Mwanzo
40 Baada ya hayo, msimamizi mkuu wa vinywaji+ na mwokaji mkuu wa mfalme wa Misri walimkosea bwana wao, mfalme wa Misri. 2 Kwa hiyo Farao akawakasirikia vikali maofisa hao wawili, msimamizi mkuu wa vinywaji na mwokaji mkuu,+ 3 akawatupa katika gereza lililokuwa katika nyumba ya mkuu wa walinzi,+ mahali ambapo Yosefu alikuwa amefungwa.+ 4 Kisha mkuu wa walinzi akamwagiza Yosefu akae nao na kuwatunza,+ nao wakakaa gerezani kwa muda fulani.*
5 Msimamizi wa vinywaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, waliokuwa wamefungwa gerezani, waliota ndoto usiku mmoja, na kila ndoto ilikuwa na maana yake.* 6 Asubuhi iliyofuata, Yosefu alipoingia na kuwaona, walionekana wamehuzunika. 7 Basi akawauliza maofisa hao wa Farao waliokuwa naye gerezani katika nyumba ya bwana wake: “Mbona nyuso zenu zina huzuni leo?” 8 Wakamjibu: “Kila mmoja wetu aliota ndoto lakini hakuna mtu wa kutueleza maana yake.”* Yosefu akawaambia: “Je, si kazi ya Mungu kueleza maana ya ndoto?+ Tafadhali, nisimulieni ndoto zenu.”
9 Basi msimamizi mkuu wa vinywaji akamsimulia Yosefu ndoto yake akisema: “Katika ndoto yangu, niliona mzabibu mbele yangu. 10 Na mzabibu huo ulikuwa na matawi matatu, na ulipokuwa ukichipua vitawi, ulichanua maua, na zabibu zilizokuwa kwenye vishada vyake zikaiva. 11 Na kikombe cha Farao kilikuwa mikononi mwangu, nami nikachukua zabibu na kuzikamua ndani ya kikombe cha Farao. Kisha nikakiweka kikombe hicho mkononi mwa Farao.” 12 Ndipo Yosefu akamwambia: “Hii ndiyo maana yake. Yale matawi matatu ni siku tatu. 13 Siku tatu kuanzia leo, Farao atakutoa gerezani* na kukurudisha kwenye cheo chako,+ nawe utaendelea kuweka kikombe cha Farao mkononi mwake kama ulivyokuwa ukifanya ulipokuwa msimamizi wake wa vinywaji.+ 14 Hata hivyo, unikumbuke mambo yatakapokwendea vema. Tafadhali, nitendee kwa upendo mshikamanifu na umwambie Farao kunihusu, ili anitoe mahali hapa. 15 Ukweli ni kwamba nilitekwa nyara kutoka katika nchi ya Waebrania,+ nami sijafanya kosa lolote linalostahili nitupwe gerezani.”*+
16 Mwokaji mkuu alipoona kwamba Yosefu amesema* jambo jema kuhusu ndoto hiyo, akamwambia: “Mimi pia niliota ndoto, kulikuwa na vikapu vitatu vyenye mikate myeupe juu ya kichwa changu, 17 na katika kikapu cha juu, kulikuwa na kila aina ya vitu vilivyookwa kwa ajili ya Farao, na kulikuwa na ndege waliokula vitu vilivyokuwa katika kikapu kilichokuwa juu ya kichwa changu.” 18 Ndipo Yosefu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Vile vikapu vitatu ni siku tatu. 19 Siku tatu kuanzia leo, Farao atakukata kichwa na kukutundika mtini, na ndege wataula mwili wako.”+
20 Sasa siku ya tatu ilikuwa sikukuu ya kuzaliwa kwa Farao,+ kwa hiyo aliwafanyia karamu watumishi wake wote, akamtoa gerezani msimamizi mkuu wa vinywaji na mwokaji mkuu, akawaleta mbele ya watumishi wake. 21 Akamrudisha msimamizi mkuu wa vinywaji kwenye cheo chake, akaendelea kumpa Farao kikombe. 22 Lakini akamtundika mwokaji mkuu, kama Yosefu alivyokuwa ameeleza.*+ 23 Hata hivyo, msimamizi mkuu wa vinywaji hakumkumbuka Yosefu; aliendelea kumsahau.+