Kuzaliwa kwa Yesu—Masimulizi Halisi
WAZIA tukio linalojulikana sana katika historia ya nchi yako. Limethibitishwa vizuri sana, na kuandikwa na wanahistoria kadhaa. Vipi sasa ikiwa mtu fulani angekuambia jambo hili halikutukia kamwe, kwamba hilo ni ngano tu? Au, ukijihusisha wewe mwenyewe, vipi ikiwa mtu fulani angedai kwamba mengi uliyoambiwa kuhusu kuzaliwa kwa babu yako na maisha yake ya mapema ni ya uwongo? Kwa vyovyote vile, jambo hili huenda lingekuudhi. Bila shaka hungeyakubali madai hayo kijuujuu tu!
Na bado, wachambuzi siku hizi huzikataa rekodi za Gospeli juu ya kuzaliwa kwa Yesu zilizoandikwa na Mathayo na Luka. Wao husema kwamba masimulizi hayo hupingana vibaya sana na hayawezi kupatanishwa, na tena hayo mawili yana uwongo mtupu na makosa makubwa ya kihistoria. Je, hilo laweza kuwa kweli? Badala ya kukubali madai kama haya, acheni sisi tujichunguzie rekodi hizi za Gospeli. Tunapofanya hivyo, acheni tuone yale ziwezazo kutufundisha leo.
Kusudi la Kuandikwa
Kwanza kabisa inafaa kukumbuka kusudi la masimulizi haya ya Kibiblia. Haya sio wasifu; bali ni Gospeli. Kutofautisha ni jambo la maana. Katika wasifu, mwandishi huenda akaandika mamia ya kurasa, akijaribu sana kuonyesha jinsi mhusika alivyokua akawa mtu anayesifika sana. Hivyo, wasifu fulani hutumia kurasa nyingi zikielezea ukoo, kuzaliwa, na maisha ya utotoni ya mtu huyo. Gospeli haziko hivyo. Kati ya zile Gospeli nne, ni Gospeli mbili tu za Mathayo na Luka zielezazo juu ya kuzaliwa kwa Yesu na maisha yake ya utotoni. Hata hivyo, lengo lao sio kuonyesha jinsi Yesu alivyokua akawa aina ya mwanamume ambaye alikuwa. Ukumbuke, wafuasi wa Yesu walijua kwamba yeye alikuwa kiumbe wa roho kabla hajaja duniani. (Yohana 8:23, 58) Kwa hivyo Mathayo na Luka hawakutegemea maisha ya utotoni ya Yesu ili kueleza aina ya mwanamume aliyekuja kuwa. Badala ya hivyo, walisimulia matukio yaliyofaa kusudi la Gospeli zao.
Kusudi lao la kuziandika lilikuwa nini? Neno “gospeli” lamaanisha “habari njema.” Hawa wanaume wawili walikuwa na ujumbe mmoja—yaani Yesu ndiye Mesiya aliyeahidiwa, ama Kristo; kwamba alikufa kwa ajili ya dhambi za wanadamu; na kwamba alifufuliwa kwenda mbinguni. Lakini hao waandishi wawili walikuwa na hali tofauti na waliandikia wasomaji mbalimbali. Mathayo, mkusanya-kodi, aliyafanya masimulizi yake yawafae zaidi wasomaji Wayahudi. Tabibu Luka, alimwandikia “Theofilo mtukuzwa zaidi”—ambaye labda alikuwa wa cheo cha juu—na, kwa upana, wasomaji Wayahudi na wasio Wayahudi. (Luka 1:1-3) Kila mwandikaji aliteua matukio yaliyofaa zaidi na yaliyoelekea kuwasadikisha wasomaji maalumu. Hivyo, rekodi ya Mathayo hukazia unabii wa Maandiko ya Kiebrania uliotimizwa kuhusu Yesu. Kwa upande mwingine, Luka hufuata ule mfikio bora zaidi wa kuandika historia ambao wasomaji wasio Wayahudi huenda wangeuelewa.
Basi haishangazi kwamba masimulizi yao hutofautiana. Lakini hawa wawili hawapingani, kama wachambuzi fulani wanavyodai. Hawa hukamilishana, wakiunganisha habari zao vizuri ili kutokeza wazo linaloeleweka vizuri zaidi.
