Wokovu Hutoka kwa Yehova
“Kwetu sisi Mungu wa kweli ni Mungu wa matendo ya kuokoa.”—ZABURI 68:20, NW.
1, 2. (a) Kwa nini twaweza kusema kwamba Yehova ndiye Chanzo cha wokovu? (b) Ungeelezaje Mithali 21:31?
YEHOVA ndiye Mwokozi wa wanadamu wampendao. (Isaya 43:11) Daudi Mfalme mashuhuri wa Israeli alijua jambo hilo kutokana na mambo aliyojionea na kwa moyo wote akaimba: “Wokovu hutoka kwa Yehova.” (Zaburi 3:8, NW) Nabii Yona alitumia maneno hayohayo katika sala yenye bidii alipokuwa katika tumbo la samaki mkubwa.—Yona 2:9.
2 Solomoni mwana wa Daudi alijua pia kwamba Yehova ndiye Chanzo cha wokovu, kwa kuwa alisema: “Farasi hutayarishwa kwa ajili ya siku ya vita, lakini wokovu hutoka kwa Yehova.” (Mithali 21:31, NW) Katika Mashariki ya Kati ya kale, ng’ombe-dume walivuta plau, punda wakabeba mizigo, watu wakasafiri kwa nyumbu, farasi wakatumiwa katika shughuli za vita. Hata hivyo, kabla ya Waisraeli kuingia katika Bara Lililoahidiwa, Mungu aliamuru kwamba mfalme wao wa wakati ujao “asifanye farasi wake kuwa wengi.” (Kumbukumbu la Torati 17:16) Farasi wa vita hawangehitajiwa kwa sababu Yehova angeokoa watu wake.
3. Ni maswali yapi yanayostahili ufikirio wetu?
3 Yehova Bwana Mwenye Enzi Kuu ni “Mungu wa matendo ya kuokoa.” (Zaburi 68:20, NW) Ni wazo lenye kutia moyo kama nini! Lakini, ni ‘matendo gani ya kuokoa’ ambayo Yehova ametekeleza? Naye ameokoa nani?
Yehova Huwaokoa Waadilifu
4. Twajuaje kwamba Yehova huokoa watu wenye ujitoaji-kimungu?
4 Wale wote wanaofuata mwenendo mwadilifu wakiwa watumishi wa Mungu waliojiweka wakfu waweza kupata faraja kutokana na maneno haya ya mtume Petro: “Yehova ajua jinsi ya kukomboa watu wenye ujitoaji-kimungu kutoka katika jaribu, bali kuweka akiba watu wasio waadilifu kwa ajili ya siku ya hukumu ili kukatiliwa mbali.” Akithibitisha jambo hilo, Petro alisema kwamba Mungu “hakuacha kuadhibu ulimwengu wa kale, bali alitunza salama Noa, mhubiri wa uadilifu, pamoja na wengine saba alipoleta gharika juu ya ulimwengu wa watu wasioogopa Mungu.”—2 Petro 2:5, 9.
5. Noa alitumikia akiwa “mhubiri wa uadilifu” chini ya hali zipi?
5 Ebu wazia ukiwa katika hali za siku ya Noa. Roho waovu waliotwaa miili ionekanayo wamo duniani. Wazao wa malaika hao wasiotii wawatenda watu kikatili, nayo ‘dunia yajaa dhuluma.’ (Mwanzo 6:1-12) Hata hivyo, Noa hawezi kutishwa aache kumtumikia Yehova. Badala yake, yeye ni “mhubiri wa uadilifu.” Yeye na familia yake wajenga safina bila kushuku kamwe kwamba uovu utaondoshwa wakati wa maisha yao. Imani ya Noa yahukumu ulimwengu huo. (Waebrania 11:7) Hali za siku hizi zafanana na zile za siku ya Noa, zikiashiria hizi kuwa siku za mwisho za mfumo huu mwovu wa mambo. (Mathayo 24:37-39; 2 Timotheo 3:1-5) Basi, kama Noa, je, utathibitika kuwa mwaminifu ukiwa mhubiri wa uadilifu, ukitumikia pamoja na watu wa Mungu huku ukingojea wokovu wa Yehova?
