Kuondolea Shela Ule Mpaka wa Mwisho wa Alaska
KWA siku mbili sasa, sisi wanne tumesongamana ndani ya chumba kidogo katika mji mdogo maarufu wa Nome, Alaska, ambako wengi huja kutafuta dhahabu. Katika 1898 watafutaji zaidi ya 40,000 walikuja hapa kutafuta kitu kimoja tu—dhahabu! Kwa upande mwingine, sisi twatafuta hazina tofauti.
Kwa sasa, sisi twapendezwa na “vitu vinavyotamaniwa” ambavyo huenda vikawa vyaishi katika vijiji vilivyotengwa vya Gambell na Savoonga kwenye Kisiwa cha St. Lawrence, kilometa 300 kuelekea magharibi katika Mlangobahari wa Bering. (Hagai 2:7) Huko Wainuiti huvumilia yale maji ya barafu ya Arktiki na kuwinda nyangumi kilometa chache tu kutoka ule uliokuwa Muungano wa Sovieti. Lakini theluji yenye kuvuma na ukungu mzito sana watuzuia tusiondoke. Ndege yetu haiwezi kuruka.
Tungojapo, nafikiria matukio ya miaka michache iliyopita na kumshukuru Yehova Mungu kwa ajili ya baraka yake juu ya ushahidi katika maeneo ya msituni. Katika Alaska—inayoitwa na wengine mpaka wa mwisho wa ulimwengu—kuna wenyeji zaidi ya 60,000 wanaoishi katika jumuiya zaidi ya 150 zilizo mbali, ambazo zimetapakaa kotekote katika jangwa lenye ukubwa la karibu kilometa za mraba 1,600,000, ambalo halijaunganishwa kwa barabara za aina yoyote. Kwa ndege ya Watch Tower Society, tayari tumefikia zaidi ya theluthi moja ya vijiji hivyo vilivyotengwa, tukileta habari njema za Ufalme wa Mungu kwavyo.—Mathayo 24:14.
Ili kufikia makazi hayo yaliyo mbali, mara nyingi ndege huhitaji kushuka kupitia mawingu na ukungu ambao huenda ukafunika bara kwa siku kadhaa. Baada ya kushuka, kuna ukungu mwingine bado ambao ni lazima upenywe. Kama shela, ukungu huo huzifunika akili na mioyo ya watu hawa wenye fadhili na wenye amani.—Linganisha 2 Wakorintho 3:15, 16.
Kipindi cha Badiliko Chenye Kuumiza
Msitu wa Alaska unakaliwa na Wainuiti, Waaleuti, na Wahindi. Kila moja ya wao wana desturi na vitabia vya kipekee kulingana na mapokeo yao. Ili kuokoka kipupwe cha Arktiki, wamejifunza kuishi pamoja na kupata riziki kutoka kwa nyenzo za bara kwa kuwinda, kuvua samaki, na kuvua nyangumi.
Walipatwa na uvutano wa kigeni katika miaka ya katikati ya miaka ya 1700. Wafanya biashara Warusi waliouza na kununua manyoya walipata watu waliojivalia ngozi za wanyama na waliotoa harufu ya mafuta ya sili, watu walioishi, si katika igloo (nyumba za Waeskimo) zenye kufanyizwa kwa barafu, bali katika nyumba zilizo nusu ardhini, zilizofanyizwa kwa majani mororo na udongo wayo, zenye paa za nyasi na ambazo milango yayo ilikuwa chini ya ardhi. Wafanya biashara hao waliwaletea watu hawa wenye kusema kwa uanana, wapole, lakini wenye bidii sana, matatizo mengi makubwa kutia na tamaduni mpya na magonjwa mapya, yaliyopunguza idadi ya makabila mengine kuwa nusu. Upesi kileo kikawa laana kwa watu hao. Uchumi mpya ulilazimisha badiliko kutoka kwenye namna ya kujipatia riziki kwa kupanda chakula hadi kujipatia riziki kwa kuchuma fedha. Hadi leo hii, wengine huhisi hicho kimekuwa kipindi cha badiliko chenye kuumiza.
Wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo walipowasili, badiliko la aina nyingine lililazimishwa juu ya wenyeji Waalaska. Ingawa wengine waliyaacha kwa kusitasita mazoea yao ya kidini ya tangu zamani—ibada ya roho za upepo, barafu, dubu, tai, na kadhalika—wengine walisitawisha mchanganyiko wa mawazo, uliosababisha muungano, au mchafuko, wa dini. Mara nyingi hayo yote yalisababisha kutilia shaka na kutotumaini wageni. Katika baadhi ya vijiji mgeni hakaribishwi sikuzote.
Kwa hiyo ugumu unaotukabili ni, Tutafikiaje wenyeji wote waliotapakaa kotekote katika mpaka huu mkubwa sana? Twaweza kukomeshaje kushuku kwao? Twaweza kufanya nini ili kuiondoa shela hiyo?
Jitihada za Mapema za Kutoa Ushahidi
Katika miaka ya mapema ya 1960, Mashahidi Waalaska kadhaa wenye bidii sana walivumilia hali mbaya sana za hewa—pepo zenye nguvu nyingi, halijoto zilizo chini ya kiwango-mgando, hali za mafuriko ya theluji—wakaziendesha ndege zao wenyewe, zenye injini moja ili kufanya safari za kuhubiri miongoni mwa vijiji vilivyotapakaa kuelekea kaskazini. Kwa kuyakumbuka hayo yaliyopita, kwa kweli ndugu hao wenye mioyo mikuu walijihatarisha sana. Kuharibikiwa injini ya ndege kwa hakika kungaliweza kusababisha msiba. Hata ingawa wangaliweza kushuka kwa usalama, wangalikuwa mbali sana na msaada wakiwa katika halijoto zilizo chini ya kiwango-mgando na bila njia ya kusafiri. Kusalimika kwao kungalitegemea kupata chakula na makao, ambavyo vingalikuwa haba. Kwa shukrani, matukio mabaya sana hayakutokea, lakini hatari hizo hazikuweza kupuuzwa. Kwa hiyo ofisi ya tawi ya Watch Tower Society ya Alaska haikuwatia moyo akina ndugu watumie njia hiyo ya kuhubiri.
Ili kuendelea na kazi, ndugu waaminifu katika makutaniko ya Fairbanks na Kizio cha Kaskazini walikazia jitihada zao za kuhubiri katika vijiji vikubwa zaidi, kama vile Nome, Barrow, na Kotzebue, vinavyotumikiwa na kampuni za ndege za kibiashara. Walitumia fedha zao wenyewe ili kusafiri hadi maeneo hayo, zaidi ya kilometa 720 kuelekea kaskazini na magharibi. Wengine walibaki Nome kwa miezi kadhaa ili kuongoza mafunzo ya Biblia pamoja na wenye kupendezwa. Katika Barrow nyumba ilikodishwa ili kuandaa mahali pazuri kutoka katika hali yenye ubaridi sana ya digrii sentigredi 45 chini ya kiwango-mgando. Baada ya miaka kadhaa, dola zaidi ya 15,000 zilitumiwa na wale waliozingatia moyoni amri ya Yesu ya kuhubiri habari njema hadi miisho ya dunia.—Marko 13:10.
Msaada Usiotazamiwa Wawasili
Kutafuta-tafuta njia ya kufikia jumuiya zilizotengwa zaidi kuliendelea, na Yehova akafungua njia. Ndege yenye injini mbili ilipatikana—kitu hasa kilichohitajiwa ili kuvuka kwa usalama ile Safu ya Milima ya Alaska yenye miamba. Kuna milima mingi sana katika Alaska yenye vilele vipitavyo meta 4,200, na kilele cha Mlima maarufu McKinley (Denali) ni meta 6,193 juu ya usawa wa bahari.
