya karibuni.” (Gazeti Voice) Ripoti nyingine yasema kwamba kufyekwa kwa misitu kumeongeza kiwango cha mafuriko katika Bangladeshi kutoka mafuriko moja kila miaka 50 hadi moja kila miaka 4. Vitendo kama hivyo vya mwingilio wa kibinadamu katika sehemu nyingine za ulimwengu vimeongoza kwenye matokeo yenye maafa kadiri iyo hiyo—ukame, mioto ya misitu, na maporomoko ya ardhi. Ndiyo vitendo vya kibinadamu—wala si ajali ya kifumbo—mara nyingi husababisha au kuzidisha maafaasilia.
Ikiwa ndivyo, vitendo vya kibinadamu vyapasa pia kufanya kinyume: kupunguza kabisa misiba. Je! ndivyo ilivyo? Ndivyo. Fikiria mambo haya ya hakika: UNICEF (Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa) laripoti kwamba kwa miaka mingi mamia ya watoto katika sehemu za ndani za Bangladeshi walikuwa vipofu. Je! hilo lilisababishwa na ajali isiyoweza kubadilishwa? Hata kidogo. Baada ya wafanya kazi wa UNICEF kusadikisha akina mama wasilishe familia yao mchele tu bali pia matunda na mboga, maradhi hayo ya macho yalianza kupungua. Kufikia sasa, badiliko hilo la chakula limeokoa na upofu mamia ya watoto katika Bangladeshi.
Vivyo hivyo, watu wasiovuta sigareti huishi, kwa wastani, kuanzia miaka mitatu hadi minne zaidi ya wavutaji sigareti. Abiria wa magari wanaovaa mikanda ya vitini hupatwa na aksidenti chache zaidi zenye kuua kushinda wale wasiofanya hivyo. Kwa wazi, vitendo vyako mwenyewe—wala si ajali—hutawala maisha yako.
Matokeo Yenye Kufisha ya Imani Katika Ajali
Kama ilivyokwisha kutajwa, imani katika ajali yaweza pia kufupiza maisha yako. Jinsi gani? Katika kuzungumzia “vielelezo vyenye kutisha zaidi vya kuamini ajali,” The Encyclopedia of Religion chataarifu hivi: “Tangu Vita ya Ulimwengu 2 twajua juu ya mashambulizi ya kujiua ya Kijapani ya makombora na ya ujiuaji katika makao ya SS (Schutzstaffel) wakati wa utawala wa Hitler kwa kuitikia dhana ya ajali (Schicksal) iliyowazwa kuwa yenye thamani zaidi ya maisha za binadamu mmoja mmoja.” Na hivi karibuni zaidi, lasema chimbuko lilo hilo, “mashambulizi ya kujiua yaliyovuviwa kidini juu ya malengo yanayowazwa kuwa tisho kwa Uislamu . . . yalikuwa takribani jambo la kawaida katika ripoti za magazeti za nchi za Mashariki.” Maelfu ya askari vijana, zasema ripoti hizo, walitembea kwenda kwenye pigano wakiwa wamesadiki kwamba “ikiwa haijaandikwa kwamba mtu atakufa, hatapatwa na dhara lolote.”
Hata hivyo, hata walimu Waislamu wanaostahiwa hukataa tabia hiyo ya kutojali. Mathalani, kalifa mmoja alisema: “Yeye aliyemo ndani ya moto apaswa anyenyekee mapenzi ya Mungu; lakini yeye ambaye bado hayumo ndani ya moto hahitaji kujitosa humo.” Kwa kusikitisha, umayamaya wa askari haukutenda kulingana na usia huo wa kalifa. Wakati wa miaka karibu minane ya vita, Irani ilipatwa na vifo vinavyokadiriwa kuwa 400,000—vifo zaidi vya piganoni kuliko ilivyokuwa navyo United States wakati wa Vita ya Ulimwengu 2! Kwa wazi, kuamini ajali kwaweza kufupiza maisha yako. Huenda hata kukahatarisha maisha yako ya wakati ujao. Jinsi gani?
Kwa kuwa mwamini-ajali husadiki kwamba wakati ujao hauepukiki na ulikwisha wekwa kama wakati uliopita, aweza kwa urahisi kusitawisha tabia yenye hatari ya kiutu. Tabia gani? Encyclopedia of Theology chajibu hivi: “Mtu huyo . . . huhisi kuwa bila ya msaada, duni, asiyehitajika katika mambo ya kijamii yanayoonekana hayaepukiki. Hilo hutokeza kujikalia tu ambako hushikilia ufafanuzi wa kishirikina wa kwamba kila jambo hutegemea ajali iliyo fumbo lakini yenye uwezo wote.”
Ni nini kinachofanya kujikalia tu kuwe hatari sana? Mara nyingi huko huongoza kwenye mtazamo wa upumbavu wa kukubali kushindwa. Huenda hilo likamzuia mwenye kuamini katika ajali asichukue hatua yoyote ya kwanza wala hata kuitikia mwaliko huu wa ajabu wa Mungu: “Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, . . . Tegeni masikio yenu, na kunijia; Sikieni, na nafsi zenu zitaishi.” (Isaya 55:1-3) Ikiwa kuamini ajali kwategemea kushindwa ‘kuja’ na ‘kusikia,’ kutakosesha fursa ya ‘kuishi’ milele katika Paradiso inayokuja itakayorudishwa duniani. Jinsi hiyo ilivyo bei kubwa kulipa!
Kwa hiyo wewe wasimama wapi? Ikiwa ulikulia katika jumuiya ambayo mawazo ya kuamini ajali ndio msingi wa kuwaza kwa watu, huenda ikawa ulikubali imani hiyo bila kusaili. Hata hivyo, makatao yaliyozungumzwa katika makala hii huenda yakawa yamekusaidia kuona kwamba kwa kadiri kubwa maisha yako ya wakati huu na ule ujao yategemea vitendo vyako mwenyewe.
Kama ulivyoona, kusababu, mambo ya hakika, na, zaidi ya yote, Maandiko Matakatifu yaonyesha kwamba hupaswi kutumbukia kwenye mtazamo wa kushindwa kiajali. Badala yake, Yesu alihimiza hivi: “Jitieni uchungu mwingi . . . ili kuingia kupitia mlango uliobanika.” (Luka 13:24, The Emphatic Diaglott, usomaji wa neno kwa neno) Yeye alimaanisha nini? Aeleza hivi mwelezaji mmoja wa Biblia: “[Ma]neno [tia uchungu mwingi] hutwaliwa kutoka michezo ya Kigiriki. Katika mbio zao . . . wao walijikakamua, au wakajitia uchungu mwingi, au walitia uwezo wao wote ili kupata ushindi.” Badala ya kukubali kushindwa maishani, Yesu alikuwa akihimiza kwamba ujikakamue kufikia ushindi pekee!
Kwa hiyo, ondosha kujikalia tu kokote kulikovuviwa na ajali. Ingia mbio za uhai kama ambavyo Neno la Mungu lahimiza, na usiruhusu kuamini ajali kupunguze mwendo wako. (Ona 1 Wakorintho 9:24-27.) Kaza mwendo kwa kuitikia upesi mwaliko huu uliovuviwa: “Chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako.” Wewe waweza kufanyaje uchaguzi huo? Kwa “kumpenda BWANA [Yehova, NW], Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye.” Kufanya hivyo kutaongoza kwenye ushindi, kwa maana Yehova atathibitika kuwa “uzima wako, na wingi wa siku zako.”—Kumbukumbu 30:19, 20.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Musa hakuhubiri ajali bali alihimiza hivi: “Chagua uzima, ili uwe hai.”