Hofu—Imeenea Sasa Lakini Si Milele!
WANAFUNZI wa Neno la Mungu hawashangai kwamba hofu imeenea sana. Kama ambavyo Mashahidi wa Yehova wametangaza sana katika huduma yao, kuna uthibitisho mwingi kwamba tunaishi katika wakati uliotiwa alama katika historia ya kibinadamu. Unajua umetiwa alama kwa hofu ambayo imeenea. Lakini muda mrefu uliopita Yesu alitia alama, au alielekezea, wakati wetu. Alikuwa akijibu maswali ya mitume kuhusu kuwapo kwake na umalizio wa mfumo wa mambo, au ‘mwisho wa ulimwengu.’—Mathayo 24:3.
Ifuatayo ni sehemu ya utabiri wa Yesu:
“Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi; na njaa na tauni mahali mahali; na mambo ya kutisha [“kutia hofu,” New World Translation] na ishara kuu kutoka mbinguni.”—Luka 21:10, 11.
Je, uliona maelezo yake juu ya “mambo ya kutia hofu”? Baadaye katika jibu lilo hilo, Yesu alitaja jambo jingine kuu kuhusu hofu inayoweza kukuathiri na wapendwa wako moja kwa moja. Lakini kabla ya kuzungumzia hilo, ebu tupitie kifupi uthibitisho mwingine wa ziada unaoonyesha kwamba tunaishi katika siku za mwisho.—2 Timotheo 3:1.
Hofu Ifaayo ya Vita
Mapigano ya kijeshi yameharibu sehemu nyingi za dunia. Kwa mfano, gazeti Geo liliita vile visima vya mafuta vilivyoachwa vikichomeka mwishoni mwa pigano la majuzi la Mashariki ya Kati kuwa “msiba mkuu zaidi wa kimazingira uliopata kusababishwa na binadamu.” Vita vimeua au kulemaza makumi ya mamilioni ya watu. Mbali na vifo vya mamilioni ya wanajeshi na raia katika Vita ya Ulimwengu 1, watu milioni 55 waliuawa katika Vita ya Ulimwengu 2. Kumbuka kwamba ikiwa sehemu ya ishara ya kwamba mwisho wa ulimwengu ulikuwa karibu, Yesu alisema “taifa li[nge]ondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme.”
Pia hatuwezi kupuuza majaribio ya mwanadamu ya kuangamiza jamii nzima-nzima au vikundi vya watu. Vifo vya mamilioni ya Waarmenia, Wakambodia, Warwanda, Waukrainia, Wayahudi, na wengine vimeongeza hatia kubwa ya damu ya wanadamu katika karne ya 20. Na machinjo huendelea katika nchi ambako chuki za kikabila zinachochewa na wanadini wenye siasa kali. Ndiyo, vita vingali vinalowesha dunia kwa damu ya wanadamu.
Vita vya kisasa huendelea kuua watu hata baada ya vita kuisha. Kwa mfano, fikiria kule kutega ovyoovyo baruti ardhini. Kulingana na ripoti moja ya shirika la utafiti liitwalo Human Rights Watch, “baruti zipatazo milioni 100 ulimwenguni pote zinahatarisha raia.” Baruti hizo huendelea kuhatarisha wanaume, wanawake, na watoto wasio na hatia muda mrefu baada ya vita zilizotumiwa kuisha. Inasemwa kwamba kila mwezi maelfu ya watu hulemazwa au kuuawa na baruti zinazotegwa ardhini katika nchi zaidi ya 60. Kwa nini tisho hili kwa uhai na mwili lisiondolewe? The New York Times lilisema: “Baruti nyingi zaidi hutegwa ardhini kila siku kuliko zile zinazoondolewa katika harakati za kuziondoa, kwa hiyo idadi ya majeruhi huzidi kupanda.”
Makala hiyo ya gazeti ya 1993 iliripoti kwamba kuuza baruti hizo kumekuwa biashara “inayochuma kufikia dola milioni 200 kila mwaka.” Hiyo yashirikisha “makampuni na mashirika ya serikali yapatayo 100 katika nchi 48” ambayo “yamekuwa yakisafirisha nje [baruti za] aina tofauti-tofauti 340.” Na kwa ukatili, baadhi ya baruti zimefanyizwa zifanane na vichezeo ili zivutie watoto! Ebu wazia, kulenga kimakusudi watoto wasio na hatia ili kuwalemaza au kuwaangamiza! Uhariri mmoja wenye kichwa “Mashine za Kulipuka Milioni 100” ulidai kwamba baruti “zimeua au kulemaza watu wengi zaidi ya vita vya kikemikali, kibiolojia, au vya kinyukilia.”
