Ufunuo
2 “Kwa malaika wa kutaniko katika Efeso andika: Haya ndiyo mambo asemayo yeye ashikaye zile nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye atembeaye katikati ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu, 2 ‘Mimi navijua vitendo vyako, na kazi yako ya jasho na uvumilivu, na kwamba huwezi kuhimili watu wabaya, na kwamba uliwatia kwenye jaribu wale ambao husema wao ni mitume, lakini wao sio, nawe uliwapata kuwa waongo. 3 Wewe unaonyesha uvumilivu pia, nawe umehimili kwa ajili ya jina langu nawe hujawa mwenye unyong’onyevu. 4 Hata hivyo, nashika hili dhidi yako, kwamba umeacha upendo uliokuwa nao hapo kwanza.
5 “‘Kwa hiyo kumbuka ni kutoka katika nini umeanguka, nawe tubu na kufanya vitendo vya kwanza. Usipofanya hivyo, mimi ninakuja kwako, nami hakika nitaondoa kinara chako cha taa kutoka mahali pacho, isipokuwa utubu. 6 Ingawa hivyo, una hili, kwamba wewe wachukia vitendo vya farakano la Nikolausi, ambavyo mimi pia nachukia. 7 Acheni yeye aliye na sikio asikie lile ambalo roho huyaambia makutaniko: Kwake ambaye hushinda hakika nitamruhusu kula kutoka katika mti wa uhai, ambao umo katika paradiso ya Mungu.’
8 “Na kwa malaika wa kutaniko katika Smirna andika: Haya ndiyo mambo asemayo, ‘Wa-Kwanza na Wa-Mwisho,’ aliyekuwa mfu akaja kwenye uhai tena, 9 ‘Najua dhiki na umaskini wako—lakini wewe ni tajiri—na kufuru la wale wasemao wao wenyewe ni Wayahudi, lakini sivyo walivyo bali wao ni sinagogi la Shetani. 10 Usiogope mambo uliyo karibu kuteseka. Tazama! Ibilisi atafuliza kutupa baadhi yenu ndani ya gereza ili mpate kutiwa kwenye jaribu kikamili, na kwamba mpate kuwa na dhiki siku kumi. Jithibitishe mwenyewe kuwa mwaminifu hata kufikia kifo, nami hakika nitakupa taji la uhai. 11 Acheni yeye aliye na sikio asikie lile ambalo roho huyaambia makutaniko: Yeye ashindaye hatadhuriwa kwa vyovyote na kifo cha pili.’
12 “Na kwa malaika wa kutaniko katika Pergamamu andika: Haya ndiyo mambo asemayo yeye aliye na upanga mkali, mrefu wenye makali kuwili, 13 ‘Najua ni wapi unapokaa, yaani, mahali kilipo kiti cha ufalme cha Shetani; na bado wafuliza kushikilia sana jina langu, nawe hukukana imani yako katika mimi hata katika siku za Antipasi, shahidi wangu, aliye mwaminifu, aliyeuawa kando yenu, mahali anapokaa Shetani.
14 “‘Hata hivyo, Nina mambo machache dhidi yako, kwamba unao hapo wale wanaoshikilia sana ufundishaji wa Balaamu, aliyeenda akimfundisha Balaki kuweka kipingamizi chenye kukwaza mbele ya wana wa Israeli, kula vitu vilivyotolewa dhabihu kwa sanamu na kufanya uasherati. 15 Ndivyo wewe, pia, ulivyo na wale wanaoshika sana hivyohivyo ufundishaji wa farakano la Nikolausi. 16 Kwa hiyo tubu. Usipofanya hivyo, mimi ninakuja kwako upesi, nami hakika nitapiga vita nao kwa ule upanga mrefu wa kinywa changu.
17 “‘Acheni yeye aliye na sikio asikie lile ambalo roho huyaambia makutaniko: Yeye ashindaye hakika nitampa baadhi ya mana iliyofichwa, nami hakika nitampa kijiwe cheupe cha mviringo, na juu ya hicho kijiwe cha mviringo jina jipya likiwa limeandikwa ambalo hakuna yeyote alijualo ila yule anayelipokea.’
18 “Na kwa malaika wa kutaniko katika Thiatira andika: Haya ndiyo mambo ambayo Mwana wa Mungu husema, yeye aliye na macho yake kama mwali wa moto, na miguu yake ni kama shaba nyekundu bora, 19 ‘Mimi navijua vitendo vyako, na upendo na imani na huduma na uvumilivu wako, na kwamba vitendo vyako vya juzijuzi ni vyenye kuzidi vile vya hapo zamani.
20 “‘Hata hivyo, nina hili dhidi yako, kwamba wamvumilia mwanamke Yezebeli, ajiitaye mwenyewe nabii wa kike, naye hufundisha na kuwaongoza vibaya watumwa wangu wafanye uasherati na kula vitu vilivyotolewa dhabihu kwa sanamu. 21 Nami nilimpa wakati wa kutubu, lakini yeye hataki kutubu juu ya uasherati wake. 22 Tazama! Mimi niko karibu kumtupa aingie katika kitanda cha ugonjwa, na wale wanaofanya uzinzi pamoja naye katika dhiki kubwa, isipokuwa wakitubu juu ya vitendo vyake. 23 Na watoto wake hakika nitawaua kwa tauni yenye kufisha, hivi kwamba makutaniko yote yatajua kwamba mimi ndimi nichunguzaye mafigo na mioyo, nami hakika nitawapa nyinyi mmoja-mmoja kulingana na vitendo vyenu.
24 “‘Hata hivyo, nawaambia wale wengine kati yenu walio katika Thiatira, wote wale wasiokuwa na ufundishaji huu, walewale ambao hawakupata kujua “mambo yenye kina kirefu ya Shetani,” kama wasemavyo: Mimi siweki juu yenu mzigo mwingine wowote wenye kulemea. 25 Hali kadhalika, shikeni sana lile mlilo nalo mpaka nije. 26 Na yeye ashindaye na kushika vitendo vyangu hadi mwisho hakika nitampa mamlaka juu ya mataifa, 27 naye hakika atachunga watu kwa fimbo ya chuma hivi kwamba watavunjwa vipande-vipande kama vyombo vya udongo wa mfinyanzi, sawa na vile mimi nimepokea kutoka kwa Baba yangu, 28 nami hakika nitampa nyota ya asubuhi. 29 Acheni yeye aliye na sikio asikie lile ambalo roho huyaambia makutaniko.’