Kuzaliwa kwa Yesu Katika Bethlehemu
Mathayo na Luka huelezea muujiza wa ajabu uhusuo kuzaliwa kwa Yesu—aliyezaliwa na bikira. Mathayo anaonyesha kwamba muujiza huu ulitimiza unabii fulani ambao Isaya alitabiri karne nyingi zilizopita. (Isaya 7:14; Mathayo 1:22, 23) Luka anaeleza kwamba Yesu alizaliwa Bethlehemu kwa sababu usajili ulioanzishwa na Kaisari uliwalazimu Yosefu na Maria kusafiri huko. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 7.) Kuzaliwa kwa Yesu huko Bethlehemu kulikuwa jambo la maana. Karne nyingi mapema, nabii Mika alikuwa ametabiri kuwa Mesiya angezaliwa katika mji ulio karibu na Yerusalemu ambao haukuonekana kuwa na umaana wowote.—Mika 5:2.
Usiku wa kuzaliwa kwa Yesu umejulikana sana kuwa msingi unaotumiwa kutokeza Mandhari za Kuzaliwa kwa Yesu. Hata hivyo, masimulizi halisi ni tofauti sana na mandhari inayoonyeshwa mara nyingi. Mwanahistoria Luka, anayetueleza juu ya ile sensa iliyofanya Yosefu na Maria waende Bethlehemu, pia atueleza kuwahusu wachungaji waliokuwa wamelala nje pamoja na mifugo yao usiku huo wa maana sana. Hali hizi mbili zimewafanya watafiti wa Biblia wengi wakate kauli kwamba haiwezekani Yesu alizaliwa Desemba. Wao husema haielekei Kaisari angewalazimisha Wayahudi wenye matata kusafiri hadi miji ya kuzaliwa kwao msimu wa baridi na mvua, jambo ambalo lingewakasirisha hata zaidi watu wenye kuasi. Wasomi huonelea haielekei vilevile kwamba wachungaji wangekuwa wakikaa nje pamoja na mifugo yao katika hali hii ya baridi kali.—Luka 2:8-14.
Ona kwamba Yehova aliamua kutangaza kuzaliwa kwa Mwana wake, si kwa wale viongozi wa kidini wa siku hizo wenye elimu na uwezo, bali kwa wachungaji wa hali ya chini waliokuwa wakiishi nje. Yaelekea waandishi na Mafarisayo hawakuchangamana sana na wachungaji, ambao ratiba yao ya kazi haikuwaruhusu kushika mambo yote ya sheria ya mdomo. Lakini Mungu aliwapendelea wanaume hawa wanyenyekevu na waaminifu kwa heshima kubwa—ujumbe wa malaika uliwafahamisha kwamba Mesiya, ambaye watu wa Mungu walikuwa wakimtarajia kwa maelfu ya miaka, alikuwa amezaliwa hivi punde katika Bethlehemu. Ni wanaume hawa, wala sio wale “wafalme watatu” ambao mara nyingi huonyeshwa katika Mandhari za Kuzaliwa kwa Yesu, waliowatembelea Maria na Yosefu na kukiona kitoto hicho kichanga kisicho na hatia kimelala horini.—Luka 2:15-20.
Yehova Huwapendelea Watu Wanyenyekevu Wanaotafuta Kweli
Mungu huwapendelea watu wanyenyekevu wanaompenda na kutamani sana kuona utimizo wa makusudi yake. Hili ni wazo kuu linalorudiwarudiwa katika yale matukio yahusuyo kuzaliwa kwa Yesu. Wakati ambapo, mwezi mmoja hivi baada ya kuzaliwa kwa mtoto huyu, Yosefu na Maria wanampeleka hekaluni kwa kuitii Sheria ya Kimusa, wao wanatoa toleo la “jozi moja ya njiwa-tetere au hua wachanga wawili.” (Luka 2:22-24) Sheria kwa hakika ilihitaji mwanakondoo atolewe, lakini iliruhusu toleo hili lisilo ghali kwa sababu ya umaskini. (Mambo ya Walawi 12:1-8) Tafakari hilo. Yehova Mungu, Mwenye Enzi Kuu ya ulimwengu, aliiteua familia, maskini wala si tajiri, ambayo ingemlea Mwana mzaliwa-pekee, mpendwa wake. Ikiwa wewe ni mzazi, hili lapaswa kuwa kikumbusho dhahiri kwamba zawadi bora zaidi uwezayo kuwapa watoto wako—bora zaidi kuliko mali za kimwili au elimu yenye sifa—ni mazingira ya nyumbani yanayozingatia mambo ya kiroho kwanza.