Lakini baruti zinazotegwa ardhini si silaha pekee zinazouzwa katika masoko ya ulimwengu. Wauza-silaha wenye pupa hufanya biashara yenye kuchuma mabilioni ya dola duniani pote. The Defense Monitor, lililochapishwa na Kitovu cha Habari za Ulinzi, laripoti: “Muda wa mwongo uliopita [taifa fulani kuu] lilisafirisha nje silaha zenye thamani ya dola Bilioni 135.” Taifa lili hili lenye nguvu “liliidhinisha [pia] uuzaji wenye thamani ya kushangaza ya dola Bilioni 63, wa silaha, ujenzi wa kijeshi, na mazoezi kwa mataifa 142.” Hivyo matayarisho yanafanywa kwa vita na mateseko ya binadamu ya wakati ujao. Kulingana na The Defense Monitor, katika “1990 pekee, vita vilifanya watu milioni 5 kuzoezwa kutumia silaha, vikagharimu zaidi ya dola Bilioni 50, na kuua robo milioni ya watu, wengi wao wakiwa raia.” Hakika unaweza kukumbuka vita vingi ambavyo vimepiganwa tangu mwaka huo, vikileta hofu na kifo kwa mamilioni zaidi ya watu!
Uharibifu Zaidi wa Dunia na Maisha Yayo
Profesa Barry Commoner aonya hivi: “Naamini kwamba ikiwa uchafuzi wa dunia unaoendelea hauzuiwi, hatimaye utaharibu dunia isiwafae binadamu kuishi.” Aendelea kusema kwamba tatizo, si kutojua, bali ni pupa ya kimakusudi. Je, wadhani kwamba Mungu wetu mwenye haki na upendo atavumilia hali hii kwa muda usio dhahiri, akituacha kwa hofu zaidi ya uchafuzi? Kuharibiwa kwa dunia kwadai wanaoiharibu watozwe hesabu kisha irekebishwe upya kwa njia ya kimungu. Hiyo ni sehemu ya kile Yesu alizungumzia katika jibu lake kwa mitume kuhusu ‘mwisho wa ulimwengu.’
Kabla ya kuzungumzia jinsi Mungu atakavyotoza hesabu, ebu tuchunguze zaidi rekodi ya mwanadamu. Hata kisehemu cha orodha ya uharibifu wa mwanadamu chahuzunisha: mvua ya asidi na mazoea ya pupa ambayo huharibu misitu mizima-mizima; kutupwa ovyoovyo kwa takataka za nyukilia, kemikali zenye sumu, na kinyesi kisichotiwa dawa; kudhoofishwa kwa lile tabaka la hewa-ozoni lenye ulinzi; na kutumia ovyoovyo dawa za kuua magugu na wadudu.
Mapendezi ya kibiashara huichafua dunia kwa njia nyingine ili kupata faida. Tani nyingi za takataka za viwanda humwagwa kila siku mitoni, baharini, hewani, na ardhini. Wanasayansi huchafua mbingu kwa takataka za vyombo vya angani, bila kuzizoa. Kwa kasi dunia inakuwa mahali pa kuzungukwa na rundo la takataka angani. Kama isingalikuwa mifumo ya kiasili ambayo Mungu alifanyiza ili dunia ijisafishe, makao yetu ya kisayari hayangaliweza kutegemeza uhai, na yaelekea kwamba mwanadamu angalisongwa pumzi zamani na takataka zake mwenyewe.
Mwanadamu hata hujichafua. Kwa kielelezo, fikiria tumbaku na matumizi mengine ya dawa za kulevya. Katika Marekani, matumizi ya dawa za kulevya yameitwa “tatizo la nambari moja la afya katika taifa hilo.” Linagharimu nchi hiyo dola bilioni 238 kila mwaka, ambazo kati yazo dola bilioni 34 hutumiwa kwa “utunzaji wa afya usio wa lazima [yaani, wenye kuepukika].” Je, wadhani tumbaku inagharimu nini kifedha na kimaisha katika nchi yenu?
Mitindo ya maisha yenye uendekevu na iliyopotoka, ambayo wengi husisitiza kuwa ni haki yao, imetokeza mazao ya kuogofya ya maradhi yenye kufisha yanayopitishwa kingono, yakisababishia wengi kifo cha mapema. Imeonwa kwamba safu za kutangaza vifo vya watu katika magazeti mashuhuri ya majiji sasa huonyesha idadi yenye kuongezeka ya watu wanaokufa wakiwa na umri wa miaka ya 30 na 40. Kwa nini? Mara nyingi ni kwa sababu tabia zao zenye uharibifu huwaua hatimaye. Ongezeko hilo lenye msiba la maradhi ya kingono na mengineyo lapatana pia na unabii wa Yesu, kwa sababu alisema kwamba kungekuwa na “tauni mahali mahali.”
Hata hivyo, uchafuzi ulio mbaya zaidi, ni ule wa akili na roho, au mtazamo wa kibinadamu. Ukifikiria zile namna zote za uchafuzi ambazo zimetajwa hadi sasa, je, si kweli kwamba nyingi kati yazo ni matokeo ya akili zilizochafuka? Angalia ule uharibifu ambao akili zenye kichaa zimetokeza kwa namna ya uuaji wa kimakusudi, unajisi, unyang’anyi wa kimabavu, na namna nyingine za ujeuri unaosababishwa na mtu kwa mwingine. Pia, wengi hutambua kwamba yale mamilioni ya mimba zinazotolewa kila mwaka ni ishara ya uchafuzi wa kiakili na wa kiroho.
