Maisha na Huduma ya Yesu
Kutoka kwa Pilato Mpaka kwa Herode na Kurudi Tena
WAYAHUDI wanaposhtaki Yesu juu ya kusema kwamba yeye ni mfalme, Pilato anaingia tena katika jumba la gavana ili kumwuliza maswali. Ingawa Yesu hafanyi jaribio lolote la kuficha kwamba yeye ni mfalme, anaeleza kwamba Ufalme wake si tisho kwa Roma.
“Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu,” Yesu anamwambia Pilato. “Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.” Hivyo Yesu anakiri mara tatu kwamba yeye ana Ufalme, ingawa si wa chanzo cha kidunia.
Hata hivyo, Pilato anamsukuma mbele zaidi: “Wewe u mfalme basi?” Yaani, wewe ni mfalme hata ingawa Ufalme wako si sehemu ya ulimwengu huu.
Yesu anaacha Pilato ajue kwamba amekata shauri vizuri, akijibu hivi: “Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.”
Ndiyo, kusudi hasa la Yesu kuwako duniani ni kutolea “kweli” ushahidi, hasa ile kweli juu ya Ufalme wake. Yesu yuko tayari kuwa mwaminifu kwa kweli hiyo hata ikiwa itagharimu uhai wake. Ingawa Pilato anauliza: “Kweli ni nini?” hangojei maelezo zaidi. Amesikia ya kutosha ili atoe hukumu.
Pilato anarudia umati unaongoja nje ya jumba lile. Kwa wazi Yesu akiwa kando yake, anawaambia wakuu wa makuhani na wale walio pamoja nao: “Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu.”
Kwa kukasirishwa na uamuzi huo, umati unaanza kusisitiza hivi: “[Yeye] huwataharakisha watu, akifundisha katika Uyahudi wote, tokea Galilaya mpaka huku.”
Ni lazima ushupavu huo wa kutosababu kwa Wayahudi uwe unashangaza Pilato. Hivyo basi, wakuu wa makuhani na wanaume wazee wanapoendelea kupaaza sauti, Pilato anageukia Yesu na kuuliza: “Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia?” Bado, Yesu hafanyi jaribio la kujibu. Utulivu wake kwa kukabiliana na yale mashtaka yasiyo na msingi wowote unasababisha Pilato kustaajabu.
Anapojua kwamba Yesu ni Mgalilaya, Pilato anaona njia ya kujiondoa asiwe na daraka juu yake. Mtawala wa Galilaya, Herode Antipa (mwana wa Herode Mkuu), yumo Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu ya Kupitwa, hivyo basi Pilato anapeleka Yesu kwake. Mapema kidogo, Herode Antipa alikuwa amefanya Yohana Mbatizaji akatwe kichwa, halafu Herode akaogopa aliposikia juu ya kazi za kimwujiza ambazo Yesu alikuwa akifanya, akihofu huenda ikawa kwa kweli Yesu ni Yohana ambaye ameinuliwa kutoka kwa wafu.
Sasa, Herode ana shangwe mno kwa tazamio la kumwona Yesu. Hii si kwa sababu anahangaikia hali njema ya Yesu au kwamba anataka kufanya jaribio lolote halisi juu ya kama mashtaka anayofanyiwa ni ya kweli au sivyo. Bali, yeye ni mdadisi tu na anatumainia kuona Yesu akifanya mwujiza fulani.
Hata hivyo, Yesu anakataa kutosheleza udadisi wa Herode. Kwa uhakika, Herode anapokuwa akimwuliza maswali, yeye hasemi neno. Kwa kukata tamaa, Herode na walinzi askari zake wanadhihaki Yesu. Wanamvika vazi jangavu na kumfanyia mzaha. Halafu wanampeleka tena kwa Pilato. Tokeo ni kwamba, Herode na Pilato, ambao hapo kwanza walikuwa wamekuwa maadui, wanakuwa marafiki wakubwa.
Yesu anaporudi, Pilato anaita wakuu wa makuhani, watawala wa Wayahudi, na watu wakusanyike pamoja na kusema hivi: “Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lo lote katika mambo hayo mliyomshitaki; wala hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lo lote alilotenda lipasalo kufa. Kwa hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua.”
Hivyo, Pilato amejulisha rasmi mara mbili kwamba Yesu hana hatia. Ana hamu ya kumwacha huru, kwa maana anafahamu kwamba ni kwa sababu ya wivu tu kwamba makuhani wamemtia mikononi mwake. Lakini Pilato anapoendelea kujaribu kumwachilia Yesu, anapata kichocheo kingine imara afanye hivyo. Anapokuwa katika kiti chake cha hukumu, mke wake anapeleka ujumbe, akimhimiza hivi: “Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto [kwa wazi yenye asili ya kimungu] kwa ajili yake.”
Hata hivyo, Pilato anawezaje kufungua mwanamume huyu asiye na hatia, kama vile anavyojua inampasa? Yohana 18:36-38; Luka 23:4-16; Mathayo 27:12-14, 18, 19; 14:1, 2; Marko 15:2-5.
◆ Yesu anajibuje swali juu ya kuwa kwake mfalme?
◆ Ni nini “kweli” ambayo Yesu alitumia maisha yake ya kidunia akiitolea ushahidi?
◆ Hukumu ya Pilato ni nini, watu wanaitikiaje, na Pilato afanyia Yesu nini?
◆ Herode Antipa ni nani, kwa nini ana shangwe nyingi mno kumwona Yesu, naye anamfanyia nini?
◆ Kwa nini Pilato ana hamu ya kumweka Yesu huru?