6. Andiko la 2 Petro 2:7, 8 huthibitishaje kwamba Yehova huokoa waadilifu?
6 Petro atoa uthibitisho zaidi kwamba Yehova huokoa waadilifu. Mtume huyo asema: “[Mungu] alimkomboa Loti mwadilifu, aliyetaabishwa sana na kujitia mno kwa watu wanaokaidi sheria katika mwenendo mlegevu—kwa maana mtu huyo mwadilifu kwa yale ambayo aliona na kusikia alipokuwa akikaa miongoni mwao kutoka siku hadi siku alikuwa akitesa-tesa nafsi yake yenye uadilifu kwa sababu ya vitendo vyao vya kuasi sheria.” (2 Petro 2:7, 8; Mwanzo 19:1-29) Ukosefu wa adili katika ngono umekuwa kawaida ya maisha ya mamilioni katika siku hizi za mwisho. Kama Loti, je, wewe ‘wataabishwa sana na kujitia mno katika mwenendo mlegevu’ kwa watu walio wengi sana leo? Ikiwa ndivyo, na ikiwa unazoea uadilifu, huenda ukawa miongoni mwa wale watakaookolewa na Yehova wakati mfumo huu mwovu ufikiapo mwisho wake.
Yehova Aokoa Watu Wake Kutoka kwa Waonezi
7. Kushughulika kwake Yehova na Israeli katika Misri huthibitishaje kwamba yeye hukomboa watu wake kutoka katika uonevu?
7 Maadamu mfumo huu wa kale waendelea kuwepo, watumishi wa Yehova watapatwa na mnyanyaso na uonevu wa adui. Lakini waweza kuwa na uhakika kwamba Yehova atawakomboa, kwa kuwa zamani aliwaokoa watu wake walioonewa. Tuseme wewe ulikuwa Mwisraeli aliyeonewa na Wamisri wa siku ya Musa. (Kutoka 1:1-14; 6:8) Mungu apiga Misri kwa tauni moja baada ya nyingine. (Kutoka 8:5–10:29) Tauni ya kumi yenye kuleta kifo iwauapo wazaliwa wa kwanza wa Misri, Farao awaruhusu Waisraeli waondoke lakini baadaye ayaandaa majeshi yake ya kivita na kuwafuata mbiombio. Hata hivyo, punde si punde yeye na watu wake wanaharibiwa katika Bahari ya Shamu. (Kutoka 14:23-28) Wewe wajiunga na Musa na Israeli wote kuimba wimbo huu: “BWANA [“Yehova,” NW] ni mtu wa vita, BWANA [“Yehova,” NW] ndilo jina lake. Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini, maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu. Vilindi vimewafunikiza, walizama vilindini kama jiwe.” (Kutoka 15:3-5) Msiba sawa na huo wawangojea waonezi wote wa watu wa Mungu katika hizi siku za mwisho.
8, 9. Toa kielelezo kutoka katika kitabu cha Waamuzi kinachothibitisha kwamba Yehova huokoa watu wake kutoka kwa waonezi.
8 Kwa miaka mingi baada ya Waisraeli kuingia katika Bara Lililoahidiwa, waamuzi walitekeleza haki miongoni mwao. Nyakati nyingine, watu waliteseka kwa kuonewa na nchi za kigeni, hata hivyo Mungu alitumia waamuzi waaminifu ili kuwakomboa. Ingawa huenda sisi ‘tukaugua vivyo hivyo kwa sababu ya watu wale wanaotuonea na kutusumbua,’ Yehova pia atatuokoa tukiwa watumishi wake waaminifu-washikamanifu. (Waamuzi 2:16-18; 3:9, 15) Kwa kweli, kitabu cha Biblia cha Waamuzi hutupa uhakikisho wa jambo hilo na wa wokovu mkubwa zaidi ambao Mungu ataandaa kupitia Hakimu wake aliyewekwa rasmi, Yesu Kristo.
