Maswali Kutoka kwa Wasomaji
◼ Je! Wayahudi walikuwa na mamlaka yo yote ya kisheria kumfisha Yesu kama inavyodokezwa na maneno ya Pilato kwenye Yohana 19:6?
Hatuwezi kuwa na uhakika kama wakati huo Waroma waliwapa Wayahudi mamlaka ya kutekeleza ufishaji wa watu.
Baada ya viongozi wa Kiyahudi kutia fitina Yesu akamatwe, wao walifanya namna fulani ya kesi ya kumjaribia Wakati wa kesi ya kumjaribu, wao “walikuwa wakitafuta ushahidi bandia dhidi ya Yesu ili wamtie kifoni “Hatimaye, walitamka rasmi kuwa Yesu ni mwenye hatia ya kukufuru na wakasema kwamba kwa njia hiyo yeye alikuwa ‘anastahili kufa.’ (Mathayo 26:59, 60, 65, 66, NW) Lakini baada ya “ushauriano dhidi ya Yesu ili, kumtia kifoni,” wao walimpeleka kwa Pilato gavana Mroma—Mathayo 27:1,2, NW.
Hali hizi zimeongoza wengi wakate shauri kwamba wakati huo Wayahudi hawakuwa na ruhusa ya Kiroma kufisha Yesu Kristo kwa kutegemea shtaka hilo la kidini. Linaloonekana kama linathibitisha maoni haya ni jibu la Wayahudi wakati Pilato alipowaambia wamhukumu mshtakiwa chini ya sheria ya Kiyahudi. Wao waliitikiza hivi: “Si jambo la kisheria kwetu kuua mtu ye yote.” (Yohana 18.31, NW) Kwa uhakika, pokeo moja linalosimuliwa katika Talmudi ya Yerusalemu linasema kwamba karibu miaka 40 kabla ya uharibifu wa Yerusalemu katika 70 W.K., Wayahudi walipoteza mamlaka yao ya kufisha watenda makosa.
Basi, inashangaza kama nini kuyasoma maneno ya Pilato kwenye Yohana 19:6, NW. Akiitikiza makelele yaliyopalizwa na viongozi wa kidini ili Yesu atundikwe mtini, Pilato aliwaambia hivi “Mchukueni ninyi wenyewe na kumtundika mtini, kwa maana mimi sipati dosari yo yote katika yeye.” Taarifa hii inaelekea kuhitilafiana na yale ambayo Wayahudi walikuwa wamesema kwenye Yohana 18:31.
Mwanahistoria Myahudi Flavio Yosefo anaandaa usimulizi ulioshuhudiwa kwa macho, ambao huenda ukaangazia nuru juu ya hitilafiano hili. Yeye anaripoti kwamba wakati wa shambulizi la Kiroma juu ya Yerusalemu katika 70 W.K., waasi walikimbilia nyuma kuingia katika ua wa hekalu. Baadhi ya wapiganaji hawa waliotiwa majeraha ya damu walikuwa katika maeneo yaliyokuwa yamekuwa hayapasi kukanyagwa kwa sababu ya utakato wayo. Kwa kuchukizwa na tendo hili la kunajisi utakatifu wa lile ambalo hata Waroma walielekea kuliona kuwa eneo takatifu, Jenerali Tito alipaaza sauti hivi:
“Ninyi watu wenye kinyaa! Je! ninyi hamkusimamisha balustradi hiyo [au kizuizi kifupi chenye kugawanya sehemu ya ua] ili kukinga Nyumba Takatifu yenu? Je! ninyi hamkuwa na vipindi-vipindi vya kuweka kando-kando yayo mabamba ya zege yaliyoandikwa katika herufi za Kigiriki na zetu wenyewe, mkikataza mtu ye yote kupita ng’ambo ya kikuta hicho? Na je! sisi hatukuwapa ninyi ruhusa ya kufisha mtu ye yote ambaye alipita ng’ambo yacho, hata kama yeye alikuwa Mroma? Kwa nini, basi, ninyi wanaume wenye hatia, sasa mnakanyaga-kanyaga miili mifu ndani yacho?”—The Jewish War, kilichotafsiriwa na G. A. Williamson, ukurasa 312. Itatiki ni zetu.
Kwa sababu hiyo, hata ikiwa Waroma hawakuacha Wayahudi watumie adhabu ya kifo kwa makosa ya wenyewe kwa wenyewe, inaonekana kama kwamba wao walitoa mamlaka ya kufisha watu kwa makosa fulani mazito ya kidini. Wayahudi waliopokeza Yesu kwa Pilato huenda wakawa walifikiri lilikuwa jambo la kutamanika kuacha Waroma wafanye ufishaji huo, labda ili kufanya kifo chake kiwe cha kuchukiza zaidi, na kwa hiyo ulalamizi wo wote wa watu ungeelekezwa dhidi ya watu hao wa kigeni. (Wagalatia 3:13; Kumbukumbu 21:23) Ingawa hivyo, inawezekana ni kwa sababu ya kutaka kuepuka tatizo hilo kwamba Pilato aliwaambia: “Mchukueni ninyi wenyewe na kumtundika mtini.” Huenda ikawa yeye alikuwa akionyesha, pia, kwamba yeye alihisi kwamba ikiwa hilo lilikuwa suala la kidini lenye uzito wa kutosha, ni lazima viongozi wa kidini wajichukulie daraka la kumfisha Yesu.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Mwandiko huu kutoka kwenye ua wa hekalu(ona kisehemu cha ndani) ulionya Wamataifa dhidi ya kupita ng’ambo ya ule ukuta mfupi wa hekalu
[Credit Line]
Reproduction of the city of Jerusalem at the time of the second temple —located on the grounds of the Holyland Hotel, Jerusalem
[Credit Line]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.