Waamuzi
9 Baada ya muda Abimeleki+ mwana wa Yerubaali akaenda Shekemu kwa ndugu za mama yake na kwa familia yote ya babu yake,* akawaambia hivi: 2 “Tafadhali waulizeni viongozi wote* wa Shekemu, ‘Je, ni afadhali zaidi kwenu kutawaliwa na wana wote 70 wa Yerubaali+ au na mtu mmoja tu? Kumbukeni kwamba mimi ni mfupa wenu na nyama yenu.’”*
3 Basi ndugu za mama yake wakawaambia viongozi wote wa Shekemu maneno hayo kwa niaba yake, nao wakaamua kumfuata* Abimeleki kwa maana walisema: “Yeye ni ndugu yetu.” 4 Wakampa Abimeleki vipande 70 vya fedha kutoka katika nyumba ya* Baal-berithi,+ naye akavitumia kuwakodi watu wazembe na wahuni ili wamfuate. 5 Kisha akaenda nyumbani kwa baba yake huko Ofra+ na kuwaua ndugu zake,+ wana 70 wa Yerubaali, juu ya jiwe moja. Yothamu mwana mdogo zaidi wa Yerubaali ndiye aliyeokoka peke yake, kwa sababu alijificha.
6 Kisha viongozi wote wa Shekemu na wakaaji wote wa Beth-milo wakakusanyika pamoja na kumweka Abimeleki kuwa mfalme,+ karibu na ule mti mkubwa, penye nguzo iliyokuwa Shekemu.
7 Walipomwambia Yothamu habari hizo, akaenda mara moja na kusimama juu ya kilele cha Mlima Gerizimu,+ akawaambia hivi kwa sauti kubwa: “Nisikilizeni, enyi viongozi wa Shekemu, naye Mungu atawasikiliza.
8 “Siku moja miti ilitaka kumtia mafuta mmoja wao awe mfalme. Basi ikauambia mzeituni, ‘Tutawale.’+ 9 Lakini mzeituni ukaiambia, ‘Je, niache kuzalisha mafuta yangu yanayotumiwa kumtukuza Mungu na wanadamu, niende kuitawala miti mingine?’ 10 Kisha miti ikauambia mtini, ‘Njoo ututawale.’ 11 Lakini mtini ukaiambia, ‘Je, niache kuzalisha matunda yangu matamu niende kuitawala miti mingine?’ 12 Kisha miti ikauambia mzabibu, ‘Njoo ututawale.’ 13 Mzabibu ukasema, ‘Je, niache kutoa divai yangu nzuri inayomfurahisha Mungu na wanadamu niende kuitawala miti?’ 14 Mwishowe miti mingine yote ikauambia mkwamba,* ‘Njoo ututawale.’+ 15 Ndipo mkwamba ukaiambia miti hiyo, ‘Ikiwa kweli mnanitia mafuta niwe mfalme wenu, njooni mkae chini ya kivuli changu. Kama sivyo, moto na utoke ndani yangu na kuiteketeza mierezi ya Lebanoni.’
16 “Je, mmetenda kwa unyoofu na heshima kwa kumweka Abimeleki kuwa mfalme,+ na je, mmemtendea wema Yerubaali na nyumba yake, je, mmemtendea anavyostahili? 17 Baba yangu alipowapigania,+ alihatarisha uhai wake* ili kuwaokoa kutoka mikononi mwa Wamidiani.+ 18 Lakini leo mmeasi nyumba ya baba yangu na kuwaua wanawe 70 juu ya jiwe moja.+ Kisha mkamweka Abimeleki, mwana wa kijakazi wake,+ awe mfalme juu ya viongozi wa Shekemu kwa sababu tu yeye ni ndugu yenu. 19 Basi ikiwa leo mmemtendea Yerubaali na nyumba yake kwa unyoofu na heshima, shangilieni pamoja na Abimeleki naye pia ashangilie pamoja nanyi. 20 Kama sivyo, moto na utoke kwa Abimeleki na kuwateketeza viongozi wa Shekemu na Beth-milo,+ pia moto utoke kwa viongozi wa Shekemu na Beth-milo na kumteketeza Abimeleki.”+
21 Ndipo Yothamu+ akakimbilia Beeri, akaishi huko kwa sababu alimwogopa Abimeleki ndugu yake.
22 Abimeleki alitawala* Israeli kwa miaka mitatu. 23 Ndipo Mungu akaacha uadui utokee* kati ya Abimeleki na viongozi wa Shekemu, nao wakamtendea Abimeleki kwa hila. 24 Hayo yalitokea ili kulipiza ukatili waliotendewa wale wana 70 wa Yerubaali, na ili hatia ya damu iwe juu ya Abimeleki ndugu yao kwa sababu aliwaua,+ na juu ya viongozi wa Shekemu kwa sababu walimsaidia kuua ndugu zake. 25 Basi viongozi wa Shekemu wakaweka watu wamvizie Abimeleki milimani, wakamwibia kila mtu aliyepita karibu nao. Abimeleki akaambiwa mambo hayo.
