Kitabu Cha Biblia Namba 18—Yobu
Mwandikaji: Musa
Mahali Kilipoandikiwa: Jangwani
Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 1473 K.W.K.
Wakati Uliohusishwa: Miaka zaidi ya 140 kati ya 1657 na 1473 K.W.K.
1. Jina la Ayubu lamaanisha nini, na ni maswali gani yanayojibiwa na kitabu cha Ayubu?
KIMOJA cha vitabu vya kale zaidi vya Maandiko yaliyopuliziwa na Mungu! Kitabu ambacho chaheshimiwa sana na ambacho hunukuliwa mara nyingi, lakini chenye kueleweka kidogo na ainabinadamu. Ni kwa nini kitabu hicho kikaandikwa, nacho kina thamani gani kwetu leo? Jibu laonyeshwa katika maana ya jina Ayubu: “Kitu cha Uhasama.” Ndiyo, kitabu hiki chajibu maswali mawili ya maana: Ni kwa nini wasio na hatia hutaabika? Ni kwa nini Mungu huruhusu uovu katika dunia? Tuna maandishi ya kutaabika kwa Ayubu na uvumilivu wake mkubwa kwa kufikiria kwetu katika kujibu maswali hayo. Yote yameandikwa, kama alivyoomba Ayubu.—Ayu. 19:23, 24.
2. Ni nini uthibitisho wa kwamba Ayubu alikuwa mtu halisi?
2 Ayubu amehusishwa na saburi na uvumilivu. Lakini je! kulipata kuwa mtu kama Ayubu? Zijapokuwa jitihada zote za Ibilisi za kuondosha kielelezo hiki bora sana cha ukamilifu kisiwe kwenye kurasa za historia, jibu liko wazi. Ayubu alikuwa mtu halisi! Yehova amtaja pamoja na mashahidi Wake Nuhu na Danieli, ambao kuishi kwao kulikubaliwa na Yesu Kristo. (Eze. 14:14, 20; linganisha Mathayo 24:15, 37.) Taifa la Kiebrania la kale lilimwona Ayubu kuwa mtu halisi. Mwandikaji Mkristo Yakobo ataja kielelezo cha Ayubu cha uvumilivu. (Yak. 5:11) Kielelezo cha maisha halisi pekee, si cha kutungwa, ndicho kingekuwa na uzito, kikisadikisha waabudu wa Mungu kwamba ukamilifu waweza kudumishwa chini ya hali zote. Zaidi ya hayo, nguvu na hisia ya hotuba mbalimbali zilizoandikwa katika Ayubu zathibitisha uhalisi wa hali hiyo.
3. Ni ushuhuda gani unaothibitisha upulizio wa Mungu wa kitabu cha Ayubu?
3 Kwamba kitabu cha Ayubu ni asilia na kimepuliziwa na Mungu yathibitishwa pia kwa kuwa Waebrania wa kale sikuzote walikitia ndani ya vitabu vya Biblia vyenye kukubaliwa, uhakika wenye kutokeza kwa vile Ayubu mwenyewe hakuwa Mwisraeli. Kuongezea marejezo ya Ezekieli na Yakobo, kitabu hicho chanukuliwa na mtume Paulo. (Ayu. 5:13; 1 Kor. 3:19) Uthibitisho wenye nguvu wa kupuliziwa na Mungu kwa kitabu hicho watolewa na upatani wacho wa kustaajabisha kulingana na mambo ya hakika ya sayansi yenye uthibitisho. Ingewezaje kujulikana kwamba Yehova ‘ananing’iniza dunia pasipo kitu,’ ambapo wakale walikuwa na madhanio ya ajabu sana juu ya jinsi dunia ilivyotegemezwa? (Ayu. 26:7, NW) Maoni fulani yaliyokuwako nyakati za kale yalikuwa kwamba dunia ilitegemezwa na ndovu kadhaa waliosimama juu ya kasa mkubwa wa baharini. Ni kwa nini kitabu cha Ayubu hakionyeshi upuuzi huo? Bila shaka ni kwa sababu Yehova aliye Muumba alitoa ukweli kupitia upulizio wa Mungu. Maelezo mengine mengi juu ya dunia na maajabu yayo na ya wanyama-mwitu na nyuni katika makao yao ya asili ni sahihi sana hivi kwamba ni Yehova Mungu tu angeweza kuwa ndiye Mtungaji na Mpuliziaji wa kitabu cha Ayubu.a
4. Drama hiyo ilitendeka wapi na lini, na ni kufikia lini kitabu cha Ayubu kilimaliza kuandikwa?
4 Ayubu aliishi katika Usi, iliyokuwa, kulingana na wanajiografia fulani, katika Arabia ya kaskazini karibu na bara lililokaliwa na Waedomi na mashariki mwa bara waliloahidiwa wazao wa Abrahamu. Wasabea walikuwa kusini, Wakaldayo upande wa mashariki. (1:1, 3, 15, 17) Wakati wa jaribio la Ayubu ilikuwa ni muda mrefu baada ya siku ya Abrahamu. Ilikuwa katika wakati ambao hakukuwako “mmoja aliye kama yeye [Ayubu] duniani, mtu mkamilifu na uelekevu.” (1:8) Hicho chaelekea kuwa kipindi baina ya kifo cha Yusufu (1657 K.W.K.), mwanamume wa imani yenye kutokeza, na wakati ambao Musa aliingia kwenye mwendo wake wa ukamilifu. Ayubu alifana katika ibada yenye kutakata katika kipindi hiki cha kuchafuliwa kwa Israeli na ibada ya roho waovu ya Misri. Zaidi ya hayo, mazoea yanayotajwa katika sura ya kwanza ya Ayubu, na Ayubu kukubaliwa na Mungu kuwa mwabudu wa kweli, vyaelekeza kwenye nyakati za wazee wa ukoo wala si kipindi cha baadaye cha kuanzia 1513 K.W.K. na kuendelea, wakati ambao Mungu alishughulika na Israeli tu chini ya Sheria. (Amo. 3:2; Efe. 2:12) Kwa hiyo, kwa kuhesabu maisha marefu ya Ayubu, yaelekea kwamba kitabu hicho chahusu kipindi cha kati ya 1657 K.W.K. na 1473 K.W.K., mwaka wa kifo cha Musa; kitabu hicho kilikamilishwa na Musa muda fulani baada ya kifo cha Ayubu na wakati Waisraeli walipokuwa wangali jangwani.—Ayu. 1:8; 42:16, 17.
