Mahakama ya Juu Zaidi ya Naijeria Yaunga Mkono Uhuru wa Kidini
WANA-KIJIJI wapora mavuno ya mkulima. Wengine waingia kwa ghafula nyumbani mwa mwashi na kutwaa vifaa vyake vya kazi. Wengine bado wamzuia mwanamke asinunue wala kuuza. Kwa nini kuwe na kutendwa vibaya hivyo? Ni kwa sababu hao wenye kutendwa vibaya, wote ambao ni Mashahidi wa Yehova, hawashiriki katika mashirika ya marika. ‘Eti katika nini?’ huenda ukataka kujua.
Shirika la marika hufanyizwa na watu, hasa wanaume, waliozaliwa karibu wakati uleule na katika kijiji kilekile. Vikundi vya marika ni vya kawaida katika mashariki mwa Naijeria. Huenda wakadhamini mradi wa jumuiya, lakini wao hushiriki pia katika ibada ya sanamu na kufanya desturi za uwasiliani-roho kuonyesha kwamba washiriki wamefikia umri wa mtu mzima. Kwa sababu Biblia hushutumu mazoea hayo kwa Wakristo wa kweli, Mashahidi wa Yehova hawashiriki hata kidogo katika vikundi hivyo.—1 Wakorintho 10:20, 21; 1 Yohana 5:21.
Samuel Okogbue alifanya kazi akiwa fundi wa nguo katika Aba, Naijeria. Mapema katika 1978, washiriki wa Shirika la Marika la Umunkalu la Alayi walitaka alipe “kodi” ili kusaidia ujenzi wa kituo cha afya. Akiwa Mkristo wa kweli, Samweli hujitahidi sana kusaidia watu wengine, lakini alikataa kwa kudhamiria kujihusisha na kikundi hicho cha marika. Katika Aprili 22 mwaka huo, washiriki sita wa kikundi hicho waliingia dukani mwake kwa nguvu na kutwaa cherehani lake, ambalo walisema wangeweka mpaka alipe pesa hizo. Samuel aliteta kwamba hakulazimika alipe chochote kwa kuwa hakuwa mshiriki wa shirika lao. Wakati ambapo hakuweza kupata tena cherehani lake, Samuel alipeleka jambo hilo mahakamani.
Kutoka Mahakama Hadi Mahakama
Katika Mahakama ya Hakimu Mkuu, kikundi hicho cha Marika kilitoa hoja ya kwamba kwa sababu ya umri wake, Samuel alikuwa tayari mmoja wa washiriki wao, mwenye daraka la kulipa kodi zozote ambazo walijiwekea wenyewe. Zaidi ya hayo, desturi ya kienyeji ilitaka kwamba ikiwa mshiriki hakulipa kodi, mali yake ingetwaliwa mpaka ailipe.
Mahakama haikuafikiana na hilo. Katika Februari 28, 1980, ilitoa hukumu kwamba Samuel hangeweza kulazimishwa kuwa mshiriki wa kikundi cha marika. Hakimu Mkuu alitaarifu hivi: “Desturi inayomnyima raia uhuru wa kuchagua shirika analopendelea ni kinyume cha S[ehemu] 37 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Naijeria na kwa hiyo haiwezi kupata nguvu ya Sheria.”
Kikundi hicho cha marika kilikata rufani hukumu hiyo kwa Mahakama ya Juu na kushinda. Hapo hakimu alimwamuru Samuel alipe kodi, akitaarifu kwamba ilikuwa njia tu ya kuchangia maendeleo ya jumuiya ya nyumbani kwake.
Kisha Samuel akakata rufani lile aliloona kutokuwa jambo la haki. Mahakama ya Rufani ilipindua hukumu ya Mahakama ya Juu, ikiamua kwa upendeleo wa Samuel. Kikikataa kukubali kushindwa, kikundi hicho cha marika kilipeleka kesi hiyo hadi Mahakama ya Juu Zaidi ya Naijeria.
Wakati uleule, washiriki wa kikundi hicho walikuwa wamekuwa wenye shughuli nyingi katika kijiji cha Samuel. Wakitoa hoja ya kwamba Mashahidi walipinga miradi ya jumuiya, walimsadikisha kiongozi wa kijiji hicho apige marufuku utendaji mbalimbali wa Mashahidi wa Yehova katika eneo hilo. Mpiga mbiu wa mji huo alitangaza kwamba kila mtu aliyeshughulika na Mashahidi wa Yehova angetozwa faini. Mashahidi kutoka miji ya jirani waliingilia na kuelewesha wazi jambo hilo kwa wazee katika kijiji hicho. Walieleza kwamba watu wa Mungu hawakupinga kwa njia yoyote maendeleo ya jumuiya. Kwa kweli, Samuel alikuwa ametokeza risiti mahakamani zikithibitisha kwamba alikuwa amechangia miradi ya jumuiya ambayo haikuwa imedhaminiwa na vikundi vya marika. Wazee wa kijiji walipindua uamuzi wao wa kuwaepuka kabisa Mashahidi.
Uhuru wa Kidini Washinda
Katika Oktoba 21, 1991, mahakimu watano wa Mahakama ya Juu Zaidi ya Naijeria walitoa hukumu kwa umoja kwa upendeleo wa Samuel. Akieleza zaidi juu ya kilichofanya uamuzi huo uchukuliwe na Hakimu Paul Nwokedi, Hakimu Abubakar Wali alitaarifu hivi: “Mshtakiwa [Samuel] hapingi kulipa kodi [iliyowekwa] bali apinga kuwa mshiriki wa jamii, kilabu, au kikundi cha marika chochote, kwa kuwa hilo ni kinyume cha itikadi yake ya kidini, yeye akiwa mshiriki wa [Ma]shahidi wa Yehova.”
Hakimu huyo aliendelea hivi: “Katiba ya 1963, sehemu 24(1) iliwahakikishia raia wote wa Naijeria uhuru wa dhamiri, wazo, na dini. Mshtakiwa ana haki ya kushikamana na itikadi ya dini, wazo na dhamiri yake inayomkataza asijiunge na kikundi cha Marika. Desturi yoyote inayodai tofauti ni kinyume cha Katiba na kwa hiyo haifai kwa kadiri hiyo.”
Kwa ufupi, mahakama hiyo ilitoa hukumu ya kwamba hakuna yeyote awezaye kulazimishwa kisheria ajiunge na kikundi cha marika hata ingawa huenda ushirika huo ukawa desturi ya jumuiya. Ilitoa hukumu pia ya kwamba hakuna yeyote awezaye kulazimishwa alipe kodi kupitia shirika ambalo yeye si mshiriki walo, hata wakati ambapo kodi hizo ni za maendeleo ya jumuiya. Kwa hiyo katika kijambo hicho kilichoonekana kuwa kidogo, uhuru wa kidini kwa Wanaijeria wote uliungwa mkono.