Hatimaye, ndege iliwasili. Ebu wazia tamauko letu wakati ndege nzee-nzee yenye rangi nyingi zilizofifia, iliposhuka kwenye uwanja. Je! kweli ilistahili kuruka? Je! tungeweza kuruhusu ndugu zetu wasafiri kwayo? Tena, mkono wa Yehova haukuwa mfupi. Wakiongozwa na mafundi wenye leseni, ndugu zaidi ya 200 walijitolea utumishi wao, wakitumia muda wa maelfu kadhaa ya saa kufanyiza upya ndege nzima.
Yapendeza macho kama nini! Kuona ikiinuka juu katika anga za Alaska, ndege ing’aayo, ionekanayo mpya, ambayo imeandikwa kwa mapambo nambari 710WT kwenye mkia! Kwa kuwa saba na kumi pia zinatumiwa katika Biblia kuwakilisha ukamilifu, 710 yaweza kuonwa kukazia utegemezo ambao tengenezo la Yehova limetoa ili kuondolea shela mioyo iliyofunikwa kwa giza.
Kuelekea Chini Hadi Mfululizo wa Visiwa vya Aleutia
Tangu kupokea ndege hiyo, tumeeneza kilometa 80,000 za jangwa, tukileta habari njema za Ufalme na fasihi ya Biblia kwenye vijiji zaidi ya 54. Hiyo ni sawa na kuvuka kontinenti ya United States mara 19!
Tumefikia mara tatu visiwa vya Aleutia vyenye urefu wa kilometa 1,600, ambavyo hutenga Bahari ya Pasifiki na Bahari ya Bering. Vile visiwa zaidi ya 200 vyenye miti michache sana vinavyofanyiza mfululizo huo ni makao ya wenyeji Waaleuti na pia wa maelfu ya ndege wa bahari, tai-vipara, na aina fulani ya bata-bukini, wenye vichwa vyeupe na manyoya dhahiri ya nyuzinyuzi ya rangi nyeusi na nyeupe.
Ingawa uzuri wa mkoa huo ni wenye kuvutia, kuna hatari pia. Tulipokuwa tukiruka kwa ndege juu ya bahari, tuliweza kuona miinuko myeupe yenye kimo cha meta 3 hadi 5 juu ya maji ya barafu yenye pofu, yaliyo baridi sana hivi kwamba hata katika kiangazi mtu aweza kuokoka kwa muda wa dakika 10 hadi 15 pekee akiwa ndani ya maji hayo. Rubani akilazimika kushusha ndege, yeye aweza tu kuchagua ama kushuka kwenye kisiwa chenye miamba ama katika bahari yenye ubaridi sana, iwezayo kufisha. Twashukuru kama nini kwa ajili ya ndugu zetu wenye ustadi, mafundi wenye vyeti vya A & E (Ndege na Injini), ambao hujitolea kudumisha hali ya ndege ikiwa bora!
Katika mojayapo safari hizo, tulikuwa tukielekea bandari iitwayo Dutch Harbor na kijiji kimoja cha uvuvi cha Unalaska. Mkoa huo unajulikana kwa ajili ya pepo zao za mwendo wa kilometa 130 hadi 190 kwa saa. Kwa furaha, hiyo ilikuwa siku yenye utulivu zaidi lakini bado ilikuwa yenye msukosuko wa kutosha kutufanya tuwe na wasiwasi mara kadhaa. Ilishangaza kama nini wakati uwanja wa ndege ulipoonekana—lilikuwa pengo tu kwenye upande wa milima wenye miamba! Kwenye upande mmoja wa uwanja huo kulikuwa na genge wima, kwenye ule mwingine, yale maji ya barafu ya Bahari ya Bering! Tuliposhuka, ilikuwa kwenye uwanja wenye umajimaji. Huko mvua hunya zaidi ya siku 200 kwa mwaka.
Ilikuwa shangwe kama nini kuzungumza juu ya Neno na kusudi la Mungu kwa wakaaji wa eneo hilo! Watu kadhaa wenye umri mkubwa zaidi walieleza uthamini wao kwa ajili ya tumaini la ulimwengu usio na vita. Bado walikuwa na kumbukumbu dhahiri za Wajapani kulipua Dutch Harbor kwa makombora katika Vita ya Ulimwengu 2. Kumbukumbu letu la safari hizo za kutoa ushahidi hazisahauliki vilevile.