5. Ni nini kinachoonyesha Musa aliandika Ayubu?
5 Ni kwa nini twasema Musa ndiye aliyekuwa mwandikaji? Hiyo ni kulingana na mapokeo ya kale zaidi, miongoni mwa Wayahudi na wasomi wa Kikristo wa mapema. Mtindo wa asilia wenye nguvu wa mashairi ya Kiebrania unaotumiwa katika kitabu cha Ayubu waonyesha wazi kwamba awali kilikuwa mtungo katika Kiebrania, lugha ya Musa. Hakiwezi kuwa kilikuwa tafsiri kutoka lugha nyingine kama vile Kiarabu. Pia, visehemu katika nathari (usemi wa kawaida) vyafanana sana na Pentateuki (vitabu vitano vya Musa) zaidi ya maandishi mengine katika Biblia. Lazima mwandikaji awe alikuwa Mwisraeli, kama vile Musa, kwa sababu Wayahudi ‘walikabidhiwa mausia ya Mungu.’ (Rum. 3:1, 2) Baada ya kukomaa, Musa alitumia miaka 40 katika Midiani, ikiwa si mbali na Usi, ambako angeweza kupokea kwa urefu habari iliyoandikwa katika Ayubu. Baadaye, alipopita karibu na bara la nyumbani kwa Ayubu wakati wa safari ya Israeli ya miaka 40 jangwani, Musa angeweza kujua na kuandika habari za kumalizia katika kitabu hicho.
6. Ni katika njia zipi kitabu cha Ayubu ni zaidi ya usanii wa kifasihi?
6 Kulingana na The New Encylopædia Britannica, kitabu cha Ayubu mara nyingi “huhesabiwa miongoni mwa usanii wa fasihi ya ulimwengu.”b Hata hivyo, kitabu hicho ni zaidi ya kuwa usanii wa kifasihi. Ayubu chatokeza miongoni mwa vitabu vya Biblia katika kutukuza nguvu za Yehova, haki, hekima, na upendo. Chafunua kwa uwazi sana suala la msingi lililo mbele ya ulimwengu wote. Kinamulikia mengi yanayosemwa katika vitabu vingine vya Biblia, hasa Mwanzo, Kutoka, Mhubiri, Luka, Warumi, na Ufunuo. (Linganisha Ayubu 1:6-12; 2:1-7 na Mwanzo 3:15; Kutoka 9:16; Luka 22:31, 32; Warumi 9:16-19 na Ufunuo 12:9; pia Ayubu 1:21; 24:15; 21:23-26; 28:28 kwa mfululizo huo na Mhubiri 5:15; 8:11; 9:2, 3; 12:13.) Chatoa majibu ya maswali mengi ya maisha. Kwa hakika hicho ni sehemu halisi ya Neno la Mungu lililopuliziwa na Mungu, kikilichangia mengi kwa namna ya uelewevu wenye mafaa.
YALIYOMO KATIKA AYUBU
7. Twamkuta Ayubu katika hali gani kitabu hicho kifungukapo?
7 Utangulizi wa kitabu cha Ayubu (1:1-5). Huu watujulisha Ayubu, mwanamume “mkamilifu na uelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu.” Ayubu ni mwenye furaha, akiwa na wana saba na mabinti watatu. Yeye ni tajiri wa kimwili mwenye mashamba akiwa na mifugo na makundi mengi ya wanyama. Ana watumishi wengi na ni “mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.” (1:1, 3) Hata hivyo, yeye si mpenda mali, kwa maana haweki tumaini lake katika mali zake za kimwili. Pia yeye ni tajiri kiroho, tajiri katika matendo mema, nyakati zote mwenye nia ya kuwasaidia wenye shida au waliosononeka, au kumpa vazi yeyote anayelihitaji. (29:12-16; 31:19, 20) Wote wamheshimu. Ayubu aabudu Mungu wa kweli, Yehova. Akataa kusujudia jua, mwezi, na nyota kama yalivyofanya mataifa ya kipagani, lakini yeye ni mwaminifu kwa Yehova, akitunza ukamilifu kwa Mungu wake na kushangilia uhusiano wa karibu pamoja Naye. (29:7, 21-25; 31:26, 27; 29:4) Ayubu atumikia akiwa kuhani kwa familia yake, akitoa dhabihu za kuteketezwa kwa ukawaida, endapo wamefanya dhambi.
8. (a) Shetani ajaje kutilia shaka ukamilifu wa Ayubu? (b) Yehova akubalije ukaidi huo?