9 Acheni tuzikumbuke siku za Mwamuzi Baraki. Kwa sababu ya ibada ya uwongo na kukataliwa na Mungu, Waisraeli wametawalwa kikatili na Mfalme Yabini Mkanaani kwa miaka 20. Sisera ndiye mkuu wa jeshi kubwa la Wakanaani. Lakini, ‘ngao wala mkuki havionekani katika watu elfu arobaini wa Israeli,’ ingawa idadi ya watu katika taifa hilo yaweza kuwa milioni nne. (Waamuzi 5:6-8) Waisraeli wamlilia Yehova kwa kutubu. Kama vile Mungu aelekezavyo kupitia nabii wa kike Debora, Baraki awakusanya wanaume 10,000 kwenye Mlima Tabori, naye Yehova awavuta adui hadi kwenye bonde lililo chini ya mlima mrefu wa Tabori. Malejioni na magari ya vita 900 ya Sisera yaja kwa kishindo yakivuka uwanda na mto mkavu wa Kishoni. Lakini mvua nyingi yafanya mto Kishoni ufurike kwa maji mengi mno. Wakati Baraki na wanaume wake wanaposhuka Mlima Tabori bila kuonekana kwa sababu ya dhoruba, wanashuhudia uharibifu mkubwa ambao watokezwa na kuachiliwa kwa ghadhabu ya Yehova. Wanaume wa Baraki wanawaua Wakanaani wenye hofu wanaokimbia, na hakuna hata mmoja anayeponyoka. Ni onyo lililoje kwa waonezi wanaothubutu kupigana dhidi ya Mungu!—Waamuzi 4:3-16; 5:19-22.
10. Kwa nini twaweza kuwa na uhakika kwamba Mungu ataokoa watumishi wake wa siku hizi kutoka kwa waonezi wao wote?
10 Yehova atawaokoa watumishi wake wa siku hizi kutoka kwa adui zao wenye kuonea, kama vile alivyookoa Waisraeli wenye kumhofu Mungu nyakati za hatari. (Isaya 43:3; Yeremia 14:8) Mungu alimkomboa Daudi “mikononi mwa adui zake zote.” (2 Samweli 22:1-3) Kwa hiyo, hata kama tunaonewa au kunyanyaswa tukiwa watu wa Yehova, acheni tuwe na moyo mkuu, kwa kuwa Mfalme wake wa Kimesiya atatuweka huru na uonevu. Naam, “nafsi za wahitaji ataziokoa. Atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimu.” (Zaburi 72:13, 14) Ukombozi huo uko karibu kwelikweli.
Mungu Huwaokoa Wale Wamtumainio
11. Daudi mchanga alitoa kielelezo gani cha kumtegemea Yehova?
11 Ili kupata wokovu wa Yehova, yatupasa tumtumaini kwa moyo mkuu. Daudi alimtegemea Mungu kwa moyo mkuu alipoondoka kwenda kukabili jitu Goliathi. Ebu wazia Mfilisti huyo mrefu akisimama mbele ya Daudi mchanga, ambaye aita kwa sauti kubwa hivi: “Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo BWANA atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba BWANA haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya BWANA.” Punde si punde, Goliathi ni mfu, nao Wafilisti wanashindwa kabisa. Kwa wazi, Yehova aliwaokoa watu wake.—1 Samweli 17:45-54.