Mwelekeo wa Kupata Ujoto wa Polepole
Tukichunguza halihewa tena, twaona kuongezeka kwa halijoto. Hilo lafanya nifikirie kazi yetu ya kutoa ushahidi msituni. Polepole na kwa taratibu tumeona mwelekeo wa kupata ujoto mioyoni mwa watu.
Imechukua wakati fulani kushinda kile kifuniko cha kutilia shaka na kutotumaini ambako watu huonyesha kuelekea wageni. Katika majaribio yetu ya mapema-mapema, lilikuwa jambo la kawaida kwa viongozi wa makanisa ya vijiji kuilaki ndege, kuuliza kusudi la ziara yetu, kisha kutuomba kwa ghafula tuondoke. Bila shaka, mapokezi hayo yalikatisha tamaa. Lakini tulikumbuka shauri la Yesu lipatikanalo kwenye Mathayo 10:16: “Iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.” Kwa hiyo tulirudi tena kwa ndege iliyojaa letasi mbichi, nyanya, tikitimajichura, na vitu vingine visivyopatikana huko kwa urahisi. Sasa wakaaji wa hapo waliokuwa wenye uhasama awali walifurahia kuona mizigo yetu.
Ndugu mmoja alipokuwa akishughulikia “duka,” akipokea michango kwa ajili ya bidhaa hizo mbichi, wengine wengi walienda nyumba kwa nyumba, wakiwaarifu wenye nyumba juu ya kuwasili kwa mizigo hiyo yenye bidhaa mbichi. Wakiwa milangoni, waliuliza hivi pia: “Oh, neno moja tu, je, wewe ni msomaji wa Biblia? Najua utafurahia msaada huu wa funzo la Biblia uonyeshao kwamba Mungu ametuahidi paradiso.” Ni nani angeweza kukataa toleo lenye kushawishi hivyo? Kila mtu alithamini chakula cha kimwili na cha kiroho pia. Ukaribishaji huo ulipendeza, fasihi nyingi ziliangushwa, na mioyo michache ilipata ujoto.
Kuvuka Mpaka
Ng’ambo katika Eneo la Yukon, Kutaniko la Whitehorse lilitupa sisi mwaliko wa “Kimakedonia” ‘tuvuke’ hadi Kanada kuzuru baadhi ya maeneo katika Sehemu za Kaskazini-Magharibi za mbali. (Matendo 16:9) Sisi watano tulikuwa katika ndege tulipoelekea Tuktoyaktuk, kijiji kilicho karibu na Ghuba ya Mackenzie kwenye Bahari ya Beaufort, kaskazini mwa Kizio cha Arktiki.
‘Jina hili la kigeni latamkwaje?’ tulikuwa tukijiuliza tulipowasili.
“Tuk,” akajibu kijana mmoja kwa tabasamu kubwa.
“Mbona hatukufikiria hilo?” tukastaajabu.
Tulishangaa kupata kwamba watu wa Tuktoyaktuk waliyajua Maandiko vizuri. Likiwa tokeo, tulikuwa na mazungumzo mengi yenye urafiki, na fasihi nyingi ziliangushwa. Mmoja wa mapainia wetu mchanga alikuwa na mazungumzo yenye kutia nuru pamoja na mwenye nyumba mmoja.
“Mimi ni Mwanglikana!” akasema huyo mwenye nyumba.
“Je! watambua kwamba Kanisa Anglikana hukubali ugoni-jinsia-moja?” painia wetu akauliza.
“Ndivyo?” mwanamume huyo akasema kwa kusitasita. “Basi, mimi si Mwanglikana tena.” Kwa tumaini nzuri, mtu mwingine alikuwa akifunguliwa moyo kupokea habari njema za Biblia.—Waefeso 1:18.