8 Shetani amkaidi Mungu (1:6–2:13). Kwa uzuri mwingi pazia la kuzuia kuonekana laondolewa ili tuone mambo ya kimbingu. Yehova aonekana akisimamia kusanyiko moja la wana wa Mungu. Shetani pia ajitokeza miongoni mwao. Yehova avuta fikira kwa Ayubu mtumishi wake mwaminfu, lakini Shetani atilia shaka ukamilifu wa Ayubu, akishtaki kwamba Ayubu hutumikia Mungu kwa sababu ya mafaa ya kimwili apokeayo. Kama Mungu akiruhusu Shetani amnyang’anye hivyo, Ayubu ataacha ukamilifu wake. Yehova akubali ukaidi huo, akiweka kizuizi kwamba Shetani asimguse Ayubu mwenyewe.
9. (a) Ni mitihani gani mikali inayompata Ayubu? (b) Ni nini kinachotoa uthibitisho kwamba anashika ukamilifu?
9 Misiba mingi yaanza kumpata Ayubu asiye na habari. Mashambulizi ya Wasabea na Wakaldayo yanyakua utajiri wake mwingi. Dhoruba yaua wana na mabinti wake. Mtihani huo mkali washindwa kumfanya Ayubu alaani Mungu au kumpa kisogo. Badala yake, yeye asema, “jina la BWANA [Yehova, NW] na libarikiwe.” (1:21) Shetani, akiwa ameshindwa na kuthibitishwa kuwa mwongo katika shtaka hilo, ajitokeza tena mbele ya Yehova na kushtaki: “Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake.” (2:4) Shetani adai kwamba kama angeruhusiwa aguse mwili wa Ayubu, angeweza kufanya Ayubu alaani Mungu mbele ya uso wake. Akiwa na ruhusa ya kufanya kila jambo isipokuwa tu kutwaa uhai wa Ayubu, Shetani ampiga Ayubu kwa maradhi ya kuogofya. Mnofu (mwili) wake wavikwa “mabuu na madongoa ya udongo,” na mwili na pumzi yake vyawa vyenye kunuka vibaya kwa mke wake na watu wa ukoo. (7:5; 19:13-20) Kuonyesha kwamba Ayubu hajavunja ukamilifu wake, mke wake amsihi hivi: “Je! wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? umkufuru Mungu, ukafe.” Ayubu amkemea naye “hakufanya dhambi kwa midomo yake.”—2:9, 10.
10. Ni ‘faraja’ gani ya kimya anayotoa Shetani?
10 Sasa Shetani atokeza wenzi watatu, wanaokuja ‘kufariji’ (NW) Ayubu. Wao ni Elifazi, Bildadi, na Sofari. Wakiwa mbali hawamtambui Ayubu, lakini ndipo wanapochukua hatua ya kuinua sauti zao na kulia na kurusha mavumbi juu ya vichwa vyao. Kisha, waketi mbele yake ardhini bila ya kunena neno. Baada ya siku saba, mchana na usiku, za ‘faraja’ hiyo ya kimya, mwishowe Ayubu avunja kimya hicho kwa kufungua mjadala (mazungumzo) mrefu pamoja na hao wapaswao kuwa wasikitikiaji.—2:11.
11-13. Ayubu afunguaje mjadala huo, ni shtaka gani analotoa Elifazi, na jibu la Ayubu lenye bidii ni nini?
11 Mjadala: duru ya kwanza (3:1–14:22). Kuanzia hapa na kuendelea, drama hii yakunjuka katika mashairi mazuri ya Kiebrania. Ayubu alaani siku yake ya kuzaliwa na ashangaa ni kwa nini Mungu ameruhusu aendelee kuishi.
12 Katika kujibu, Elifazi ashtaki Ayubu kuwa anakosa ukamilifu. Wanyoofu hawajapata kuangamia, ajulisha rasmi. Akumbuka njozi moja ya usiku ambayo katika hiyo sauti ilimwambia kwamba Mungu hana imani katika watumishi wake, hasa wale wa udongo duni, mavumbi ya ardhi. Yeye aonyesha kwamba kutaabika kwa Ayubu ni nidhamu kutoka Mungu Mwenye Nguvu Zote.
13 Kwa bidii Ayubu amjibu Elifazi. Alia kama ambavyo kiumbe mwingineye yote angefanya akinyanyaswa na kusononeka. Kifo kingekuwa faraja. Alaumu wenzi wake kwa ajili ya kumtungia hila na ateta hivi: “Nifunzeni, nami nitanyamaa kimya; mkanijulishe ni jambo gani nililokosa.” (6:24) Ayubu ashindania uadilifu wake mwenyewe mbele ya Mungu, aliye “mlinda wanadamu.”—7:20.
14, 15. Ubishi wa Bildadi ni nini, na ni kwa nini Ayubu ahofu atashindwa kesi yake kwa Mungu?
14 Sasa Bildadi atoa hoja yake, akidokeza kwamba wana wa Ayubu wamefanya dhambi na kwamba Ayubu mwenyewe si mnyoofu, ama sivyo angesikiwa na Mungu. Yeye aagiza Ayubu atazame vizazi vilivyopita na mambo yaliyotafutwa na mababu wao kuwa kiongozi.