26 Basi Gaali mwana wa Ebedi na ndugu zake wakavuka kuingia Shekemu,+ nao viongozi wa Shekemu wakamtumaini. 27 Wakaenda kuvuna zabibu katika mashamba yao ya mizabibu na kuzikanyaga katika shinikizo la divai, wakafanya sherehe, kisha wakaingia katika nyumba ya mungu wao,+ wakala, wakanywa, na kumlaani Abimeleki. 28 Ndipo Gaali mwana wa Ebedi akasema, “Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani ili tumtumikie? Je, yeye si mwana wa Yerubaali,+ na je, Zebuli si mjumbe wake? Watumikieni wana wa Hamori, baba ya Shekemu! Kwa nini tumtumikie Abimeleki? 29 Laiti watu hawa wangekuwa chini ya amri yangu, ningemwondoa Abimeleki.” Kisha akamwambia hivi Abimeleki: “Ongeza jeshi lako, uje tupigane.”
30 Zebuli mkuu wa jiji aliposikia maneno ya Gaali mwana wa Ebedi, akakasirika sana. 31 Kwa hiyo akawatuma kwa siri* wajumbe kwa Abimeleki, akisema, “Gaali mwana wa Ebedi na ndugu zake wako Shekemu, wanalichochea jiji likupinge. 32 Basi njoo usiku pamoja na watu wako mwavizie shambani. 33 Mara tu jua linapochomoza asubuhi, amkeni mapema mlishambulie jiji; atakapokuja na watu wake kuwashambulia, jitahidini kabisa kumshinda.”*
34 Basi Abimeleki na watu wake wote wakaja usiku, wakalivizia jiji la Shekemu wakiwa vikosi vinne. 35 Gaali mwana wa Ebedi alipotoka nje na kusimama kwenye lango la jiji, Abimeleki na watu wake wakatoka mafichoni. 36 Gaali alipowaona, akamwambia Zebuli, “Tazama! Kuna watu wanaoshuka kutoka milimani.” Lakini Zebuli akamwambia, “Unaona vivuli vya milima ukifikiri ni watu.”
37 Baadaye Gaali akasema, “Tazama! Watu wanashuka kutoka katikati ya nchi, na kikosi kimoja kinakuja kupitia njia ya mti mkubwa wa Meonenimu.” 38 Ndipo Zebuli akamwambia, “Umesahau ulivyojigamba ukisema, ‘Abimeleki ni nani ili tumtumikie?’+ Je, hawa si wale watu uliowadharau? Sasa nenda upigane nao.”
39 Basi Gaali akawaongoza viongozi wa Shekemu kupigana na Abimeleki. 40 Gaali akashindwa na kukimbia, naye Abimeleki akamkimbiza, na watu wengi wakauawa mpaka kwenye lango la jiji.
41 Abimeleki akaendelea kukaa Aruma, naye Zebuli+ akawafukuza Gaali na ndugu zake kutoka Shekemu. 42 Kesho yake watu wakatoka na kwenda shambani, na Abimeleki akaambiwa jambo hilo. 43 Basi akachukua watu wake na kuwagawa katika vikosi vitatu na kuvizia shambani. Alipoona watu wakitoka jijini, akawashambulia na kuwaua. 44 Abimeleki na kikosi chake wakaenda mbio na kusimama kwenye lango la jiji, na vikosi viwili vikawashambulia na kuwaua watu wote waliokuwa shambani. 45 Abimeleki akapigana na jiji hilo siku nzima na kuliteka. Akawaua wakaaji wake, kisha akalibomoa jiji hilo+ na kulitia chumvi.
46 Viongozi wote wa mnara wa Shekemu waliposikia habari hizo, wakaenda haraka katika ngome ya nyumba ya* El-berithi.+ 47 Abimeleki alipoambiwa kwamba viongozi wote wa Shekemu wamekusanyika pamoja, 48 akapanda Mlima Salmoni pamoja na watu wake. Akachukua shoka, akakata tawi la mti na kulibeba begani, akawaambia hivi watu wake: “Mlivyoona nikifanya, fanyeni vivyo hivyo haraka!” 49 Basi watu wote wakakata pia matawi na kumfuata Abimeleki. Kisha wakayaweka kuzunguka ile ngome na kuiteketeza. Na watu wote waliokuwa ndani ya mnara wa Shekemu wakafa pia, watu karibu 1,000, wanaume na wanawake.
50 Kisha Abimeleki akaenda Thebesi; akalishambulia jiji la Thebesi na kuliteka. 51 Kulikuwa na mnara imara katikati ya jiji hilo, wanaume na wanawake wote, na viongozi wote wa jiji hilo wakakimbilia humo. Wakajifungia ndani yake na kupanda juu ya paa lake. 52 Abimeleki akaenda kwenye mnara huo na kuushambulia. Akaenda kwenye mlango wa mnara ili auchome moto. 53 Ndipo mwanamke fulani akaangusha jiwe la kusagia juu ya kichwa cha Abimeleki na kumpasua kichwa.+ 54 Abimeleki akamwita haraka mtumishi aliyembebea silaha na kumwambia, “Chomoa upanga wako uniue, watu wasije wakasema, ‘Mwanamke ndiye aliyemuua.’” Basi mtumishi wake akamchoma upanga, naye akafa.
55 Wanaume Waisraeli walipoona kwamba Abimeleki amekufa, wote wakarudi nyumbani. 56 Hivyo Mungu akalipiza kisasi kwa sababu ya uovu ambao Abimeleki alimtendea baba yake kwa kuwaua ndugu zake 70.+ 57 Pia Mungu akafanya watu wa Shekemu waadhibiwe kwa sababu ya uovu wao wote. Basi laana ya Yothamu+ mwana wa Yerubaali+ ikawapata.