Maisha na Huduma ya Yesu
Atiwa Mikononi na Kuelekezwa Kwingineko
WAKATI Pilato, kwa kusukumwa na fahari tulivu ya Yesu mteswa, apojaribupo tena kumfungua, wakuu wa makuhani wakasirika hata zaidi. Wamepiga moyo konde kutoacha chochote kivuruge kusudi lao bovu. Hivyo basi wao wafanya upya kupaaza sauti hivi: “Msulibishe! Msulibishe [Mtundike, mtundike, NW]!”
“Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe,” Pilato ajibu kwa kuchukizwa sana. Tofauti na madai yao ya mapema kidogo, Wayahudi huenda wakawa na mamlaka ya kufisha wahalifu kwa makosa ya kidini yaliyo na uzito wa kutosha. Halafu, kwa mara isiyopungua ya tano, Pilato amtangaza Yesu kuwa hana hatia, akisema hivi: “Mimi sioni hatia kwake.”
Wayahudi, kwa kuona kwamba mashtaka yao ya kisiasa yameshindwa kutokeza matokeo, waangukia nyuma kwenye lile shtaka la kidini la kukufuru lililotumiwa mapema kidogo kwenye kesi ya Yesu mbele ya Sanhedrini. “Sisi tunayo sheria,” wao wasema, “na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.”
Shtaka hili ni jipya kwa Pilato, nalo lafanya awe na hofu zaidi. Kufikia sasa afahamu kwamba Yesu si mtu wa kawaida tu, hata kama vile ndoto ya mke wake na imara nyingi ajabu ya utu wa Yesu yaonyesha. Lakini eti “Mwana wa Mungu”? Pilato ajua kwamba Yesu ni wa kutoka Galilaya. Hata hivyo, je! angeweza kuwa aliishi kabla ya hapo? Akimrudisha tena ndani ya jumba la utawala, Pilato auliza hivi: “Wewe umetokapi?”
Yesu abaki kimya. Mapema kidogo alikuwa amemwambia Pilato kwamba yeye ni mfalme, lakini kwamba Ufalme wake si sehemu ya ulimwengu huu. Sasa hakuna elezo lolote zaidi lingetimiza kusudi lenye mafaa. Hata hivyo, fahari ya Pilato yaumizwa na katao la kujibu, naye amwamkia Yesu kwa maneno haya: “Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulibisha [kukutundika, NW]?”
“Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu,” Yesu ajibu kwa staha. Amaanisha mamlaka ambayo Mungu amewapa watawala wa kibinadamu kusimamia mambo ya kidunia. Yesu aongezea hivi: “Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.” Kwa kweli, kuhani wa juu Kayafa na wenzi wake na Yuda Iskariote wote wana daraka zito kuliko Pilato kwa ajili ya kutendwa kwa Yesu isivyo haki.
Kwa kuvutiwa hata zaidi na Yesu na akiwa na hofu kwamba huenda ikawa Yeye ana asili ya kimungu, Pilato afanya upya jitihada zake za kumwachilia Yeye. Hata hivyo, Wayahudi wamjibu vikali Pilato. Wao warudia shtaka lao la kisiasa, wakitisha hivi kwa ujanja: “Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari.”
Ijapokuwa hilo lamaanisha matokeo ya kuogopesha sana, Pilato amleta Yesu nje tena. “Tazama, Mfalme wenu!” bado awasihi tena.
“Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe [Mtundike, NW]!” laja jibu.
“Je! nimsulibishe [nimtundike, NW] mfalme wenu!” Pilato auliza kwa kukata tamaa.
Wayahudi wamekuwa wakiudhika chini ya utawala wa Waroma. Kwa kweli, wao wadharau kutawalwa na Roma! Na bado, kwa unafiki, wakuu wa makuhani wasema hivi: “Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.”
Akihofu cheo na sifa yake ya kisiasa, Pilato mwishowe ajilegeza kushindwa na madai ya Wayahudi yasiyokoma, yenye kutisha. Amtia Yesu mikononi mwao. Askari wamvua Yesu joho la zambarau na kumvika mavazi yake ya nje. Yesu aongozwapo kutundikwa, afanywa abebe mti wake mwenyewe wa mateso.
Kufikia sasa ni asubuhi katikati siku ya Ijumaa, Nisani 14; labda yakaribia kuwa mchana katikati. Yesu amekuwa macho tangu asubuhi ya mapema ya Alhamisi, naye amepatwa na mateso makali moja baada ya jingine. Basi inaeleweka kwa nini imara inamwishia chini ya uzito wa ule mti. Hivyo basi mpitaji njia, Simoni fulani wa Kirene katika Afrika, anakazwa ndani ya utumishi wa kumbebea. Wanaposonga mbele, idadi kubwa ya watu wanafuata, kutia na wanawake wengi wanaojipiga-piga kwa kuomboleza na kupiga mayowe kwa ajili ya Yesu.
Akigeukia wanawake hao, Yesu anasema hivi: “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri [wenye furaha ni, NW] walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?”
Yesu anarejezea mti wa taifa la Kiyahudi, ambao ungali una umajimaji fulani wa uhai ndani yao kwa sababu ya kuwapo kwa Yesu na kuwako kwa mabaki wanaomwamini. Lakini hawa wakiisha kuondolewa katika lile taifa, ni mti mfu tu wa kiroho utakaobaki, ndiyo, tengenezo la kitaifa lililonyauka. Loo, kutakuwa na sababu iliyoje ya kulia machozi wakati majeshi ya Kiroma, yakitumikia kuwa wafishaji wa Mungu, yatakapolifanya ukiwa taifa la Kiyahudi! Yohana 19:6-17; 18:31; Luka 23:24-31; Mathayo 27:31, 32; Marko 15:20, 21.
◼ Ni shtaka gani ambalo viongozi wa kidini wanafanya dhidi ya Yesu wakati mashtaka yao ya kisiasa yanapokosa kuzaa matokeo?
◼ Kwa nini Pilato labda anakuwa mwenye hofu zaidi?
◼ Ni nani wanaochukua dhambi iliyo kubwa zaidi kwa ajili ya yale yanayopata Yesu?
◼ Makuhani wanamfanyaje Pilato amtie Yesu mikononi ili afishwe?
◼ Yesu anawaambia nini wanawake wanaomlilia, naye anamaanisha nini kwa kurejezea mti kuwa “mbichi” kisha “mkavu”?