15 Ayubu ajibu, akishikilia kwamba Mungu si dhalimu. Wala Mungu hana lazima ya kumtolea mwanadamu hesabu, kwa maana Yeye ndiye “atendaye mambo makuu yasiyotafutikana; naam, mambo ya ajabu yasiyohesabika.” (9:10) Ayubu hawezi kumshinda Yehova akiwa mpinzani wake katika sheria. Aweza tu kusihi kibali cha Mungu. Na ingawaje, je! kuna mafaa yoyote kutafuta kufanya yaliyo haki? “Yeye huangamiza wakamilifu na waovu pia.” (9:22) Hakuna hukumu ya uadilifu duniani. Ayubu ahofu atashindwa kesi yake hata kwa Mungu. Ahitaji mpatanishi. Auliza ni kwa nini anajaribiwa na asihi Mungu akumbuke kwamba yeye amefanyizwa kwa “udongo.” (10:9) Athamini fadhili za Mungu zilizopita, lakini asema Mungu ataudhika zaidi tu kama akibisha, hata ingawa yuko upande wa haki. Afadhali afe!
16, 17. (a) Sofari atoa ushauri gani wa kujikweza? (b) Ayubu akadiriaje ‘wafariji’ wake, naye aonyesha uhakika gani wenye nguvu?
16 Sasa Sofari aingia kwenye mjadala huo. Yeye ni kama kwamba anasema: Je! kwani sisi ni watoto, tusikilize upuuzi? Wewe wasema u safi kabisa, lakini laiti Mungu angeweza kunena, angefunua hatia yako. Amwuliza Ayubu hivi: “Je! wewe waweza kuuvumbua ukuu wa Mungu?” (11:7) Ashauri Ayubu aondoe mazoea yenye kudhuru, kwa maana baraka zitawajia wale wafanyao hivyo, na hali “macho ya waovu yataingia kiwi.”—11:20.
17 Ayubu alia kwa dhihaka kali: “Hapana shaka ninyi ndinyi watu halisi, nanyi mtakapokufa, ndipo na hekima itakoma.” (12:2) Huenda akawa kitu cha kuchekwa, lakini yeye si mnyonge. Ikiwa wenzi wake wangetazama viumbe vya Mungu, hivyo pia vingewafundisha jambo fulani. Nguvu na hekima itumikayo ni vya Mungu, anayeongoza vitu vyote, hata ‘kuyaongeza mataifa ili ayaangamize.’ (12:23) Ayubu apendezwa kutoa hoja ya kesi yake kwa Mungu, lakini kwa habari ya ‘wafariji’ wake watatu—“ninyi hubuni maneno ya uongo, ninyi nyote ni matabibu wasiofaa.” (13:4) Ingekuwa ni hekima kwa upande wao kunyamaza! Aonyesha uhakika katika uhaki wa kesi yake na amwitia Mungu amsikie. Ageukia wazo la kwamba “mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu.” (14:1) Mwanadamu apita upesi, kama ua au kivuli. Huwezi kutokeza mtu safi kutoka kwa mtu mchafu. Katika kusali kwamba Mungu angemtunza sirini katika Sheoli hadi kasirani Yake igeuke, Ayubu auliza: “Mtu akifa, je! atakuwa hai tena?” Katika kujibu yeye aonyesha tumaini lenye nguvu: “Mimi ningengoja siku zote za vita vyangu, hata kufunguliwa kwangu kunifikilie.”—14:13, 14.
18, 19. (a) Elifazi afungua duru ya pili ya mjadala kwa dhihaka gani? (b) Ayubu aonaje ‘faraja’ ya wenzi wake, naye amtumainia Yehova kwa ajili ya nini?
18 Mjadala: duru ya pili (15:1–21:34). Katika kufungua mjadala wa pili, Elifazi adhihaki maarifa ya Ayubu, akisema ‘amejaza tumbo lake upepo wa mashariki.’ (15:2) Kwa mara nyingine azomea dai la Ayubu la ukamilifu, akishikilia kwamba wala mwanadamu anayekufa wala watakatifu katika mbingu hawawezi kuwa wenye imani machoni pa Yehova. Kwa njia isiyo ya moja kwa moja ashtaki Ayubu kuwa ajaribu kujionyesha mwenyewe kuwa mkuu zaidi ya Mungu na kuwa azoea uasi-imani, rushwa, na kudanganya.
19 Ayubu ajibu vikali kwamba wenzi wake ni ‘wafariji wenye kutaabisha wenye maneno mengi.’ (16:2, 3) Kama wangalikuwa mahali pake, hangewatukana. Atamani sana kuthibitishwa kuwa wa haki, na amtumaini Yehova, aliye na maandishi yake na ambaye ataamua kesi yake. Ayubu hapati hekima yoyote kwa wenzi wake. Wanaondoa tumaini lote. ‘Faraja’ yao ni sawa na kusema usiku ndio mchana. Tumaini pekee ni ‘kushuka kuzimuni [Sheoli, NW].’—17:15, 16.
20, 21. Ni uchungu gani wa moyoni anaoonyesha Bildadi kwa kusema, Ayubu apinga juu ya nini, na Ayubu aonyesha tumaini lake li wapi?
20 Ubishi unapamba moto. Bildadi sasa ni mwenye uchungu wa moyo, kwa maana ahisi Ayubu amelinganisha marafiki wake na wanyama wasio na uelewevu. Amwuliza Ayubu, “Je! dunia itaachwa kwa ajili yako wewe?” (18:4) Aonya kwamba Ayubu ataanguka katika kitanzi kibaya, iwe kielelezo kwa wengine. Ayubu hatakuwa na wazao wa kuishi baada yake.
21 Ayubu ajibu: “Je! mtanichukiza nafsi yangu hata lini, na kunivunja-vunja kwa maneno?” (19:2) Amepoteza familia na marafiki, mke na nyumba yake wamempa kisogo, na yeye mwenyewe ‘ameokoka na ngozi ya meno yake.’ (19:20) Atumaini atatokea mkombozi asuluhishe suala hilo kwa niaba yake, ili kwamba ‘amwone Mungu’ mwishowe.—19:25, 26.