Pale hekaluni, watu wengine waaminifu wawili, waabudu wanyenyekevu wanapendelewa na Yehova. Mmoja ni Ana, mjane wa miaka 84 ambaye “hakosi kamwe kuwa katika hekalu.” (Luka 2:36, 37) Mwingine ni mwanamume mzee-mzee mwaminifu aitwaye Simeoni. Wote wawili wamesisimuliwa sana na hili pendeleo ambalo Mungu amewapa—kumwona yule ambaye angekuwa Mesiya aliyeahidiwa kabla hawajafa. Simeoni ataja unabii kumhusu mtoto huyo. Ni unabii uliojaa matumaini lakini kwa kiasi fulani umechanganywa huzuni pia. Anatabiri kwamba mama huyu mchanga, Maria, siku moja atachomwa kwa maumivu juu ya mwana wake mpendwa.—Luka 2:25-35.
Mtoto Hatarini
Unabii wa Simeoni ni kikumbusha chenye kutia hofu kwamba mtoto huyu asiye na hatia atachukiwa. Hata wakati angali mtoto, chuki hii imeanza tayari. Masimulizi ya Mathayo yanatueleza kindani namna jambo hili linavyotokea. Miezi kadha imepita, na Yosefu, Maria, na Yesu sasa wanaishi katika nyumba fulani mjini Bethlehemu. Wanatembelewa na wageni kadha wasiowatarajia. Licha ya yale ambayo nyingi za Mandhari za Kuzaliwa kwa Yesu huonyesha, Mathayo haelezi waziwazi idadi ya wanaume hawa waliokuja, wala hawaiti “wanaume wenye hekima,” sembuse “wafalme watatu.” Yeye hutumia neno la Kigiriki maʹgoi, linalomaanisha “wanajimu.” Hili pekee lapasa kumfahamisha msomaji kwamba jambo fulani ovu laendelea, kwa sababu unajimu ni kazi ambayo Neno la Mungu hulaani na pia Wayahudi waaminifu waliiepuka kabisa.—Kumbukumbu la Torati 18:10-12; Isaya 47:13, 14.
Wanajimu hawa wameifuata nyota fulani kutoka mashariki na wanamletea zawadi “yule aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi.” (Mathayo 2:2) Lakini nyota hiyo haiwaelekezi Bethlehemu. Yawaelekeza Yerusalemu mpaka kwa Herode Mkuu. Hakuna mwanadamu mwingine yeyote duniani aliye na huo uwezo na nia ya kumdhuru Yesu mchanga. Huyu muuaji wa kimakusudi, mwenye kutaka makuu alikuwa amewaua watu kadhaa wa familia yake mwenyewe ya karibu aliowaona kuwa ni vitisho.a Akiwa amevurugwa na habari juu ya kuzaliwa kwa “mfalme wa Wayahudi” wa wakati ujao, anawatuma hao wanajimu kumtafuta Huyo katika Bethlehemu. Wanapoondoka, jambo la ajabu latendeka. Ile “nyota” iliyowaongoza hadi Yerusalemu yaonekana kuwa inasonga!—Mathayo 2:1-9.
Sisi hatujui kama hii ilikuwa nuru halisi katika anga au lilikuwa ono tu. Tujualo ni kwamba “nyota” hii haikutoka kwa Mungu. Ikiwa na lengo baya, inawaongoza waabudu wapagani hawa bila kukosea hadi kwa Yesu—mtoto asiye salama na asiyejiweza, akilindwa tu na seremala maskini na mke wake. Wanajimu hawa, ambao wanadanganywa na Herode bila kujua, yaelekea wangemrudishia ripoti mtawala huyu mlipiza-kisasi, na hilo lingesababisha kuangamizwa kwa mtoto huyo. Lakini Mungu anaingilia kati kupitia ndoto na kuwafanya warudi kwao kwa njia tofauti. Hivyo, hiyo “nyota” lazima ilikuwa mbinu ya Shetani, adui ya Mungu, ambaye angefanya lolote ili kumdhuru Mesiya. Ni jambo lililo kinyume kabisa kama nini kwamba ile “nyota” na wanajimu huonyeshwa katika Mandhari za Kuzaliwa kwa Yesu kama wajumbe wa Mungu!—Mathayo 2:9-12.
Hata hivyo, Shetani hachoki. Kibaraka wake katika jambo hili, Mfalme Herode, anaamuru watoto wote katika Bethlehemu walio chini ya miaka miwili wauawe. Lakini Shetani hawezi kushinda pambano dhidi ya Yehova. Mathayo asema kuwa Mungu alikuwa ameona mapema sana hata mauaji haya yenye ukatili ya watoto wasio na hatia. Yehova alimkabili Shetani tena kwa kumtuma malaika amwonye Yosefu atorokee Misri ili kupata usalama. Mathayo anaripoti kwamba baada ya muda fulani Yosefu aliisafirisha tena familia yake ndogo na hatimaye akakaa nayo Nazareti, ambako Yesu na ndugu na dada zake wachanga walikulia.—Mathayo 2:13-23; 13:55, 56.
Kuzaliwa kwa Kristo—Kunachomaanisha Kwako
Je, umeshangazwa kwa namna fulani na muhtasari huu wa matukio yanayozunguka kuzaliwa kwa Yesu na maisha yake ya utotoni? Wengi hushangazwa. Wanashangaa kutambua kwamba masimulizi haya yanapatana vizuri na ni sahihi, licha ya madai ya watu fulani wanaopinga kwa dhati. Wameshangaa kutambua kwamba matukio fulani yalitabiriwa mamia ya miaka mapema. Na pia wameshangaa kwamba mambo fulani muhimu katika Gospeli hutofautiana sana na jinsi yanavyoonyeshwa katika masimulizi ya Mandhari ya Kuzaliwa kwa Yesu na ya zile hori.
Labda la kushangaza kupita yote, ni kwamba sherehe nyingi za kidesturi za Krismasi hazihusishi mambo makuu ya masimulizi ya Gospeli. Kwa mfano, wengi hawamfikirii Baba ya Yesu, ambaye ni Yehova Mungu, bali si Yosefu. Hebu wazia hisia zake alipowakabidhi Yosefu na Maria mwana wake mpendwa ili wamlee na kumtunza. Wazia maumivu makali ya Baba wa mbinguni kumruhusu Mwana wake kulelewa katika ulimwengu ambamo mfalme aliyejaa chuki angepanga njama ya kumwua hata wakati angali mtoto mchanga tu! Upendo mkubwa sana kwa mwanadamu ulimfanya Yehova aandae dhabihu hii.—Yohana 3:16.
Yule Yesu wa kweli mara nyingi hukosekana wakati wa misherehekeo ya Krismasi. Naam, hakuna rekodi yoyote inayoonyesha kamwe kwamba aliwaambia wanafunzi wake juu ya siku ya kuzaliwa kwake; wala hakuna chochote kinachoonyesha kwamba wafuasi wake walisherehekea siku ya kuzaliwa kwake.
Yesu hakuwaamuru wafuasi wake wakumbuke kuzaliwa kwake, bali kifo chake—kuwa tukio muhimu lililoathiri historia ya ulimwengu. (Luka 22:19, 20) Yesu hakutaka akumbukwe kama kitoto kichanga horini kisichojiweza, kwa kuwa yeye hayuko hivyo sasa. Zaidi ya miaka 60 baada ya kuuawa kwake, Yesu alijitokeza kwa mtume Yohana katika ono kama Mfalme mwenye uwezo akipanda kuelekea vitani. (Ufunuo 19:11-16) Twahitaji kumjua Yesu leo kuwa Mtawala wa Ufalme wa Mungu wa mbinguni, kwa kuwa yeye ni Mfalme atakayeubadilisha ulimwengu.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa kweli, Kaisari Augusto alisema kwamba ilikuwa salama zaidi kuwa nguruwe wa Herode kuliko kuwa mwana wa Herode.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Je, Luka Alikosea?
