Hoja Tano Bandia Zilizo za Kawaida —Usipumbazwe Nazo!
“MSIACHE binadamu yeyote awadanganye nyinyi kwa maneno matupu.”a Ushauri huu ulitolewa karibu miaka 2,000 iliyopita na ungali wa kweli kabisa. Leo, sisi twapatwa na miminiko kubwa sana la sauti zenye ushawishi: mabingwa wa kuigiza sinema wakitangaza ununuzi wa marashi, wanasiasa wakiendeleza sera zao, wauzaji wakipendekeza bidhaa, makasisi wakifafanua mafundisho. Mara nyingi mno sauti hizo zenye ushawishi huthibitika kuwa za udanganyifu—kama maneno matupu tu. Hata hivyo, watu kwa ujumla huongozwa vibaya nazo.
Mara nyingi hiyo ni kwa sababu watu hushindwa kupambanua ukweli na hoja bandia. Wanafunzi wa mantiki hutumia neno “hoja bandia” kusimulia mwondoko wowote wa kuacha kijia cha fikira zilizo timamu. Kwa kutaarifu kisahili, hoja bandia ni sababu yenye kuongoza vibaya au isiyo timamu, moja ambamo kukata shauri hakutegemei taarifa, au kusababu kwa utimamu, ambazo huwa zimekwisha kutangulia. Hata hivyo, huenda mapumbazo yakawa na ushawishi wenye nguvu nyingi kwa sababu mara nyingi huvutia hisia-moyo—si usababu.
Ufunguo wa kuepuka kudanganywa ni kujua utendaji wa hoja bandia. Kwa hiyo acheni tutazame mapumbazo matano ya kawaida, kwa kusudi la kunoa “uwezo wa kusababu” tuliopewa na Mungu.—Warumi 12:1, NW.
HOJA BANDIA NAMBA 1
Kumshambulia Mtu Namna hii ya hoja bandia hujaribu kuthibitisha kutofaa kwa hoja au taarifa ifaayo kabisa au kuiondolea ustahili kwa kufanya shambulio lisilofaa juu ya mtu anayeitoa.
Fikiria kielezo kutoka kwenye Biblia. Wakati mmoja Yesu Kristo alijitahidi kuwaangazia wengine maarifa juu ya kifo chake chenye kuja na ufufuo. Hayo yalikuwa mawazo mapya yaliyo magumu kueleweka na wasikilizaji wake. Lakini badala ya kupima ustahili wa mafundisho ya Yesu, baadhi yao walimshambulia Yesu mwenyewe, wakisema: “Ana pepo huyu, tena ana wazimu; mbona mnamsikiliza?”—Yohana 10:20; linganisha Matendo 26:24, 25.
Ni rahisi kama nini kubandika mtu jina la “mpumbavu,” “mkichaa,” au “mkosa maarifa” wakati asemapo jambo tusilotaka kusikia. Mbinu nyingine kama hiyo ni kushambulia mtu kwa mashutumu mengi ya werevu. Vielelezo vya aina hiyo ni: “Kama ungekuwa ukilielewa jambo hilo kikweli, hungekuwa na maoni hayo” au, “Wewe waamini jambo hilo kwa sababu tu umeambiwa uliamini.”
Lakini ingawa mashambulio kwa mtu binafsi, ya werevu na yasiyo ya werevu sana, huenda yakatisha na kushawishi, hayakanushi kamwe jambo ambalo limesemwa. Kwa hiyo uwe chonjo kuona pumbazo hili!
HOJA BANDIA NAMBA 2
Kutumia Mamlaka Namna hii ya ogopesho la maneno hufanywa kwa kuomba shuhuda za wale waitwao eti wastadi au watu maarufu. Bila shaka, ili kupata ushauri ni jambo la kiasili kutegemea watu wajuao mengi juu ya jambo fulani kuliko sisi. Lakini si matumizi yote ya mamlaka huwa na msingi wa kusababu mambo kwa utimamu.
Tuseme daktari wako akuambia: “Una maleria.” Nawe wajibu: “Wajuaje, daktari?” Jinsi lingekuwa jambo la kutosababu mambo vizuri yeye kusema: “Tazama, mimi ni daktari. Mimi najua mengi zaidi juu ya mambo haya kuliko wewe. Sikia tu ninavyosema, wewe una maleria.” Ingawa yaelekea kwamba maelezo yake ni sahihi kuhusu ugonjwa, kusababu kwamba wewe una maleria kwa sababu tu yeye asema hivyo ni hoja bandia. Ingefaa zaidi yeye azungumze mambo ya uhakika: dalili zako, matokeo ya uchunguzi wa damu, na kadhalika.
Kielelezo kingine cha kutumia mamlaka kwa njia ya kuogopesha chasimuliwa kwenye Yohana 7:32-49. Hapo twapata habari kwamba maofisa wa polisi walitumwa wakamkamate Yesu Kristo. Hata hivyo, walivutiwa sana na fundisho lake hivi kwamba badala ya kumkamata, waliwaambia wakuu wao hivi: “Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena.” Katika kujibu, adui za Yesu walisema: “Je! ninyi nanyi mmedanganyika? Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo?” Angalia kwamba hakuna jaribio lililofanywa kukanusha fundisho la Yesu. Bali, viongozi Wayahudi walitumia mamlaka yao wenyewe wakiwa “wastadi” katika Sheria ya Musa kuwa ndiyo sababu ya kupuuza lolote lililosemwa na Yesu.
Kwa kupendeza, makasisi leo wajulikana kuwa hugeukia mbinu kama hizo wasipoweza kuthibitisha kutokana na Biblia mafundisho kama Utatu, kutokufa kwa nafsi, na moto wa helo.
Matumizi ya mamlaka yasiyo halali ni mengi sana pia katika matangazo ya bidhaa, ambamo mabingwa waadhimishwa hutoa sana shuhuda katika nyanja zisizohusiana hata kidogo na ujuzi wao. Mchezaji mwenye mafanikio katika mchezo wa golfu akutia moyo ununue mashine ya fotokopi. Mchezaji kikazi wa mpira wa miguu atia moyo ununuzi wa mashine za barafu. Mwanamichezo wa mazoezi ya mwili katika michezo ya Olimpiki apendekeza ule nafaka fulani katika kiamsha-kinywa. Wengi hawangoji kidogo na kufikiri kwamba “mamlaka” hizo labda zajua kidogo tu au hazijui lolote juu ya bidhaa wanazozitembeza.
Ung’amue, pia, kwamba hata wastadi halali—kama kila mtu mwingine yeyote—huenda wakawa na maoni ya kuegemea upande mmoja. Mtafiti mwenye sifa nzuri nyingi huenda akadai kwamba tumbako haina madhara. Lakini ikiwa yeye atumiwa na biashara ya tumbako, je! ushuhuda huo wa ‘ustadi’ haupasi kutiliwa shuku?
HOJA BANDIA NAMBA 3
‘Jiunge na Umati’ Hapa kinachotumiwa ni hisia-moyo, maoni ya ubaguzi, na imani za walio wengi. Kwa ujumla watu hupenda kujipatanisha na wenzao. Sisi huelekea kujikunyata tusiseme wazi dhidi ya maoni yaliyopo kwa wingi. Elekeo hili la kuyaona maoni ya walio wengi kuwa ndiyo sahihi kwa vyovyote hutumiwa kwa matokeo yenye nguvu katika ile hoja bandia ya kwamba ‘jiunge na umati.’
Kwa kielelezo, tangazo moja la bidhaa katika gazeti maarufu la United States lilionyesha watu kadhaa wenye kutabasamu, kila mmoja akipata shangwe ya kunywa bilauri ya kileo cha miwa. Usemi huu uliandamana na picha hiyo: “Hilo Ndilo Linalotukia. Kila mahali Amerika, watu wanageukia . . . kileo cha miwa.” Hili ni ombi la wazi kwamba ‘jiunge na umati.’
Lakini ingawa huenda wengine wakafikiri au wakafanya jambo fulani, je! hiyo yamaanisha kwamba wewe wapaswa kulifanya? Zaidi ya hilo, maoni ya walio wengi si kipimo chenye kutegemeka cha ukweli. Muda wa karne zilizopita mawazo ya kila aina yamepokewa na walio wengi, lakini baadaye yakaja kuthibitishwa kuwa yenye makosa. Na bado, ile hoja bandia ya ‘jiunge na umati’ ingali yaendelea. Ule msemo wa watu wengi kwamba, ‘Kila mtu anafanya hivyo!’ husukuma watu watumie dawa za kulevya, wafanye uzinzi, waibe kutoka kwa waajiri kazi, na kudanganya juu ya kodi.
Uhakika ni kwamba, si kila mtu ambaye hufanya mambo hayo. Na hata kama kila mtu angefanya hivyo, hiyo haingekuwa sababu ya wewe kufanya hivyo. Hivyo ushauri utolewao kwenye Kutoka 23:2 ni kanuni njema ya mwenendo wa ujumla: “Usiandamane na mkutano kutenda uovu.”
HOJA BANDIA NAMBA 4
Ule Usababu wa Ama/Au Sivyo Hii hoja bandia hupunguza machaguo mengi ambayo mtu aweza kufanya yawe mawili tu. Kwa kielelezo, huenda mtu akaambiwa: ‘Ama kubali kutiwa damu mishipani au sivyo utakufa.’ Mashahidi wa Yehova hukutana mara nyingi na usababu huo kwa kisa cha uamuzi wao wenye msingi wa Biblia kwamba ‘washike mwiko wa damu’ kwa namna yoyote. (Matendo 15:29, NW) Ni nini udhaifu wa njia hii ya kusababu? Hiyo huweka nje mawezekano mengine yaliyo halali. Mambo ya uhakika yaonyesha kwamba kuna matibabu mengine, na upasuaji mwingi waweza kufanywa kwa mafanikio bila damu. Madaktari wenye ujuzi hupasua mara nyingi kukiwa na potezo dogo sana la damu. Uwezekano mwingine ni kutumia umajimaji usio damu, vitanua kiasi cha plazima.b Zaidi ya hilo, wengi wamekubali kutiwa damu mishipani wakafa. Kwa hali iyo hiyo, wengi wamekataa damu wakaishi. Hivyo pengo lililo katika usababu wa ama/au sivyo ni kubwa sana.
Hivyo basi wewe utolewapo usababu wa ama/au sivyo, jiulize, ‘Je! kweli ni machaguo mawili tu yawezayo kufanywa? Je! kungeweza kuwa na mengine?’
HOJA BANDIA NAMBA 5
Kusahilisha (Kurahisisha) Mambo Mno Hapa taarifa au hoja fulani hupuuza kufikiria mambo yafaayo, kusahilisha mno suala ambalo huenda likawa ni lenye kutatanisha.
Yakubalika kwamba si kosa kusahilisha habari isiyoeleweka kwa urahisi—walimu wazuri hufanya hivyo wakati wote. Lakini nyakati fulani jambo husahilishwa kufikia hatua ya kupotosha ukweli. Kwa kielelezo, huenda ukasoma hivi: ‘Ongezeko la haraka sana la idadi ya watu ndicho kisababishi cha umaskini katika nchi zinazositawi.’ Mna ukweli fulani katika jambo hilo, lakini lapuuza mafikirio mengine ya maana, kama vile usimamizi mbaya wa kisiasa, unyonyaji wa biashara, na vigezo vya halihewa.
Kusahilisha mambo mno kumetokeza hali nyingi za kutoelewana kwa habari ya Neno la Mungu, Biblia. Kwa kielelezo, fikiria usimulizi kwenye Matendo 16:30, 31. Hapo mtunza gereza aliuliza swali juu ya wokovu. Paulo alijibu hivi: “Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka.” Wengi wamekata shauri kutokana na hilo kwamba kumkubali Yesu kwa usahili tu akilini ndilo jambo litakwalo ili kupata wokovu!
Huku ni kusahilisha mambo mno. Ni kweli, imani katika Yesu kuwa Mkombozi wetu ni ya maana sana. Lakini pia yahitajiwa kabisa kuamini mambo ambayo Yesu alifundisha na kuyaamuru, kujipatia uelewevu kamili wa kweli za Biblia. Hiyo yaonyeshwa na uhakika wa kwamba baada ya hapo Paulo na Sila ‘walisema neno la Yehova kwa mtunza jela pamoja na wote wale walio katika nyumba yake.’ (Matendo 16:32, NW) Wokovu wahusisha utii pia. Baadaye Paulo alionyesha hilo alipoandika kwamba Yesu “akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.”—Waebrania 5:9.
Mithali moja ya kale husema: “Mjinga huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.” (Mithali 14:15) Hivyo usivutwe na hoja bandia. Jifunze kutofautisha kati ya mashambulio yafaayo kuhusu maneno yasemwayo na mashambulio hafifu juu ya watu binafsi. Usipumbazwe na matumizi yasiyofaa ya ushahidi wa “mamlaka,” mihimizo ya kwamba ‘jiunge na umati’, usababu wa ama/au sivyo, au masahilisho ya kupita kiasi—hasa wakati jambo lililo muhimu kama ukweli wa kidini lihusikapo. Chunguza mambo yote ya uhakika, au kama vile Biblia iwekavyo wazo lenyewe, ‘hakikisha mambo yote.’—1 Wathesalonike 5:21, NW.
[Maelezo ya Chini]
a Imetolewa katika Biblia kwenye Waefeso 5:6, NW.
b Ona kijitabu Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.