22, 23. (a) Ni kwa nini Sofari ahisi ameudhika, naye asema nini juu ya madai ya dhambi za Ayubu? (b) Ayubu ajibu kwa hoja gani yenye kubomoa?
22 Sofari, kama vile Bildadi, ahisi ameudhika kwa kulazimika kusikiliza ‘maonyo yenye kutahayarisha’ ya Ayubu. (20:3) Arudia kwamba hatimaye matokeo ya dhambi za Ayubu yamempata. Sikuzote waovu hupokea adhabu kutoka kwa Mungu, nao hawana pumziko, asema Sofari, hata wanapoonea shangwe ufanisi.
23 Ayubu ajibu kwa kutoa hoja yenye kubomoa: Ikiwa sikuzote Mungu anaadhibu waovu jinsi hivyo, ni kwa nini waovu waendelea kuishi, kuzeeka, kuwa wakuu katika utajiri? Wanatumia siku zao katika nyakati njema. Ni mara ngapi wanapatwa na afa? Aonyesha kwamba matajiri na maskini hufa namna moja. Kwa kweli, mwovu mara nyingi hufa ‘salama na kwa kustarehe,’ ambapo mwadilifu huenda akafa “katika uchungu wa roho [nafsi, NW].”—21:23, 25.
24, 25. (a) Elifazi mwenye kujihesabia haki aleta juu ya Ayubu uchongezi gani wa uwongo? (b) Ni mkanusho gani wa ukali na wito wa ushindani anaotoa Ayubu katika kujibu?
24 Mjadala: duru ya tatu (22:1–25:6). Elifazi arejea kwa shambulizi la ukatili, akidhihaki dai la Ayubu la kuwa hana lawama mbele ya Mweza Yote. Atokeza uchongezi wa udanganyifu juu ya Ayubu, akidai kwamba yeye ni mbaya, amenyonya maskini, amenyima mwenye njaa mkate, na amedhulumu wajane na wavulana wasio na baba. Elifazi asema kwamba maisha ya faraghani ya Ayubu si yenye kutakata kama anavyodai na kwamba hilo laeleza sababu ya hali mbaya ya Ayubu. Lakini “ukimrudia Mwenyezi,” kwa sauti ya kuimba asema Elifazi, “atakusikia.”—22:23, 27.
25 Kwa kujibu Ayubu akanusha vikali shtaka la upumbavu la Elifazi, akisema kwamba atamani kusikizwa mbele ya Mungu, anayetambua mwendo wake wa uadilifu. Kuna wale wanaoonea wasio na baba, mjane, na maskini na wanaoua, kuiba, na kufanya uzinzi. Huenda wakaonekana wanafanikiwa kwa muda, lakini watapata thawabu yao. Watabatilishwa. “Sasa, ni nani atakayenihukumu kuwa ni mwongo?” Ayubu ataka uthibitisho.—24:25.
26. Bildadi na Sofari wana nini zaidi ya kusema?
26 Bildadi ajibu vikali kwa kifupi kuhusu hilo, akishindilia hoja yake kwamba hakuna mwanadamu anayeweza kubaki safi mbele ya Mungu. Sofari ashindwa kushiriki duru hii ya tatu. Hana la kusema.
27. Ayubu asifuje ukuu wa Mweza Yote?
27 Hoja ya kumalizia ya Ayubu (26:1–31:40). Katika hotuba ya kumalizia, Ayubu anyamazisha wenzi wake kabisa. (32:12, 15, 16) Kwa kudhihaki sana asema: “Jinsi ulivyomsaidia huyo asiye na uwezo! . . . Jinsi ulivyomshauri huyo asiye na hekima!” (26:2, 3) Hata hivyo, hakuna chochote hata Sheoli, kiwezacho kuficha lolote machoni pa Mungu. Ayubu aeleza juu ya hekima ya Mungu katika anga ya juu, dunia, mawingu, bahari, na upepo—vyote hivyo akiwa ameviona binadamu. Hayo ni matamvua (kingo) tu ya njia za Mweza Yote. Hata si mnong’ono wa utukufu wa Mwenye Nguvu Zote.
28. Ni taarifa gani ya moja kwa moja anayotoa Ayubu juu ya ukamilifu?
28 Akiwa amesadikishwa juu ya kutokuwa kwake na hatia, ajulisha hivi rasmi: “Hata nitakapokufa sitajiondolea uelekevu [ukamilifu, NW] wangu.” (27:5) La, Ayubu hajafanya lolote la kustahili yaliyompata. Kinyume cha mashtaka yao, Mungu atathawabisha ukamilifu kwa kuhakikisha kwamba vitu vilivyowekwa akiba na waovu katika fanaka yao vitakuwa urithi wa waadilifu.
29. Ayubu anaelezaje hekima?
29 Binadamu ajua mahali zinakotoka hazina za dunia (fedha, dhahabu, shaba), “basi hekima yatoka wapi?” (28:20) Ameitafuta miongoni mwa walio hai; ametazama ndani ya bahari; haiwezi kununuliwa kwa dhahabu au fedha. Mungu ndiye anayeelewa hekima. Yeye huona hadi miisho ya dunia na mbingu, huagiza upepo na maji, na huongoza mvua na mawingu ya dhoruba. Ayubu amalizia hivi: “Tazama, kumcha Bwana [Yehova, NW] ndiyo hekima, Na kujitenga na uovu ndio ufahamu.”—28:28.