12. Kwa nini huenda ikasaidia kumkumbuka Eleazari, shujaa wa Daudi?
12 Tunapokabili wanyanyasaji, huenda tukahitaji ‘kujionyesha kuwa wenye moyo mkuu’ na kumtumaini Mungu kikamili zaidi. (Isaya 46:8-13, NW; Mithali 3:5, 6) Ona jambo hili lililotukia mahali paitwapo Pasdamimu. Israeli wameyakimbia majeshi ya Wafilisti. Lakini hofu haimzuii mmojawapo wa mashujaa watatu wa Daudi, Eleazari, asiendelee kupigana. Yeye asimama mahali pake katika shamba la shayiri na bila kusaidiwa awaua Wafilisti kwa upanga. Hivyo, ‘Yehova awaokoa Israeli kwa wokovu mkuu.’ (1 Mambo ya Nyakati 11:12-14, NW; 2 Samweli 23:9, 10) Hakuna yeyote atutarajiaye tushinde jeshi la kivita bila kusaidiwa. Hata hivyo, huenda nyakati nyingine tukawa peke yetu na tumesongwa na maadui. Je, tutamtegemea Yehova kwa sala, Mungu wa matendo ya kuokoa? Je, tutatafuta msaada wake ili kuepuka kusaliti waamini wenzetu kwa wanyanyasaji?
Yehova Huwaokoa Wanaoshika Uaminifu-Maadili
13. Kwa nini ilikuwa vigumu kudumisha uaminifu-maadili kwa Mungu katika ufalme wa Israeli wa makabila kumi?
13 Ili kupata wokovu wa Yehova, ni lazima tudumishe uaminifu-maadili kwake hata hali iweje. Watu wa Mungu wa nyakati za kale walipatwa na majaribu ya namna mbalimbali. Ebu fikiria yale ambayo yangelikupata kama ungeliishi katika ufalme wa Israeli wa makabila kumi. Ukali wa Rehoboamu ulikuwa umechochea makabila kumi yaache kumwunga mkono kisha wakafanyiza ufalme wa kaskazini wa Israeli. (2 Mambo ya Nyakati 10:16, 17; 11:13, 14) Kati ya wafalme wake wengi, Yehu ndiye aliyekuwa mfalme bora kabisa, lakini hata yeye ‘hakuenda katika sheria ya BWANA kwa moyo wake wote.’ (2 Wafalme 10:30, 31) Hata hivyo, ufalme huo wa makabila kumi ulikuwa na walioshika uaminifu-maadili. (1 Wafalme 19:18) Walidhihirisha imani katika Mungu, naye alithibitika kuwa pamoja nao. Licha ya kujaribiwa kwa imani yako, je, unadumisha uaminifu-maadili kwa Yehova?
14. Yehova alitekeleza wokovu gani katika siku za Mfalme Hezekia, na ni nini kilichosababisha ushindi wa Babiloni dhidi ya Yuda?
14 Kutojali Sheria ya Mungu kulikoenea sana, kuliletea ufalme wa Israeli maafa. Waashuru walipoushinda ufalme huo mwaka wa 740 K.W.K., bila shaka watu mmoja-mmoja kutoka katika makabila yake kumi walikimbilia ufalme wa Yuda wa makabila mawili, ambako wangeweza kumwabudu Yehova hekaluni mwake. Wanne kati ya wafalme wa Yuda 19 wa ukoo wa Daudi—Asa, Yehoshafati, Hezekia, na Yosia—walikuwa wenye kutokeza katika kujitoa kwao kwa Mungu. Katika siku za Hezekia, aliyeshika uaminifu-maadili, Waashuru walishambulia Yuda kwa jeshi kubwa. Katika kujibu maombi ya bidii ya Hezekia, Mungu alitumia malaika mmoja tu kuua Waashuru 185,000 katika usiku mmoja, hivyo akawaokoa waabudu Wake! (Isaya 37:36-38) Baadaye, kushindwa kwa watu kushika Sheria na kusikiza maonyo ya manabii wa Mungu kulisababisha ushindi wa Babiloni dhidi ya Yuda na kuharibiwa kwa jiji lake kuu, Yerusalemu, na hekalu pia katika mwaka wa 607 K.W.K.
