2 Wakorintho
Ya Pili kwa Wakorintho
1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu kupitia mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu kwa kutaniko la Mungu lililo katika Korintho, pamoja na watakatifu wote ambao wako Akaya yote:
2 Na mwe na fadhili isiyostahiliwa na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
3 Mbarikiwa na awe Mungu na Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo, Baba ya rehema nyororo na Mungu wa faraja yote, 4 ambaye hutufariji katika dhiki yetu yote, ili tupate kuweza kufariji wale walio katika namna yoyote ya dhiki kupitia faraja ambayo kwayo sisi wenyewe tunafarijiwa na Mungu. 5 Kwa maana kama vile mateso ya Kristo yazidivyo katika sisi, ndivyo pia faraja tupatayo izidivyo kupitia Kristo. 6 Basi kama tumo katika dhiki, hiyo ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu; au kama tunafarijiwa, hiyo ni kwa ajili ya faraja yenu itendayo ili kuwafanya mvumilie mateso yaleyale ambayo sisi pia twateseka. 7 Na kwa hiyo tumaini letu kwa ajili yenu ni lisiloyumbayumba, tukijua kama tujuavyo, kama vile nyinyi mlivyo washiriki wa hayo mateso, kwa njia hiyohiyo nyinyi pia mtaishiriki faraja.
8 Kwa maana sisi hatutaki nyinyi mwe wasio na ujuzi, akina ndugu, juu ya dhiki iliyotupata katika wilaya ya Asia, kwamba tulikuwa chini ya mkazo mkali mno upitao nguvu yetu, hivi kwamba tulikuwa bila hakika kabisa hata juu ya uhai wetu. 9 Kwa kweli, tulihisi ndani yetu wenyewe kwamba tulikuwa tumeipokea hukumu ya kifo. Hiyo ilikuwa ili tupate kuwa na itibari yetu, si katika sisi wenyewe, bali katika Mungu awafufuaye wafu. 10 Kutoka katika kitu kikubwa sana kama kifo alituokoa na atatuokoa; na tumaini letu limo katika yeye kwamba atatuokoa zaidi pia. 11 Nyinyi pia mwaweza kushiriki kusaidia kwa dua yenu kwa ajili yetu, ili shukrani zipate kutolewa na wengi kwa ajili yetu kwa lile ambalo limepewa kwetu kwa fadhili kwa sababu ya nyuso nyingi zenye sala.
12 Kwa maana jambo tunalojisifia ni hili, ambalo kwalo dhamiri zetu zatoa ushahidi, kwamba kwa utakatifu na weupe wa moyo wa kimungu, si kwa hekima ya kimwili bali kwa fadhili isiyostahiliwa ya Mungu, sisi tumejiendesha wenyewe katika ulimwengu, lakini zaidi hasa kuwaelekea nyinyi. 13 Kwa maana kwa kweli hatuwaandikii nyinyi mambo ila yale myajuayo vema au kuyatambua pia; na ambayo mimi natumaini mtaendelea kuyatambua hadi mwisho, 14 kama vile pia mmetambua, kwa kadiri fulani, kwamba sisi ni sababu yenu ya kujisifu, kama vile nyinyi pia mtakavyokuwa kwetu katika siku ya Bwana wetu Yesu.
15 Kwa hiyo, nikiwa na uhakika huu, nilikuwa nikikusudia hapo mbele kuja kwenu, ili mpate kuwa na pindi ya pili ya kuwa na shangwe, 16 na niende Makedonia baada ya kufanya kituo kuwa pamoja nanyi, na kurudi kutoka Makedonia kuja kwenu na kusindikizwa nanyi kwenda Yudea. 17 Basi, nilipokuwa na kusudio la namna hiyo, sikufanya ugeugeu, ndivyo? Au mambo yote nikusudiayo, je, nakusudia hayo kulingana na mwili, ili kwangu kuwe “Ndiyo, Ndiyo” na “La, La”? 18 Lakini Mungu aweza kutegemewa ili usemi wetu ulioelekezwa kwenu usiwe ni Ndiyo na kumbe ni La. 19 Kwa maana Mwana wa Mungu, Kristo Yesu, aliyehubiriwa miongoni mwenu kupitia sisi, yaani, kupitia mimi na Silvano na Timotheo, hakuwa Ndiyo na kumbe ni La, bali Ndiyo imekuwa Ndiyo katika kisa chake. 20 Kwa maana hata ahadi za Mungu ziwe ni ngapi, zimekuwa Ndiyo kwa njia yake. Kwa hiyo kupitia yeye pia ni “Ameni” isemwayo kwa Mungu kwa ajili ya utukufu kupitia sisi. 21 Lakini yeye atoaye uhakikisho kamili kwamba nyinyi na sisi ni wa Kristo na yeye ambaye ametutia mafuta ni Mungu. 22 Yeye ameweka pia muhuri wake juu yetu na ametupa arbuni ya kitakachokuja, yaani, roho, katika mioyo yetu.
23 Sasa naita Mungu awe shahidi dhidi ya nafsi yangu mwenyewe ya kuwa ni kuwahurumia nyinyi kwamba sijaja Korintho bado. 24 Si kwamba sisi ndio mabwana-wakubwa juu ya imani yenu, bali sisi ni wafanyakazi wenzi kwa shangwe yenu, kwa maana ni kwa imani yenu kwamba nyinyi mnasimama.