30. Ni mrejesho gani anaotamani Ayubu, lakini hali yake ya sasa ni nini?
30 Kisha Ayubu mwenye kuteseka aeleza historia ya maisha yake. Atamani kurejeshwa kwenye hali ya ukaribu sana na Mungu aliyokuwa nayo awali, wakati alipostahiwa hata na viongozi wa mji. Alikuwa mwokoaji wa wenye kuteseka na macho kwa vipofu. Shauri lake lilikuwa zuri, na watu walingojea maneno yake. Lakini sasa, badala ya kuwa na msimamo wenye heshima, achekwa hata na wale wa siku chache, ambao mababa zao hawakustahili hata kuwa pamoja na mbwa wa kundi lake la mifugo. Wanamtema mate na kumpinga. Sasa, katika mateso yake makubwa zaidi, hawampi pumziko.
31. Ayubu ana uhakika juu ya hukumu ya nani, naye asema nini juu ya maandishi ya kweli ya maisha yake?
31 Ayubu ajieleza kuwa binadamu aliyejiweka wakfu na aomba ahukumiwe na Yehova. ‘Atanipima katika mizani iliyo sawasawa, na Mungu ataujua uelekevu [ukamilifu, NW] wangu.’ (31:6) Ayubu atetea vitendo vyake vya wakati uliopita. Yeye hajapata kuwa mzinzi, wala mtunga hila juu ya wengine. Hajapata kupuuza wenye uhitaji. Hajapata kutumainia utajiri wa kimwili, hata ingawa alikuwa tajiri. Hajapata kuabudu jua, mwezi, na nyota, kwa maana “hilo nalo lingekuwa uovu wa kuadhibiwa na waamuzi; kwani ningemwambia uongo Mungu aliye juu.” (31:28) Ayubu aalika mpinzani wake katika sheria apeleke mashtaka juu ya kumbukumbu ya kweli ya maisha yake.
32. (a) Ni nani anayenena sasa? (b) Ni kwa nini kasirani ya Elihu yawakia Ayubu na wenzi wake, na ni nini kinachomsukuma anene?
32 Elihu anena (32:1–37:24). Muda huo wote, Elihu, mzao wa Buzi, mwana fulani wa Nahori, na hivyo mtu wa ukoo wa mbali wa Abrahamu, amekuwa akisikiliza mjadala huo. Amengojea kwa sababu ya kuhisi kwamba wale wenye umri mkubwa wapasa kuwa na maarifa mengi zaidi. Hata hivyo, si umri unaoleta uelewevu, bali roho ya Mungu. Kasirani ya Elihu yamwakia Ayubu “kwa sababu alikuwa amejipa haki mwenyewe zaidi ya Mungu,” lakini ina moto hata zaidi kwa wenzi watatu wa Ayubu kwa ajili ya ukosefu wao mkubwa wa hekima katika kumtangaza Mungu kuwa mwovu. Elihu ‘amejaa maneno,’ na roho ya Mungu yamsukuma ayatoe lakini bila ya kuegemea upande wala ‘kujipendekeza kwa mtu ye yote.’—Ayu. 32:2, 3, 18-22; Mwa. 22:20, 21.
33. Ayubu amekosea wapi, hata hivyo ni kibali gani ambacho Mungu atamwonyesha?
33 Elihu anena katika weupe wa moyo, akikiri kwamba Mungu ndiye Muumba wake. Ataja kwamba Ayubu amekuwa mwenye kuhangaikia zaidi ondoleo la lawama lake kuliko lile la Mungu. Haikuwa lazima kwa Mungu kujibu maneno yote ya Ayubu, kama kwamba Yeye alipaswa kutetea haki ya vitendo Vyake, na hali Ayubu alikuwa ameshindana na Mungu. Hata hivyo, nafsi ya Ayubu ikaribiapo kifo, Mungu ampendelea kwa mjumbe, akisema: “Mwokoe asishuke shimoni; Mimi nimeuona ukombozi. Nyama ya mwili wake itakuwa laini kuliko ya mtoto; huzirudia siku za ujana wake.” (Ayu. 33:24, 25) Mwadilifu atarejeshwa!
34. (a) Ni makaripio gani mengine anayotoa Elihu? (b) Badala ya kuadhimisha uadilifu wake mwenyewe, Ayubu apaswa kufanya nini?
34 Elihu atoa wito kwa wenye hekima wasikilize. Akaripia Ayubu kwa ajili ya kusema hakuna faida kuwa mshika ukamilifu: “Mungu asidhaniwe kutenda udhalimu; wala Mwenyezi kufanya uovu. Kwani atamlipa binadamu kwa kazi yake.” (34:10, 11) Aweza kuondoa pumzi ya uhai, na mnofu wote uishe. Mungu huhukumu bila upendeleo. Ayubu amekuwa akitanguliza mno uadilifu wake. Amefanya harara, si kimakusudi, bali “pasipo maarifa”; na Mungu amekuwa mwenye kumstahimili. (34:35) Mengi zaidi yahitaji kusemwa kwa ajili ya kuondolea Mungu lawama. Mungu hataondoa macho yake kwa mwadilifu, bali atamkaripia. “Hauhifadhi uhai wa waovu; lakini huwapa wateswao haki yao.” (36:6) Kwa kuwa Mungu ndiye Mfunzi mkuu zaidi, Ayubu apaswa kutukuza utendaji Wake.
35. (a) Ayubu apaswa kuelekeza uangalifu kwenye nini? (b) Yehova ataonyesha nani kibali?
