Kulinda Kisheria Habari Njema
KADIRI ambavyo mwanadamu amekuwa akijenga majiji, ndivyo amekuwa akijenga kuta. Hasa siku zilizopita, ngome hizo zilikuwa ulinzi. Walinzi walipigana wakiwa juu ya vizuizi hivyo, ili kuzuia kuta zisivunjwe wala kudhoofishwa na washambulizi. Kuta hizo zilikuwa ulinzi kwa wakazi wa jiji hilo na pia mara nyingi zilikuwa kimbilio la wakazi wa miji iliyozunguka.—2 Samweli 11:20-24; Isaya 25:12.
Vivyo hivyo, Mashahidi wa Yehova wamejenga ukuta—ukuta wa kisheria—wa kulinda. Ukuta huo haukujengwa ili kuwatenganisha Mashahidi na jamii iliyosalia, kwa maana Mashahidi wa Yehova wajulikana kwa kuwa watu wenye urafiki, wachangamfu. Badala ya hivyo, umetia nguvu dhamana za kisheria za uhuru wa msingi wa watu wote. Wakati huohuo, ukuta huo hulinda haki za kisheria za Mashahidi ili waweze kuabudu kwa uhuru. (Linganisha Mathayo 5:14-16.) Ukuta huu hulinda njia yao ya kuabudu na haki yao ya kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu. Huo ni ukuta gani, nao umejengwaje?
Kujenga Ukuta wa Kisheria wa Kulinda
Ingawa Mashahidi wa Yehova wana uhuru wa ibada katika nchi nyingi, katika nchi fulani wameshambuliwa bila msingi wowote. Uhuru wao wa kuabudu kwa kukusanyika pamoja au kwa kuhubiri nyumba hadi nyumba upingwapo, wamefuatia mambo kisheria. Ulimwenguni pote, kumekuwa na maelfu ya kesi za kisheria zinazohusu Mashahidi.a Hawajapata ushindi katika kesi zote. Lakini mahakama za chini zitoapo uamuzi dhidi yao, mara nyingi wamekata rufani kwenye mahakama za juu zaidi. Kumekuwa na matokeo gani?
Kwa makumi ya miaka ya karne ya 20, ushindi wa kisheria katika nchi nyingi umeweka vigezo vyenye kutegemeka ambavyo Mashahidi wa Yehova wametumia katika kesi zilizofuata. Sawa na matofali au mawe yanayoufanyiza ukuta, maamuzi hayo yenye kutufaa hufanyiza ukuta wa kisheria wa kulinda. Wakiwa juu ya ukuta huo wa vielelezo, Mashahidi wameendelea kupigania uhuru wao wa kidini wa kuabudu.
Kwa kielelezo, fikiria kesi ya Murdock v. Commonwealth of Pennsylvania, iliyoamuliwa na Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani, Mei 3, 1943. Swali lililozushwa katika kesi hiyo lilikuwa: Je, Mashahidi wa Yehova wapaswa kupata leseni ya kibiashara ya uchuuzi ili wagawanye vichapo vyao vya kidini? Mashahidi wa Yehova walisisitiza kwamba hawatakikani kufanya hivyo. Kazi yao ya kuhubiri si—wala haijapata kuwa—biashara. Lengo lao, si kuchuma fedha, bali kuhubiri habari njema. (Mathayo 10:8; 2 Wakorintho 2:17) Katika uamuzi wa kesi hiyo ya Murdock, Mahakama ilikubaliana na Mashahidi, ikisisitiza kwamba takwa lolote la kulipa kodi ya leseni kabla ya kugawanya vichapo vya kidini si halali.b Uamuzi huo uliweka kielelezo muhimu, nao Mashahidi wametumia kisa hicho kwa mafanikio katika kesi kadhaa baadaye. Uamuzi katika kesi ya Murdock umethibitika kuwa tofali thabiti katika ukuta wa kisheria wa kulinda.
Kesi kama hizo zimesaidia sana kulinda uhuru wa kidini wa watu wote. Kuhusu fungu lililotimizwa na Mashahidi katika kutetea haki za kiraia Marekani, kichapo University of Cincinnati Law Review kilisema hivi: “Mashahidi wa Yehova wameathiri sana kusitawi kwa sheria za kikatiba, hasa kwa kupanua mipaka ya ulinzi wa usemi na wa dini.”
Kuutia Nguvu Ukuta
Baada ya kila ushindi wa kisheria, ukuta hupata nguvu zaidi. Fikiria baadhi ya maamuzi ya miaka ya 1990 ambayo yamewanufaisha Mashahidi wa Yehova, na pia wapenda uhuru wengineo wote, ulimwenguni pote.
