Ufunuo
3 “Na kwa malaika wa kutaniko katika Sardisi andika: Haya ndiyo mambo ayasemayo yeye aliye na zile roho saba za Mungu na zile nyota saba, ‘Mimi navijua vitendo vyako, kwamba una jina kuwa uko hai, lakini wewe ni mfu. 2 Uwe mwenye kulinda, na uyatie nguvu mambo yanayobaki yaliyokuwa tayari kufa, kwa maana sikukuta vitendo vyako vimefanywa kikamili mbele ya Mungu wangu. 3 Kwa hiyo, endelea kuzingatia akilini jinsi umepokea na jinsi ulivyosikia, nawe endelea kukitunza, na utubu. Hakika usipoamka, nitakuja kama mwizi, na hutajua hata kidogo ni saa gani nitakapokuja juu yako.
4 “‘Hata hivyo, unayo majina machache katika Sardisi ambayo hayakutia unajisi mavazi yao ya nje, nao kwa hakika watatembea pamoja nami wakiwa wamevaa meupe, kwa sababu yanastahili. 5 Yeye ambaye hushinda atapambwa hivyo mavazi meupe ya nje; na hakika sitalifuta kwa vyovyote jina lake kutoka katika kitabu cha uhai, bali hakika nitalikiri jina lake mbele ya Baba yangu na mbele ya malaika zake. 6 Acheni yeye aliye na sikio asikie lile ambalo roho huyaambia makutaniko.’
7 “Na kwa malaika wa kutaniko katika Filadelfia andika: Haya ndiyo mambo ayasemayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, afunguaye hivi kwamba hakuna yeyote atakayefunga, na afungaye hivi kwamba hakuna yeyote afunguaye, 8 ‘Mimi navijua vitendo vyako—tazama! nimeweka mbele yako mlango uliofunguliwa, ambao hakuna yeyote awezaye kuufunga—kwamba una nguvu kidogo, na ulitunza neno langu na hukuthibitika kuwa asiye wa kweli kwa jina langu. 9 Tazama! Hakika mimi nitawapa wale wa kutoka sinagogi la Shetani wasemao ni Wayahudi, lakini sivyo walivyo bali wanasema uwongo—tazama! hakika mimi nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako na kuwafanya wajue nimekupenda wewe. 10 Kwa sababu ulitunza neno juu ya uvumilivu wangu, hakika mimi pia nitakutunza utoke katika saa ya jaribu, itakayokuja juu ya dunia nzima inayokaliwa, ili kutia jaribu juu ya wale wanaokaa juu ya dunia. 11 Mimi ninakuja upesi. Fuliza kushika sana lile ulilo nalo, ili yeyote asipate kuchukua taji lako.
12 “‘Yeye ashindaye—hakika mimi nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, naye hakika kwa vyovyote hataenda kutoka katika hilo tena kamwe, nami hakika nitaandika juu yake jina la Mungu wangu na jina la jiji la Mungu wangu, Yerusalemu jipya lishukalo kutoka mbinguni kwa Mungu wangu, na jina langu jipya. 13 Acheni yeye aliye na sikio asikie lile ambalo roho huyaambia makutaniko.’
14 “Na kwa malaika wa kutaniko katika Laodikia andika: Haya ndiyo mambo ayasemayo Ameni, shahidi mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa uumbaji wa Mungu, 15 ‘Mimi navijua vitendo vyako, kwamba wewe si baridi wala moto. Laiti ungalikuwa baridi au moto. 16 Kwa hiyo, kwa sababu wewe ni vuguvugu wala si moto wala baridi, nitakutapika kutoka kinywani mwangu. 17 Kwa sababu wasema: “Mimi ni tajiri na nimejipatia utajiri na sihitaji kitu chochote hata kidogo,” lakini hujui wewe ni mwenye taabu na wa kusikitikiwa na maskini na kipofu na uchi, 18 nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa sana kwa moto ili upate kuwa tajiri, na mavazi meupe ya nje ili upate kuwa umevishwa mavazi na kwamba aibu ya uchi wako isipate kudhihirika, na dawa ya macho ya kusugua katika macho yako ili upate kuona.
19 “‘Wote wale niwaoneao shauku nawakaripia na kuwatia nidhamu. Kwa hiyo uwe mwenye bidii na utubu. 20 Tazama! Mimi nimesimama mlangoni na kubisha. Ikiwa yeyote asikia sauti yangu na kuufungua mlango, hakika mimi nitakuja ndani ya nyumba yake na kula mlo wa jioni pamoja naye na yeye pamoja nami. 21 Yeye ashindaye hakika nitamruhusu kuketi pamoja nami katika kiti changu cha ufalme, kama vile mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha ufalme. 22 Acheni yeye aliye na sikio asikie lile ambalo roho huyaambia makutaniko.’”