INAWEZEKANAJE Yesu, aliyelelewa Nazareti na watu wengi wakamwita Mnazareti, awe alizaliwa Bethlehemu, umbali wa kilometa 150? Luka afafanua: “Basi katika siku hizo [kabla ya kuzaliwa kwa Yesu] agizo kutoka kwa Kaisari Augusto likatoka kwamba dunia yote inayokaliwa ipate kusajiliwa; (usajili huu wa kwanza ulitendeka wakati Kirenio alipokuwa gavana wa Siria;) na watu wote wakaanza kusafiri kwenda kusajiliwa, kila mmoja kwenye jiji lake mwenyewe.”—Luka 1:1; 2:1-3.
Wachambuzi hukosoa sana kifungu hiki wakisema kina makosa makubwa au, vibaya zaidi, chasema uwongo. Wao husisitiza kuwa sensa hii na pia utawala wa Kirenio zilikuwako mwaka wa 6 au 7 W.K. Ikiwa wanayosema ni kweli, hili lingetilia shaka kubwa masimulizi ya Luka, kwa kuwa ushahidi waonyesha kwamba Yesu alizaliwa mwaka wa 2 K.W.K. Lakini wachambuzi hawa huyapuuza mambo mawili muhimu. Kwanza, Luka anakubali kwamba kulikuwako sensa zaidi ya moja—ona kwamba anarejezea “usajili huu wa kwanza.” Yeye alijua vyema juu ya usajili mwingine wa baadaye. (Matendo 5:37) Sensa hii ya baadaye ndiyo ileile aliyoifafanua mwanahistoria Yosefo, iliyofanywa mwaka wa 6 W.K. Pili, utawala wa Kirenio hautushurutishi kuiteua tarehe hiyo ya baadaye kuwa ndio mwaka aliozaliwa Yesu. Kwa nini? Kwa sababu yaonekana Kirenio alitumika katika cheo hicho mara mbili. Wasomi wengi hukubali kwamba kipindi cha kwanza cha utawala wake kilitia ndani mwaka wa 2 K.W.K.
Wachambuzi fulani husema kwamba Luka alibuni sensa hii ili kueleza sababu ya Yesu kuzaliwa Bethlehemu na kwa njia hiyo kutimiza unabii wa Mika 5:2. Nadharia hii humfanya Luka kuwa mwongo wa kukusudia, na hakuna mchambuzi awezaye kuyapatanisha madai hayo na mwanahistoria huyu mwangalifu aliyeandika Gospeli na kitabu cha Matendo.
Kitu kingine ambacho hakuna mchambuzi anayeweza kueleza: Sensa yenyewe ilitimiza unabii! Karne ya sita K.W.K., Danieli alitabiri juu ya mtawala “atakayepitisha mwenye kutoza ushuru kati ya utukufu wa ufalme wake.” Je, unabii huu ulielekezwa kwa Augusto na agizo lake la kufanya sensa katika Israeli? Unabii huu waendelea kutabiri kwamba Mesiya, au ‘mkuu wa agano,’ ‘angevunjwa’ wakati wa utawala wa mwandamizi wa Augusto. Yesu kwa kweli ‘alivunjwa,’ yaani aliuawa, wakati wa utawala wa mwandamizi wa Augusto, Tiberio.—Danieli 11:20-22.
[Picha]
Kaisari Augusto (27 K.W.K.–14 W.K.)
Tiberio Kaisari (14-37 W.K.)
[Hisani]
Musée de Normandie, Caen, France
Photograph taken by courtesy of the British Museum
[Picha katika ukurasa wa 8]
Malaika wa Yehova aliwapendelea wachungaji wanyenyekevu kwa kuwatangazia habari njema za kuzaliwa kwa Kristo