Ugiriki. Mei 25, 1993, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ilitegemeza haki ya raia wa Ugiriki ya kuwafundisha wengine itikadi zake za kidini. Kesi hiyo ilimhusu Minos Kokkinakis, aliyekuwa na umri wa miaka 84 wakati huo. Akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, Kokkinakis alikuwa amekamatwa zaidi ya mara 60 tangu mwaka wa 1938, alikuwa amefikishwa kwenye mahakama za Ugiriki mara 18, naye alikuwa amefungwa kwa zaidi ya miaka sita. Alikuwa ameshtakiwa hasa chini ya sheria ya Ugiriki ya mwaka wa 1930 iliyokataza kugeuza watu kidini—sheria iliyofanya Mashahidi wa Yehova wapatao 20,000 wakamatwe tangu 1938 hadi 1992. Mahakama ya Ulaya iliamua kwamba serikali ya Ugiriki ilikuwa imehalifu uhuru wa kidini wa Kokkinakis na kuamuru alipwe dola 14,400 za Marekani. Katika uamuzi wake, Mahakama hiyo iliamua kwamba Mashahidi wa Yehova kwa kweli ni “dini ijulikanayo.”—Ona Mnara wa Mlinzi la Septemba 1, 1993, ukurasa wa 27-31.
Mexico. Julai 16, 1992, hatua kubwa katika kutetea uhuru wa kidini ilipigwa huko Mexico. Tarehe hiyo, Law of Religious Associations and Public Worship ilianzishwa. Kupitia sheria hiyo, kikundi cha kidini chaweza kupata hadhi ya kisheria ya kuwa shirika la kidini kwa kupata kusajiliwa itakiwavyo. Hapo zamani, Mashahidi wa Yehova, sawa na dini nyingine nchini, walikuwepo ingawa hawakupewa wadhifa wa kuwa shirika halali. Aprili 13, 1993, Mashahidi waliomba kusajiliwa. Kwa furaha, Mei 7, 1993, walisajiliwa kisheria kuwa La Torre del Vigía, A. R., na Los Testigos de Jehová en México, A. R., yote mawili yakiwa mashirika ya kidini.—Ona Amkeni! la Julai 22, 1994, ukurasa wa 12-14.
Brazili. Novemba 1990, National Institute of Social Security ya Brazili (INSS) iliiarifu ofisi ya tawi ya Watch Tower Society kwamba wahudumu wa kujitolea kwenye Betheli (jina la ofisi za tawi za Mashahidi wa Yehova) hawangeonwa tena kuwa wahudumu na hivyo wangekuwa chini ya sheria za kazi za Brazili. Mashahidi walikata rufani dhidi ya uamuzi huo. Juni 7, 1996, Judicial Advisory of the Office of the Attorney General huko Brasília walitoa uamuzi uliotegemeza wadhifa wa wahudumu kwenye Betheli wakiwa washiriki wa jumuiya halali ya kidini, wala si wafanyakazi wa kazi zisizo za kidini.
Japani. Machi 8, 1996, Mahakama Kuu Zaidi ya Japani ilitoa uamuzi juu ya suala la elimu na uhuru wa dini—ili kumnufaisha kila mmoja huko Japani. Mahakama hiyo ilitoa uamuzi kwa kuafikiana kwamba Kobe Municipal Industrial Technical College ilihalifu sheria kwa kumfukuza Kunihito Kobayashi kwa sababu alikataa kushiriki katika mazoezi ya kivita. Uamuzi huo ni wa kwanza ambao Mahakama Kuu Zaidi imetoa kwa kutegemea uhuru uliodhaminiwa na Katiba ya Japani. Akifuata dhamiri yake iliyozoezwa na Biblia, Shahidi huyo mchanga alihisi kwamba mazoezi hayo hayakupatana na kanuni za Biblia kama vile ile ipatikanayo kwenye Isaya 2:4, isemayo: “Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.” Uamuzi wa Mahakama hiyo uliweka kielelezo cha kufuatwa katika kesi za wakati ujao.—Ona Mnara wa Mlinzi la Novemba 1, 1996, ukurasa wa 19-21.
Februari 9, 1998, Mahakama Kuu ya Tokyo ilitoa uamuzi mwingine wa maana sana uliotegemeza haki ya Shahidi aitwaye Misae Takeda ya kukataa matibabu yasiyopatana na amri ya Biblia ya ‘kujiepusha na damu.’ Kesi hiyo imepelekwa kwenye Mahakama Kuu Zaidi, na kama uamuzi huo wa Mahakama kuu utategemezwa, ni jambo lisilojulikana bado.—Matendo 15:28, 29.
Filipino. Katika uamuzi uliotolewa Machi 1, 1993, Mahakama Kuu Zaidi ya Filipino iliamua kwa mwafaka ikipendelea Mashahidi wa Yehova katika kesi iliyohusisha vijana Mashahidi waliofukuzwa shuleni kwa sababu walikataa kwa heshima kuisalimu bendera.
Kila uamuzi wenye kutufaa ni kama jiwe au tofali lililoongezwa linalotia nguvu ukuta wa kisheria ambao hulinda haki za Mashahidi wa Yehova na za watu wote pia.