15. Kwa nini wahamishwa Wayahudi katika Babiloni walihitaji kuvumilia, naye Yehova aliwaokoaje hatimaye?
15 Wahamishwa Wayahudi walihitaji kuvumilia ili wadumishe uaminifu-maadili kwa Mungu walipotekwa huko Babiloni kwa miaka 70 yenye kuhuzunisha. (Zaburi 137:1-6) Nabii Danieli alikuwa mwenye kushika uaminifu-maadili mwenye kutokeza. (Danieli 1:1-7; 9:1-3) Ebu wazia shangwe yake wakati amri ilipotolewa na Koreshi, Mfalme Mwajemi, mwaka wa 537 K.W.K., ikiwaruhusu Wayahudi kurudi Yuda ili kujenga upya hekalu! (Ezra 1:1-4) Danieli na wengineo walikuwa wamevumilia kwa miaka mingi, lakini hatimaye waliona kushindwa kwa Babiloni na kukombolewa kwa watu wa Yehova. Hilo lapaswa kutusaidia kuonyesha uvumilivu tungojeapo kuharibiwa kwa “Babiloni Mkubwa,” milki ya ulimwengu ya dini isiyo ya kweli.—Ufunuo 18:1-5.
Sikuzote Yehova Huwaokoa Watu Wake
16. Ni wokovu gani ambao Mungu alileta katika siku za Malkia Esta?
16 Sikuzote Yehova huwaokoa watu wake wanapokuwa waaminifu kwa jina lake. (1 Samweli 12:22; Isaya 43:10-12) Fikiria siku za Malkia Esta—karne ya tano K.W.K. Mfalme Ahasuero (Zaksi I) amemweka Hamani rasmi kuwa waziri mkuu. Akiwa amekasirika kwa sababu ya Mordekai Myahudi kukataa kumwinamia, Hamani anapanga njama ya kumwangamiza yeye na Wayahudi wote katika Milki ya Waajemi. Awafafanua kuwa wavunja-sheria, aongeza kutoa kishawishi cha kiuchumi, naye aruhusiwa kutumia pete yenye muhuri ya mfalme ili kuidhinisha hati inayoagiza waangamizwe. Kwa moyo mkuu, Esta afunua ukoo wake wa Kiyahudi kwa mfalme na kufichua njama ya Hamani ya kuua kimakusudi. Punde si punde, Hamani ananing’inia penye mti uleule aliotayarisha kwa ajili ya kuua Mordekai. Mordekai afanywa waziri mkuu, akiwa na mamlaka ya kuwaruhusu Wayahudi wajitetee. Wanapata ushindi mkubwa dhidi ya maadui wao. (Esta 3:1–9:19) Tukio hilo lapaswa kuimarisha imani yetu kwamba Yehova atatekeleza matendo ya kuokoa kwa niaba ya watumishi wake watiifu wa siku hizi.
17. Utii ulitimiza fungu gani katika kukombolewa kwa Wakristo Wayahudi wa karne ya kwanza walioishi Yudea?
17 Sababu nyingine ambayo hufanya Mungu awaokoe watu wake ni kwamba wao humtii yeye na Mwana wake. Ebu wazia kwamba ulikuwa mmoja wa wanafunzi Wayahudi wa Yesu wa karne ya kwanza. Yeye awaambia: “Mwonapo Yerusalemu limezingirwa na majeshi yaliyopiga kambi, ndipo jueni kwamba kufanywa ukiwa kwalo kumekaribia. Ndipo waacheni wale walio katika Yudea waanze kukimbia hadi kwenye milima.” (Luka 21:20-22) Miaka yapita, nawe wajiuliza maneno hayo yatatimizwa lini. Kisha Wayahudi waasi mwaka wa 66 W.K. Majeshi ya Waroma chini ya Sesho Galo yazingira Yerusalemu nayo yasonga mbele hadi penye kuta za hekalu. Kwa ghafula, Waroma waondoka kwa sababu isiyo dhahiri. Wakristo Wayahudi watafanya nini? Katika kichapo chake Ecclesiastical History (Kitabu cha 3, sura ya V, 3), Eusebius asema kwamba walikimbia kutoka Yerusalemu na Yudea. Walisalimika kwa sababu walitii onyo la kiunabii la Yesu. Je, wewe uko tayari hivyo kufuata mwongozo wa Kimaandiko utolewao kupitia “msimamizi-nyumba mwaminifu” aliyewekwa rasmi juu ya “mali” zote za Yesu?—Luka 12:42-44.
