Kuutazama Ulimwengu
RIPOTI YA AFYA YA ULIMWENGU
Asilimia 20 ya idadi ya watu wa ulimwengu—karibu watu milioni elfu moja—hupatwa na matatizo makubwa ya afya, kulingana na Ripoti juu ya Afya ya Ulimwengu iliyotolewa na WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni). Yaliyo makubwa zaidi ni maradhi ya watoto, maambukizo ya pumu, maradhi ya kuhara, maradhi ya kuambukia kingono (kutia ndani UKIMWI), kifua kikuu, kichocho, na malaria. Matatizo makubwa zaidi ya afya husemekana kuwa yamo katika mataifa yaliyo Afrika iliyo kusini mwa Sahara, ambako watu milioni 160 wana UKIMWI, maradhi ya viini, malaria, na magonjwa mengine; na katika Asia ya kusini na mashariki, ambako asilimia 40 ya idadi ya watu, karibu milioni 500 hupatwa na maradhi na ukosefu wa chakula kinachofaa. Wengi hupatwa na madhara yenye kufuatana ambamo umaskini huleta maradhi ambayo nayo hutokeza umaskini na magonjwa yaliyoongezeka. Matumizi ya kiafya ya kila mwaka katika nchi zilizo maskini zaidi yana wastani wa dola zinazopungua 5 kwa kila mtu. Kulingana na Dakt. Hiroshi Nakajima, mkurugenzi mkuu wa WHO, kuongezwa dola 2 kwa kila mtu kungewezesha uchanjaji na tiba yenye kufaulu kwa kutumia madawa kwa magonjwa yaliyo mengi.
KUFANYA MAAMUZI
Ni wakati gani unapofanya maamuzi yako yaliyo bora zaidi—wakati umesimama au wakati umeketi? Kulingana na uchunguzi mmoja wa Chuo Kikuu cha California ya Kusini, “watu walio chini ya msongo hufanya maamuzi karibu 20% upesi zaidi wakisimama badala ya kuketi,” laripoti gazeti American Health. Uchunguzi huo ulihusisha mfululizo wa maswali yaliyoonyeshwa kwenye kiambaza cha kompyuta, huku wakishiriki wakijibu wakiwa wameketi na kisha wamesimama. Kusimama kulitokeza matokeo bora zaidi. Wale wenye umri mkubwa zaidi na wanaoshindia kuketi walifanya maendeleo zaidi walipofanya maamuzi wakiwa wamesimama. Hilo halishangazi, kwa kuwa mpigo wa moyo huongezeka karibu midundo kumi kwa dakika moja unaposimama, hilo likichochea “maeneo ya akili yanayoongoza msisimuko.” Kusimama na kujinyoosha kwa ukawaida wakati wa siku ya kazi kwapendekezwa kwa wafanya kazi wa ofisi wanaoshinda wameketi.
UKIMWI KUPITIA UGAVI WA DAMU
Wengi kufikia asilimia 40 ya wenye UKIMWI katika Soviet wamepata kiini hicho kupitia damu chafu, laripoti The Toronto Star. Akitaja hali hiyo kuwa “yenye kushtua sana,” Valentin Pokrovsky, kiongozi wa Chuo cha Soviet cha Sayansi za Tiba, akubali hivi: “Tuna asilimia kubwa sana ya visa vya kiini cha UKIMWI kikienezwa kupitia damu wakati wa upasuaji.” Katika majiji ya kusini ya Elista na Volgograd, mieneo ya UKIMWI imeletwa na sindano chafu zinazotumiwa katika hospitali. Angalau watoto 81 wameambukizwa kiini hicho huko.
ORODHA YA HESABU YA NYIKA YA TUFE
Ni kadiri gani ya ulimwengu ambayo ingali nyika, isiyoingiliwa sana na binadamu? Kwa ujumla theluthi moja ya umbo la bara la sayari hii—karibu kilometa za mraba milioni 48.24—asema mchanganuzi wa maongozi ya mazingira J. Michael McCloskey na mwanajiografia Heather Spalding, ambao walifanya utafiti wa hilo kwa miezi 18. Katika kuchunguza-chunguza ramani za usafirio za hewani, “walipuuza majimbo yenye kuonyesha barabara, kambi, majengo, viwanja vya ndege, reli, mabomba, waya za umeme, silanga, maji yaliyowekwa akiba na visima vya mafuta,” lasema Science News. Pia “hesabu yao ilitia ardhi zinazohusisha angalau hektari 405,000.” Ya kwanza kwenye orodha, ikiwa na jumla ya nyika, ni Antarctica. Kisha yafuata Amerika Kaskazini (asilimia 37.5); Soviet Union (asilimia 33.6); Australasia, ambayo yatia ndani visiwa vya Pasifiki ya kusini-magharibi (asilimia 27.9); Afrika (asilimia 27.5); Amerika ya Kusini (asilimia 20.8); Asia (asilimia 13.6); na Ulaya (asilimia 2.8). Asilimia inayopungua 20 ya maeneo ya nyika ya ulimwengu yamelindwa kisheria yasitumiwe vibaya.
TUMBILI WA KUKODISHWA
Akikabiliwa na upungufu mkubwa wa wafanya kazi wa kutumia mikono, mkulima mmoja wa Korea nje tu ya Seoul ametumikisha tumbili kukusanya nazi za msunobari kwenye shamba lake. Mainichi Daily News la Japan liliripoti kwamba tumbili hao 20 walioajiriwa “walipatikana kuwa wanafanya kazi kwa bidii sana katika shamba hilo baada ya kipindi kifupi cha mazoezi hivi kwamba kila tumbili alifanya kazi inayolingana na ya wafanya kazi watano kwa siku moja.” Maofisa wa serikali wa mahali hapo wanasema wataingiza nchini tumbili zaidi mwaka huu kutoka Thailand ili waajiriwe kwenye mashamba mengine. Ingawa wafanya kazi wa kigeni wenye kutumia mikono wamepigwa marufuku katika Jamhuri ya Korea, kwa wazi sivyo ilivyo kwa tumbili wa kigeni.