Mtu mmoja mwenye umri mkubwa zaidi alivutiwa na azimio letu la kufikia kila nyumba katika eneo hilo. Kwa kawaida, tulikuwa tukilazimika kufanya kazi yetu yote kwa kutembea. Kwa kawaida kulikuwa na mwendo wa kutembea wa kilometa moja au zaidi kutoka kwenye uwanja wa ndege hadi kijiji. Kisha, ili kufikia kila nyumba, tulilazimika kutembea kwenye vijia vya changarawe vya matope. Mtu huyo alituazima lori lake dogo, nalo lilikuwa baraka iliyoje! Kuvuka mpaka na kusaidia katika eneo la Kanada lilikuwa pendeleo zuri.
Jitihada Hizo Zote Zastahili?
Halihewa ikiwa mbaya na twazuiwa kwenda au twacheleweshwa kwa muda wa wakati usiojulikana, kama vile sasa, au wakati siku ndefu ya kutoa ushahidi yaonekana kama kwamba haikuwa na matokeo yoyote ila kutopendezwa au hata uhasama, ndipo twaanza kujiuliza kama huo wastahili wakati, nishati, na gharama zote hizo. Twaweza kufikiria watu ambao waonekana kuonyesha kupendezwa na ambao waahidi kujifunza kwa kuandika barua lakini ambao washindwa kufanya hivyo. Ndipo twakumbuka kwamba si desturi ya wenyeji wengi kuandika barua, na urafiki waweza kuonwa vibaya kuwa kupendezwa katika ujumbe wa Biblia. Nyakati nyingine yaonekana vigumu sana kupima mafanikio.
Mawazo hayo yasiyofaa yatoweka upesi tukumbukapo maono mazuri ya wahubiri wa Ufalme wengineo. Kwa kielelezo, Shahidi mmoja kutoka Fairbanks alihubiri katika kijiji cha Barrow huko kaskazini ya mbali. Akiwa huko alikutana na tineja mmoja aliyekuwa likizoni nyumbani kutoka chuoni Kalifornia. Dada huyo aliendeleza kupendezwa huko kwa kuandika barua akaendelea kumtia moyo msichana huyo hata baada ya yeye kurudi chuoni. Leo, mwanamke huyo mchanga ni mtumishi wa Yehova mwenye furaha, aliyebatizwa.
Kubishwa kwa mlango kwakatiza fikira zangu juu ya maono hayo na kwanipa ithibati nyingine kwamba hayo yote yastahili. Hapo mlangoni asimama Elmer, ambaye kufikia sasa ndiye Shahidi Mwinuiti pekee katika Nome, aliyejiweka wakfu na kubatizwa.
“Mkiweza kuondoka, je, naweza kwenda nanyi?” yeye akaomba. Akiwa anaishi eneo lililotengea sana na zaidi ya kilometa 800 kutoka kwenye kutaniko la karibu zaidi, yeye ataka kushiriki katika huduma pamoja na ndugu zake akiwa angali na fursa.
Mwanga wa jua waanza kutokea kupitia mawingu, na twajua kwamba karibuni tutapokea ruhusa ya kuondoka. Elmer apandapo ndege, twachangamshwa na uso wake mkunjufu, wenye furaha. Hii ni siku ya pekee kwa Elmer. Anakuja pamoja nasi kwenye kijiji tuendako ili kuhubiri kwa watu wake mwenyewe Wainuiti, akijiunga nasi katika jaribio letu la kuondolea shela mioyo ya wale wanaoishi kwenye mpaka wa mwisho wa ulimwengu.—Imechangwa.
[Ramani katika ukurasa wa 23]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
1: Gambell
2: Savoonga
3: Nome
4: Kotzebue
5: Barrow
6: Tuktoyaktuk
7: Fairbanks
8: Anchorage
9: Unalaska
10: Dutch Harbor
[Picha katika ukurasa wa 24]
Ili kufikia jumuiya zilizotengwa, mara nyingi ni lazima kuvuka mojayapo safu nyingi za milima za Alaska
[Picha katika ukurasa wa 25]
Betty Haws, Sophie Mezak, na Carrie Teeples wana jumla iliyounganishwa ya zaidi ya miaka 30 katika utumishi wa wakati wote