Kuulinda Ukuta
Mashahidi wa Yehova wamesajiliwa kisheria katika nchi 153, wakiwa na uhuru mwingi halali, sawa na dini nyingine zenye kutambuliwa. Baada ya makumi ya miaka ya kunyanyaswa na kupigwa marufuku katika Ulaya Mashariki na katika uliokuwa Muungano wa Sovieti, Mashahidi wa Yehova sasa wanatambuliwa kisheria katika nchi kama vile Albania, Belarus, Jamhuri ya Cheki, Georgia, Hungaria, Kazakstan, Kyrgyzstan, Rumania, na Slovakia. Hata hivyo, katika nchi nyingine leo, kutia na baadhi ya nchi za Ulaya Magharibi zenye mifumo ya kisheria ya muda mrefu, haki za Mashahidi wa Yehova zapingwa kwelikweli au kukataliwa. Wapinzani wanajaribu sana ‘kutunga madhara kwa njia ya sheria’ dhidi ya Mashahidi. (Zaburi 94:20) Wao huitikiaje?c
Mashahidi wa Yehova wanataka kushirikiana na serikali zote, lakini pia wanataka kuwa na uhuru wa kisheria wa kuabudu. Wanasadiki kabisa kwamba sheria au uamuzi wowote wa mahakama ambao ungewazuia wasitii amri za Mungu—kutia ndani amri ya kuhubiri habari njema—ni ubatili. (Marko 13:10) Ikiwa makubaliano ya amani hayawezi kufikiwa, Mashahidi wa Yehova watashambulia katika uwanja wa kisheria, wakifuatia hatua zote za kukata rufani zinazohitajiwa ili kupata ulinzi wa kisheria kwa ajili ya haki yao ya kuabudu waliyopewa na Mungu. Mashahidi wa Yehova wana uhakika kabisa katika ahadi hii ya Mungu: “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa.”—Isaya 54:17.
[Maelezo ya Chini]
a Ili kupata maelezo zaidi juu ya rekodi ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova, tafadhali ona sura ya 30 ya kitabu Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
b Katika uamuzi wa kesi ya Murdock, Mahakama Kuu Zaidi ilitangua uamuzi wake wenyewe katika kesi ya Jones v. City of Opelika. Katika kesi ya Jones, mwaka wa 1942, Mahakama Kuu Zaidi ilikuwa imeunga mkono uamuzi wa mahakama ndogo iliyokuwa imemhukumia hatia Rosco Jones, mmoja wa Mashahidi wa Yehova, kwa kushiriki katika kugawanya vichapo kwenye mitaa ya Opelika, Alabama, bila kulipa kodi ya leseni.
c Ona makala “Wachukiwa kwa Sababu ya Imani Yao” na “Kutetea Imani Yetu,” kwenye ukurasa wa 8-18.
[Sanduku katika ukurasa wa 21]
Kutetea Haki za Mashahidi wa Yehova
Kuwanyanyasa Mashahidi wa Yehova kumewafanya waburutwe mbele ya mahakimu na maofisa wa serikali ulimwenguni pote. (Luka 21:12, 13) Mashahidi wa Yehova wamejitahidi sana kutetea haki zao. Ushindi mbalimbali mahakamani katika nchi nyingi umesaidia kulinda uhuru wa kisheria wa Mashahidi wa Yehova, kutia ndani haki yao ya:
◻ kuhubiri kutoka nyumba hadi nyumba bila vizuizi vinavyowekewa wafanya-biashara—Murdock v. Commonwealth of Pennsylvania, Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani (1943); Kokkinakis v. Greece, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) (1993).
◻ kukusanyika kwa uhuru kwa ajili ya ibada—Manoussakis and Others v. Greece, ECHR (1996).
◻ kuamua jinsi wanavyoweza kuheshimu kwa kudhamiria bendera au mfano wa kitaifa—West Virginia State Board of Education v. Barnette, Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani (1943); Mahakama Kuu Zaidi ya Filipino (1993); Mahakama Kuu Zaidi ya India (1986).
◻ kukataa utumishi wa kijeshi unaohalifu dhamiri yao ya Kikristo—Georgiadis v. Greece, ECHR (1997).
◻ kuchagua matibabu na dawa ambazo hazihalifu dhamiri yao—Malette v. Shulman Ontario, Kanada, Mahakama ya Rufani (1990); Watch Tower v. E.L.A., Mahakama Kuu Zaidi, San Juan, Puerto Rico (1995); Fosmire v. Nicoleau, New York, Marekani, Mahakama ya Rufani (1990).
◻ kulea watoto wao kulingana na itikadi zao zinazotegemea Biblia hata wakati ambapo itikadi hizo zapingwa katika mabishano ya malezi ya watoto—St-Laurent v. Soucy Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada (1997); Hoffmann v. Austria, ECHR (1993).
◻ kuwa na, na kuendesha wakala za kisheria ambazo hupokea ondoleo la kodi ambalo hupewa wakala zinazotumiwa na dini nyingine zenye kutambuliwa—People v. Haring, New York, Marekani, Mahakama ya Rufani (1960).
◻ wale waliowekwa rasmi katika aina fulani ya utumishi wa pekee wa wakati wote kutendwa ifaavyo kwa habari ya kodi kama vile wafanyakazi wa kidini wa dini nyingine wanavyotendwa—National Institute of Social Security ya Brazili, Brasília, (1996).
[Picha katika ukurasa wa 20]
Minos Kokkinakis na mkewe
[Picha katika ukurasa wa 20]
Kunihito Kobayashi
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 19]
The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck