Marko
14 Sasa baada ya siku mbili ilikuwa sikukuu ya kupitwa na msherehekeo wa keki zisizotiwa chachu. Na makuhani wakuu na waandishi walikuwa wakitafuta sana jinsi ya kumkamata kwa mbinu ya kiufundi na kumuua; 2 kwa maana walisema kwa kurudia-rudia: “Si kwenye msherehekeo; labda kungeweza kuwa na ghasia ya watu.”
3 Na alipokuwa Bethania katika nyumba ya Simoni mwenye ukoma, akiwa ameegama kwenye mlo, mwanamke akaja na chupa ya alabasta iliyo na mafuta yenye marashi, nardo halisi, ghali sana. Akivunja ili kufungua hiyo chupa ya alabasta akaanza kuyamwaga juu ya kichwa chake. 4 Ndipo kukawa na wengine wenye kuonyesha ghadhabu miongoni mwao wenyewe: “Kwa nini umetendeka upotevu huu wa bure wa mafuta yenye marashi? 5 Kwa maana mafuta hayo yenye marashi yangaliweza kuuzwa kwa dinari zaidi ya mia tatu na kupewa kwa maskini!” Nao walikuwa wakihisi chuki kubwa juu ya huyo mwanamke. 6 Lakini Yesu akasema: “Mwacheni. Kwa nini mwajaribu kumsumbua? Alifanya kitendo bora kunielekea mimi. 7 Kwa maana sikuzote mna maskini pamoja nanyi, na wakati wowote ule mtakapo mwaweza sikuzote kuwafanyia mema, lakini mimi hamnami sikuzote. 8 Alifanya lile ambalo angeweza; alijitwalia daraka kimbele kutia mafuta yenye marashi juu ya mwili wangu kwa kufikiria maziko. 9 Kwa kweli nawaambia nyinyi, Kokote ambako habari njema yahubiriwa katika ulimwengu wote, alilofanya mwanamke huyu hakika litasimuliwa pia kuwa ukumbuko juu yake.”
10 Na Yudasi Iskariote, mmoja wa wale kumi na wawili, akaenda zake kwa makuhani wakuu kusudi amsaliti kwao. 11 Waliposikia hilo, wakashangilia na kuahidi kumpa sarafu ya fedha. Kwa hiyo yeye akaanza kutafuta jinsi ya kumsaliti kwa wakati ufaao.
12 Sasa siku ya kwanza ya keki zisizotiwa chachu, wakati ambapo kidesturi walidhabihu kafara ya sikukuu ya kupitwa, wanafunzi wake wakamwambia: “Ni wapi wataka twende na kukutayarishia kula sikukuu ya kupitwa?” 13 Ndipo akatuma wawili wa wanafunzi wake na kuwaambia: “Nendeni mwingie katika jiji, na mwanamume mwenye kuchukua chombo cha udongo cha maji atakutana nanyi. Mfuateni, 14 na popote pale aingiapo ndani mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu asema: “Kiko wapi chumba cha wageni kwa ajili yangu ambacho katika hicho naweza kula sikukuu ya kupitwa pamoja na wanafunzi wangu?”’ 15 Naye atawaonyesha nyinyi chumba kikubwa cha juu, chenye vifaa kikiwa tayari; na humo tayarisheni kwa ajili yetu.” 16 Kwa hiyo wanafunzi wakatoka kwenda, nao wakaingia katika jiji na kukuta kama vile alivyowaambia; nao wakatayarisha kwa ajili ya sikukuu ya kupitwa.
17 Baada ya kuwa jioni akaja pamoja na wale kumi na wawili. 18 Na walipokuwa wameegama kwenye meza wakila, Yesu akasema: “Kwa kweli nawaambia nyinyi, Mmoja kati yenu, anayekula pamoja nami, atanisaliti.” 19 Wakaanza kutiwa kihoro na kumwambia mmoja-mmoja; “Si mimi, je, ni mimi?” 20 Akawaambia: “Ni mmoja wa wale kumi na wawili, anayechovya pamoja nami ndani ya bakuli la shirika. 21 Kweli, Mwana wa binadamu anaenda zake, kama vile imeandikwa kumhusu, lakini ole wa mtu huyo ambaye kupitia yeye Mwana wa binadamu asalitiwa! Ingalikuwa bora zaidi kwa mtu huyo kama hangalizaliwa.”
22 Na walipokuwa wakiendelea kula, akachukua mkate, akasema baraka, akaumega akawapa wao, na kusema: “Chukueni, huu wamaanisha mwili wangu.” 23 Na akichukua kikombe, akashukuru akawapa hicho, nao wote wakanywa kutoka hicho. 24 Naye akawaambia: “Hii yamaanisha ‘damu yangu ya agano,’ inayopaswa kumwagwa kwa ajili ya wengi. 25 Kwa kweli nawaambia nyinyi, kwa vyovyote sitakunywa tena kamwe kutokana na zao la mzabibu hadi siku ile nitakapolinywa likiwa jipya katika ufalme wa Mungu.” 26 Mwishowe, baada ya kuimba sifa, wakatoka kwenda kwenye Mlima wa Mizeituni.
27 Na Yesu akawaambia: “Nyinyi nyote mtakwazika, kwa sababu imeandikwa, ‘Hakika nitapiga mchungaji, nao kondoo watatawanywa huku na huku.’ 28 Lakini baada ya mimi kuwa nimefufuliwa hakika nitawatangulia kuingia Galilaya.” 29 Lakini Petro akamwambia: “Hata ikiwa wengine wote wakwazika, hata hivyo hakika mimi sitakwazika.” 30 Ndipo Yesu akamwambia: “Kwa kweli nakuambia, Wewe leo, ndiyo, usiku huu, kabla ya jogoo kuwika mara mbili, naam, utanikana mimi mara tatu.” 31 Lakini yeye akaanza kusema maneno kwa kusisitiza: “Ikinibidi mimi kufa pamoja nawe, hakika sitakukana kwa vyovyote.” Pia, wengine wote wakaanza kusema jambo lilelile.
32 Kwa hiyo wakaja hadi mahali paitwapo jina Gethsemane, naye akawaambia wanafunzi wake: “Ketini hapa wakati nisalipo.” 33 Naye akachukua Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, naye akaanza kufadhaika na kutaabika sana. 34 Naye akawaambia: “Nafsi yangu ina kihoro sana, hata kufikia kifo. Kaeni hapa na kufuliza kulinda.” 35 Na akienda mbele kidogo akaanza kujiangusha juu ya ardhi akaanza kusali kwamba, kama ingewezekana, hiyo saa ipate kupitilia mbali kutoka kwake. 36 Naye akaendelea kusema: “Abba, Baba, mambo yote yawezekana kwako; niondolee kikombe hiki. Lakini si lile nitakalo, bali lile utakalo.” 37 Naye akaja akawakuta wamelala usingizi, naye akamwambia Petro: “Simoni, unalala usingizi? Hukuwa na nguvu ya kufuliza kulinda saa moja? 38 Nyinyi watu, fulizeni kulinda na kusali, ili msije kuingia katika kishawishi. Bila shaka, roho ni yenye hamu, lakini mwili ni dhaifu.” 39 Naye akaenda zake tena akasali, akisema neno hilohilo. 40 Na tena akaja na kuwakuta wamelala usingizi, kwa maana macho yao yalikuwa yamelemewa, na kwa hiyo hawakujua wamjibu nini. 41 Naye akaja mara ya tatu na kuwaambia: “Kwa wakati kama huu nyinyi mmelala usingizi na kupumzika! Yatosha! Saa imekuja! Tazama! Mwana wa binadamu asalitiwa kuingia katika mikono ya watenda-dhambi. 42 Inukeni, acheni twende. Tazameni! Msaliti wangu amekaribia.”
43 Na mara, alipokuwa bado akisema, Yudasi, mmoja wa wale kumi na wawili, akawasili na pamoja naye umati ukiwa na mapanga na marungu umetoka kwa makuhani wakuu na waandishi na wanaume wazee. 44 Basi msaliti wake alikuwa amewapa ishara waliyokubaliana, akisema: “Yeyote yule nibusuye, huyo ndiye; mkamateni na kumwongoza mmpeleke salama.” 45 Naye akaja moja kwa moja akamkaribia na kusema: “Rabi!” na kumbusu kwa wororo sana. 46 Kwa hiyo wakaweka mikono juu yake wakamkamata. 47 Hata hivyo, mtu fulani kati ya hao waliosimama kando akafuta upanga wake akampiga mtumwa wa kuhani wa cheo cha juu akaondoa sikio lake. 48 Lakini kwa kujibu Yesu akawaambia: “Je, mlitoka mkiwa na mapanga na marungu kama dhidi ya mpokonyaji ili kunikamata? 49 Siku baada ya siku nilikuwa pamoja nanyi katika hekalu nikifundisha, na bado hamkunikamata. Hata hivyo, ni ili Maandiko yapate kutimizwa.”
50 Nao wote wakamwacha wakakimbia. 51 Lakini mwanamume fulani kijana aliyevaa vazi la kitani bora juu ya mwili wake ulio uchi akaanza kumfuata karibu-karibu; nao wakajaribu kumkamata, 52 lakini yeye akaacha nyuma vazi lake la kitani akaponyoka akiwa uchi.
53 Sasa wakamwongoza kumpeleka Yesu kwa kuhani wa cheo cha juu, na makuhani wote wakuu na wanaume wazee na waandishi wakakusanyika. 54 Lakini Petro, akiwa umbali wa kutosha, akamfuata hadi katika ua wa kuhani wa cheo cha juu; naye alikuwa ameketi pamoja na mahadimu wa nyumba na kujipasha moto mwenyewe mbele ya moto mwangavu. 55 Wakati huohuo makuhani wakuu na Sanhedrini yote walikuwa wakitafuta ushuhuda dhidi ya Yesu ili kufanya auawe, lakini hawakuwa wakipata wowote. 56 Kwa kweli, wengi walikuwa wakitoa ushahidi usio wa kweli dhidi yake, lakini shuhuda zao hazikukubaliana. 57 Pia, watu fulani walikuwa wakiinuka na kutoa ushahidi usio wa kweli dhidi yake, wakisema: 58 “Sisi tulimsikia akisema, ‘Hakika mimi nitaliangusha chini hekalu hili lililofanyizwa kwa mikono na katika siku tatu hakika nitajenga jingine lisilofanyizwa kwa mikono.’” 59 Lakini wala juu ya misingi hii ushuhuda wao haukupatana.
60 Mwishowe kuhani wa cheo cha juu akainuka katikati yao na kumuuliza Yesu, akisema: “Je, husemi lolote kwa kujibu? Ni nini hawa wanashuhudia dhidi yako?” 61 Lakini yeye akafuliza kukaa kimya na hakutoa jibu hata kidogo. Tena kuhani wa cheo cha juu akaanza kumuuliza na kumwambia: “Wewe ndiwe Kristo Mwana wa Mbarikiwa?” 62 Ndipo Yesu akasema: “Mimi ndiye; na nyinyi watu mtamwona Mwana wa binadamu ameketi kwenye mkono wa kuume wa nguvu akija pamoja na mawingu ya mbinguni.” 63 Ndipo kuhani wa cheo cha juu akararua mavazi yake ya ndani na kusema: “Ni uhitaji gani zaidi tulio nao wa mashahidi? 64 Mlilisikia kufuru. Ni nini lililo dhahiri kwenu?” Wao wote wakamhukumu kuwa mwenye kustahili kupata kifo. 65 Na wengine wakaanza kumtemea mate na kufunika uso wake wote na kumpiga kwa ngumi zao na kumwambia: “Toa unabii!” Na, wakimpiga makofi usoni, mahadimu wa mahakama wakamchukua.
66 Sasa Petro alipokuwa chini uani, mmoja wa wasichana-watumishi wa kuhani wa cheo cha juu akaja, 67 na, alipomwona Petro akijipasha moto mwenyewe, akamtazama moja kwa moja na kusema: “Wewe, pia, ulikuwa pamoja na Mnazareti, Yesu huyu.” 68 Lakini yeye akakana hilo, akisema: “Simjui yeye wala sielewi lile unalosema,” naye akaenda nje kwenye sebule. 69 Huko yule msichana-mtumishi, alipomwona, akaanza tena kuwaambia wale waliosimama kando: “Huyu ni mmoja wao.” 70 Tena akawa akikana hilo. Na mara nyingine zaidi baada ya muda kidogo wale waliosimama kando wakaanza kumwambia Petro: “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana, kwa kweli, wewe ni Mgalilaya.” 71 Lakini yeye akaanza kulaani na kuapa: “Simjui mtu huyu ambaye mwasema juu yake.” 72 Na mara jogoo akawika mara ya pili; na Petro akakumbuka usemi ambao Yesu alimwambia: “Kabla ya jogoo kuwika mara mbili, utanikana mimi mara tatu.” Naye akazidiwa hisia na kutokwa na machozi.