35 Katika mazingira yenye kutisha ya dhoruba yenye kuongezeka, Elihu anena juu ya mambo makuu yaliyofanywa na Mungu na juu ya kuongoza Kwake nguvu za asili. Kwake Ayubu asema: “Simama kimya, uzifikiri kazi za Mungu za ajabu.” (37:14) Fikiria uzuri wa kidhahabu na adhama yenye kutisha ya Mungu, zinazozidi mno binadamu hata asiweze kuzifunua. “Yeye ni mkuu mwenye uweza; tena mwenye hukumu, na mwingi wa haki, hataonea.” Ndiyo, Yehova atawaheshimu wale wanaomhofu, si wale “walio na hekima mioyoni” mwao wenyewe.—37:23, 24.
36. Ni kupitia somo gani la kitendo na kwa mfululizo gani wa maswali Yehova mwenyewe sasa afunza Ayubu?
36 Yehova ajibu Ayubu (38:1–42:6). Ayubu alikuwa ameuliza Mungu anene naye. Sasa Yehova kwa fahari amjibu kutoka kwenye dhoruba. Aweka mbele ya Ayubu mfululizo wa maswali ambayo yenyewe ni somo lenye kitendo juu ya uduni wa binadamu na utukufu wa Mungu. “Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? . . . Ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni, hapo nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha?” (38:4, 6, 7) Hiyo ilikuwa zamani za kale kabla ya wakati wa Ayubu! Moja baada ya jingine, maswali yazushwa ambayo Ayubu hawezi kujibu, wakati Yehova aelekezapo kwenye bahari ya dunia, vazi layo la wingu, mapambazuko, malango ya kifo, na nuru na giza. “Hukosi unajua, maana ulizaliwa wakati huo, na hesabu ya siku zako ni kubwa!” (38:21) Na vipi juu ya maghala ya theluji na mawe-barafu ya mvua, dhoruba na mvua na matone ya umande, barafu na sakitu, vikundi vikubwa vya nyota za kimbingu, umeme na tabaka za mawingu, na hayawani na nyuni?
37. Ni maswali gani zaidi yanayomnyenyekeza Ayubu, naye alazimika kukubali na kufanya nini?
37 Kwa unyenyekevu Ayubu akubali: “Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu.” (40:4) Yehova aamuru Ayubu akabiliane na suala hilo. Atokeza mfululizo mwingine wa maswali yenye kutokeza wito wa ushindani yanayokweza adhama, ukuu, na nguvu zake, kama zionyeshwavyo katika viumbe vyake vya asili. Hata Behemothi na Leviathani ni wenye nguvu zaidi ya Ayubu! Akiwa amenyenyekezwa kabisa, Ayubu akiri maoni yake yenye kosa, naye akubali kwamba alinena bila ya maarifa. Akimwona Mungu sasa, si kwa kusikia tu bali kwa uelewevu, atangua aliyosema na kutubu “katika mavumbi na majivu.”—42:6.
38. (a) Yehova amaliziaje kwa Elifazi na wenzi wake? (b) Ni kibali na baraka gani anayompa Ayubu?
38 Hukumu na baraka ya Yehova (42:7-17). Kisha Yehova ashtaki Elifazi na wenzi wake wawili kwa kutonena mambo ya ukweli juu Yake. Ni lazima watoe dhabihu na kuuliza Ayubu awaombee. Baada ya hilo, Yehova arekebisha hali ya utumwa ya Ayubu, akimbariki maradufu. Nduguze, dadaze, na marafikize wa hapo awali wamrudia wakiwa na zawadi, naye abarikiwa na kondoo, ngamia, ng’ombe, na punda-jike maradufu ya ilivyokuwa hapo awali. Kwa mara nyingine ana watoto kumi, binti zake watatu wakiwa wanawake warembo zaidi katika bara lote. Maisha yake yarefushwa kimwujiza kwa miaka 140, hivi kwamba aja kuona vizazi vinne vya wazao wake. Afa “mzee sana mwenye kujawa na siku.”—42:17.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
39. Ni katika njia gani mbalimbali kitabu cha Ayubu kinatukuza na kuadhimisha Yehova?
39 Kitabu cha Ayubu chatukuza Yehova na kushuhudia hekima na nguvu zake zisizo na kipimo. (12:12, 13; 37:23) Katika kitabu hiki kimoja, Mungu arejezewa kuwa Mweza Yote mara 31, ambazo ni zaidi sana ya Maandiko mengine yote. Simulizi hilo laadhimisha umilele wake na cheo chake kilichotukuka (10:5; 36:4, 22, 26; 40:2; 42:2) na pia haki, fadhili za upendo, na rehema zake (36:5-7; 10:12; 42:12). Chakazia kuondolewa lawama kwa Yehova kuliko wokovu wa binadamu. (33:12; 34:10, 12; 35:2; 36:24; 40:8) Yehova, Mungu wa Israeli, aonyeshwa pia kuwa Mungu wa Ayubu.
40. (a) Ni jinsi gani kitabu cha Ayubu kinaadhimisha na kueleza kazi za uumbaji za Mungu? (b) Kinatoaje muono wa kimbele na kupatana na mafundisho ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo?