Twaona mengi katika mtazamo wa vijana. Kutostahi mamlaka ya wazazi na mamlaka nyinginezo kunachangia mvunjiko wa familia na kutotii sheria na utaratibu. Ukosefu huo wa hofu ifaayo kuelekea mamlaka wahusiana moja kwa moja na ukosefu wa hali ya kiroho wa vijana. Kwa hiyo, wale wanaofundisha mageuzi, kutokuwako kwa Mungu, na nadharia nyingine zinazoharibu imani wana hatia kubwa sana. Wenye hatia pia ni walimu wa kidini ambao, katika jitihada za kukubalika kuwa wa kisasa na “sahihi,” wamekataa kufuata Neno la Mungu. Wao pamoja na wengine ambao wameloweshwa chepechepe na hekima ya ulimwengu hufundisha falsafa za kibinadamu zenye kulipinga.
Matokeo yanaonekana wazi leo. Watu hawachochewi na kumpenda Mungu na kupenda mwanadamu mwenzao, bali na pupa na chuki. Matunda yao mabaya ni ukosefu wa adili ulioenea, ujeuri, na hali ya kukata tamaa. Kwa kusikitisha, hilo huwatia hofu watu wenye kufuatia haki, kutia ndani hofu ya kwamba mwanadamu atajiangamiza na kuangamiza dunia pia.
Je, Hali Itakuwa Mbaya Zaidi au Bora?
Wakati ujao ulio karibu una nini kwa habari ya hofu? Je, hofu itazidi kuongezeka, au itashindwa? Ebu tuone tena kile ambacho Yesu aliwaambia mitume wake.
Alitaja kitu ambacho kitatukia katika wakati ujao ulio karibu—dhiki kubwa. Alisema maneno haya: “Mara baada ya ile dhiki ya siku hizo jua litatiwa giza, nao mwezi hautatoa nuru yao, nazo nyota zitaanguka kutoka mbinguni, nazo nguvu za mbinguni zitatikiswa. Na ndipo ishara ya Mwana wa binadamu itakapoonekana mbinguni, na ndipo makabila yote ya dunia yatakapojipiga yenyewe kwa maombolezo, nayo yatamwona Mwana wa binadamu akija juu ya mawingu ya mbinguni na nguvu na utukufu mkubwa.”—Mathayo 24:29, 30, NW.
Hivyo twaweza kutazamia kwamba karibuni dhiki kubwa itaanza. Unabii mwingine mbalimbali wa Biblia waonyesha kwamba sehemu yao ya kwanza itakuwa ni kulipiza kisasi kwa dini bandia duniani pote. Kisha yatafuata mambo hayo ya kushtusha ambayo yametoka kunakiliwa, kutia ndani matukio fulani ya ajabu ya kimbingu. Matokeo yatakuwa nini kwa mamilioni ya watu?
Ebu fikiria masimulizi sawia ya jibu la Yesu, yanayotupa maelezo zaidi ya kiunabii:
“Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; watu wakivunjika mioyo [“wakizimia,” NW] kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika.”—Luka 21:25, 26.
Tukio hilo lingali mbele yetu. Lakini si wanadamu wote watakaokuwa na hofu hiyo kiasi cha kuzimia. Tofauti na hilo, Yesu alisema: “Mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.”—Luka 21:28.
Aliwaeleza wafuasi wake wa kweli maneno hayo yenye kutia moyo. Badala ya kuzimia au kumalizwa na hofu, wao wangepata sababu ya kuinua vichwa vyao bila hofu, hata kama wangejua ya kwamba upeo wa dhiki kubwa ungekuwa karibu sana. Kwa nini wasiwe na hofu?
Kwa sababu Biblia yasema wazi kwamba kutakuwa na waokokaji wa hii “dhiki kubwa” yote. (Ufunuo 7:14, NW) Masimulizi yanayoahidi jambo hili yasema kwamba tukiwa miongoni mwa waokokaji, twaweza kupata baraka zisizo na kifani kutoka kwa Mungu. Yamalizia kwa uhakikisho kwamba Yesu “atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao.”—Ufunuo 7:16, 17.
Hao—nasi twaweza kutiwa ndani—wanaopata baraka hizo hawatakuwa na hofu zinazopata watu leo. Lakini, hiyo haimaanishi kwamba hawatakuwa na hofu kabisa, kwa sababu Biblia yaonyesha kwamba kuna hofu nzuri ifaayo. Makala ifuatayo itazungumzia maana ya hofu hiyo na jinsi inavyopasa kutuhusu.
[Picha katika ukurasa wa8]
Waabudu wa Yehova wangojea kwa furaha ulimwengu mpya unaokuja
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 7]
Uchafuzi: Picha: Godo-Foto; roketi: Picha ya U.S. Army; miti inayochomeka: Richard Bierregaard, Smithsonian Institution