Kuokoka Kupata Uhai Udumuo Milele
18, 19. (a) Kifo cha Yesu kilifanya wokovu gani uwezekane, na kwa ajili ya nani? (b) Mtume Paulo aliazimia kufanya nini?
18 Kutii onyo la Yesu kuliokoa uhai wa Wakristo Wayahudi katika Yudea. Lakini kifo cha Yesu hufanya kuokoka ili kupata uhai wa milele kuwezekane kwa “namna zote za watu.” (1 Timotheo 4:10) Uhitaji wa wanadamu wa fidia ulitokea wakati Adamu alipofanya dhambi, hivyo akipoteza uhai wake mwenyewe na kusababisha jamii ya kibinadamu kuingia katika utumwa wa dhambi na kifo. (Waroma 5:12-19) Dhabihu za wanyama zilizotolewa chini ya Sheria ya Kimusa zilikuwa ishara tu ya kufunika dhambi. (Waebrania 10:1-4) Kwa kuwa Yesu hakuwa na baba wa kibinadamu, nayo roho takatifu ya Mungu kwa wazi ‘ilimfunika Maria kivuli’ tangu alipopata mimba hadi Yesu alipozaliwa, yeye alizaliwa bila kurithi dhambi au kutokamilika kwokwote. (Luka 1:35; Yohana 1:29; 1 Petro 1:18, 19) Yesu alipokufa akiwa mwenye kushika uaminifu-maadili mkamilifu, alitoa uhai wake mkamilifu ili akomboe na kuweka wanadamu huru. (Waebrania 2:14, 15) Hivyo, Kristo ‘alijitoa mwenyewe kuwa fidia inayolingana kwa ajili ya wote.’ (1 Timotheo 2:5, 6) Si wote watakaojinufaisha na uandalizi huo wa wokovu, lakini Mungu hukubali kutumiwa kwa uandalizi huo ili kunufaisha wale wanaoukubali kwa imani.
19 Kristo alikomboa uzao wa Adamu kwa kuwakilisha thamani ya dhabihu yake ya fidia kwa Mungu mbinguni. (Waebrania 9:24) Hivyo, Yesu apata Bibi-Arusi, ambaye hufanyizwa na wafuasi wake watiwa-mafuta 144,000 wanaofufuliwa kwenye uhai wa kimbingu. (Waefeso 5:25-27; Ufunuo 14:3, 4; 21:9) Yeye pia awa “Baba wa milele” kwa wale wanaokubali dhabihu yake na kupokea uhai udumuo milele wa kidunia. (Isaya 9:6, 7; 1 Yohana 2:1, 2) Ni mpango wenye upendo kama nini! Kama vile makala inayofuata itakavyoonyesha, uthamini wa Paulo wa mpango huo uko wazi katika barua yake ya pili yenye kupuliziwa aliyoandikia Wakristo katika Korintho. Kwa kweli, Paulo alikuwa ameazimia kutoruhusu chochote kimzuie asiwasaidie watu kujinufaisha na uandalizi wa ajabu wa Yehova wa kuokoka ili kupata uhai udumuo milele.
Ungejibuje?
◻ Kuna ithibati gani ya Kimaandiko kwamba Mungu huokoa watu wake walio waadilifu?
◻ Twajuaje kwamba Yehova huokoa wale ambao humtumaini na kudumisha uaminifu-maadili wao?
◻ Mungu amefanya uandalizi gani wa kuokoka kupata uhai udumuo milele?
[Picha katika ukurasa wa 12]
Daudi alimtumaini Yehova, “Mungu wa matendo ya kuokoa.” Je, wewe hufanya hivyo?
[Picha katika ukurasa wa 15]
Yehova huwaokoa watu wake sikuzote, kama alivyothibitisha siku ya Malkia Esta