40 Maandishi katika Ayubu yaadhimisha na kueleza kazi ya Mungu ya uumbaji. (38:4–39:30; 40:15, 19; 41:1; 35:10) Chapatana na taarifa ya Mwanzo kwamba binadamu amefanyizwa kutoka kwa mavumbi na kwamba yeye hurudi kwayo. (Ayu. 10:8, 9; Mwa. 2:7; 3:19) Pia hutumia semi ‘mteteaji [mkombozi, NW],’ “ukombozi,” na ‘kuwa hai tena,’ hivyo kutoa muono wa kimbele wa mafundisho mashuhuri katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. (Ayu. 19:25; 33:24; 14:13, 14) Nyingi za semi za kitabu hicho zimetumiwa au zikalinganishwa na za manabii na waandikaji Wakristo. Linganisha, kwa kielelezo, Ayubu 7:17—Zaburi 8:4; Ayubu 9:24—1 Yohana 5:19; Ayubu 10:8—Zaburi 119:73; Ayubu 12:25—Kumbukumbu la Torati 28:29; Ayubu 24:23—Mithali 15:3; Ayubu 26:8—Mithali 30:4; Ayubu 28:12, 13, 15-19—Mithali 3:13-15; Ayubu 39:30—Mathayo 24:28.c
41. (a) Ni viwango gani vya kitheokrasi vinavyokaziwa katika Ayubu? (b) Ayubu mtumishi wa Mungu ni kielelezo kizuri kwetu leo hasa katika jambo gani?
41 Viwango vya uadilifu vya Yehova vya maisha vimeonyeshwa katika vifungu vingi. Kitabu hicho chalaani kwa nguvu kupenda mali (Ayu. 31:24, 25), ibada ya sanamu (31:26-28), uzinzi (31:9-12), kusimanga (31:29), kukosa haki na upendeleo (31:13; 32:21), ubinafsi (31:16-21), na kukosa unyofu na kusema uwongo (31:5), kikionyesha kwamba mtu anayezoea mambo hayo hawezi kupata kibali cha Mungu na uhai wa milele. Elihu ni kielelezo kizuri cha heshima nyingi na kiasi, pamoja na ujasiri, moyo mkuu, na kutukuza Mungu. (32:2, 6, 7, 9, 10, 18-20; 33:6, 33) Kutumia ukichwa kwa Ayubu mwenyewe, kufikiria familia yake, na ukaribishaji-wageni pia kwatoa somo zuri. (1:5; 2:9, 10; 31:32) Hata hivyo, Ayubu akumbukwa zaidi kwa ajili ya kushika ukamilifu na uvumilivu wenye saburi, akiweka kielelezo ambacho kimekuwa buruji lenye kutia nguvu imani kwa watumishi wa Mungu katika vizazi vyote na hasa katika hizi nyakati zenye kujaribu imani. “Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana [Yehova, NW] ya kwamba Bwana [Yehova, NW] ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”—Yak. 5:11.
42. Ni suala gani la msingi la Ufalme linalobainishwa katika Ayubu, na ni sehemu gani za kupendeza za suala hilo zinazoelezwa?
42 Ayubu hakuwa mmoja wa mbegu ya Abrahamu ambao walipewa ahadi za Ufalme, hata hivyo maandishi yanayohusu ukamilifu wake yatimiza mengi katika kubainisha uelewevu kwa makusudi ya Ufalme wa Yehova. Kitabu hicho ni sehemu ya muhimu ya maandishi ya kimungu, kwa maana chafunua suala la msingi baina ya Mungu na Shetani, linalohusu ukamilifu wa binadamu kwa Yehova akiwa Mwenye Enzi wake. Chaonyesha kwamba malaika, walioumbwa kabla ya dunia na binadamu, ni watazamaji pia na wapendezwa sana na dunia hii na matokeo ya ubishi huo. (Ayu. 1:6-12; 2:1-5; 38:6, 7) Chaonyesha kwamba ubishi huo ulikuwako kabla ya siku ya Ayubu na kwamba Shetani ni mtu halisi wa kiroho. Ikiwa kitabu cha Ayubu kiliandikwa na Musa, hilo ndilo tokeo la kwanza la usemi has·Sa·tanʹ katika maandishi ya Kiebrania ya Biblia, likitoa kitambulisho zaidi cha “nyoka wa zamani.” (Ayu. 1:6, NW, kielezi-chini; Ufu. 12:9) Pia kitabu hiki chatoa uthibitisho kwamba Mungu si ndiye kisababishi cha taabu, ugonjwa, na kifo cha ainabinadamu, na chaeleza ni kwa nini waadilifu wananyanyaswa, huku waovu na uovu vikiruhusiwa viendelee. Chaonyesha kwamba Yehova apendezwa kulisukuma suala hilo kwenye utatuzi wa kukata maneno.
43. Kwa kupatana na ufunuo wa kimungu katika kitabu cha Ayubu, ni mwendo gani unaopasa kufuatwa sasa na wote wanaotafuta baraka za Ufalme?
43 Sasa ndio wakati ambao wote wanaotaka kuishi chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu wapaswa kujibu Shetani, “mshitaki,” kwa mwendo wao wa ukamilifu. (Ufu. 12:10, 11) Hata katikati ya ‘majaribu yenye kutatanisha,’ washika ukamilifu lazima waendelee kusali kwa ajili ya jina la Mungu litakaswe na kwa ajili ya Ufalme wake kuja na kukomesha Shetani na mbegu yake yote yenye kudhihaki. Hiyo itakuwa siku ya Mungu ya “mapigano na vita,” itakayofuatwa na faraja na baraka ambazo Ayubu alitumainia kuzishiriki.—1 Pet. 4:12, NW; Mt. 6:9, 10; Ayu. 38:23; 14:13-15.
[Maelezo ya Chini]
a Insight on the Scriptures, Vol. 1, pages 280-1, 663, 668, 1166; Vol. 2, pages 562-3
b Insight on the Scriptures, Vol.2. page 83
c 1987, Buku 6, ukurasa 562.